Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Marekani yasema Mlango Bahari wa Hormuz uko wazi huku ikiendelea kushambuliana na Iran
Mapigano, ambayo yalichacha tena wiki hii, yaliendelea siku ya Jumamosi baada ya Marekani kusema kuwa ilishambulia zaidi ya maeneo 140 nchini Iran.
Muhtasari
- Marekani yasema Mlango Bahari wa Hormuz uko wazi huku ikiendelea kushambuliana na Iran
- Zuchu atangaza 'kuvunjika kwa penzi lake na Diamond'
- Aliyekuwa Amir wa Qatar, Sheikh Hamad bin Khalifa Al Thani, amefariki dunia
- Watu wakimbilia usalama wao huku Urusi ikishambulia karibu na mgahawa Ukraine
- Iran yasema uzalishaji wa droni umeongezeka mara tatu licha ya vita
- Messi atarajiwa kuikabili England kwa mara ya kwanza
- Rooney: Messi anafanana Kidogo na Bellingham
- Raia wa Marekani agundulika na Ebola baada ya kurejea kutoka DRC
- "Labda Tuchel hajui ilivyo kucheza na wachezaji kama Haaland – Bellingham amjibu Tuchel
- Kombe la Dunia 2026: "Sijafurahishwa na Mchezaji Wetu – Kwa Kila Kitu" - Kocha wa England
- Bellingham aiongoza England kuichabanga Norway na kufuzu nusu fainali
- Kombe la Dunia 2026: Argentina yafuzu hatua ya nusu fainali baada ya kuichapa Uswisi
- Watu 16 wafariki kwa njaa Uganda
- Marekani yafanya mashambulizi mapya dhidi ya Iran
Moja kwa moja
Na Asha Juma
Marekani yasema Mlango Bahari wa Hormuz uko wazi huku ikiendelea kushambuliana na Iran
Marekani imesisitiza kuwa Mlango Bahari wa Hormuz uko wazi, licha ya Iran kutangaza kuwa imeufunga kufuatia kuongezeka tena kwa mashambulizi.
Mapigano, ambayo yalichacha tena wiki hii, yaliendelea Jumamosi baada ya Marekani kusema kuwa ilishambulia zaidi ya maeneo 140 nchini Iran.
Marekani ilisema mashambulizi hayo yalijibu vikosi vya Iran kushambulia meli iliyokuwa ikipita katika Mlango wa Hormuz, ikidai kuwa meli hiyo ilitumia njia ambayo haikuwa imeidhinishwa.
Iran imekuwa ikijaribu kuimarisha udhibiti wake wa njia hiyo muhimu ya baharini, na mapema Jumapili ilitangaza kuwa Mlango wa Hormuz umefungwa hadi itakapotolewa taarifa nyingine.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) pia lilianzisha mashambulizi makubwa dhidi ya vituo vya kijeshi vya Marekani na washirika wake katika eneo hilo siku ya Jumapili, hatua iliyoashiria kuongezeka kwa kiwango cha uhasama.
IRGC ilisema ililenga kambi ya kijeshi ya Marekani nchini Jordan, huku Falme za Kiarabu (UAE), Qatar, Kuwait, Oman na Bahrain zikisema zilijibu mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani kutoka Iran.
Qatar, ambayo imekuwa mpatanishi katika mazungumzo ya kusitisha mapigano, haikuwa imeshambuliwa tangu Aprili, wakati UAE haikuwa imeshambuliwa tangu Mei.
Soma Zaidi:
Zuchu atangaza ‘kuvunjika kwa penzi lake na Diamond’
Msanii wa muziki wa Bongo Fleva Zuhura Othman maarufu kama Zuchu, ametangaza kuwa yeye na mwenza wake Naseeb Abdul anayejulikana kama Diamond Platnumz wameachana baada ya kuwa kwenye uhusiano kwa takribani miaka sita.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Zuchu ametoa ujumbe mzito akieleza kuwa ameamua kuchukua hatua hiyo bila kinyongo, akisisitiza kuwa sababu za ndani zitabakia kuwa siri yao, huku akibainisha kuwa "riziki imeisha."
Katika ujumbe huo, Zuchu amesema: "Namtakia Nasibu kila la kheri. Nimeamua maamuzi haya bila kinyongo. Kwa sasa focus ni mimi na kazi. ALHAMDULILLAH Nimejaribu nilipopaweza lakini Mungu ana mipango yake."
Ujumbe huo umewaacha mashabiki zake na maswali mengi wakihoji iwapo anamaanisha alichoandika au pengine ilikuwa ‘kiki’.
Ndoa ya Diamond & Zuchu
Diamond Platnumz na Zuchu, walitangaza kufunga ndoa mwanzoni mwa mwezi Juni mwaka jana na wakati huo pia ujumbe wao ulionekana kuchanganya wengi wanaowafuatilia wengine wakidai kwamba wawili hao tayari walikuwa wameachana.
Ndoa yao ilikuwa ya siri na watu walionekana kujitokeza mitandaoni na kuwapa hongera pengine baada ya kuona ujumbe wa mama mzazi wa Diamond, Mama Dangote ambaye kupitia Instagram yake, alithibitisha kuwa wamefunga ndoa.
Aidha, hili linatokea wakati Zuchu anasemeka kuwa mjamzito na anatarajia kupata mtoto na Diamond.
Pia unaweza kusoma:
Aliyekuwa Amir wa Qatar, Sheikh Hamad bin Khalifa Al Thani, amefariki dunia
Aliyekuwa mtawala wa Qatar, Sheikh Hamad bin Khalifa Al Thani, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 74. Taarifa za kifo chake zilitangazwa Jumapili na mamlaka kuu ya serikali ya Qatar.
Sheikh Hamad alitawala Qatar kwa kipindi cha miaka 18 baada ya kumuondoa madarakani baba yake kupitia mapinduzi yasiyomwaga damu mwaka 1995.
Mwaka 2013, alimkabidhi madaraka mwanawe, hatua iliyotajwa kuwa nadra miongoni mwa tawala za kifalme za eneo la Ghuba ya Uajemi.
Katika kipindi cha utawala wake, aliiongoza Qatar kushuhudia ukuaji mkubwa wa uchumi, kupanua sekta ya mafuta na gesi, na kuanzishwa kwa kituo cha habari cha Al Jazeera.
Pia alianzisha katiba ya kudumu, akaendesha uchaguzi wa serikali za mitaa, na kuiongoza Qatar kupata haki ya kuandaa Kombe la Dunia la FIFA 2022.
Sheikh Hamad alifahamika kwa msimamo wake wa kujitegemea katika siasa za kimataifa, jambo ambalo mara kadhaa lilisababisha kutofautiana na baadhi ya nchi jirani za Kiarabu pamoja na washirika wa Magharibi.
Alisomea katika Chuo cha Kijeshi cha Sandhurst nchini Uingereza, na baadaye aliwahi kuwa kamanda wa jeshi, waziri wa ulinzi, na hatimaye mrithi wa kiti cha utawala kabla ya kuwa Amir wa Qatar.
Nani ataibuka mshindi kati ya England na Argentina?
Zikiwa zimesalia mechi nne pekee kabla ya kumalizika kwa mashindano, kampuni ya takwimu za michezo Opta imesasisha utabiri wake kuhusu kitakachotokea katika mechi zilizosalia kwenye mashindano ya Kombe la Dunia 2026.
Kwa mujibu wa utabiri huo, England ina nafasi ya asilimia 50.94 ya kufuzu fainali, huku Argentina ikipewa asilimia 49.06 ya kutinga mchezo wa mwisho utakaochezwa New York–New Jersey.
Kuhusu uwezekano wa kutwaa ubingwa wa mashindano, Three Lions imepewa nafasi ya asilimia 21.94, ikiwa nyuma ya Hispania na Ufaransa, ambazo ndizo zinaonekana kuwa na nafasi kubwa zaidi ya kutwaa taji.
Hata hivyo, kama ilivyoonekana katika mechi za hivi karibuni, bahati nayo ina mchango mkubwa katika matokeo ya mashindano ya mtoano, jambo ambalo hata mifumo ya kompyuta inayotabiri matokeo hushindwa kulikadiria kikamilifu.
Soma Zaidi:
Watu wakimbilia usalama wao huku Urusi ikishambulia karibu na mgahawa Ukraine
Video za kamera za usalama (CCTV) kutoka duka la mgahawa mmoja katika mji wa Sumy, nchini Ukraine, zimerekodi wakati watu wakijilaza chini kwa hofu baada ya milipuko kusikika karibu na mgahawa wao.
Kamera hizo zilionyesha matukio kutoka pembe tatu tofauti—moja ikiwa nje ya duka na mbili upande wa ndani.
Watu watano, akiwemo msichana mwenye umri wa miaka 13, walifariki dunia na wengine wasiopungua 30 kujeruhiwa baada ya mabomu ya aina ya glide bombs kulenga mji wa Sumy, ulioko kaskazini mashariki mwa Ukraine, siku ya Jumamosi, kwa mujibu wa meya wa mji huo, Artem Kobzar, kupitia mtandao wa Telegram.
Soma pia:
Iran yasema uzalishaji wa droni umeongezeka mara tatu licha ya vita
Kaimu Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema kuwa wakati wa vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran, miradi ya utengenezaji wa makombora na ndege zisizo na rubani haikusitishwa, badala yake utengenezaji droni uliongezeka mara tatu.
Brigedia Jenerali Majid Ibn-e-Reza alisema hayo Jumamosi katika kikao cha pamoja kilichowakutanisha maafisa wa Wizara ya Ulinzi na wajumbe wa Kamati ya Usalama wa Taifa na Sera ya Mambo ya Nje ya Bunge la Iran.
"Tunaufahamu vizuri udhaifu wa adui, na pia tunafahamu kikamilifu uwezo wetu," Jenerali Majid Ibn-e-Reza alisema.
Waziri huyo aliongeza kuwa Marekani na Israel ziliingia vitani zikiwa na lengo la kuuangusha utawala wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, lakini zimeshindwa kufanikisha azma hiyo.
"Vita vya hivi karibuni vimeonyesha kuwa wasomi wa Iran pamoja na uwekezaji katika teknolojia za kisasa ni nguzo muhimu zaidi za kuimarisha uwezo wa ulinzi wa nchi. Kwa hiyo, kuongezwa kwa bajeti ya ulinzi, teknolojia za hali ya juu, na kutumia utaalamu wa wasomi waliopo ndani na nje ya nchi ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele ili kufanikisha maendeleo ya teknolojia," alisema Majid Ibn-e-Reza.
Kaimu Waziri amewahi pia kusisitiza kuwa, "Uwezo wa ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hususan katika makombora na ndege zisizo na rubani, ni mstari ambao haupaswi kuvuka kuhusiana na usalama wa taifa na haujawahi kuwa wala hautakuwa sehemu ya mazungumzo."
Soma Zaidi:
Messi atarajiwa kuikabili England kwa mara ya kwanza
Kuna mambo machache ambayo Lionel Messi hajawahi kuyafanya ndani ya uwanja wa mpira wa soka.
Hata hivyo, mchezo wa nusu fainali kati ya Argentina na England utakaochezwa Jumatano saa 4:00 usiku kwa saa za Uingereza (BST) mjini Atlanta, utamletea nahodha huyo wa Argentina na uzoefu mpya kabisa.
Licha ya kucheza zaidi ya mechi 200 na kufunga mabao 125 akiwa na timu ya taifa ya Argentina, mshindi huyo wa Ballon d'Or mara nane hajawahi kuikabili England katika mechi ya kimataifa.
Kwa muda ilionekana huenda ndoto hiyo isitimie baada ya Uswisi kuonekana kuwa na nguvu katika robo fainali ya Jumamosi, lakini Argentina ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 baada ya muda wa ziada na kufuzu nusu fainali.
Katika ushindi huo, Messi alishindwa kufunga kwa mara ya kwanza kwenye mashindano haya. Hata hivyo, bado anaongoza kwenye (Golden Boot) pamoja na nyota wa Ufaransa, Kylian Mbappe, wakiwa wamefunga mabao manane kila mmoja. Pia Messi ndiye mfungaji bora wa muda wote katika historia ya Kombe la Dunia.
“England inaweza kuizidi Argentina kwa nguvu na kasi, lakini Argentina ina kipaji cha kipekee kinachoitwa Messi. Wachezaji wote wanacheza kwa ajili yake. Kila mtu anapaswa kuusubiri kwa hamu mchezo huu,” Mchambuzi wa BBC na beki wa zamani wa England, Micah Richards alisema.
Richards aliongeza kuwa kumzuia Messi ni kazi ngumu sana.
“Kumkaba inakaribia kuwa jambo lisilowezekana kwa sababu harudi sana kusaidia ulinzi. Anaingia kwenye nafasi ndogo ambazo huwezi kutarajia. Anajua wakati sahihi wa kujitokeza, ana ufundi wa hali ya juu, anaelewa vizuri matumizi ya nafasi uwanjani na ana uwezo mkubwa wa kupiga mashuti.”
“Jambo muhimu zaidi ni kwamba ana kile ambacho Jude Bellingham pia anacho—haiba na uwezo wa kuiongoza timu. Lakini kwa Messi, kiwango chake cha haiba ni cha kipekee kabisa. Itakuwa mechi ya kuvutia sana.”
Soma Zaidi:
Rooney: Messi anafanana kidogo na Bellingham
Mshambuliaji wa zamani wa England, Wayne Rooney, ameipa England ushauri kuhusu namna bora ya kudhibiti ushawishi wa Lionel Messi katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya Argentina.
“Kwa upande wa ulinzi, Messi anaweza kuwa udhaifu kwa Argentina,” alisema Rooney baada ya England kuichapa Norway mabao 2-1 na kufuzu nusu fainali, ambapo itakutana na Argentina kwa mara ya kwanza huku ikimkabili Messi.
“Harudi sana kusaidia ulinzi, lakini ana uwezo wa kubadili mchezo kwa muda mfupi, sawa na Jude Bellingham. Ana nyakati chache, lakini zenye ubora wa hali ya juu.”
Rooney aliongeza kuwa nguvu kubwa ya Messi iko kwenye uwezo wake wa kufanya maamuzi sahihi wakati muhimu.
“Kinachomtofautisha Messi ni uwezo wake wa kufanya maamuzi. Anaibuka katika nyakati muhimu za mchezo na karibu kila mara huchagua uamuzi sahihi.”
Kuhusu jinsi ya kumzuia, Rooney alisema“Kumdhibiti Lionel Messi kunahitaji umakini wa hali ya juu na mawasiliano mazuri. Ni lazima wachezaji wawasiliane vizuri kuhusu nafasi wanazopaswa kuziba, hata kama si nafasi walizozoea kucheza.”
Raia wa Marekani agundulika na Ebola baada ya kurejea kutoka DRC
Raia mmoja wa Marekani anayefanya kazi katika shirika la misaada ya kibinadamu nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) amegundulika kuwa na ugonjwa wa Ebola, kwa mujibu wa uthibitisho uliotolewa Ijumaa na Vituo vya Marekani vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC).
Kisa hicho kimezua tena taharuki na kuongeza umakini kuhusu mapambano ya Congo dhidi ya moja ya magonjwa hatari zaidi ya virusi duniani.
Kwa mujibu wa taarifa za CBS News na Associated Press, huyu ni raia wa pili wa Marekani kuhusishwa na mlipuko wa sasa wa Ebola, baada ya kisa cha awali kuripotiwa mwezi Mei.
CDC imesema inashirikiana na mwajiri wa mgonjwa huyo, mashirika ya Marekani pamoja na mamlaka za afya nchini Congo, ili kuzuia kuenea zaidi kwa maambukizi na kufuatilia watu waliokuwa na mawasiliano ya karibu na mgonjwa huyo.
Kwa sasa, jina, jinsia na eneo halisi analopatikana mfanyakazi huyo wa shirika la kutoa misaada havijafichuliwa. Hakuna taarifa zaidi zilizotolewa kuhusu hali ya mgonjwa huyo.
Kisa hicho cha maambukizi kinatokea wakati DRC ikiendelea kukabiliana na mlipuko wa Ebola unaoendelea katika majimbo ya mashariki ya Ituri, Kivu Kaskazini, na Kivu Kusini.
Jitihada za DRC za kudhibiti Ebola zinaendelea kukabiliwa na changamoto huku uratibu wa kitaifa ukiimarishwa katika maeneo ya Ituri, North Kivu na South Kivu.
Mamlaka zimethibitisha jumla ya maambukizi 1,830, ambapo wagonjwa 780 wanaendelea kupatiwa matibabu, 284 wamepona, na 648 wamefariki dunia.
Maafisa wanasema ufuatiliaji wa watu waliokutana na wagonjwa umefikia asilimia 78.1, kiwango muhimu katika kufuatilia waliotangamana na mgonjwa kupitia utambuzi na ufuatiliaji wa haraka watu wote walio katika athari ya kuathiriwa na virusi vya Ebola.
Miongoni mwa wahudumu wa mstari wa mbele wanaoshiriki katika kukabiliana na mlipuko huo, wahudumu 112 wa afya wameambukizwa virusi vya Ebola, na 35 wamepoteza maisha, jambo linaloonyesha hatari kubwa wanazokabiliana nazo timu za matibabu.
Aidha, Mkuu wa Africa CDC, Jean Kaseya, alisema kuwa maambukizi ya hivi karibuni yanaonyesha gharama kubwa ya kuchelewa kuchukua hatua dhidi ya ugonjwa huo.
Alieleza kuwa Africa CDC imetuma timu za wataalamu kutoka nyanja mbalimbali katika maeneo yaliyoathirika zaidi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), ambako maambukizi mengi ya Ebola yameendelea kuripotiwa.
Soma Zaidi:
“Labda Tuchel hajui ilivyo kucheza na wachezaji kama Haaland – Bellingham amjibu Tuchel
Kauli ya kocha wa England, Thomas Tuchel, kwamba timu yake “inapaswa kucheza vizuri zaidi” huenda haikuwa maneno ambayo shujaa wa mchezo huo, Jude Bellingham, alitaka kuyasikia baada ya kipenga cha mwisho.
Kiungo huyo wa Real Madrid alivaa jezi namba 10 na kuonyesha kiwango kikubwa cha nguvu katika mchezo uliodumu dakika 120, uliochezwa kwenye joto kali na hali ya unyevunyevu kupita kiasi, akisaidia England kufuzu hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia.
Juhudi hizo za aina yake zimefikiwa chini ya wiki moja baada ya wachezaji hao hao wa England, wakiwa pungufu kwa mchezaji mmoja, kufanya kazi ya ziada ya ulinzi na kuichapa Mexico katika uwanja wake wa Azteca kwenye hatua ya 16 bora.
Kauli ya Tuchel kwamba England ilishinda kwa “nguvu ya akili” lakini “inapaswa kucheza vizuri zaidi” ilimfanya Bellingham kuitikia kwa kutikisa mabega.
“Ndiyo, ni sawa, vyovyote vile,” alisema Bellingham katika mahojiano yake baada ya mchezo kwenye uwanja mjini Miami.
“Hali ni ngumu kule, ni kazi kubwa sana. Wachezaji wote wamejituma kupita kiasi. Mawazo yangu na shukrani zangu zinaenda kwa wachezaji waliopambana na kufanya kazi ya ziada,” amesema Bellingham.
“Labda yeye (Tuchel) hajui ilivyo kucheza katika mazingira kama yale dhidi ya wachezaji kama Erling Haaland, Martin Odegaard, Antonio Nusa na Alexander Sorloth,” Bellingham aliongeza:
“Si timu rahisi kucheza nayo. Sifa zote nawamiminia wachezaji wenzangu.
“Huwezi kushinda kila mchezo kwa kupiga pasi nyingi na njia bora. Wakati mwingine lazima ushinde kwa kupambana na kwa njia ngumu, na ndivyo tulivyofanya leo.”
Soma Zaidi:
Kombe la Dunia 2026: “Sijafurahishwa na Mchezo Wetu – Kwa Kila Kitu” - Kocha wa England
Kocha wa England, Thomas Tuchel, amekiri kutofurahishwa na kiwango cha mchezo wa timu yake katika ushindi wa kushtua dhidi ya Norway kwenye robo fainali ya Kombe la Dunia.
Tuchel amesema Three Lions walicheza kwa uzembe, na ushindi wao umepatikana kibahati tu ila hawakuwa katika kiwango cha mchezo kinachotakiwa “kwa kila hali” licha ya kufuzu hatua ya nusu fainali.
“Tumebahatika,” alisema Tuchel baada ya mchezo ambao Norway ilitangulia kufunga, ikakosa nafasi kubwa ya kuongeza bao la pili, ikakataliwa bao jingine na pia kupiga mpira uliogonga mwamba wa goli.
“Tumefanya mambo kuwa magumu sana kwetu wenyewe. Matokeo ni mazuri. Tumefika hatua ya nusu fainali. Ni jambo la kufurahia, lakini sijafurahishwa na uchezaji wetu — kwa kila hali.
“Tumefanya maisha kuwa magumu kupitia namna tulivyocheza. Tumecheza kwa uzembe, tumefanya makosa mengi ya kiufundi, hatukuwa na kasi ya kutosha na hatukuwa na mwendelezo wa kutosha.”
Tuchel amesema kuna jambo moja lililosaidia England kufuzu hatua inayofuata.
“Hii ni nguvu ya akili na dhamira ya timu,” amesema kocha huyo.
Soma zaidi:
Kombe la Dunia 2026: Bellingham aiongoza England kuichabanga Norway na kufuzu nusu fainali
England imebakisha ushindi mmoja kufika fainali ya kwanza ya Kombe la Dunia kwa wanaume tangu mwaka 1966, baada ya Jude Bellingham kuonyesha mchezo bora na kufunga mabao mawili katika ushindi wa kusisimua dhidi ya Norway baada ya muda wa ziada mjini Miami.
Timu ya kocha Thomas Tuchel ililazimika kupambana katika mchezo wa robo fainali uliochezwa kwenye joto kali na unyevunyevu, lakini Bellingham kwa mara nyingine alithibitisha kuwa ndiye mchezaji muhimu wa England kwa kuipeleka timu hiyo hatua ya timu nne bora, ambako itakutana na Argentina.
Katika mchezo mkali na wenye shinikizo, Norway ilitangulia kupata bao dakika ya 36 kupitia Andreas Schjelderup, ambaye shuti lake la juu lilimshinda nguvu kipa wa England, Jordan Pickford.
Hata hivyo, England ilijibu haraka kabla ya mapumziko, ambapo Bellingham alifunga bao la kusawazisha baada ya kupokea pasi ya Anthony Gordon na kumzidi ujanja kipa wa Norway, Orjan Nyland.
Kocha Tuchel alilazimika kufanya mabadiliko kipindi cha mapumziko, akiwatoa Declan Rice, ambaye alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa na majeraha, pamoja na Noni Madueke, na kuwaingiza Eberechi Eze na Bukayo Saka.
Norway iliendelea kuwa tishio baada ya mapumziko, lakini bao la Torbjorn Heggem lilikataliwa baada ya Erling Haaland kuonekana kumsukuma bila sababu Elliot Anderson. Pia David Moller Wolfe alipiga mpira wa kichwa uliogonga mwamba wa goli.
Haaland alishindwa kuonyesha makali yake na baadaye alitolewa mwanzoni mwa muda wa nyongeza. Dakika tatu tu baada ya kuanza kwa kipindi hicho, Bellingham alifunga bao lake la pili baada ya kipa Nyland kuzuia kwa mkono shuti la mchezaji wa akiba Morgan Rogers.
England sasa imefuzu kwa mara ya tatu katika historia yake kucheza nusu fainali ya Kombe la Dunia tangu ilipotwaa ubingwa mwaka 1966. Timu hiyo inatarajia kubadilisha historia baada ya kuondolewa na Ujerumani Magharibi mwaka 1990 na Croatia mwaka 2018 katika hatua hiyo.
Soma Zaidi:
Kombe la Dunia 2026: Argentina yatinga nusu fainali baada ya kuichapa Uswisi
Argentina imefuzu hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia 2026 baada ya kuichapa Uswisi katika mchezo wa kusisimua uliochezwa jijini Kansas City, na sasa itakutana na England.
Mshambuliaji Julian Alvarez ndiye aliyekuwa shujaa wa Argentina baada ya kufunga bao la ushindi katika muda wa ziada, akipiga shuti kali la umbali wa takribani yadi 25 lililomshinda nguvu kipa wa Uswisi, Gregor Kobel, na kuipeleka Argentina kwenye nusu fainali dhidi ya timu ya Thomas Tuchel.
Kwa upande wa Uswisi, ilikuwa ni huzuni kubwa baada ya kuonyesha ulinzi imara licha ya kucheza wakiwa wachezaji 10 katika kipindi cha pili.
Mshambuliaji nyota wa Uswisi Breel Embolo, alipewa kadi nyekundu.
Awali, Embolo alionekana kufanyiwa madhambi karibu na mstari wa katikati ya uwanja na Leandro Paredes, ambaye alionyeshwa kadi ya njano lakini uamuzi huo ulibatilishwa baada ya ukaguzi wa VAR na Embolo ambaye tayari alikuwa na kadi moja ya njano akatolewa nje kwa kadi nyekundu, hatua iliyoleta huzuni kwa mchezaji huyo na malalamiko kutoka upande wa Uswisi.
Soma Zaidi:
Watu 16 wafariki kwa njaa Uganda
Serikali ya Uganda imesema kuwa watu wasiopungua 16 wamefariki dunia kutokana na njaa katika wiki za hivi karibuni kwenye eneo la Karamoja, kaskazini mashariki mwa nchi, kufuatia ukame wa muda mrefu.
Wakulima wanasema wamepoteza mazao yao baada ya eneo hilo kushuhudia mvua chache sana au kutopata mvua kabisa tangu mnamo mwezi Aprili, ambao kwa kawaida ndiyo mwanzo wa msimu wa upandaji.
Wataalamu wanaonya kuwa upungufu wa chakula unaojirudia katika eneo hilo unasababishwa na mabadiliko ya tabianchi, mvua zisizotosheleza, ukataji wa miti, malisho kupita kiasi na wadudu waharibifu wa mazao. Sababu hizi kwa pamoja zimeendelea kuweka jamii katika hatari kubwa ya kukumbwa na njaa.
Waziri Mkuu wa Uganda, Robinah Nabbanja, amesema maelfu ya familia zimeachwa bila chakula baada ya ukame kuharibu mazao, na kwamba ofisi yake itawasilisha ombi kwa Baraza la Mawaziri siku ya Jumatatu ili kuidhinisha ununuzi wa chakula zaidi kwa ajili ya maeneo yaliyoathirika.
Serikali imesema tayari imeanza kusambaza msaada wa dharura wa chakula kwa wananchi.
Maeneo makubwa yaliyolimwa mahindi, mtama na soya yamekauka kutokana na ukame, hali iliyokatisha matumaini ya kupata mavuno mengi msimu huu.
Eneo la kaskazini mashariki mwa Uganda lenye hali ya ukame wa mara kwa mara limewahi kukumbwa na uhaba mkubwa wa chakula hapo awali.
Mwaka 2022, zaidi ya watu 2,200 walifariki dunia kutokana na njaa na magonjwa yanayohusiana na utapiamlo katika kaskazini mashariki mwa Uganda, kwa mujibu wa ripoti ya chombo rasmi cha haki za binadamu nchini humo.
Marekani yafanya mashambulizi mapya; Iran yafunga mlango wa bahari wa Hormuz
Marekani imesema imeanzisha wimbi jipya la mashambulizi dhidi ya Iran baada ya Iran kushambulia meli iliyokuwa ikipita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) limetangaza kufungwa kwa njia hiyo muhimu ya baharini hadi itakapotolewa taarifa nyingine, huku likionya kuhusu hatua kali dhidi ya kile lilichokiita "uchokozi" wa Marekani, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali.
Saa chache baada ya mashambulizi ya Marekani, IRGC ilidai kuwa imelenga kambi ya kijeshi ya Marekani nchini Jordan. Wakati huo huo, Falme za Kiarabu (UAE), Qatar na Bahrain ziliripoti kuchukua hatua za kukabiliana na makombora na ndege zisizo na rubani zilizorushwa kutoka Iran.
Mvutano huo unafuatia matukio ya mapema wiki hii ambapo meli tatu za kibiashara za kubeba mafuta zilishambuliwa, hali iliyosababisha mashambulizi ya kulipizana kisasi kati ya Marekani na Iran.
Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) ilisema imeanzisha duru ya tatu ya mashambulizi wiki hii baada ya IRGC kushambulia "waziwazi" meli yenye usajili wa Cyprus, MV GFS Galaxy, iliyokuwa ikivuka Mlango wa Bahari wa Hormuz.
Kwa mujibu wa CENTCOM, meli hiyo iliharibiwa vibaya katika chumba cha injini na haikuweza kuendelea na safari yake. Aidha, mfanyakazi mmoja wa kiraia wa meli hiyo anaripotiwa kutojulikana alipo.
Shirika la Uingereza la UK Maritime Trade Operations (UKMTO) limesema lilifahamishwa na mamlaka za kijeshi kuwa wafanyakazi wa meli walilazimika kuiacha baada ya kushambuliwa na kuanza kutumia boti ya kujiokoa.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X, CENTCOM ilisema Iran ilipewa fursa nyingine ya kuonyesha kwamba inazingatia makubaliano ya Maelewano baada ya kuwajibishwa kwa mashambulizi ya awali dhidi ya meli za kibiashara, lakini "imeshindwa kufanya hivyo kwa mara nyingine."
Soma Zaidi Hapa:
Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara, tarehe ni 12/07/2026.