Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Iran na Marekani zakubaliana kusitisha mashambulizi na kufanya mazungumzo Doha - Axios

Kwa mujibu wa Axios Marekani na Iran zinatarajiwa kukutana mjini Doha siku ya Jumanne kutafuta suluhu ya tofauti zao kuhusu Mlango wa Hormuz.

Muhtasari

Iran na Marekani zakubaliana kusitisha mashambulizi na kufanya mazungumzo Doha - Axios

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Baadhi ya wanazuoni wa Iran watoa fatwa ya kutaka kuuawa kwa Trump na Netanyahu

    Mgawanyiko usio wa kawaida umeripotiwa ndani ya Baraza la Wataalamu wa Iran, chombo cha juu zaidi cha wanazuoni wa kidini nchini humo.

    Takriban theluthi mbili ya wajumbe wa baraza hilo lenye wanachama 88 walitoa fatwa ya kidini inayotaka kuuawa kwa Rais wa Marekani Donald Trump na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

    Fatwa hiyo ilieleza kuwa ni wajibu wa Waislamu kuwaua viongozi hao wawili iwapo watapata fursa ya kufanya hivyo.

    Hata hivyo, uongozi wa Baraza la Wataalamu umeitaja fatwa hiyo kuwa "isiyo ya kawaida", ukisema maudhui yake yanahitaji mjadala na uchambuzi zaidi.

    Fatwa hiyo, iliyotolewa na wanazuoni wenye misimamo mikali, ilijumuishwa katika barua iliyotumwa kwa umma wa Iran.

    Barua hiyo pia ilisema kuwa Tehran haipaswi kukubali kufunguliwa kwa Mlango wa Hormuz wala kujadili mpango wake wa nyuklia katika mazungumzo na Marekani.

    Maelezo zaidi:

  2. Serikali ya Tanzania yasema kukatika kwa umeme Jumamosi kulizuia janga kubwa zaidi

    Serikali ya Tanzania imesema kukatika kwa umeme nchini kote siku ya Jumamosi kulisababishwa na mfumo wa kiotomatiki wa usalama wa Gridi ya Taifa, ambao ulijizima ili kuzuia uharibifu mkubwa zaidi wa mtandao wa umeme.

    Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema Gridi ya Taifa imewekewa mifumo ya kisasa ya kidijitali ya ulinzi ambayo hujitenga au kuzima sehemu za mtandao moja kwa moja inapobaini hitilafu kubwa.

    Amesema teknolojia hiyo imeundwa kuzuia kusambaratika kwa mfumo mzima wa umeme na kulinda miundombinu muhimu.

    Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya hitilafu ya kiufundi kwenye Gridi ya Taifa kusababisha kukatika kwa umeme katika maeneo yote yaliyounganishwa na gridi hiyo.

    Hitilafu hiyo iliathiri shughuli za biashara, usafiri, mawasiliano na huduma nyingine muhimu kwa saa kadhaa, huku maelfu ya wananchi wakikumbwa na usumbufu katika shughuli zao za kila siku.

    Kwa mujibu wa Msigwa, hatua ya mfumo kujizima moja kwa moja inaonesha kuwa miundombinu ya umeme ya Tanzania imejengwa kwa teknolojia za kisasa zenye uwezo wa kubaini hitilafu na kuchukua hatua za haraka bila kusubiri uingiliaji wa kibinadamu.

    Hata hivyo, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amemuagiza Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Umeme na Nishati kuunda kamati ya uchunguzi kubaini chanzo cha hitilafu hiyo na kupendekeza hatua za kuzuia tatizo kama hilo kujitokeza tena.

    TANESCO imetakiwa kuwasilisha taarifa ya awali ndani ya wiki moja ili kuiwezesha serikali kuchukua hatua stahiki, huku uchunguzi wa kina ukiendelea.

    Soma Zaidi:

  3. Rais wa Shirikisho la Soka Saudi Arabia ajiuzulu baada ya timu kutolewa Kombe la Dunia

    Rais wa Shirikisho la Soka la Saudi Arabia, Yasser Al Mashal, amejiuzulu kufuatia kutolewa kwa timu ya taifa ya nchi hiyo katika hatua ya makundi ya Kombe la Dunia.

    Katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, Al Mashal amesema kutofuzu kwa timu hiyo kwenda hatua inayofuata ya mashindano hayo ni matokeo ambayo hayaendani kwa namna yoyote na matarajio na malengo ya taifa hilo.

    "Kutofuzu kwa timu ya taifa kwenda hatua inayofuata ya Kombe la Dunia ni matokeo yasiyoendana na matarajio yetu," aliandika Al Mashal kwenye mitandao ya kijamii.

    "Ninabeba jukumu kamili kwa matokeo haya na naomba radhi kwa wote waliotarajia kuiona timu yetu ikifanya vizuri zaidi.

    Kwa kuamini kwamba uwajibikaji unahitaji kutoa nafasi kwa mwanzo mpya, nimeamua kutoendelea hadi mwisho wa muhula wangu wa uongozi."

    Saudi Arabia ilimaliza mkiani mwa Kundi H ikiwa na pointi mbili, baada ya kutoka sare dhidi ya Uruguay na Cape Verde na kupoteza mechi dhidi ya Hispania.

    Al Mashal alikuwa ameongoza Shirikisho la Soka la Saudi Arabia kwa miaka saba na alihusika kwa kiasi kikubwa katika jitihada zilizoiwezesha Saudi Arabia kupata haki ya kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia la mwaka 2034.

    Saudi Arabia ilikuwa ikishiriki Kombe la Dunia kwa mara ya tatu mfululizo na mara ya saba kwa ujumla. Hata hivyo, maandalizi yake yaliathiriwa na uamuzi wa kumwondoa kocha Herve Renard na kumteua Georgios Donis chini ya miezi miwili kabla ya mashindano kuanza.

    Soma pia:

  4. WHO: Vifo 1,300 Ulaya vyahusishwa na wimbi kali la joto

    Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema wimbi la joto lisilo la kawaida linaloikumba Ulaya huenda limesababisha vifo vya ziada vya zaidi ya watu 1,300 tangu Juni 21.

    Rekodi za viwango vya joto zimeendelea kuvunjwa katika mataifa kadhaa ya Ulaya, yakiwemo Ujerumani, Poland na Jamhuri ya Czech, huku wimbi hilo la joto kali likiendelea kuelekea mashariki mwa bara hilo.

    Katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, Tedros alisema joto kali mara nyingi huitwa "muuaji kimya" kwa sababu linaweza kusababisha vifo bila dalili za wazi.

    Aliongeza kuwa nyumba, maeneo ya kazi na shule nyingi barani Ulaya hazikujengwa kuhimili viwango hivyo vya juu vya joto.

    Wizara ya Afya ya Ufaransa imesema takriban vifo 1,000 zaidi ya vilivyotarajiwa vimerekodiwa nchini humo tangu Jumatano, huku idadi kubwa ya vifo hivyo ikiwa ni ya watu wenye umri wa miaka 65 na kuendelea.

    WHO imeonya kuwa Ulaya ndiyo bara linaloongezeka joto kwa kasi zaidi duniani, kwa kiwango cha mara mbili ya wastani wa ongezeko la joto duniani.

    "Mamilioni ya watu barani Ulaya kwa sasa wanaishi chini ya wimbi kali la joto, mamia wamefariki, shule zimefungwa na mifumo ya usambazaji umeme iko chini ya shinikizo kubwa," alisema Tedros.

    Soma Zaidi:

  5. Iran na Marekani zakubaliana kusitisha mashambulizi na kufanya mazungumzo Doha - Axios

    Axios imeripoti kuwa Tehran na Washington zimekubaliana kusitisha mashambulizi katika Ghuba ya Uajemi na kufanya mazungumzo ya moja kwa moja katika siku chache zijazo mjini Doha, Qatar.

    Mwandishi wa Axios, Barak Ravid, aliandika Jumapili jioni kwamba afisa mmoja mwandamizi wa Marekani amesema Marekani na Iran zimekubaliana kuacha kushambuliana, na kwamba pande hizo mbili zinatarajiwa kukutana mjini Doha siku ya Jumanne kutafuta suluhu ya tofauti zao kuhusu Mlango wa Hormuz.

    Kwa mujibu wa Axios, mazungumzo hayo yataangazia zaidi suala la Mlango wa Hormuz.

    Iran imehusisha mapigano mapya na Marekani na kile inachodai kuwa ni kuingilia usimamizi wake wa Mlango wa Hormuz.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, amesema wakati wa ziara yake nchini Iraq kwamba kufunguliwa kikamilifu kwa Mlango wa Hormuz, kwa mujibu wa makubaliano na Marekani, ni jukumu la Tehran pekee, na kwamba kuingilia mchakato huo kutavuruga juhudi hizo na kuongeza mvutano katika eneo hilo.

    Maelezo zaidi:

  6. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya tarehe 29 Juni 2026.