Lebanon yasema usitishaji mapigano lazima uzingatiwe kabla ya mazungumzo na Israel

Hili limewadia huku Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akisema serikali yake inaanza mazungumzo ya moja kwa moja na Lebanon.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma & Ambia Hirsi

  1. Mashirika ya ndege Ulaya yaonya uhaba wa mafuta Mlango wa Bahari wa Hormuz usipofunguliwa

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Ulaya huenda ikakabiliwa na uhaba wa mafuta ya ndege ikiwa Mlango wa Bahari wa Hormuz hautafunguliwa katika kipindi cha wiki tatu zijazo, kulingana na shirika la biashara la viwanja vya ndege vya Ulaya.

    ACI Ulaya imewaandikia Makamishna wa Uropa wa nishati na utalii, ikionya juu ya "kuongezeka kwa wasiwasi" kati ya wanachama wake kuhusu upatikanaji wa mafuta ya ndege.

    "Kupungua kwa usambazaji kunaweza kutatiza sana shughuli za usafiri wa anga - na hii itasababisha athari mbaya za kiuchumi kwa jamii zilizoathirika, na kwa bara Ulaya," mkurugenzi mkuu wa ACI Barani Ulaya aliandika.

    "Katika hatua hii, tunaelewa kwamba ikiwa njia ya kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz haitafunguliwa ndani ya wiki tatu zijazo, Umoja wAa Ulaya utakumbwa na uhaba wa mafuta."

    Nchi za Ghuba ni chanzo kikuu cha mafuta ya ndege, zikisafirisha takriban 50% ya bidhaa zinazoagizwa kutoka Ulaya.

    Mashirika kadhaa ya ndege tayari yamepunguza safari za ndege na kuongeza gharama za usafiri kwa abiria kutokana na wasiwasi kuhusu uhaba wa mafuta.

    Wiki iliyopita, bei ya mafuta ya ndege ya Ulaya ilifikia kiwango cha juu kabisa cha dola 1,838 za Kimarekani kwa tani, ikilinganishwa na dola 831 kabla ya vita kuanza.

    Soma zaidi:

  2. Kiongozi wa upinzani wa Taiwan akutana na Xi Jinping mjini Beijing

    .

    Chanzo cha picha, CTI

    Rais Xi Jinping wa China amempokea kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Taiwan leo Ijumaa, katika mkutano nadra ambao ulishuhudia pande zote mbili zikitilia mkazo hamu ya kufikiwa kwa amani kati ya pande hizo mbili.

    Cheng Li-wun ndiye kiongozi wa kwanza wa Kuomintang (KMT) kuzuru China katika muongo mmoja.

    Mnamo mwaka wa 2016, Beijing ilikata mawasiliano ya ngazi ya juu na Taiwan baada ya Tsai Ing-wen wa chama tawala cha Democratic Progressive Party (DPP) kuwa rais, akitaja kukataa kwake kuidhinisha dhana ya taifa moja la China.

    DPP ni miongoni mwa walioikosoa safari ya Cheng, wakimtuhumu kuwa "mtiifu" kwa Beijing.

    Beijing inadai Taiwan kama sehemu ya eneo lake na haijakataza kuchukua kisiwa hicho kinachojitawala kwa nguvu.

    "Viongozi wa vyama vyetu viwili wanakutana leo ili kulinda amani na utulivu wa nchi yetu ya pamoja, kuhimiza maendeleo ya amani ya uhusiano kati ya pande hizo mbili, na kuruhusu vizazi vijavyo kushiriki katika mustakabali mzuri na mzuri," Xi alisema katika mkutano kwenye Ukumbi Mkuu wa Watu wa China siku ya Ijumaa.

    Aliongeza kuwa China iko tayari kuimarisha kubadilishana na mazungumzo pamoja na pande mbalimbali, ikiwa ni pamoja na KMT - ingawa itabidi iwe kwa masharti ya kupinga uhuru wa Taiwan.

    Xi pia alisisitiza kwamba wale wa pande zote mbili za Strait ya Taiwan ni Wachina, na kwamba wote wanataka amani.

    Akijibu, Cheng alisema "kufufuliwa kwa watu wa China ni matarajio ya pamoja ya watu wa pande zote za Mlango wa Bahari".

    Pia unaweza kusoma:

  3. Habari za hivi punde, Lebanon itashiriki katika mazungumzo na Israel mapigano yakisitishwa

    Moshi kutoka kwa mashambulizi ya anga ya Israel umetanda angani katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut.

    Chanzo cha picha, Dylan COLLINS / AFP via Getty Images

    Maelezo ya picha, Moshi kutoka kwa mashambulizi ya anga ya Israel umetanda angani katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut.

    Afisa mkuu katika ofisi ya rais wa Lebanon muda mfupi uliopita ameithibitishia BBC kwamba Lebanon itashiriki katika mazungumzo ya moja kwa moja na Israel wiki ijayo vita vitakapositishwa.

    Siku na saa ya mkutano huo haijawekwa wazi.

    Mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Lebanon na Israel hayajawahi kufanyika, lakini tamko hilo si la kawaida.

    Nchi hizo mbili zimekuwa zikiwasiliana kupitia wapatanishi, kama vile Marekani.

    Juhudi za kuanzisha mazungumzo zimekuwa zikiendelea tangu makubaliano ya kusitisha mapigano mnamo Novemba 2024, na wajumbe wa Marekani hapo awali walisimamia mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya pande hizo mbili.

    Huku hayo yakijiri kundi la kisiasa na kijeshi la Waislamu wa madhehebu ya Shia, lenye makao yake makuu nchini Lebanon, linasema kuwa linalenga mji wa kaskazini mwa Israel kujibu kile inachoeleza kama "ukiukaji" wa Israel wa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Marekani na Iran.

    Hezbollah inasema ilirusha makombora huko Kiryat Shmona, karibu na mpaka wa Israel-Lebanon, saa 10:00 kwa saa za huko siku ya Ijumaa (06:00 BST) na Misgav Am katika eneo la Galilee kaskazini mwa Israel.

    "Shambulio hili litaendelea hadi uchokozi wa Israel na Marekani dhidi ya nchi yetu na watu wetu ukome," inasema katika taarifa hiyo.

    Maelezo zaidi:

  4. Msanii maarufu wa Tanzania Matonya ashtakiwa kwa unyanyasaji Kenya

    Matonya

    Chanzo cha picha, JAMBOMAIL

    Msanii wa Tanzania, Sefu Shabani, kwa jina maarufu Matonya, amekamatwa na kufunguliwa mashtaka katika nchi jirani ya Kenya kwa tuhuma za unyanyasaji wa kijinsia, na hivyo kuzua hisia tofauti nchini Tanzania.

    Msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 alifikishwa mahakamani mjini Mombasa pwani ya Kenya siku ya Alhamisi ambapo alikanusha shtaka la kumnyanyasa mwanamke kingono.

    Waendesha mashtaka waliambia mahakama kisa hicho kinachodaiwa kilitokea Jumanne (Aprili 7) katika eneo la Nyali, Kaunti ya Mombasa.

    Alikamatwa muda mfupi baadaye. Upande wa mashtaka uliitaka mahakama kuweka masharti magumu ya dhamana, ukisema kuwa mwanamuziki huyo ni raia wa kigeni asiye na makazi maalum nchini Kenya na anaweza kutoroka

    Mahakama ilimpa dhamana ya shilingi 500,000 za Kenya (kama dola 3,800), na kumuamuru akabidhi hati yake ya kusafiria ya Tanzania, na kumzuia kuondoka nchini bila idhini ya mahakama.

    Mamlaka nchini Tanzania haijatoa tamko lolote kuhusiana na kesi hiyo.

    Kesi dhidi ya Matonya imeibua hisia mseto mtandaoni baadhi ya watu wakimtetea na wengine wakilaani vitendo anavyodaiwa kufanya.

    Matonya alipata umaarufu mwishoni mwa miaka ya 2000 kwa nyimbo nyingi zilizovuma kote Afrika Mashariki, zikiwemo Vaileti, Anita, Siamini, Taxi bubu na Mapito, ilizoimba kwa mtindo wa kimapenzi akisimulia hadithi.

    Yeye sio msanii wa kwanza wa Kitanzania kukabiliwa na masuala ya kisheria nchini Kenya.

    Mnamo 2022, polisi katika mji mkuu wa Kenya Nairobi walimkamata Rajabu Abdul, anayejulikana zaidi kama Harmonize, kwa madai ya kukiuka mkataba wa kutumbuiza katika maonyesho yaliyopangwa katika vilabu kadhaa. Suala hilo lilitatuliwa baadaye.

  5. Marekani yasitisha huduma ya viza Abuja baada ya kuwaagiza wafanyakazi wake kuondoka Nigeria

    .

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Marekani imesitisha shughuli za utoaji viza katika ubalozi wake katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja, kutokana na hofu ya usalama.

    Katika ilani iliyotolewa Alhamisi, Ubalozi wa Marekani ulisema miadi ya viza mjini Abuja imeahirishwa hadi notisi nyingine itakapotolewa, na kuwashauri wale walioathiriwa kuangalia barua pepe zao kwa taarifa juu ya tarehe zilizopangwa upya.

    Hatua hiyo inafuatia uamuzi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kuidhinisha kuondoka kwa wafanyakazi wasio wa lazima na familia katika Ubalozi wa Abuja, kutokana na kile ilichokitaja kuwa kuzorota kwa hali ya usalama katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.

    Kando na kufungwa kwa ubalozi huo, Washington iliwatahadharisha raia wake dhidi ya kusafiri kwenda Nigeria, ikiororedhesha majimbo kadhaa hadi (Ngazi ya 4) "Usisafiri."

    Ushauri huo ulitaja hatari zinazohusishwa na ugaidi, utekaji nyara na uhalifu uliopitiliza

    Serikali ya Nigeria imekosoa hatua hiyo ya Marekani, na kuelezea ushauri wa usafiri kama "usio na usawa" na usiozingatia hali halisi iliyopo nchini.

    Maafisa wamesema kwamba tathmini pana za usalama zinaweza kuharibu taswira ya Nigeria na kuibua hofu miongoni mwa raia wa kigeni na raia wa nchi hiyo pia.

    Serikali inasisitiza kuwa imepiga hatua kubwa kukabiliana na changamoto za kiusalama na inasema bado inashirikiana na washirika wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na Marekani, katika kukabiliana na ugaidi na kuzuia uhalifu.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Urusi na Ukraine zakubaliana kusitisha mapigano kipindi cha Pasaka ya Orthodox

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Urusi na Ukraine zimekubaliana kusitisha mapigano kwa ajili ya Pasaka ya Orthodox, huku Vladimir Putin akisema amewaamuru wanajeshi wa Urusi kusitisha mapigano "pande zote" wikendi hii.

    Tamko hilo kutoka Moscow limetolewa baada ya Volodymyr Zelensky kutoa wito mara kwa mara wa kusitisha mapigano, yote yakipuuzwa na Kremlin.

    Sasa Putin ametangaza kusitisha mapigano kuanzia saa 16:00 kwa saa za eneo (saa 14:00 BST) Jumamosi tarehe 11 Aprili hadi Jumapili ya Pasaka, akiongeza kwamba alitarajia Ukraine "kufuata mfano" wa Urusi.

    Aliamuru vikosi vyake viwe tayari kuingilia kati "vitendo vyovyote vya uchokozi vinavyoweza kutokea upande wa adui".

    Zelensky alichapisha ujumbe hivi karibuni kwenye mtandao wa X kwamba Ukraine ilikuwa "tayari kwa hatua zenye kulingana".

    "Watu wanahitaji kusherehekea Pasaka bila vitisho na uhalisia wa kuelekea amani," aliandika. "Urusi ina nafasi ya kutorudi kwenye mashambulizi baada ya Pasaka pia."

    Mapema wiki hii, Zelensky alisema alikuwa ameiomba Marekani kupitisha pendekezo la makubaliano ya kusitisha mapigano ya wikendi ya likizo, kama hatua ya kwanza.

    Soma zaidi:

  7. Uingereza yasema vita vya Iran vinaonyesha lazima ichukue mwelekeo mpya

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waziri Mkuu Keir Starmer siku ya Alhamisi alisema vita vya Iran lazima viwe hatua muhimu kwa Uingereza baada ya miongo miwili ya migogoro, na kuahidi kuimarisha uchumi na jeshi la nchi hiyo ili kukabiliana na ulimwengu "tete na hatari zaidi".

    Siku ya Jumanne, Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza kusitisha mapigano katika mzozo wa Iran kwa wiki mbili, lakini bado hakuna dalili ya Iran kuondoa kizuizi chake kabisa karibu na Mlango-Bahari wa Hormuz, ambako kumesababisha msukosuko mbaya zaidi wa usambazaji wa mafuta katika historia ya dunia.

    Starmer alisema mgogoro huo, ambao tayari umeongeza bei ya mafuta nchini Uingereza na unatarajiwa kusababisha mfumuko wa bei zaidi na matatizo ya kiuchumi, unapaswa kuwa "mstari wa ukomo" kwa nchi.

    "Uingereza imekumbwa na migogoro kwa karibu miongo miwili sasa," aliandika katika gazeti la Guardian, akinukuu kuanguka kwa uchumi duniani mwaka 2008 na kubana matumizi kulikofuata, Brexit, janga la COVID na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

    "Vita nchini Iran sasa lazima viwe mstari wa ukomo, kwa sababu jinsi tutakavyotoka katika mgogoro huu vitatutambulisha sote kwa kizazi kijacho. Na badala ya kurudi katika ulimwengu wa 2008, tutatengeneza njia mpya kwa Uingereza - njia ambayo itaimarisha nishati yetu, ulinzi wetu na usalama wetu wa kiuchumi katika enzi mpya.

    Soma zaidi:

  8. Melania Trump akanusha kuwa na uhusiano na Jeffrey Epstein

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mke wa Rais Melania Trump amekanusha kuwa na uhusiano na Jeffrey Epstein, akiwaambia waandishi wa habari katika Ikulu ya White House kwamba madai yoyote yanayowaunganisha wawili hao "yanahitaji kumalizika haraka".

    Katika tangazo la kushtukiza siku ya Alhamisi, mke wa rais alitoa wito wa vikao vya bunge kwa ajili ya manusura wa biashara haramu ya ngono iliyoendeshwa na Epstein.

    Pia alikanusha uvumi mtandaoni kwamba Epstein alimtambulisha kwa Donald Trump, akiuita "majaribio ya kikatili ya kunichafulia sifa".

    Haijulikani ni nini kilisababisha atoe tangazo hilo.

    Hakukuwa na dalili yoyote kutoka ofisini kwake kwamba atatoa taarifa kuhusu Epstein, na Ikulu ya White House haikushirikisha mada hiyo mapema.

    Alisema hakuwa mwathirika wa Epstein, ambaye "alikutana naye" kwa muda mfupi tu mwaka wa 2000.

    "Sijawahi kuwa na ufahamu wowote kuhusu unyanyasaji wa Epstein dhidi ya waathiriwa wake," alisema. "Sijawahi kushiriki katika nafasi yoyote. Sikuwa mshiriki."

    Pia alikana kumjua Ghislaine Maxwell, mshirika wa Epstein aliyefungwa jela.

    Soma zaidi:

  9. Trump ataka ahadi ya kusaidiwa suala la Hormuz - Katibu Mkuu wa NATO

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Katibu Mkuu wa NATO, Mark Rutte, amearifu baadhi ya wanachana kwamba Rais wa Marekani Donald Trump anataka ahadi thabiti ndani ya siku chache zijazo za kusaidia kuhakikisha Mlango-Bahari wa Hormuz unafunguliwa, wanadiplomasia wawili wa Ulaya waliambia Reuters siku ya Alhamisi.

    Rutte alikutana na Trump mjini Washington siku ya Jumatano, huku kukiwa na mvutano ndani ya muungano kuhusu vita vya Iran.

    “Tulibaini kuwa hali haiko sawa huko Washington, lakini hawakuwasiliana na washirika kabla au baada ya kuanza kwa vita hivi,” alisema mmoja wa wanadiplomasia.

    “NATO haitaingilia vita dhidi ya Iran, lakini washirika wanataka kusaidia katika kutafuta suluhu za muda mrefu kwa njia ya Hormuz. Kwa mazungumzo yanayoendelea na Iran, hii inaweza kusaidia,” mwanadiplomasia huyo alisema.

    Rais wa Marekani amerudia kusema NATO ni kama “kisu butu” na kutishia kujiondoa katika muungano huo wa nchi za Atlantic wenye wanachama 32 katika wiki za hivi karibuni, akisema kwamba washirika wa Washington wa Ulaya wametegemea dhamana za usalama za Marekani huku wakitoa usaidizi usiotosha kwa viya vya Marekani na Israel nchini Iran.

    Ingawa Trump alisema siku ya Jumanne kwamba mashambulizi dhidi ya Iran yatasitishwa chini ya makubaliano ya wiki mbili, athari mbaya kutokana na mzozo huo imeendelea kuathiri uhusiano wa pande mbili.

    Trump alichapisha kwenye mtandao wa Truth Social kwamba “NATO haikuwepo wakati tulipowahitaji, na hawatakuwepo ikiwa tutawahitaji tena.

    Rutte, ambaye amekabiliwa na ukosoaji kwa kumsifu kiongozi huyo wa Marekani mara kwa mara, alisema katika mahojiano na CNN baada ya mkutano wa Jumatano kwamba Trump “amekatishwa tamaa na washirika wengi wa NATO, na ninaona hoja yake”.

    Soma

  10. Iran inavyoshughulikia Hormuz 'sio makubaliano tuliyo nayo' – Trump

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani Donald Trump ameishutumu Iran kwa "kushughulikia vibaya" meli za mafuta zinazopita kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz, akisema "sio makubaliano tuliyo nayo".

    Maoni hayo yanaonyesha udhaifu wa makubaliano ya kusitisha mapigano, huku ripoti zikionyesha migongano kuhusu kile kilichojumuishwa katika makubaliano hayo.

    Hili limewadia huku Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akisema serikali yake inaanza mazungumzo ya moja kwa moja na Lebanon, ikizingatia Hezbollah kuweka chini silaha zao, kundi la wanamgambo linaloungwa mkono na Iran, na kuanzisha uhusiano wa amani.

    Afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani alithibitisha kuwa ataandaa mkutano wiki ijayo huko Washington "kujadili mazungumzo yanayoendelea ya kusitisha mapigano na Israel na Lebanon".

    Maafisa wa Lebanon walikuwa wameomba kusitisha mapigano kabla ya mazungumzo kuanza, lakini Netanyahu alisema katika hotuba iliyofuata kwa wakazi wa kaskazini mwa Israeli: "Hakuna kusitisha mapigano nchini Lebanon."

    Baada ya mashambulizi ya Israeli kuendelea huko Lebanon Alhamisi nzima - yakilenga kile ilichokielezea kama maeneo ya kurusha roketi za Hezbollah upande wa kusini - mashambulizi yalionekana kupungua kwa muda usiku kucha katika eneo hilo.

    Trump alisema katika mahojiano kwamba Israeli "itapunguza" mashambulizi yake Lebanon ili kuunga mkono mazungumzo ya amani.

    Soma zaidi:

  11. Hujambo msomaji wetu. Karibu katika matangazo ya moja kwa moja ya tarehe 10/04/2026.