Uganda yakubali mpango wa Marekani wa kuwaweka Wamarekani karantini kufuatia mlipuko wa Ebola
Uganda imethibitisha kuwa Marekani imeiomba nchi hiyo kuanzisha kituo maalumu cha kuwaweka karantini na kuwahudumia Wamarekani waliokumbana na virusi vya Ebola, huku hofu ikiongezeka kuhusu kuenea kwa mlipuko huo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Akizungumza katika mahojiano na BBC, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Uganda, Diana Atwine, amesema Kampala iko tayari kushirikiana katika mpango huo kutokana na uzoefu mkubwa wa nchi hiyo katika kukabiliana na milipuko ya Ebola.
“Ndiyo, walitufikia kuhusu kuanzisha kituo cha Ebola hapa. Tuko wazi kwa hilo. Tuna utaalamu mkubwa nchini,” alisema Dkt Atwine.
Kauli yake imekuja wakati Uganda ikiimarisha udhibiti mipakani baada ya watu wanaoshukiwa kuwa na Ebola kujaribu kuingia nchini humo kutoka maeneo yaliyoathirika zaidi mashariki mwa DRC.
“Siku tatu zilizopita tuliona wagonjwa wakijaribu kuvuka na kuingia nchini mwetu. Wana ndugu hapa ambao wamekuwa wakiwaambia kuwa wakifika Uganda watapata matibabu na kupona,” amesema.
Kwa mujibu wa Dkt Atwine, baadhi ya watu hao tayari walikuwa na dalili kali za Ebola na walikiri kupoteza ndugu zao kutokana na ugonjwa huo.
“Walikuwa wanatoka katika maeneo yaliyo kitovu cha mlipuko, walikuwa na dalili kubwa za Ebola na pia walikuwa wakikiri kuwa wamepoteza baadhi ya ndugu zao.”
Uganda ina hofu kuwa kuacha mipaka ikiwa wazi kutafanya iwe vigumu kudhibiti maambukizi hayo.
“Tuligundua kuwa tukiendelea kuweka mipaka wazi hatutaweza kuudhibiti mlipuko huu,” aliongeza.
Serikali ya Uganda pia imesema inashirikiana na DRC kuanzisha vituo vya upimaji na matibabu karibu na maeneo ya mpakani ili kupunguza watu kuvuka mipaka wakitafuta huduma za afya.
“Tunafanya kazi pia na DRC kuanzisha vituo vya upimaji na matibabu upande wa mpakani kwa watu wanaotafuta huduma za afya na wanaojaribu kuvuka mpaka.”
Hatua hizo zinakuja wakati Shirika la Afya Duniani likiendelea kuhimiza juhudi za haraka kudhibiti mlipuko huo wa Ebola ambao umeibua wasiwasi mkubwa wa kiafya katika eneo la Afrika ya Kati na Mashariki.
Soma zaidi: