Mlipuko wa Ebola mbaya zaidi katika historia ya DR Congo
Mlipuko wa ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umesababisha vifo vya watu 2,325, kulingana na takwimu za serikali zilizotolewa Jumapili.
Idadi hiyo imezidi ya mlipuko wa miaka ya 2018-2020 na kuufanya kuwa mlipuko mbaya zaidi kuwahi kutokea nchini humo.
Taasisi ya afya ya umma ya Kongo ilisema katika ripoti yake ya hivi karibuni kuwa idadi ya visa vilivyothibitishwa imefikia 4,945, ikiwa ni pamoja na visa vipya 101 vilivyogunduliwa katika saa 24 zilizopita.
Mlipuko huu wa 17 nchini Kongo,tayari ulikuwa mkubwa zaidi katika historia ya nchi hiyo kwa kuzingatia idadi ya visa, hatua iliyofikiwa mwishoni mwa mwezi wa Julai.
Takwimu za hivi punde za serikali zinaonyesha kuwa jumla ya vifo imezidi idadi ya vifo 2,299 vilivyorekodiwa wakati wa mlipuko wa mwaka 2018-2020, ambao hapo awali ulikuwa mbaya zaidi kuwahi kurekodiwa nchini humo.
Takwimu zinaonyesha kuwa sasa kuna visa 4,945 vilivyothibitishwa. Miezi mitatu baada ya kutangazwa rasmi, mlipuko huu sasa unazidi mlipuko wa Ebola wa Afrika Magharibi wa miaka ya 2014-2016 pekee, ambapo visa 28,616 na vifo 11,310 vilirekodiwa nchini Guinea, Liberia na Sierra Leone, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani.
Ilichukua takriban miezi mitano kutangazwa kwa mlipuko huo uliofikia vifo 1,000, ilhali mlipuko wa sasa nchini Kongo ulifikisha vifo 2,000 ndani ya miezi mitatu tu.