Marekani yasitisha mauzo ya silaha za dola bilioni 14 kwa Taiwan kutokana na vita vya Iran

Chanzo cha picha, CQ-Roll Call, Inc. via Getty Images
Marekani imesema imesitisha kwa muda mauzo ya silaha yenye thamani ya dola bilioni 14 kwa Taiwan ili kuhakikisha ina akiba ya kutosha ya silaha na risasi kwa ajili ya uwezekano wa vita dhidi ya Iran.
Kaimu Katibu wa Jeshi la Wanamaji la Marekani, Hong Kao, amethibitisha hatua hiyo wakati wa kikao cha Kamati ya Seneti kilichofanyika jana.
Hatua hiyo imekuja licha ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kutotoa msimamo wa wazi kuhusu mauzo hayo siku chache zilizopita, akisema angejadili suala hilo na Rais wa Taiwan.
Ofisi ya Rais wa Taiwan imesema Ijumaa kwamba haijapokea taarifa yoyote kuhusu kile ilichokiita “mabadiliko katika mchakato wa mauzo ya silaha wa Marekani”.
Kwa muda mrefu, mauzo ya silaha za Marekani kwa Taiwan yamekuwa chanzo cha mvutano kati ya Washington na Beijing. China inaichukulia Taiwan kuwa sehemu ya eneo lake na haitambui utawala wake wa kujitegemea, huku ikiwa haijaondoa uwezekano wa kutumia nguvu kuirejesha chini ya udhibiti wake.
“Tumesitisha mauzo haya kwa sasa ili kuhakikisha tuna risasi na vifaa vya kutosha kwa ajili ya Operesheni Epic Fury dhidi ya Iran, na bila shaka kuhakikisha tuna akiba ya kutosha,” Hong Kao aliiambia Seneti.
Alipoulizwa kuhusu msimamo wa Taiwan kufuatia uamuzi huo wa Marekani, alisema bado hajazungumza na maafisa wa Taiwan.
“Tunachofanya ni kuhakikisha tuna kila kitu tunachohitaji. Serikali itakapoona inafaa, mauzo ya silaha kwa mataifa ya kigeni yataendelea tena,” alisema.
Soma zaidi:




