Kuanzia kwa makaribisho makubwa hadi mazungumzo magumu: China inataka nini kutoka kwa Trump?

.

Chanzo cha picha, Reuters

    • Author, Laura Baker
    • Nafasi, BBC China
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Xi Jinping amemkaribisha rasmi Donald Trump katika ziara yake, ambayo inaweza kurejesha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili yenye ushawishi mkubwa duniani.

Gwaride la kijeshi liliandaliwa nje ya Ukumbi wa Great Hall kumkaribisha Bw. Trump, akisindikizwa na saluti ya mizinga na bendi inayopiga wimbo wa taifa wa Marekani. Rais wa Marekani alisimama mara mbili kuwasalimia wanafunzi waliokuwa wakipeperusha bendera za China na Marekani.

Aliinama mbele kumuamkua Xi, kwa heshima kisha akamsifu mwenyeji wake.

"Wewe ni kiongozi mzuri," alisema katika matamshi ambayo yalionekana kuwa hayana maandishi. "Namwambia kila mtu hivyo." Baadaye, alipokuwa akizuru Hekalu la Mbinguni la karne ya 15, Bw. Trump aliwaambia waandishi wa habari kwamba China ilikuwa nzuri. Wakati wa chakula cha jioni, alielezea mazungumzo hayo kama fursa "ya thamani".

Hii ilikuwa siku muhimu, kwa sababu Donald Trump alikuwa amejinadi kisiasa kwa kuchukua msimamo mkali dhidi ya China.

''Hatuwezi kuendelea kuangalia China ikivamia nchi yetu, na ndivyo inavyofanya,'' alisema katika mkutano wa kampeni mwaka 2016.

Bw. Trump alidai mnamo 2020 kwamba China "ilidanganya Marekani kuliko nchi nyingine yoyote" na akaelezea janga la Covid-19 kama "virusi vya China." Kabla ya kurejea madarakani, alikuwa ameahidi "kuibana China vilivyo."

Mwaka jana vita vya kibiashara vilipofikia kilele chake, pande zote mbili ziliwekeana ushuru wa zaidi ya asilimia 100 kwa kila mmoja. Baadaye walifikia makubaliano dhaifu ya kusitisha mzozo huo wa kibiashara, lakini swali ni je, ziara hii itagubikwa na masuala hayo?

Maswali mengine yanahusu Iran. Je, Beijing inaweza kusaidia Marekani kumaliza mzozo wa Iran? Na Taiwan, mshirika wa Marekani na kisiwa kinachojitawala ambacho China inakichukulia kuwa sehemu ya eneo lake.

Donald Trump alionekana kufurahishwa na makaribisho aliyopokea mjini Beijing.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Donald Trump alionekana kufurahishwa na makaribisho aliyopokea mjini Beijing.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Beijing ilikuwa imepanga onyesho lililolenga kumsifu Donald Trump kabla ya makubaliano yoyote na kuthibitisha kwamba milango ya China iko wazi kwa wageni. Hata hivyo, muda mfupi baada ya mazungumzo hayo kuanza, vyombo vya habari vya serikali vilichapisha taarifa kutoka kwa Bw Xi na kuashiria kuwa mvutano kuhusu Taiwan unaweza kuwa changamoto.

Lakini hatua hii ya kina haikuwa tu ya Donald Trump na Wakurugenzi Wakuu 30 walioandamana naye. Ilikuwa pia onyesho la nguvu. Moja ambayo Beijing inajua itaonyeshwa moja kwa moja kote nchini Marekani na ulimwengu mzima.

"Tunashuhudia mabadiliko ya kihistoria," anasema John Delory, mwenzake mwandamizi katika Kituo cha Jumuiya ya Asia juu ya Mahusiano ya U.S.-China.

"Ninasitasita kusisitiza zaidi mkutano huu muhimu," anasema, "lakini kupanda kuepukika kwa China hadi kufikia nafasi ambayo inaweza kushindana kikweli na Marekani kunatokea mbele ya macho yetu. Beijing sasa ni mji mkuu wa pili wa dunia."

Onyesho la kila mtu

Xi Jinping amekuwa na nia ya kujionyesha kama kiongozi thabiti wa kimataifa mbele ya rais asiyetabirika wa Marekani. Kwa kuzingatia ukubwa wa uchumi wa China, viongozi kadhaa wa dunia wakiwemo washirika wa Marekani Canada, Uingereza na Ujerumani, wamezuru nchi hiyo kujaribu kufanya makubaliano na Beijing.

Biashara ya China na mataifa mengine duniani imepanuka tangu muhula wa kwanza wa Donald Trump kama rais, huku Beijing ikijiandaa kwa kile Bw. Trump alionya kuhusu: ushuru zaidi.

China ilionyesha uwezo wake wa kiuchumi na kidiplomasia mwaka jana kwa kuweka ushuru wa kulipiza kisasi dhidi ya Donald Trump na kuzuia usafirishaji wa madini adimu, ambayo ni muhimu kwa tasnia ya hali ya juu. Washington ilikuja kwenye meza ya mazungumzo na ushuru ukapunguzwa.

Bw. Xi anaamini kuwa ameionyesha Marekani na dunia jinsi wanavyotegemea viwanda na teknolojia ya China. China sasa inazalisha theluthi moja ya bidhaa zote duniani, inasindika zaidi ya asilimia 90 ya madini adimu, na kutengeneza takriban asilimia 60 hadi 80 ya paneli za jua, mitambo ya upepo, na magari yanayotumia umeme.

Ingawa rekodi ya haki za binadamu ya China na uhusiano wake na serikali kama vile Urusi na Korea Kaskazini bado inaibua wasiwasi, masuala hayo yamepigwa teka huku Donald Trump akionekana kubadilisha utaratibu wa kimataifa.

Wengine wanachukulia hali hii kama ishara ya mabadiliko katika usawa wa madaraka kwa maslahi ya China.

Iran kama chambo cha mazungumzo

Huenda China inahisi kuwa ina mchango mkubwa katika mazungumzo haya, huku Bw Xi akikabiliana na Donald Trump aliyedhoofishwa na vita na Iran. Kufungwa kwa Mlango-Bahari wa Hormuz kumetikisa uchumi wa dunia, na Bw Trump anatarajiwa kuiomba Beijing kusaidia kufungua tena njia hiyo kuu ya majini.

Beijing na Tehran zina uhusiano ambao umekuzwa kwa miongo kadhaa, na China ndio mshirika mkubwa wa kibiashara wa Iran. Ikiwa Bw. Xi atafanikiwa kuileta Tehran kwenye meza ya mazungumzo, atakuwa na ushawishi zaidi.

Xi akimkaribisha Donald Trump kwenye dhifa ya chakula cha jioni katika Ukumbi wa kijamii wa Great Hall

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Xi akimkaribisha Donald Trump kwenye dhifa ya chakula cha jioni katika Ukumbi wa kijamii wa Great Hall

"Ni kwa manufaa yao kutatua suala hili, na tunatumai kuwashawishi kuchukua jukumu kubwa zaidi," Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio aliambia Fox News kabla ya safari.

Lakini China itategemea kupata kitu kama malipo.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya China, Xi Jinping hapo awali alimuonya Trump wakati wa mazungumzo kwamba suala la Taiwan linaweza kutumbukiza nchi hizo mbili kwenye mgogoro.

Anaweza kuishinikiza Marekani kuchelewesha au kusitisha uuzaji wa silaha kwa Taiwan, ingawa Washington ina wajibu wa kisheria kutoa mbinu za kujilinda kwa kisiwa hicho. Hata hivyo, maafisa wa Taipei roho juu kyfuatilia mkutano huo.

Wakati waandishi wa habari walipowauliza viongozi hao wawili kama wameijadili Taiwan, hakuna aliyejibu swali hilo.

Ziara ya sasa ya Trump ni tofauti kabisa ukilinganisha na ile aliyofanya wakati wa muhula wake wa kwanza madarakani aliyoambatana na mke wake Melania Trump,.

Ujumbe ulioandamana naye unajumuisha watu kama Elon Musk, Tim Cook, na Mkurugenzi Mtendaji wa Nvidia Jensen Huang unatoa taswira ya kibiashara na wote walihudhuria dhifa hiyo ya chakula cha jioni.

Donald Trump anataka ujumbe huo kuwa kitovu cha tahadhari kwa sababu anataka China ifungue milango yake zaidi kwa makampuni ya Marekani.

Mpango huo haujabainika unaelekea wapi kwasababu hakuna maelezo yoyote yaliyotolewa.

Taarifa ya Ikulu ya Marekani ilisema tu kwamba pande hizo mbili zilijadili "njia za kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi," ikiwa ni pamoja na kupanua upatikanaji wa makampuni ya Marekani kwenye soko la China na uwekezaji wa China katika viwanda vya Marekani.

Kuhusu Iran, pia inasema kwamba "nchi zote mbili zinakubali kwamba Iran haipaswi kamwe kupata silaha ya nyuklia" na "Mlango wa bahari wa Hormuz lazima usalie wazi ili kusaidia mtiririko huru wa nishati."

Ni nini kitakachofuata?

Maelezo zaidi yanaweza kujitokeza leo Ijumaa Mei 15, wakati viongozi hao wawili watakapokutana tena. Donald Trump anapania kufikia mafanikio ambayo anaweza kuonyesha nyumbani huku umaarufu wake ukiendelea kushuka.

Xi amealikwa Marekani mwezi Septemba

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Xi amealikwa Marekani mwezi Septemba

Xi Jinping amesema pande hizo mbili zinapaswa kupanua mawasiliano na ushirikiano katika maeneo kama vile biashara na kilimo, pengine ishara kwamba China iko tayari kununua maharage ya soya zaidi, nyama ya ng'ombe na ndege za Boeing kutoka Marekani.

Viongozi hao wawili pia walikubaliana kufafanua uhusiano wao kama "wa kujenga, wa kimkakati, na dhabiti," mfumo mpya ambao utaongoza uhusiano wa nchi hizo mbili katika miaka mitatu ijayo.

China inakabiliwa na changamoto kubwa za kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa ukosefu wa ajira, ukuaji usio na usawa, mgogoro wa soko la mali isiyohamishika, na viwango vya juu sana vya deni la serikali za mitaa.

Kwa hivyo Beijing huenda haitaki ulimwengu ambapo Washington inadhibiti ulimwengu, lakini inahitaji kutafuta njia ya kukubaliana na .Marekani

Na huo ndio ujumbe ulionekana kuwasilishwa na viongozi wote wawili wakati wa dhifa ya chakula cha jioni.

Donald Trump, akifurahia "makaribisho mazuri na yasiyo na kifani" aliyokuwa amepokea, alimwalika Bw Xi kwenye Ikulu ya White House mnamo Septemba.

Xi aliongeza kuwa China na Marekani zinaweza kuwa ''washirika badala ya wapinzani.''

Alikamilisha hotuba yake kwa kuitakia Marekani na China mustakabali mwema na kusema, "Kwaheri."