Madagascar yatangaza hali ya dharura kutokana na uhaba mkubwa wa mafuta unaohusishwa na vita vya Iran

Chanzo cha picha, Getty Images
Madagascar imetangaza hali ya dharura kwa muda wa wiki mbili kufuatia uhaba mkubwa wa mafuta uliosababishwa na vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Mamlaka zimesema uamuzi huo ulifikiwa baada ya kikao cha baraza la mawaziri Jumanne, kutokana na hofu kwamba hali hiyo inaweza kusababisha vurugu za kijamii.
Kisiwa hicho cha Bahari ya Hindi, ambacho hutegemea mafuta kuzalisha sehemu kubwa ya umeme wake, kinategemea uagizaji wa mafuta kutoka Mashariki ya Kati na usambazaji unatarajiwa kuathirika kwa muda, licha ya kusitishwa kwa mapigano kwa wiki mbili kulikotangazwa usiku.
Mwaka jana, kukatika kwa mara kwa mara kwa umeme na maji nchini Madagascar kulisababisha maandamano yaliyoongozwa na vijana, ambayo baadaye yaligeuka kuwa machafuko ya kisiasa na kusababisha jeshi kuchukua madaraka.
Haijulikani wazi hatua mahsusi ambazo serikali inapanga kuchukua, lakini imesema sasa ina mamlaka ya kuimarisha sekta ya umeme, kupunguza usumbufu zaidi, kudhibiti matumizi, na kuhakikisha huduma za umma zinaendelea.
Unaweza kusoma;





