Zaidi ya watu 160 wamefariki nchini Nepal, huku mamia ya watalii wakiwa hawajulikani walipo baada ya mafuriko makubwa ya ghafla na maporomoko ya udongo katika eneo la mpaka kati ya Nepal na Tibet.
Nchini China, idadi ya watu ambao hawajulikani walipo baada ya maporomoko ya udongo katika kaunti ya Gyirong, Tibet, imefikia 558, kwa mujibu wa shirika la utangazaji la serikali CCTV.
Kati yao, 260 ni raia wa kigeni. Idadi ya waliofariki imeendelea kuwa watatu.
Mpaka wa Gyirong ni njia kuu inayotumiwa na watalii na magari kusafiri kati ya China na Nepal.
Nepal awali ilisema watu 579 hawajulikani walipo, wakiwemo raia 466 wa kigeni. Haijafahamika mara moja iwapo baadhi ya watu hao wamehesabiwa mara mbili katika takwimu za nchi hizo mbili.
Jeshi la Nepal limetuma wanajeshi 2,000 kushiriki katika shughuli za utafutaji na uokoaji kwa njia ya ardhini na angani katika maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko.
Msemaji wa jeshi, Brigedia Jenerali Rajaram Basnet, ameiambia BBC kuwa wanajeshi hao wamejikita katika maeneo yaliyoathirika zaidi, yakiwemo wilaya za Rasuwa na Nuwakot.
Jeshi hadi sasa limefanikiwa kuwaokoa watu 97 waliokuwa wamekwama kwenye mafuriko. Watatu kati yao walikuwa wafanyakazi waliokwama katika handaki la mradi wa kuzalisha umeme wa maji wa Trishuli A.
Polisi na kikosi cha polisi wenye silaha cha Nepal pia vimepeleka maafisa katika maeneo yaliyoathiriwa kusaidia shughuli za utafutaji.
Awali mamlaka zilidhani kuwa huenda tetemeko la ardhi lilitangulia mafuriko hayo. Hata hivyo, Utafiti wa Jiolojia wa Marekani, USGS, sasa umesema nishati iliyosababisha mtikisiko huo ilitokana na maporomoko ya udongo, badala ya tetemeko la ardhi.