Waasi wa M23 waweka vikwazo vipya vya usafiri Mashariki mwa DRC baada ya kuenea kwa Ebola

Chanzo cha picha, Getty Images
Muungano wa waasi wa M23 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), umeanza kuingilia kati katika kukabiliana na kuenea kwa ugonjwa wa Ebola katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wake.
Kundi hilo ambalo linadhibiti baadhi ya maeneo yaliyoko Mashariki mwa DRC, imesema itakuwa inaweka vikwazo vipya vya usafiri kwa watu wanaoingia au kutoka maeneo yaliyoathiriwa na Ebola.
Baadhi ya vikwazo hivyo ni kama;
Magari ya uchukuzi aina ya teksi zinazofanya safari kati ya mji wa Goma na Kirumba zitasitishwa kwa mwezi mmoja kuanzia siku ya Jumamosi, pamoja na boti zinazobeba abiria katika baadhi ya njia kwenye Ziwa Edward zitasitishwa , kulingana na taarifa iliyotolewa na kundi hilo.
Mabasi ya abiria bado yataruhusiwa kufanya safari katika barabara ya Goma-Kirumba, lakini yatapaswa kuzingatia masharti ya afya na usalama. Malori yanayosafirisha mizigo pia yataruhusiwa kuendelea na safari.
Hatua hiyo mpya imechukuliwa baada ya wasafiri wawili kutoka mji wa Lubero unaodhibitiwa na serikali kupatikana na Ebola katika kijiji kilicho chini ya udhibiti wa kundi la M23, hii ni kulingana na timu ya kukabiliana na Ebola iliyoanzishwa na waasi hao.
Kwa sasa waasi wa M23 wanadhibiti maeneo makubwa ya majimboya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini baada ya kusonga mbele mwanzoni mwa mwaka 2025 na kuteka mji wa Goma na Bukavu, miji miwili mikubwa zaidi mashariki mwa Congo.
Waasi hao wametumia mlipuko wa Ebola wa mwaka huu kuonyesha uwezo wao wa kutawala mashariki mwa Congo.
Mwishoni mwa mwezi Juni, waasi hao walitangaza maeneo yaliyo chini ya udhibiti wake kuwa hayana Ebola.
Idadi ya visa vilivyothibitishwa vya Ebola nchini Congo vimepita visa 5,000, kulingana na takwimu zilizotolewa na serikali ya DRC.
Soma pia:































