Kenya yapata leseni ya kutengeneza dawa mpya ya kuzuia HIV
Kenya imepewa leseni ya kutengeneza dawa mpya ya kuzuia maambukizi ya virusi vya HIV kwa ajili ya soko la Afrika, hatua inayoiweka miongoni mwa nchi tatu za kwanza barani kushiriki katika uzalishaji wa dawa hiyo tangu hatua za awali za maendeleo yake.
Kampuni ya dawa ya Merck ilitangaza kuwa imezipa kampuni saba duniani leseni za kutengeneza toleo la bei nafuu la dawa ya kila mwezi ya kuzuia HIV inayojulikana kama alimatravir, iwapo itathibitishwa kuwa salama na yenye ufanisi baada ya kukamilika kwa majaribio ya kitabibu yanayoendelea. Miongoni mwa kampuni hizo ni Universal Corporation Limited (UCL) ya Kenya.
Hatua hiyo ni ya kwanza kwa wazalishaji wa Afrika kushirikishwa katika leseni za dawa ya HIV tangu mwanzo wa mchakato wa maendeleo ya dawa hiyo, badala ya kusubiri baada ya kuidhinishwa rasmi.
Majaribio ya hatua ya mwisho ya alimatravir yanaendelea nchini Kenya, Uganda na Afrika Kusini yakihusisha wasichana na wanawake vijana. Utafiti huo unafanywa kwa ushirikiano na taasisi mbalimbali za afya, ukiwemo Kemri, huku ushahidi wa kisayansi ukikusanywa barani Afrika ambako dawa hiyo inatarajiwa kutumika kwa kiwango kikubwa.
Leseni hizo hazitozwi mrabaha na zinahusu nchi 129 zenye kipato cha chini na cha kati. Merck pia imesema itatoa akiba ya awali ya dawa hiyo kwa bei isiyoleta faida ili kuhakikisha upatikanaji wa haraka endapo majaribio yatathibitisha mafanikio ya dawa hiyo mwaka ujao.
Akizungumza katika mkutano wa kando wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Rais William Ruto alisema Afrika imekuwa ikibeba mzigo mkubwa wa magonjwa duniani huku ikizalisha sehemu ndogo ya dawa na chanjo zinazotumika barani humo. Alisema ushiriki wa Afrika katika utengenezaji wa dawa mpya ni hatua muhimu ya kujitegemea katika sekta ya afya.
Kwa mujibu wa Merck, iwapo itaidhinishwa, alimatravir inaweza kuwa dawa ya kwanza ya kila mwezi ya kumeza kwa ajili ya kuzuia maambukizi ya HIV, jambo ambalo linaweza kuongeza upatikanaji wa huduma za kinga katika maeneo yenye kiwango kikubwa cha maambukizi.
Unaweza kusoma pia: