Afrika yaweka rekodi Kombe la Dunia, je, safari ya kutwaa taji imekaribia?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 2

Afrika imeandika historia mpya katika fainali za Kombe la Dunia la 2026 baada ya nchi tisa kati ya 10 zilizoshiriki kufuzu hatua ya mtoano ya timu 32, idadi ambayo haijawahi kufikiwa na bara hilo katika historia ya mashindano hayo.

Morocco, Misri, Afrika Kusini, Ivory Coast, Cape Verde, Senegal, Ghana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo) na Algeria zimefanikiwa kutinga hatua hiyo, huku Tunisia ikiwa taifa pekee la Afrika lililoshindwa kusonga mbele.

Mafanikio hayo yanakuja miaka minne tu baada ya Kombe la Dunia la 2022, ambapo Afrika ilikuwa na timu tano pekee zilizoshiriki. Htaa hivyo Afrika Kusini imechapwa 1-0 na Canada na kuondolewa katika hatua ya 32.

Kabla ya mashindano haya, ni mataifa sita tu ya Afrika yaliyowahi kufuzu hatua ya mtoano katika historia ya Kombe la Dunia: Cameroon, Nigeria, Senegal, Ghana, Algeria na Morocco. Kwa jumla, zilifika hatua ya mtoano mara 11 pekee, lakini kwa timu 9 kufika mtoano mwaka huu, sasa Afrika imefika hatua ya mtoano mara 20.

Morocco ndiyo iliyoweka rekodi kubwa zaidi mwaka 2022 ilipofika hatua ya nusu fainali, jambo lililoifanya kuwa timu ya kwanza kutoka Afrika kufikia hatua hiyo.

Safari ya mwaka huu imezua matumaini mapya kuwa huenda Afrika ipo karibu zaidi kuliko wakati mwingine wowote kutwaa Kombe la Dunia.

Katika hatua ya makundi, timu za Afrika zimeonyesha ushindani mkubwa dhidi ya baadhi ya mataifa yenye historia kubwa ya soka duniani, zikiwemo Brazil, England, Ureno, Hispania, Uruguay na Ubelgiji.

Kwa wengi, mafanikio hayo ni ishara ya ukuaji wa soka la Afrika, uwekezaji unaoendelea katika maendeleo ya mchezo huo na kuongezeka kwa idadi ya wachezaji wa Afrika wanaocheza katika ligi kubwa duniani.

Morocco, ambayo itakuwa mwenyeji mwenza wa Kombe la Dunia la 2030 pamoja na Hispania na Ureno, imeendelea kutajwa kama mfano wa mafanikio ya uwekezaji wa muda mrefu katika soka.

Mchambuzi wa FOX Sports, Peter Crouch, anaamini ni suala la muda kabla ya timu kutoka Afrika kutwaa taji hilo.

"Ni suala la muda kabla timu ya Afrika haijashinda Kombe la Dunia."

Ratiba ya mataifa ya Afrika hatua ya 32 bora (saa za Afrika Mashariki)

Juni 29

Afrika Kusini vs Canada — saa 4:00 usiku (22:00 EAT)

Juni 30

Morocco vs Uholanzi — saa 10:00 alfajiri (04:00 EAT)

Ivory Coast vs Norway — saa 2:00 usiku (20:00 EAT)

Julai 1

DR Congo vs England — saa 1:00 usiku (19:00 EAT)

Senegal vs Ubelgiji — saa 5:00 usiku (23:00 EAT)

Julai 3

Algeria vs Uswisi — saa 4:00 asubuhi (04:00 EAT)

Misri vs Australia — saa 3:00 usiku (21:00 EAT)

Cape Verde vs Argentina — saa 7:00 usiku (01:00 EAT, Julai 4)

Julai 4

Ghana vs Colombia — saa 2:30 usiku (20:30 EAT)

Iwapo mataifa hayo yataendelea kufanya vizuri katika hatua ya mtoano, Kombe la Dunia la 2026 linaweza kuwa mashindano yatakayobadili historia ya soka la Afrika.