Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Trump atangaza hatua kali zaidi za kiuchumi dhidi ya Iran na washirika wake
Shinikizo hili jipya la kulenga zaidi uchumi wa Iran linakuja wakati vita vya Iran vikielekea kutimiza miezi sita bila ya juhudi zozote madhubuti za kidiplomasia wala kijeshi.
Muhtasari
- DRC kupokea dozi 70,000 za chanjo ya Ebola
- Mke wa Besigye alaani kuendelea kwa kesi ya mumewe licha ya hali yake ya afya
- Watu waliojihami wateka meli ya mizigo na kuielekeza Somalia
- China yaitaka Korea Kusini kutounga upande wowote mkono katika mzozo na Marekani
- Aliyekuwa Waziri Zambia auawa katika operesheni ya vikosi vya usalama dhidi ya upinzani
- Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Liberia, akabiliwa na mashtaka ya ulanguzi wa dawa za kulevya
- Mwanamfalme Harry na Meghan Markle kurejea Uingereza
- Waasi wa M23 waweka vikwazo vipya vya usafiri Mashariki mwa DRC baada ya kuenea kwa Ebola
- Wanigeria 83 warejea nyumbani kwa kuhofia ghasia dhidi ya wahamiaji Afrika Kusini
- 13 wauawa Kyiv Ukraine ikikabiliwa na uhaba wa mifumo ya ulinzi wa anga
- Deni la taifa la Marekani lavuka dola trilioni 40
- Mhadhiri wa Chuo Kikuu Tanzania adaiwa kutaka kuchoma majengo ya polisi
- Israel yatangaza zabuni ya mradi 'tata' wa makazi katika Ukingo wa Magharibi
- Mkuu wa idara ya ujasusi ya Ecuador afariki katika ajali ya helikopta Kenya
- Jeshi la Israel lakiri kumuua msichana wa Kipalestina
- Trump atangaza kuiwekea Iran vikwazo vikali vya kiuchumi
Moja kwa moja
Na Ambia Hirsi & Beldeen Waliaula
DRC kupokea dozi 70,000 za chanjo ya Ebola
Dozi elfu 70,000 za chanjo ya Ebola zitapelekwa nchini DRC, ili kupambana na mlipuko wa ugonjwa huo.
Kundi la Kimataifa la Kuratibu Ugavi wa Chanjo limesema kuwa shehena hiyo inajumuisha dozi elfu 50,000 kwa ajili ya wahudumu wa afya walioko katika mstari wa mbele katika kukabiliana na mlipuko huo ambao maambukizi yake yanazidi kuongezeka kila siku.
Dozi hizo 70,000 ni za chanjo ya Ervebo, iliyotengenezwa kupambana na aina ya virusi vya Ebola ya Zaire ambayo ndiyo ya kawaida zaidi.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema kuwa chanjo hiyo imeonyesha ufanisi fulani katika majaribio dhidi ya aina adimu ya Ebola ya Bundibugyo, ambayo inaenea nchini DRC kwa sasa
Kati ya dozi hizo,elfu 20,000 zinazopelekwa nchini humo zimetengwa kwa ajili ya majaribio ya kitabibu, huku zilizosalia zikiwa kwa ajili ya wahudumu wa afya walio katika mstari wa mbele.
Chanjo mbili tofauti zilizotengenezwa mahususi dhidi ya aina hiyo ya virusi pia zinaanza kufanyiwa majaribio kwa binadamu kwa mara ya kwanza.
Hadi kufikia sasa, imethibitishwa kuwa watu 2,378 wamefariki dunia kutokana na Ebola huko DRC, huku kukiwa na visa 5,021 vilivyothibitishwa.
Soma pia:
Mke wa Besigye alaani kuendelea kwa kesi ya mumewe licha ya hali yake ya afya
Mke wa kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye, Winnie Byanyima amelaani hatua ya kuendelea kusikilizwa kwa kesi ya Besigye kwa siku ya pili, huku mwanasiasa huyo akiwa amelazwa gerezani.
Besigye, mwenye umri wa miaka 70, amekuwa kizuizini, akikabiliwa na mashtaka ya uhainikutokana na madai ya kupanga njama ya kutaka kumpindua Rais wa muda mrefu, Yoweri Museveni, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka wa 1986.
Winnie Byanyima, ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa UNAIDS, ameshtumu vikali kuendelea kwa kesi hiyo wakati Besigye hawezi kufika mahakamani kutokana na hali yake ya kiafya.
“Hii si kesi, ni utani, kwa sababu Kizza Besigye hajakataa kufika mahakamani amelazwa kitandani, ni mgonjwa sana, hawezi kuzungumza,” Byanyima aliiambia shirika la habari la AFP.
Besigye alitekwa nyara nchini Kenya mwaka 2024 na baadaye kusafirishwa hadi nchini Uganda, ambako alifikishwa mbele ya mahakama ya kijeshi kabla kesi yake kuhamishiwa katika mahakama ya kiraia.
Mwanasiasa huyo awali alikuwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) baada ya kuanguka akiwa mahakamani, lakini alirejeshwa gerezani mapema mwezi huu licha ya ushauri wa madaktari kuwa hali yake ya afya si nzuri.
Mapema mwezi huu, Byanyima aliiomba serikali ya Uganda imwachilie Besigye kwa dhamana ili aweze kupata matibabu.
Watu waliojihami wateka meli ya mizigo na kuielekeza Somalia
Shirika la usalama wa baharini la Uingereza limesema kuwa, meli moja ya mizigo iliyokuwa ikisafiri katika Ghuba ya Aden imetekwa na watu sita wenye silaha ambao wamielekeza kuelekea Somalia.
Tukio hilo limetokea wakati kuna ongezeko la mashambulizi ya maharamia wa Somalia baada ya zaidi ya muongo mmoja wa kupungua kwa visa hivyo.
Tukio hilo pia limetokea wakati Iran imekuwa ikitishia kwamba washirika wake, wanamgambo wa Kihouthi nchini Yemen, watazuia meli zinazopita katika Bahari Nyekundu kupitia Ghuba ya Aden.
Bado haijafahamika ni nani aliyeiteka meli hiyo, lakini tukio hilo, ni la hivi karibuni zaidi tangu kuongezeka tena kwa shughuli za uharamia wa Somalia tangu mwezi Aprili.
Soma pia:
China yaitaka Korea Kusini kutounga upande wowote mkono katika mzozo na Marekani
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa China, Wang Yi, ameishauri Korea Kusini kutounga upande wowote mkono kati ya Beijing na Washington, akisema Marekani inapaswa kuachana na sera yake ya “uadui” dhidi ya Korea Kaskazini ili kupunguza mvutano katika Rasi ya Korea.
Wang alitoa kauli hiyo katika mkutano na Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Korea Kusini, Wi Sung-lac, mjini Seoul siku hii leo, na baadaye kukutana na Rais wa Korea Kusini, Lee Jae Myung.
Shirika la habari Xinhua lilimnukuu Wang akisema kuwa, “suluhisho la msingi la mvutano katika Rasi ya Korea ni kushughulikia chanzo cha tatizo iliyopo na Marekani kuachana na sera yake ya uadui dhidi ya Korea Kaskazini.”
Kauli hiyo imekuja baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kusema hapo jana kuwa anapanga kukutana na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, baadaye mwaka huu. Trump pia alisema Korea Kaskazini ina silaha za nyuklia 57 zenye nguvu kubwa.
Soma pia:
Aliyekuwa Waziri Zambia auawa katika operesheni ya vikosi vya usalama dhidi ya upinzani
Aliyekuwa waziri wa Zambia amesemekana aliuawa katika uvamizi uliofanywa na vikosi vya usalama katika nyumba inayosemekana kuwa ya kiongozi wa upinzani Brian Mundubile, siku moja baada ya uchaguzi wa urais Zambia.
Msemaji wa polisi amesema Mutotwe Kafwaya alijeruhiwa vibaya na kufariki baada ya kupigwa risasi na maafisa wa usalama wakati wa kile ambacho mamlaka zimesema kilikuwa ni majibizano ya risasi katika operesheni ya kiusalama mjini Lusaka siku ya Ijumaa.
Watu 11 walikamatwa katika uvamizi huo, huku mamlaka zikiishutumu chama cha NRPUP, kinachoongozwa na Mundubile, kwa “kuhusika na uasi” na “shughuli za kijeshi za wanamgambo”, pamoja na kuhifadhi silaha za “kiwango cha juu”.
Mundubile, ambaye tangu wakati huo amejificha, ameyapinga madai hayo na kuyaita “uzushi.”
Kulingana matokeo rasmi, Rais aliye madarakani Hakainde Hichilema alishinda muhula wake wa pili wa miaka mitano kwa kupata asilimia 60 ya kura. Mundubile, alishikilia nafasi ya pili kwa asilimia 38, na amepanga kupinga matokeo hayo mahakamani baada ya kudai kuwa mchakato wa kujumlisha kura uliingiliwa.
Polisi walithibitisha kifo cha Kafwaya Jumatano usiku, huku kukiwa na ongezeko la madai ya kutaka mamlaka kutoa taarifa kuhusu kilichotokea.
Soma pia:
Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Liberia, akabiliwa na mashtaka ya ulanguzi wa dawa za kulevya
Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Liberia, Jewel Howard-Taylor, ameshtakiwa kwa tuhuma za kuhusika na usafirishaji wa dawa za kulevya, utakatishaji fedha na makosa mengine kadhaa, katika uchunguzi wa kimataifa wa ulanguzi wa dawa za kulevya.
Howard-Taylor alizuiliwa hapo jana kabla ya kupanda ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Roberts, katika mji mkuu wa Monrovia.
Mkuu wa Polisi nchini Liberia, Gregory Coleman, amemhusisha makamu huyo wa zamani na kukamatwa kwa dawa ya kulevya aina ya cocaine yenye thamani ya dola milioni 317mwezi uliopita.
Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 63 bado hajatoa tamko lolote kuhusu tuhuma hizo. Wakili wake aliiambia BBC kuwa hawezi kutoa maoni hadi Howard-Taylor afikishwe rasmi mahakamani na kusomewa mashtaka.
Howard-Taylor anakabiliwa na mashtaka yakiwemo kuingiza nchini, kuuza na kusafirisha dawa zinazodhibitiwa bila leseni, biashara haramu ya dawa za kulevya, kuchochea uhalifu na kuwezesha uhalifu.
Howard-Taylor aliingia katika siasa za Liberia baada ya aliyekuwa mume wake, Rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor, kuondoka madarakani. Charles Taylor alikuwa kiongozi wa zamani wa waasi ambaye alichaguliwa kuwa rais wa Liberia mwaka wa 1997 hadi 2003.
Miaka kadhaa baadaye, George Weah alimchagua Howard-Taylor kuwa mgombea mwenza wake. Alikuwa makamu wake wa rais wakati wa utawala wake kuanzia mwaka 2018 hadi 2024.
Mwanamfalme Harry na Meghan Markle kurejea Uingereza
Mwanamfalme Harry na mkewe Meghan Markle wanapanga kurejea kuishi nchini Uingereza.
Wawili hao wanatarajiwa kuondoka Marekani baadaye mwezi huu na kuhamia katika makazi binafsi, yasiyo rasmi ya kifalme, nje ya mji wa London. Taarifa hiyo iliripotiwa na gazeti la Daily Telegraph na The Sun.
Watoto wao, Archie mwenye umri wa miaka saba na Lilibet mwenye miaka mitano, wamesajiliwa kuanza masomo katika shule moja nchini Uingereza mwezi Septemba.
Mfalme Charles aliarifiwa kuhusu mpango huo siku ya Jumapili.
Kwa sasa, hakuna mipango ya Mwanamfalme Harry au Meghan kurejea katika majukumu yao ya kifalme.
Wawili hao walihama nchini Uingereza na kujiondoa katika majukumu yao ya kifalme mwanzoni mwa mwaka wa 2020, na kuhamia jimbo la California mwezi Machi mwaka huo.
Tangu wakati huo, uhusiano wao na familia ya kifalme ya Uingereza ilikuwa na misukosuko.
Hata hivyo, ziara ya Harry na Meghan ya mwezi Julai ya kumtembelea Mfalme Charles na Malkia Camilla ilionekana kuwa hatua muhimu katika kuboresha uhusiano wao.
Soma pia:
Waasi wa M23 waweka vikwazo vipya vya usafiri Mashariki mwa DRC baada ya kuenea kwa Ebola
Muungano wa waasi wa M23 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), umeanza kuingilia kati katika kukabiliana na kuenea kwa ugonjwa wa Ebola katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wake.
Kundi hilo ambalo linadhibiti baadhi ya maeneo yaliyoko Mashariki mwa DRC, imesema itakuwa inaweka vikwazo vipya vya usafiri kwa watu wanaoingia au kutoka maeneo yaliyoathiriwa na Ebola.
Baadhi ya vikwazo hivyo ni kama;
Magari ya uchukuzi aina ya teksi zinazofanya safari kati ya mji wa Goma na Kirumba zitasitishwa kwa mwezi mmoja kuanzia siku ya Jumamosi, pamoja na boti zinazobeba abiria katika baadhi ya njia kwenye Ziwa Edward zitasitishwa , kulingana na taarifa iliyotolewa na kundi hilo.
Mabasi ya abiria bado yataruhusiwa kufanya safari katika barabara ya Goma-Kirumba, lakini yatapaswa kuzingatia masharti ya afya na usalama. Malori yanayosafirisha mizigo pia yataruhusiwa kuendelea na safari.
Hatua hiyo mpya imechukuliwa baada ya wasafiri wawili kutoka mji wa Lubero unaodhibitiwa na serikali kupatikana na Ebola katika kijiji kilicho chini ya udhibiti wa kundi la M23, hii ni kulingana na timu ya kukabiliana na Ebola iliyoanzishwa na waasi hao.
Kwa sasa waasi wa M23 wanadhibiti maeneo makubwa ya majimboya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini baada ya kusonga mbele mwanzoni mwa mwaka 2025 na kuteka mji wa Goma na Bukavu, miji miwili mikubwa zaidi mashariki mwa Congo.
Waasi hao wametumia mlipuko wa Ebola wa mwaka huu kuonyesha uwezo wao wa kutawala mashariki mwa Congo.
Mwishoni mwa mwezi Juni, waasi hao walitangaza maeneo yaliyo chini ya udhibiti wake kuwa hayana Ebola.
Idadi ya visa vilivyothibitishwa vya Ebola nchini Congo vimepita visa 5,000, kulingana na takwimu zilizotolewa na serikali ya DRC.
Soma pia:
Jiji la Mekelle huko Tigray lashambuliwa kwa ndege zisizo na rubani
Jeshi la Ethiopia limefanya shambulio la ndege zisizo na rubani asubuhi ya leo katika mji mkuu wa mkoa wa Tigray, Mekelle, huku kukiwa na hofu kubwa ya kuzuka tena kwa vita kati ya serikali kuu na chama cha Tigray People’s Liberation Front (TPLF).
Kwa mujibu wa chombo cha habari cha kikanda Tigray TV, shambulio hilo lilipiga eneo la makazi katika kitongoji cha Daero, na kuwajeruhi akina mama na watoto waliokuwa wakicheza karibu.
Kituo hicho kiliripoti kwamba nyumba kadhaa ziliharibiwa.
Mamlaka ya Tigray inaishtumu jeshi la taifa kwa kufanya msururu wa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani katika siku za hivi karibuni.
Mnamo Agosti 18, maafisa waliiambia BBC kwamba mashambulizi mawili karibu na Dandera, mwedo wa kilomita 15 kutoka mji mkuu wa mkoa wa Mekelle, yalisababisha kifo cha mtu mmoja na kumjeruhi mwingine.
Zaidi ya wiki moja iliyopita, mmoja aliuawa na wengine watatu kujeruhiwa katika mashambulizi ya ndege zisizo na rubani dhidi ya wilaya ya Raya-Alamata iliyopo eneo la Merewa kusini mwa Tigray.
Serikali haijatoa tamko lolote kuhusiana na mashambulizi ya hivi karibuni.
Soma zaidi:
Wanigeria 83 warejea nyumbani kwa kuhofia ghasia dhidi ya wahamiaji Afrika Kusini
Kundi la raia 83 wa Nigeria limewasili mjini Lagos usiku wa Jumatano, huku kukiwa na wasiwasi unaoongezeka vurugu dhidi ya wahamiaji nchini Afrika Kusini.
Watu hao walirejea nyumbani wakiandamana na maafisa wawili wa Ubalozi wa Nigeria jijini Johannesburg.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria imrsema kuwa watu binafsi waligharamia usafiri wao, ikiongeza kuwa "zoezi la kurejesha nyumbani kundi hili la watu liliweezeshwa na wahisani wenye nia njema, ambao msaada wao uliwawezesha kuwarejesha salama nchini Nigeria."
Mpango wa serikali wa kurejesha watu kwa hiari ulimalizika rasmi mwezi Julai.
Waigeria 1,500 walirejeshwa nyumbani chini ya mpango huo.
Serikali ilisema safari hizo ziligharamiwa kwa fedha za umma na kwamba watu hao hawakulazimika kulipia safari zao.
Wanigeria wengine 66 walirejea mwezi Juni kwa safari tofauti ya ndege iliyoandaliwa na kugharamiwa na watu binafsi, kulingana na Wizara ya Mambo ya Nje.
Waliowasili hivi karibuni walipokelewa na Balozi Haruna Ali-Gombe, Mkurugenzi wa Idara ya Masuala ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria.
Kisha walikabidhiwa kwa taasisi husika za serikali kwa ajili ya taratibu za nyaraka na utambuzi kabla ya kuunganishwa tena na familia zao.
Kurejea kwao kunakuja wakati Afrika Kusini inakabiliwa na maandamano mapya dhidi ya wahamiaji wasio na vibali halali.
Baadhi ya makundi yametoa wito kwa wageni wasio na hadhi ya kisheria kuondoka nchini humo na yametoa makataa ya hadi Septemba 30 kwa wahamiaji wasio na vibali kuondoka.
Afrika Kusini imeshuhudia maandamano kadhaa kuhusu uhamiaji mwaka huu, huku waandamanaji wakitaka kuwepo kwa udhibiti mkali zaidi.
Serikali imelaani mashambulizi dhidi ya wahamiaji na kusema inaongeza juhudi za kutekeleza sheria za uhamiaji na kushughulikia uhamiaji usiofuata taratibu.
Mamlaka za Afrika Kusini zinasema zaidi ya wahamiaji 80,000 wasio na vibali wamefurushwa nchini humo kama sehemu ya kampeni pana ya utekelezaji wa sheria.
Serikali inasema itaendelea kuimarisha usalama wa mipakani na kutekeleza sheria za uhamiaji.
Maelzo zaidi:
Watu 13 wauawa Kyiv huku Ukraine ikikabiliwa na uhaba wa mifumo ya ulinzi wa anga
Takriban watu 13 wameuawa na wengine 34 kujeruhiwa katika mashambulizi ya hivipunde ya Urusi yaliyolenga mji mkuu wa Ukraine, huku Kyiv ikiendelea kukabiliwa na uhaba wa makombora ya ulinzi wa anga.
Majengo ya makazi na maghala yalishambuliwa sehemu mbalimbali za jiji hilo usiku kucha, kulingana na Huduma ya Dharura ya Serikali ya Ukraine (DSNS), huku hospitali ya watoto na shule pia zikiharibiwa.
Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema kuwa ilitumia silaha za angani, nchi kavu na baharini kupiga vituo vya kijeshi na maghala, na kuongeza kuwa ndege zisizo na rubani 726 za Ukraine zilidunguliwa.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema vifo hivyo vilitokana na uhaba wa makombora ya ulinzi wa anga, ambayo Kyiv hutegemea kupewa na washirika wake wa Magharibi.
Akiandika kwenye mtandao wa Telegram, alisema "madamu Ukraine haina makombora ya kutosha ya kuzuia makombora ya balistiki, Urusi haitafikiria kwa uzito kuhusu amani".
Mashambulizi hayo dhidi ya Kyiv yalianza majira ya saa sita usiku kwa saa za ndani huku ving'ora vya tahadhari ya mashambulizi ya anga vikilia jijini kote, yakifuatiwa na milipuko ya takriban makombora 20 ya Urusi.
Mashambulizi hayo yalikatiza huduma za umeme katika maelfu ya majengo, na kuzitumbukiza baadhi ya sehemu za eneo la Kyiv gizani.
Serikali imetangaza Ijumaa kuwa siku ya maombolezo kwa heshima ya watu waliouawa katika mashambulizi hayo.
Deni la taifa la Marekani lavuka dola trilioni 40
Takwimu kutoka Wizara ya Fedha ya Marekani zinaonyesha kuwa deni la taifa la Marekani limeongezeka maradufu ndani ya muongo mmoja, na kufikia dola trilioni 40.
Ongezeko hilo linatokana na miaka kadhaa ya matumizi makubwa chini ya uongozi wa marais Donald Trump na Joe Biden, pamoja na kupanda kwa viwango vya riba ambavyo vimeendelea kuongeza jumla ya deni hilo.
Mnamo mwaka wa 2016, deni la taifa la Marekani lilikuwa chini ya dola trilioni 20.
Ofisi ya Bajeti ya Bunge ilikuwa imekadiria kuwa jumla ya deni hilo ingefikia dola trilioni 39.6 kufikia mwisho wa mwaka wa fedha wa 2026.
Ongezeko hilo la kasi kuliko ilivyotarajiwa limezua wasiwasi kuhusu kasi ya ongezeko la mahitaji ya serikali ya Marekani ya kukopa fedha na athari zake kwa ongezeko la viwango vya riba hapo baadaye.
Ofisi ya Bajeti ya Bunge inasema kuwa Marekani inakaribia dola trilioni 1.41 na inatarajiwa kufikia takriban dola trilioni 64 kufikia mwaka wa 2036.
Wakati serikali ya Marekani ikitumia fedha zaidi kuziba pengo la bajeti yake, walaji wamejikuta wakikabiliwa na viwango vya juu vya riba na mfumuko wa bei.
Soma zaidi:
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Tanzania adaiwa 'kutaka kuchoma majengo ya polisi'
Wakili wa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Melkisedeki Kitunzi Kaijage anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi anasema mteja wake sasa anatuhumiwa kwamba alikuwa na nia ya kuchoma majengo ya umma pamoja na makazi ya askari Polisi katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania, ikiwemo Zanzibar.
Akizungumza Agosti 19, 2026 jijini Dodoma, baada ya kesi dhidi ya mhadhiri huyo kuahirishwa, wakili Godfrey Wasonga alisema “Si majengo ya umma tu, pia anatuhumiwa kwamba anataka kuchoma makazi ya askari Polisi Tanzania nzima ikiwepo na Zanzibar”.
Bw. Wesonga amesema tuhuma hizo zinahusisha majengo mbalimbali ya umma, ikiwemo shule, zahanati, mahakama na majengo mengine ya Serikali, huku akieleza kuwa suala hilo liko chini ya vifungu vya sheria ya kuzuia ugaidi.Wakili Wasonga amesema hatua inayofuata katika kesi hiyo ni uchunguzi wa awali, ambao unalenga kuwezesha shauri hilo kuwasilishwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikilizwa.
Hata hivyo, kikao cha kesi hiyo kilichopangwa kufanyika Agosti 19 kiliahirishwa kwa sababu Hakimu Mkazi anayesikiliza shauri hilo, Zabibu Mpangule, hakuwepo.
Kwa mujibu wa Wasonga, shauri hilo lilitajwa mbele ya Hakimu Kombe na sasa limepangwa kutajwa tena Agosti 27, 2026, ambapo pande zote zinatarajiwa kufahamisha mahakama hatua inayofuata.
Wakili huyo amesema siku hiyo itatoa mwelekeo wa namna shauri hilo litakavyoendelea.
Pia unaweza kusoma:
Israel yatangaza zabuni ya mradi 'tata' wa makazi katika Ukingo wa Magharibi
Israel imetangaza zabuni ya kujenga takriban nyumba 1,200 kwa ajili ya walowezi katika eneo lenye umuhimu wa kimkakati katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, huku ikijaribu kuondoa kabisa uwezekano wa kuwepo kwa taifa la Palestina.
Mipango ya ujenzi katika eneo linalojulikana kama "E1" huko Jerusalem Mashariki imekuwa ikikosolewa vikali na jumuiya ya kimataifa kwa muda mrefu, na makazi hayo yanachukuliwa kuwa haramu kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
Kupitia mpango huu, Ukingo wa Magharibi utagawanywa katika sehemu mbili, na Jerusalem Mashariki itatenganishwa na maeneo mengine.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Ed Miliband, alikemea kutangazwa kwa zabuni hiyo akiitaja kuwa "kitendo kisichokubalika na kilicho na madhara" na kuitaka Israel "kusitisha mara moja mipango ya E1, kuondoa zabuni hiyo na kukomesha upanuzi wa makazi ya walowezi."
Tangu Israel ilipokalia kwa mabavu Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki wakati wa Vita vya Mashariki ya Kati vya mwaka 1967, imejenga takriban makazi 160, ambayo ni makazi ya Wayahudi wapatao 700,000.
Wapalestina wanataka maeneo haya, pamoja na Ukanda wa Gaza, kwa ajili ya taifa lao la baadaye.
Hivi sasa, takriban Wapalestina milioni 3.3 wanaishi sambamba na walowezi hao.
Licha ya upinzani mkali kutoka kwa jumuiya ya kimataifa, serikali mfululizo za Israel zimeendelea kuruhusu upanuzi wa makazi hayo.
Maelezo zaidi:
Mkuu wa Ujasusi Ecuador, Wamarekani 5 wafariki ajali ya helikopta Kenya
Serikali ya Ecuador imesema mkuu wake wa Idara ya Ujasusi na mke wake wamefariki dunia katika ajali ya helikopta iliyoanguka jana Jumatano katika kaunti ya Samburu nchini Kenya.
Raia watano wa Marekani pia walifariki dunia katika ajali hiyo, Msemaji wa Idara ya Mambo ya Nje ya Marekani alisema.
Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Kenya (KCAA) ilisema kuwa helikopta hiyo ilikuwa katika safari ya kutalii mandhari ikitoka kwenye hifadhi ya wanyamapori ya Loisaba kuelekea Ewaso Nyiro, mto unaopita kando ya hifadhi kadhaa za taifa.
Kaunti ya Samburu ni mojawapo ya maeneo maarufu ya utalii nchini Kenya, ikiwa na hifadhi nyingi za wanyamapori zinazomilikiwa na sekta binafsi, na inajulikana kwa mandhari yake ya kuvutia na ya kipekee.
Picha kutoka eneo la tukio zinaonesha moshi ukifuka katika eneo lenye miti ambapo helikopta hiyo ilianguka kwenye Mlima Ololokwe, huku wahudumu wa Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya wakikaribia mabaki ya helikopta ambayo bado yalikuwa yakiteketea kwa moto.
Ecuador haijatoa maelezo kuhusu kifo cha Sensi-Contugi, mwenye umri wa miaka 44, ambaye aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Ujasusi wa Kimkakati mwaka 2024.
Jeshi la Israel lakiri kumuua msichana wa Kipalestina
Jeshi la Israel limethibitisha kwa mara ya kwanza kuwa wanajeshi wake walilifyatulia risasi gari alimokuwa Hind Rajab,msichana wa Kipalestina wa umri wa miaka mitano aliyeuawa pamoja na jamaa zake sita wakisafiri Gaza mnamo mwaka 2024.
Gari la wagonjwa lililotumwa kumfikia—katika hatua iliyoratibiwa na jeshi la Israel—lilishambuliwa kwa makombora, na kusababisha vifo vya wahudumu wawili wa afya.
Mwili wa Hind ulipatikana siku kadhaa baadaye, pamoja na miili ya watu wengine waliouawa.
Katika taarifa, Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limesema linaanzisha uchunguzi kuhusu vifo hivyo pamoja na mauaji ya wahudumu wawili wa afya waliotumwa kuokoa maisha ya Hind.
Uchunguzi pia utaanzishwa kuhusu mauaji ya maafisa 15 wa kutoa misaada ya dharura waliouawa na wanajeshi wa Israel mjini Rafah mwaka jana.
Matukio yote mawili yalilaaniwa kimataifa.
Awali, Jeshi la Israel (IDF) lilisema kuwa hakuna hata mmoja wa askari wake aliyekuwa katika eneo hilo wakati Hind alipouawa. Hata hivyo, kauli hiyo ilianza kutiliwa shaka.
Baadaye, IDF ilisema kuwa ilikuwa "imefanya operesheni dhidi ya maeneo yanayotumiwa na magaidi" kwa kutumia vikosi vilivyokuwa vikifanya kazi katika vitongoji vya Jiji la Gaza, ikiwemo Tel al-Hawa, ambapo Hind alikuwepo.
Trump atangaza kuiwekea Iran vikwazo vikali vya kiuchumi
Rais wa Marekani Donald Trump amesema anaanzisha vikwazo vipya vya kiuchumi dhidi ya Iran na nchi yoyote ile itakayoisaidia au kufanya biashara nayo.
Kupitia mtandao wake wa kijamii wa Truth Social,Bwana Trump amesema anachukua hatua hiyo kwasababu Iran imeshindwa kufikia makubaliano na Marekani.
Rais Trump ambaye mara kwa mara ametishia kuichukulia hatua kali zaidi Iran kwa kutoridhia kufikia makubaliano ya kuumaliza mzozo wa Mashariki ya Kati amesema leo anatangaza operesheni kali zaidi ya kiuchumi kuwahi kuchukuliwa dhidi ya nchi yoyote ile na itakuwa vita vya kiuchumi na kubaguliwa kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa.
Aidha ametangaza kuwa nchi yoyote itakayoruhusu asasi zake za kifedha,biashara,viwanja vya ndege au asasi zake za kiserikali kuisadia kivyovyote vile Iran nayo itaathirika vibaya kiuchumi.
Hata hivyo,hajatoa maelezo zaidi kuhusu hatua hizo mpya dhidi ya Iran au kutaja ni nchi zipi nyingine zitakazolengwa na vikwazo hivyo vipya.
Kauli ya Trump inakuja wiki moja baada ya waziri wake wa fedha Scott Bessent kusema Marekani itaiwekea vikwazo vya kiuchumi Iran kwa viwango ambavyo havijashuhudiwa katika kipindi cha nyuma.
Makubaliano ya kusitisha vita vya Iran kwa siku sitini yalikamalika Jumatatu wiki hii huku kukiwa hakuna dalili za kukomeshwa kwa mzozo huo wa Mashariki ya Kati.
Shinikizo hilo jipya la kuulenga zaidi uchumi wa Iran linakuja wakati vita vya Iran vikielekea kutimiza miezi sita bila ya juhudi zozote madhubuti za kidiplomasia wala kijeshi.
Rais Trump aliyevianzisha vita hivyo mwishoni mwa mwezi Februari pamoja na Israel, anamulikwa darubini kali kisiasa nchini mwake wakati nchi hiyo ikijiandaa kwa uchaguzi wa katikati mwa muhula unaotarajiwa mwezi Novemba.
Mshirika wake katika vita hivyo vya Iran,Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu naye anakabiliwa na shinikizo la kisiasa kuhusu anavyoshughulikia mzozo wa Iran na wa Gaza kuelekea uchaguzi mkuu wa Israel unaotarajiwa mwezi Oktoba mwaka huu.
Licha ya mashambulizi ya makombora kupungua katika siku za hivi karibuni kati ya Iran na Marekani,Iran imeendelea kuzuia meli kupita katika Mlango Bahari wa Hormuz licha ya shinikizo kali kutoka kwa Marekani kutaka njia hiyo muhimu ya safari za meli za mizigo baharini kufunguliwa.
Soma zaidi:
Karibu kwa matangazo ya moja kwa moja leo Alhamisi 20.08.2026.