Mama mkatili: "Alinilazimisha kuishi kama mgonjwa kwa miaka mingi"

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Alipozaliwa nchini Uholanzi katika miaka ya 1970 na 1980, Nina Blom alionekana kuwa mtoto wa kawaida. Alipenda muziki, kuimba na kucheza, na ana kumbukumbu za furaha za kucheza na dada yake nyumbani kwao.

Hata hivyo, nyakati hizo za furaha zilikuwa chache.

Aliruhusiwa kutoka nyumbani mara chache tu, na alipofika umri wa miaka minane, mama yake alimshawishi kwamba alikuwa mgonjwa sana. Mama yake alimpeleka hospitalini mara kwa mara kwa ajili ya vipimo na matibabu.

Nina alipelekwa hospitalini zaidi ya mara 15 katika hospitali sita tofauti ndani ya kipindi cha miaka michache tu. Baadaye, alimlazimisha kutumia kiti cha magurudumu na kumwambia kuwa alikuwa na ugonjwa wa misuli usiotibika na kwamba alikuwa anakaribia kufa.

Kwa miaka mingi, wataalamu wengi wa afya walimchunguza, lakini hakuna aliyefanikiwa kueleza tatizo lake. Hatimaye, daktari mmoja makini aliunganisha vipande vya simulizi ya Nina na kugundua chanzo halisi na cha kutisha cha "ugonjwa" wake ambao ulikuwa 'mama yake mwenyewe.'

Paediatric Condition Falsification (PCF), inayojulikana pia kama Fabricated or Induced Illness (FII) au Munchausen Syndrome by Proxy, ni aina ya unyanyasaji wa watoto ambapo mlezi, kwa kawaida mzazi huzidisha, hubuni, au husababisha kwa makusudi dalili za ugonjwa kwa mtoto. Sababu zinazowafanya baadhi ya walezi kufanya hivyo bado hazijabainika.

Kulazwa hospitalini kwa mara ya kwanza

Nina alipokuwa na umri wa miaka minane, alianza kusumbuliwa na matatizo ya mara kwa mara ya tumbo na akapunguza uzani wa mwili.

Alipolazwa hospitalini, alipewa sharubati ya tufaha na supu, na kwa njia ya kushangaza alianza kujisikia nafuu.

Daktari akasema, 'Nina yuko mzima anaweza kurudi nyumbani.'"

Lakini mama yake Nina alisisitiza warudi hospitalini tena na akamtaka awaambie madaktari kwamba tumbo lake bado linauma, ingawa kwa kweli halikuwa linauma.

Hali hiyo iliendelea kujirudia tena na tena katika miaka iliyofuata.

Siku moja, wakati familia yake ilikuwa likizoni, Nina alilalamika kuwa alihisi maumivu baada ya kuogelea. Mara moja mama yake aliamua kwamba alikuwa na ugonjwa wa misuli na kwamba alihitaji kupelekwa hospitalini tena.

Nina alipokataa, mama yake alimwambia, "Usinifanye nionekane mjinga. Una maumivu, na hivyo ndivyo utakavyomwambia daktari."

Kwa Nina, hali hiyo ilikuwa ya kutatanisha sana.

"Nilihisi vibaya kwa sababu nilikuwa nimelazwa chumba kimoja na watoto waliokuwa na saratani, ambao kweli walikuwa wagonjwa, nilikuwa nikijiambia, mimi sina tatizo lolote."

Mvulana aliyekuwa amelazwa kwenye kitanda kilichokuwa karibu na chake alifariki dunia akiwa bado hospitalini, jambo lililoongeza hisia zake za hatia

"Hakuwa na huruma"

Nina alifanyiwa vipimo vingi, ikiwa ni pamoja na uchunguzi wenye maumivu makali kama vile kuchukuliwa sampuli ya uboho wa mfupa . Hata hivyo, madaktari hawakupata tatizo lolote.

Mama yake alikuwa karibu naye kila wakati, na kila alipomwona Nina akitabasamu, alikasirika na kumwadhibu.

Baada ya kulazwa hospitalini kwa muda wa wiki nne, hatimaye madaktari waliamua kumruhusu Nina arudi nyumbani. Mara tu walipofika nyumbani, mama yake alimketisha kwenye kiti cha magurudumu, akamwondoa shuleni, na kumlazimisha alale katika kitanda kilichowekwa sebuleni mwa nyumba yao.

Hakuruhiswa tena kuwaona marafiki zake, na mama yake alimnyang'anya muziki alioupenda kuusikiliza. Faraja yake pekee ilikuwa kushona kwa sindano, lakini mikono yake ilianza kuchoka na kuuma.

Mama yake alisisitiza mara moja kwamba kulikuwa na tatizo kubwa na akaifunga mikono yake kwa bandeji zilizobana sana.

Bandeji hizo zilikuwa zimekazwa kiasi kwamba mikono na vidole vyake vilikosa hisia. Jambo hilo lilionekana kumfurahisha mama yake.

"Siwezi kueleza jinsi nilikuwa nasikitika kumwona mama yangu akionekana kana kwamba anafurahia hali hiyo."

'Unaenda kufariki'

Kadri miaka zilivyokwena, simulizi la mama yake lilibadilika. Alimwambia Nina,

"Nikigundua kwamba huna maumivu na kwamba umebuni yote haya mwenyewe, nitakuumiza."

Nina alizidi kuchanganyikiwa na anasema kwamba "alijipoteza."

Kwa sababu alitumia muda mwingi kitandani na mikono yake ikiwa imefungwa bandeji, polepole alipoteza nguvu za mwili. Hatimaye, madaktari walimpeleka katika kituo cha urekebishaji wa afya ili apate matibabu ya mazoezi ya viungo.

Akiwa huko, alijifunza kutembea tena na hata akampenda mvulana mmoja ambaye pia alikuwa mgonjwa katika kituo hicho.

Kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi, alianza kujihisi mwenye furaha.

Lakini kila kliniki ilipomruhusu kwenda nyumbani mwishoni mwa wiki, mama yake alimlazimisha tena kuvaa bandeji zilizokuwa zikimsababishia maumivu makali na akamzuia kabisa kutoka kitandani.

Mama yake alimwambia kwamba alikuwa na tatizo la moyo, na siku moja akamwambia,"utakufa."

"Hiyo ndiyo ilikuwa mara ya kwanza nilihisi kuwa niko peke yangu kabisa," Nina anasema, "kana kwamba nilikuwa nikianguka ndani ya shimo jeusi lisilo na mwisho."

'Tunataka kusaidiwa kufariki"

Kisha mambo yakaanza kubadilika.

Wakati alipolazwa hospitalini tena, Nina alikutana na daktari mpya wa watoto, Dk. Vrienten.

Daktari huyo alimwambia kwamba alitaka kumtafutia mahali ambapo wataalamu wangeweza kumsaidia kuboresha uwezo wa kusogeza viungo na maungo yake ili aweze kutembea tena.

Nina alishangaa sana.

Kwa miaka yote, mama yake alikuwa amemwambia kwamba alikuwa na ugonjwa wa misuli usiotibika ambao ungemuua. Moyoni alikuwa na mashaka, lakini hakuwahi kuthubutu kuuliza maswali.

Mama yake alikasirika sana. Waliporudi nyumbani, alimlazimisha kuweka miguu yake katika umbo la herufi X na akaifunga kwa mito ili ibaki katika hali hiyo. Pia alimnyima chakula cha kutosha, akaingiza bomba la kulishia kupitia puani, na kumlazimisha kumeza vidonge 20 kila siku.

Katika moja ya safari ya kumuona daktari, mama yake aliomba Nina afanyiwe euthanasia au kuuawa kwa huruma ili awache kuteseka. Nina, akiwa mgonjwa na amechoka kupita kiasi, alikubali.

"Daktari, nataka kufa," alimwambia. "Je, unaweza kunisaidia?"

Daktari alirudi nyuma, akazungumza kwa muda mfupi na mama yake, kisha akaagiza apewe dawa ya morphine kwa saa 24.

"Tutamfanya alale muda wote," Daktari alisema.

Kuokolewa

Lakini Dkt. Vrienten alikuwa ameunganisha vipande vyote vya fumbo la ugonjwa wake na kugundua ukweli, kisha akawasiliana na huduma za ulinzi wa watoto.

Siku moja, mwanamke mmoja aliingia katika chumba cha Nina na kumwambia kwamba alikuwa anampeleka katika hospitali nyingine. Nina alimsihi,

"Hapana, tafadhali. Acha nife."

Aligundua kwamba mama yake alikuwa ameanza kuingiwa na hofu. Maafisa wawili wa polisi walikuwa wamesimama karibu.

Muda mfupi baadaye, Nina aliwekwa kwenye machela na kupelekwa kwa gari la wagonjwa.

Bandeji ziliondolewa kwenye mikono na miguu yake. Kamera ya video iliwekwa ndani ya chumba chake.

Kwa siku mbili, hakumwona yeyote isipokuwa wazazi wake.

Walipokuja kumtembelea hatimaye, Nina aliendelea kuwaambia:

"Mimi si mgonjwa."

Alisema hivyo tena na tena mara 18 kwa jumla.

Mama yake alisahau kwamba kamera ilikuwa ikirekodi na akakasirika, jambo ambalo lilikuwa ushahidi wa yale yaliyokuwa yakitokea kwa miaka yote hiyo.

Kuanza maisha upya

Baada ya muda, Nina aliamua kukata mawasiliano yote na wazazi wake. Alihamishiwa katika kituo cha matibabu ambako alipokea tiba ya mwili na msaada wa kisaikolojia, na hatimaye akaanza maisha mapya katika mji mwingine akiwa na utambulisho tofauti.

Alianza maisha mapya: alihitimu kutoka shule ya sanaa, akapata kazi hatimaye akapata mchumba.

Wazazi wake hawakuwahi kukiri walichomfanyia na wakati fulani waliajiri mpelelezi binafsi ili kumtafuta. Jambo hilo lilimsababishia Nina msongo mkubwa wa mawazo na maumivu mapya.

Alifikiria kuwaripoti, jambo ambalo hakuna mtu aliyekuwa amefanya wakati alipookolewa. Lakini mwishowe aliachana na suala hilo, na miaka michache baadaye, wazazi wake wote wawili walifariki mmoja baada ya mwingine.

"Walichonifanyia wazazi wangu kilikuwa uhalifu," Nina anasema. "Ulikuwa unyanyasaji mkubwa dhidi ya mtoto, na nilinusurika kwa bahati sana."

Lakini anashukuru kwamba sasa yuko katika hali nzuri.

"Nina furaha sana kwamba nilinusurika, na kuna mambo mengi yanayonipa msukumo wa kuishi kila uchao."