Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Iran yaishutumu Marekani kwa kushambulia miundombinu ya kiraia
Tehran inasema mashambulio ya Marekani yalilenga madaraja, huku Marekani ikidhibiti meli katika Mlango wa Bahari wa Hormuz.
Muhtasari
- Iran yaishutumu Marekani kwa kushambulia miundombinu ya kiraia
- Wanajeshi wa Kuwait wajeruhiwa katika shambulio la Iran
- Mwanamume ashtakiwa Uingereza kwa kushirikiana na Iran kijasusi
- Marekani yafanya mashambulizi mapya, Iran ikisema miundombinu ya kiraia ililengwa
- Mshawishi wa TikTok wa Ghana afungwa jela kwa kueneza taarifa za uongo kumhusu rais
- IRGC: Tumeshambulia meli kadhaa za mafuta na ndege za kivita za Marekani nchini Jordan
- Wamarekani saba wawekwa karantini katika kituo cha Ebola nchini Kenya
- Iran yazionya nchi za Ghuba dhidi ya kuruhusu Marekani kutumia ardhi yake kushambulia Iran
- Kombe la Dunia kusafirishwa kwa sanduku maalum la Louis Vuitton
- JD Vance aishutumu Israel kwa kujaribu kushawishi Wamarekani kuendeleza vita dhidi ya Iran
- Takriban wanafunzi 19 wafariki dunia katika ajali ya basi la shule mashariki mwa Uganda
- Wahouthi watishia kulenga miundombinu ya mafuta ya Saudi Arabia
- Pakistan yasema upatanishi wa Marekani na Iran umekwama
- Trump: Matokeo ya vita dhidi ya Iran yatajulikana hivi karibuni
- Marekani yaendelea na mashambulizi dhidi ya Iran huku miundombinu ya Bandar Abbas ikilengwa
Moja kwa moja
Na Mariam Mjahid & Ambia Hirsi
Iran yaishutumu Marekani kwa kushambulia miundombinu ya kiraia
Iran imeishutumu Marekani kwa kushambulia miundombinu ya kiraia katika wimbi la hivi punde la mashambulizi ya anga tangu mazungumzo ya amani yalipovunjika.
Vyombo vya habari vya serikali na mamlaka za mikoa zinasema kuwa madaraja, kituo cha treni na uwanja wa ndege vilishambuliwa. Kitengo cha BBC Verify kimethibitisha shambulio dhidi ya daraja moja katika mkoa wa Hormozgan.
Kamandi Kuu ya Marekani (Centcom) haijatoa orodha ya maeneo yaliyolengwa, lakini imesema mashambulizi hayo yalilenga "kudhoofisha uwezo wa kijeshi wa Iran".
Rais Donald Trump ametishia kushambulia madaraja na vituo vya kuzalisha umeme vya Iran ili kuishinikiza Tehran kurejea kwenye mazungumzo ya kumaliza vita vilivyoanza tarehe 28 Februari kwa mashambulizi ya Marekani na Israel—hatua iliyochochea Iran kulipiza kisasi dhidi ya Israel na mataifa ya uarabuni ambayo ni washirika wa Marekani katika eneo la Ghuba.
Kwa usiku sita mfululizo, Marekani imekuwa ikifanya mashambulizi ya anga dhidi ya Iran.
Soma pia:
Wanajeshi wa Kuwait wajeruhiwa katika shambulio la Iran
Kuwait imetangaza kuwa baadhi ya wanajeshi wake walijeruhiwa katika shambulio la ndege isiyo na rubani ya Iran.
Saa moja iliyopita, Kuwait ilisema kuwa kituo chake cha kusafisha maji ya bahari na kituo cha kuzalisha umeme vimeharibiwa katika mashambulio ya Iran.
Awali, Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi wa Mapinduzi ya Iran IRGC kilitangaza katika taarifa kwamba kilishambulia vikosi vya Marekani nchini Kuwait katika "Awamu ya 15 ya Operesheni Nasr 2."
Huku hayo yakijiri Kamanda wa vikosi vya anga vya IRGC ameonya kwamba mashambulizi ya Iran yataendelea hadi "utulivu urejee kwenye ukanda wa pwani wa kusini na Mlango-Bahari wa Hormuz."
Awali IRGC ilitangaza kuwa limeshambulia vituo vya ijeshi vya Marekani vkatika mataifa ya Oman, Kuwait, Jordan, Qatar na Syria kulipiza kisasi mashambulizi ya Marekani.
Duru mpya ya mashambulizi ya Marekani dhidi ya Iran ilianza tarehe 6 Julai kujibu mashambulizi ya meli kadhaa katika Mlango wa Bahari wa Hormuz.
Tangu wakati huo, Iran imefanya mashambulizi ya kulipiza kisasi ambayo inasema yanalenga maslahi ya Marekani katika eneo la Ghuba.
Maelezo zaidi:
Mwanamume ashtakiwa Uingereza kwa kushirikiana na Iran kijasusi
Mwanamume mmmoja aliye na umri wa miaka 39 ameshtakiwa nchini Uingereza kwa kushirikiana na idara ya ujasusi ya Iran.
Hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa. Wahid Abri, mkaazi wa Liverpool, alikamatwa siku ya Jumatano (Julai 15) kufuatia uchunguzi wa polisi wa kupambana na ugaidi uliofanyika Birmingham, na kupelekwa katika kituo cha polisi huko West Midlands.
Maafisa wa polisi walifanya upekuzi katika maeneo kadhaa huko Birmingham na Liverpool kama sehemu ya uchunguzi wao.
Bw. Abri ameshtakiwa kwa kushirikiana na idara ya ujasusi ya kigeni chini ya Sheria ya Usalama wa Taifa ya Uingereza ya mwaka 2023 na anatarajiwa kufikishwa mahakamani.
"Katika miaka ya hivi karibuni, kiwango cha shughuli zetu za uchunguzi wa usalama wa taifa kimeimarishwa kwa kiasi kikubwa," alisema Helen Flanagan, mkuu wa kitengo cha polisi wa kupambana na ugaidi jijini London.
"Kesi hii ni mfano mwingine wa juhudi zetu za kuzuia shughuli zenye utata zinazohusishwa na idara za ujasusi za kigeni," aliongeza.
Bi. Flanagan pia alisema: "Mtu mmoja tayari ameshtakiwa lakini hatuwezi kutoa maelezo zaidi kuhusu mashtaka hayo. Hata hivyo, ningependa kuuhakikishia umma kwamba hakuna tishio la moja kwa moja dhidi ya raia, kundi lolote katika jamii au mtu yeyote ambalo limebainishwa katika uchunguzi huu."
Marekani yafanya mashambulizi mapya, Iran ikisema miundombinu ya kiraia ililengwa
Jeshi la Marekani limefanya wimbi la mashambulizi dhidi ya Iran kwa usiku wa sita mfululizo, huku pande hizo mbili zikipambana kudhibiti Mlango-Bahari wa Hormuz.
Kamandi Kuu ya Marekani (Centcom) ilisema mashambulizi hayo yalilenga "kudhoofisha uwezo wa kijeshi wa Iran," na baadaye ikatangaza kuwa ilipanda na kukagua meli moja ikiwa ni sehemu ya hatua yake ya kuzuia meli kuingia na kutoka katika bandari za Iran.
Vyombo vya habari vya serikali na mamlaka za mikoa viliripoti kuwa Marekani ilishambulia miundombinu ya kiraia, ikiwemo madaraja, kituo cha treni na uwanja wa ndege.
Kitengo cha BBC Verify kimethibitisha shambulio dhidi ya daraja moja magharibi mwa Bandar Abbas katika mkoa wa Hormozgan.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) linasema limejibu mashambulizi hayo kwa kushambulia vituo vya rada vya ufuatiliaji wa shuguliza baharini vya Marekani nchini Oman, pamoja na maeneo mengine nchini Kuwait na Bahrain.
Pia linadai kushambulia kituo cha amri cha operesheni maalum za Marekani nchini Syria.
IRGC ilisema shambulio la kushtukiza dhidi ya eneo la al-Tanf nchini Syria, karibu na mpaka na Jordan, lilikuwa ni jibu la kulipiza kisasi mauaji ya askari wa Iran yaliyotokea siku mbili zilizopita.
Hata hivyo chanzo cha kijeshi nchini Syria kimepinga madai hayo ya IRGC kwa mujibu wa shirika la habari la AFP.
"Tunakanusha shambulio lolote la mabomu la Iran linalolenga eneo la Tanf," kilisema chanzo hicho ambacho hakikutajwa jina.
Huku hayo yakijiri Jeshi la Jordan limesema lkuwa lilidungua makombora matatu ya Iran, na hakuna majeruhi wala uharibifu wowote ulioripotiwa.
Kwa mujibu wa televisheni ya taifa, IRGC ilidai kushambulia ndege za kivita za Marekani zilizokuwa katika nchi hiyo ya Ghuba.
Soma zaidi:
Mshawishi wa TikTok wa Ghana afungwa jela kwa kueneza taarifa za uongo kumhusu rais
Mshawishi mmoja wa TikTok nchini Ghana amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja gerezani baada ya kukiri makosa ya kusambaza taarifa za uongo kupitia machapisho aliyotoa kumhusu Rais John Mahama.
Mwezi uliopita na mwanzoni mwa mwezi huu, Camilla Alhassan alichapisha video kadhaa mtandaoni akidai, bila kutoa ushahidi, kwamba rais alitoa kafara ya ng'ombe 32 kama sehemu ya tambiko la kumsaidia kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2024.
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 43 pia alidai kuwa mpango wa serikali wa kugawa pedi kwa waathiriwa wa hivi karibuni wa mafuriko ulikuwa jaribio la kuficha jambo alilodai kuwa rais alilifanya.
Jaji alitupilia mbali ombi la kupunguziwa adhabu, kuamua kuwa adhabu ya kifungo gerezani itasaidia kuzuia mwenendo kama huu siku zijazo.
Waendesha mashtaka walikuwa wamesema kuwa Alhassan, ambaye ana wafuasi zaidi ya 70,000 kwenye mtandao wa TikTok, alitoa madai kadhaa ya uongo na ya kuchafulia sifa rais.
Video zake zilizosambazwa sana, na kumfanya Alhassan kukamatwa mapema mwezi huu, zilichochea mjadala mpya nchini Ghana kuhusu taarifa potofu kwenye mitandao ya kijamii na jinsi ya kuweka uwiano kati ya adhabu za kisheria na uhuru wa kujieleza.
Jaji alisema kuwa adhabu hiyo itasaidia kudhibiti kuenea kwa taarifa za uongo, mwenendo ambao umezidi kuongezeka kwenye mitandao ya kijamii.
Hii si mara ya kwanza kwa mtu mwenye ushawishi mkubwa mtandaoni (influencer) kufungwa jela nchini Ghana.
IRGC: Tumeshambulia meli kadhaa za mafuta na ndege za kivita za Marekani nchini Jordan
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislam ya Iran IRGC linasema kuwa limeshambulia ndege za kivita za Marekani nchini Jordan kwa makombora na ndege zisizo na rubani kujibu mashambulizi ya Marekani ya Alhamisi usiku.
Taarifa kutoka kwa kitengo cha uhusiano wa umma ya IRGC ilisema kwamba vikosi vyake "katika wimbi la 14 la Operesheni ya Nasr 2... vililenga ndege za kivita za Marekani na meli za kivita zilizokuwa Jordan kwa makombora kadhaa ya balistiki na ndege kadhaa zisizo na rubani, katika tukio ambalo liliwasababishia uharibifu mkubwa."
IRGC iliishutumu Marekani kwa "kutumia kambi zake nchini Jordan kufanya uhalifu mkubwa wa kivita jana usiku kwa kushambulia miundo mbinu ya kiraia, ikiwa ni pamoja na madaraja kadhaa, maeneo ya makazi, na kituo cha usafirishaji maji huko Bandar Abbas kusini mwa Iran."
IRGC pia ilitangaza kufanya shambulio lingine dhidi ya vikosi vya Marekani nchini Kuwait katika "Wimbi la 15 la Operesheni ya Nasr 2."
Wamarekani saba wawekwa karantini katika kituo cha Ebola nchini Kenya
Wafanyakazi saba wa misaada kutoka Marekani, ambao walikuwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kusaidia juhudi za kukabiliana na mlipuko wa Ebola, wamewekwa karantini nchini Kenya baada ya serikali ya Marekani kuweka masharti mapya ya usafiri kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters na mkuu wa shirika la misaada la Marekani lililowaajiri.
Wafanyakazi hao wa misaada ni wa kwanza kuwekwa karantini katika kituo hicho, ambacho ujenzi wake ulipingwa vikali nchini Kenya na kesi dhidi yake inaendelea mahakamani, baada ya jaji kuamuru shughuli katika za kuistishwa hadi uamuzi utakapotolewa.
Licha ya agizo hilo la mahakama kituo hicho kimeendelea na shughuli zake, kulingana na maafisa wa Marekani na picha za satelaiti zilizochunguzwa na Reuters.
Sera mpya ya Washington inaeleza kuwa raia wa Marekani wanaorejea kutoka DR Congo, ambako kuna mlipuko wa Ebola, lazima wakae kwa wiki tatu katika nchi ya tatu kabla ya kuingia Marekani.
Mwezi uliopita, Waziri wa Afya wa Kenya Adan Duale alitangaza kusimamishwa mara moja kwa ujenzi wa kituo hicho baada ya serikali kupatikana na hatia ya kupuuza mahakama kwa kushindwa kutii amri za kusimamisha ujenzi wa kituo hicho cha karantini.
Unaweza kusoma:
Iran yazionya nchi za Ghuba dhidi ya kuruhusu Marekani kutumia ardhi yake kushambulia Iran
Iran imezionya nchi za Ghuba dhidi ya kuruhusu Marekani kutumia ardhi, anga au maji yake kuanzisha mashambulizi dhidi ya Iran, ikisema hatua hiyo itakuwa na matokeo makubwa kwa mataifa husika.
Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Ndani ya Bunge la Iran, Mohammad Saleh Jokar, amesema iwapo Marekani itatumia eneo la nchi hizo kushambulia Iran, zitakabiliwa na “gharama kubwa sana” kutokana na uamuzi huo.
Wakati huo huo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema kurejeshwa kwa vizuizi vya shughuli za majini ni sehemu nyingine ya kile ilichokitaja kuwa ukiukaji wa makubaliano kati ya Tehran na Washington.
Katika taarifa yake, wizara hiyo pia iliishutumu Marekani kwa kile ilichodai ni uhalifu wa kivita, ikitaja mashambulizi dhidi ya miundombinu na huduma za kiraia.
Iran iliorodhesha miongoni mwa maeneo yaliyolengwa kuwa ni kituo cha matibabu cha Kikosi cha 388 cha Jeshi la Iran mjini Bampour, eneo la kuhifadhi nafaka la Hoveizeh na mnara wa ulinzi wa wanamaji wa Chabahar.
Aidha, Tehran imedai kuwa hii ni mara ya tatu ndani ya mwaka mmoja kwa Marekani kuishambulia Iran wakati mazungumzo kati ya pande hizo yakiendelea.
Iran imezitaka nchi za eneo hilo kutoruhusu ardhi, anga au maji yake kutumiwa katika mashambulizi dhidi yake, ikisema inalenga kuimarisha uelewano na ushirikiano wa kikanda bila uwepo au kuingiliwa na Marekani.
Jokar pia amezitaka nchi za Ghuba kujifunza kutokana na kile alichokiita “uzoefu wa Vita vya Ramadhani” na kutozikabidhi ardhi na fukwe zao kwa majeshi ya Marekani.
Pia Soma:
Kombe la Dunia kusafirishwa kwa sanduku maalum la Louis Vuitton
Kombe la Dunia litawasili katika uwanja wa New York New Jersey likiwa ndani ya sanduku maalum lililobuniwa na kampuni ya kifahari ya Louis Vuitton, ambayo imeendelea kuaminiwa na FIFA kubuni kifaa cha kubebea moja ya tuzo zenye hadhi kubwa zaidi katika mchezo wa soka.
Sanduku hilo limepambwa kwa herufi ya dhahabu V, inayowakilisha neno Victory yaani ushindi, pamoja na jina la kampuni hiyo. Pia lina nembo maarufu ya Louis Vuitton na kingo za shaba zilizopakwa dhahabu.
Kwa ndani, sanduku hilo limefunikwa kwa ngozi ya rangi ya beige na lina alama maalum ya kuadhimisha ushirikiano kati ya FIFA na Louis Vuitton.
Hii ni mara ya tano mfululizo kwa kampuni hiyo ya Ufaransa kubuni sanduku la kubebea Kombe la Dunia, baada ya kufanya hivyo katika fainali za mwaka 2010, 2014, 2018 na 2022.
"Mashirikiano ya Louis Vuitton na FIFA kwa zaidi ya muongo mmoja yamejengwa juu ya dhamira ya pamoja ya ubora na imani kwamba michezo ina uwezo wa kuhamasisha na kuwaunganisha watu duniani," alisema Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Louis Vuitton, Pietro Beccari.
Kwa muda mrefu, kampuni za bidhaa za kifahari zimekuwa zikijenga ushirikiano na michezo ya kiwango cha juu. Louis Vuitton pia hutengeneza masanduku maalum ya kubebea makombe ya Formula One, huku Tiffany and Co. ikiwa imetengeneza Kombe la Vince Lombardi linalotolewa kwa mabingwa wa Super Bowl tangu mwaka 1967.
Kombe la Dunia, ambalo kwa kawaida huhifadhiwa katika Makumbusho ya FIFA mjini Zurich, ni kombe moja pekee linalotolewa kwa mabingwa wa dunia kila baada ya miaka minne. Hivyo, jukumu la kubuni sanduku lake maalum la usafirishaji linaendelea kuwa moja ya heshima kubwa katika ushirikiano kati ya FIFA na Louis Vuitton.
Soma Zaidi:
JD Vance aishutumu Israel kwa kujaribu kushawishi Wamarekani kuendeleza vita dhidi ya Iran
Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance amesema baadhi ya maafisa wa serikali ya Israel wanajaribu kuishawishi Marekani kuendeleza vita dhidi ya Iran.
Katika mahojiano yaliyochapishwa Jumatano kwenye podikasti ya The Joe Rogan Experience, Vance amesema ana imani na baadhi ya viongozi wa Israel lakini akadai wengine “wanacheza michezo ya kisiasa na kujaribu kuwavuta Wamarekani katika vita visivyo na mwisho.”
Vance alisema anaamini wasikilizaji wameelewa kile alichokiita "mpango wa siri na wa gharama kubwa" unaolenga kuvuruga mazungumzo na kuzuia kufikiwa kwa makubaliano kati ya Marekani na Iran.
"Nina hakika mmeona mpango huu wa siri na wa gharama kubwa unaolenga kuvuruga mazungumzo na kuzuia kufikiwa kwa makubaliano," alisema.
Mwezi uliopita, Marekani na Iran zilitangaza kuwa zimefikia makubaliano ya awali ya kuendelea na mazungumzo. Kwa mujibu wa taarifa hizo, pande hizo pia zilikubaliana kufanyia kazi mpango wa usitishaji mapigano wa siku 60 na hatua za kufungua tena Mlango wa Hormuz, ingawa mazungumzo hayo yamekuwa yakikumbwa na changamoto.
Serikali ya Israel haikutoa tamko la haraka kujibu kauli hizo.
Vance amesema ni jambo la kawaida katika mahusiano ya kimataifa kwa maafisa wa nchi washirika kujaribu kushawishi sera za Marekani, lakini akasisitiza kuwa wasiwasi wake ni iwapo maafisa wa Marekani watakubali shinikizo hilo.
Kauli hizo zinakuja wakati utawala wa Donald Trump ukiendelea kutafuta njia ya kumaliza mzozo na Iran kupitia mazungumzo au hatua za kijeshi.
Wakati huo huo, Baraza la Wawakilishi la Marekani limekataa pendekezo la kupunguza mabilioni ya dola ya msaada wa Marekani kwa Israel.
Pia Soma:
Takriban wanafunzi 20 wafariki dunia katika ajali ya basi la shule mashariki mwa Uganda
Takriban wanafunzi 20 wamefariki dunia baada ya basi la King David Junior School, Ndejje kupata ajali usiku wa kuamkia leo katika wilaya ya Kapchorwa, mashariki mwa Uganda, mamlaka zimesema.
Basi hilo lilikuwa likiwarejesha wanafunzi kutoka ziara ya masomo Alhamisi usiku lilipodaiwa kupata hitilafu ya kiufundi majira ya saa mbili usiku.
Kwa mujibu wa taarifa za awali za polisi, dereva alipoteza udhibiti wa basi kabla ya kugonga, na kusababisha ajali hiyo mbaya.
"Uchunguzi wa awali unaashiria kuwa basi lilipoteza mwelekeo kutokana na hitilafu ya kiufundi. Pia tumebaini kupitia ushahidi wa mashuhuda kuwa gari hilo lilisimama mara kadhaa kabla ya ajali kutokea," polisi walisema katika taarifa iliyotumwa kwa mitandao ya kijamii.
Shughuli za uokoaji zinaendelea huku majeruhi wakipelekwa katika vituo vya afya vilivyo karibu.
Uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo halisi cha ajali hiyo.
Ajali hiyo imezua simanzi nchini Uganda, wakati familia za wanafunzi na viongozi wa shule wakisubiri taarifa rasmi kuhusu hatima ya waliokuwa ndani ya basi hilo.
Wahouthi watishia kushambulia miundombinu ya mafuta ya Saudi Arabia
Waasi wa Kihouthi nchini Yemen wameionya Saudi Arabia kuwa watalenga miundombinu ya mafuta na maeneo mengine muhimu iwapo mapigano kati ya pande hizo yataongezeka.
Kiongozi wa Wahouthi, Abdulmalik Al Houthi, amesema iwapo Saudi Arabia itaanzisha mashambulizi makubwa dhidi ya Yemen na kuzidisha mzozo huo, vituo vyake vya mafuta na maeneo mengine muhimu vitakuwa shabaha ya makombora na ndege zisizo na rubani za Wahouthi.
“Endapo Saudi Arabia itaanzisha mashambulizi makubwa dhidi ya nchi yetu na kuchochea mivutano, vituo vyake vyote vya mafuta na maeneo muhimu vitakuwa malengo ya makombora na ndege zetu zisizo na rubani,” alisema.
Wahouthi wameishutumu Saudi Arabia kwa kushambulia Uwanja wa Ndege wa Sanaa Jumatatu, wakisema hatua hiyo ilikuwa jibu la shambulio lililolenga uwanja wa ndege nchini Saudi Arabia.
Mashambulizi ya pande hizo yameelezwa kuwa makubwa zaidi tangu makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa mwaka 2022.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, Abdulmalik Al Houthi pia ametishia kuushambulia Uwanja wa Ndege wa Riyadh iwapo mashambulizi zaidi yatafanywa dhidi ya Uwanja wa Ndege wa Sanaa.
“Kanuni ni hii: shamba likilengwa, nasi tutalenga shamba; bandari ikilengwa, nasi tutalenga bandari. Na tutaijibu hali ya mzingiro kwa mzingiro,” alisema.
Serikali ya Yemen yenye makao yake mjini Aden, inayoungwa mkono na Saudi Arabia, imesema shambulio la Jumatatu dhidi ya Uwanja wa Ndege wa Sanaa lililenga kuzuia ndege kutoka Iran kutua katika uwanja huo.
Kwa zaidi ya muongo mmoja, ndege zote zinazoingia katika anga ya Yemen zimekuwa zikihitaji kibali kutoka muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia.
Serikali ya Yemen na washirika wake wanadai Wahouthi na Iran wamekuwa wakikiuka utaratibu huo kwa kuanzisha safari za moja kwa moja za ndege kutoka Iran kuelekea Sanaa.
Unaweza Kusoma Pia:
Pakistan yasema upatanishi wa Marekani na Iran umekwama
Pakistan imesema juhudi zake za kupatanisha Marekani na Iran zinakabiliwa na changamoto kutokana na kuongezeka kwa mivutano kati ya mataifa hayo mawili, lakini mchakato huo haujasitishwa.
Akizungumza katika mkutano wa kila wiki na wanahabari mjini Islamabad, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan, Tahir Andrabi, alikanusha madai kwamba Islamabad imeachana na jukumu lake la upatanishi baada ya mivutano kuzidi.
“Tunatumaini mantiki ya amani na mazungumzo ndiyo itakayoshinda mwishowe,” alisema Andrabi.
Aliongeza kuwa mchakato wa amani haukomi kabisa, bali unaweza kusimama kwa muda kabla ya kuendelea tena.
Kwa mujibu wa Andrabi, misingi iliyowekwa katika Hati ya Makubaliano ya Islamabad kati ya Marekani na Iran bado ipo, na inaweza kutumika kurejesha mazungumzo pindi pande husika zitakapoona kuwa kuendelea kwa mivutano hakutaleta suluhisho.
Pakistan imezitaka tena pande zote kujizuia na kuepuka hatua zozote zinazoweza kuzidisha mivutano na kuhatarisha amani na utulivu wa eneo hilo.
Andrabi alisema Hati ya Makubaliano ya Islamabad, iliyowezeshwa na Pakistan, ni mfumo wa kudumu wa kukuza amani, kuheshimiana na ustawi wa pamoja, huku Islamabad ikiendelea kuhimiza kurejelewa kwa mazungumzo katika ngazi ya wataalamu.
Pia alieleza matumaini kuwa pande zote zitaendelea kujikita katika njia ya mazungumzo na diplomasia ili kutatua masuala yaliyosalia.
Akizungumzia kufungwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz kufuatia mashambulizi ya Marekani na Iran dhidi ya kila upande, Andrabi alisema Pakistan inatumaini hali itarejea kuwa ya kawaida haraka na kusisitiza umuhimu wa kuhakikisha usalama wa njia hiyo muhimu ya kimataifa ya usafirishaji baharini.
Pia Soma:
Trump: Matokeo ya vita dhidi ya Iran yatajulikana hivi karibuni
Rais wa Marekani Donald Trump amesema matokeo ya vita vinavyoendelea dhidi ya Iran yatajulikana hivi karibuni, akidai kuwa Marekani na Israel zinaendelea kupata mafanikio katika operesheni zao za kijeshi.
Akizungumza katika hotuba yake, Trump alisema Marekani ina mkono wa juu katika mapambano hayo.
“Mtaona matunda ya juhudi hizi hivi karibuni sana,” alisema. Trump pia alidai kuwa, “Tunashinda ushindi mkubwa dhidi ya Iran.”
Hata hivyo, hakufafanua alichomaanisha kwa kauli hiyo wala kutoa ushahidi unaounga mkono madai yake.
Kauli zake zimejiri wakati mapigano kati ya Iran, Marekani na Israel yakiendelea kushuhudia mashambulizi ya pande zote, huku Iran ikiwa haijatoa jibu la haraka kuhusu matamshi ya Trump.
Maelezo zaidi:
Marekani yaendelea na mashambulizi dhidi ya Iran huku miundombinu ya Bandar Abbas ikilengwa
Marekani imeanzisha wimbi la sita la mashambulizi ya anga dhidi ya Iran, yakilenga uwanja wa ndege, kituo cha reli na madaraja kadhaa kusini mwa nchi karibu na Mlango Bahari wa Hormuz, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya Iran.
Shirika la habari la Tasnim limeripoti kuwa ndege za kivita za Marekani zilirusha makombora yaliyolenga Uwanja wa Ndege wa Iranshahr, bila kutoa taarifa kuhusu kiwango cha uharibifu au iwapo kulikuwa na majeruhi.
Shirika rasmi la habari la Iran na televisheni ya taifa vilisema milipuko mitatu ilisikika karibu na uwanja huo wa ndege, vikiongeza kuwa angalau kombora moja la Marekani lilipiga uwanja huo.
Wakati huo huo, shirika la habari la Fars liliripoti kuwa daraja katika mji wa Bandar Khamir lililengwa katika shambulio la Marekani.
Tasnim pia lilisema mashambulizi ya Marekani yalilenga madaraja matatu katika eneo la Khamir, mkoani Hormozgan.
Mojawapo ya madaraja hayo linaunganisha Bandar Abbas na mji wa Lar katika mkoa wa Fars.
Kwa mujibu wa Tasnim, mashambulizi hayo yalisababisha kukatika kwa umeme katika baadhi ya maeneo na kuvuruga huduma za mawasiliano ya simu. Marekani haijatoa tamko rasmi kuhusu mashambulizi hayo wala madai yaliyotolewa na vyombo vya habari vya Iran.
Maelezo zaidi:
Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja