Leo Juni 30, 2026 ni mwisho wa muda ambao Tanzania na Kenya zilijiwekea kuondoa vikwazo visivyo vya ushuru vinavyokwamisha biashara kati ya nchi hizo mbili.
Hatua hiyo inalenga kuongeza biashara, uwekezaji na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Eneo huru la biashara barani Afrika (AfCFTA).
Ahadi hiyo ilitolewa Mei 4 mwaka huu na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Kenya, William Ruto, wakati wa Jukwaa la Biashara la Tanzania na Kenya lililofanyika Dar es Salaam.
Viongozi hao waliagiza taasisi zinazohusika na biashara, forodha na mipaka kuhakikisha vikwazo vilivyosalia vinaondolewa ifikapo Juni 30.
"Ni lazima tuondoe kwa haraka vikwazo visivyo vya ushuru, ikiwemo ucheleweshaji mipakani, kutokuwiana kwa viwango na vikwazo vya upatikanaji wa masoko," alisema Rais Ruto.
Aliongeza kuwa nchi hizo mbili zimeweka lengo la kuongeza biashara mpya yenye thamani ya dola bilioni moja pamoja na uwekezaji wa kuvuka mipaka wa dola milioni 504.
Kwa upande wake, Rais Samia alisema Tanzania itaendelea kuboresha mifumo ya forodha kwa njia ya kidijitali na kuanzisha dirisha la siku 30 la kushughulikia migogoro ya wafanyabiashara kupitia Baraza la Pamoja la Biashara la Tanzania na Kenya.
Vikwazo visivyo vya ushuru ni pamoja na ucheleweshaji wa mizigo mipakani, ukaguzi unaojirudia wa bidhaa, tofauti za viwango vya ubora, mabadiliko ya ghafla ya leseni na taratibu za forodha.
Kwa mujibu wa wadau wa biashara, changamoto hizo huongeza gharama za bidhaa kwa kati ya asilimia 10 hadi 40.
Jitihada za kuviondoa si za leo.
Mwaka 2022, mawaziri wa biashara na uwekezaji wa Tanzania na Kenya walitambua vikwazo 68 vya biashara. Kufikia mwaka huu, 54 vilikuwa vimeondolewa, huku vingine vinne vikiondolewa Oktoba mwaka jana. Serikali zilisema vilivyosalia ndivyo vilivyolengwa kuondolewa ifikapo leo.
Utafiti wa mwaka 2024 uliofanywa na Yohana Hasinati D. ulibaini kuwa vikwazo vya kiutawala bado vinaendelea katika eneo la Namanga. Utafiti huo ulieleza kuwa kutokuaminiana kati ya taasisi, hatua za kulipizana kisera, masuala ya kisiasa na tofauti za kodi vinaendelea kuchangia changamoto hizo, na kupendekeza utekelezaji kamili wa Itifaki ya Soko la Pamoja la Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa Baraza la Biashara Afrika Mashariki (EABC), licha ya kuwepo kwa Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki tangu mwaka 2005, tofauti za kanuni na ucheleweshaji katika vituo vya mipakani bado vinaathiri biashara.
Hatua hiyo inakuja wakati biashara kati ya nchi hizo mbili ilipopungua kwa mara ya kwanza ndani ya muongo mmoja. Takwimu za Kenya National Bureau of Statistics (KNBS) Economic Survey 2026 zinaonyesha biashara kati ya Tanzania na Kenya ilishuka kwa asilimia 9.4 mwaka 2025, kutoka shilingi za Kenya bilioni 125.9 mwaka 2024 hadi shilingi bilioni 114.1.
Mmoja wa wafanyabiashara wa mahindi kutoka Moshi anayesafirisha mazao yake kwenda Kenya ana matumaini kuwa kuondolewa kwa vikwazo hivyo kutarahisisha biashara.
"Tutafarijika kama vikwazo vyote vitaondolewa.
Kenya na Tanzania ni ndugu; ni watu mmoja waliotenganishwa na mipaka ya kikoloni. Tukirahisishiwa biashara, sote tutanufaika na kuinuka kiuchumi," anasema.
Sekta binafsi kupitia EABC pia imezitaka serikali mbili kuharakisha utekelezaji wa makubaliano hayo.
"Kuna haja ya kuchukua hatua za haraka kuondoa vikwazo visivyo vya ushuru, kuboresha utabirikaji wa sera, kuoanisha viwango na kuharakisha taratibu za forodha ili kuongeza ushindani wa biashara katika ukanda," limesema Baraza hilo.
Hata hivyo, hadi kufikia leo haijawekwa wazi iwapo vikwazo vyote vilivyokuwa vimesalia vimeondolewa kama ilivyoahidiwa.