Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Rais wa Iran: Marekani inataka kuipindua serikali ya Iran
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, ameishutumu Marekani kwa kutaka kuipindua serikali ya Iran na kusema Israel pia inalenga kuiondoa madarakani badala ya kushiriki mazungumzo.
Muhtasari
- Umati mkubwa wamlaki Papa Leo Paris wakati wa Misa ya wazi
- Watu 11 wauawa katika shambulio la bomu Pakistan
- Rais wa Iran: Marekani inataka kuipindua serikali ya Iran
- Rouhani: Mafanikio ya vita si kuzuia mashambulizi pekee
- CNN yazuiwa kusafiri na Trump ndani ya ndege ya Air Force One
- Iran yatoa onyo jipya kwa Marekani
- Iraq yataka Marekani iruhusu kurejea kwa ndege za Iran
- Polisi: Mwanamke aliyepatikana amening'inia mtini alikuwa amefariki tayari
- Kampuni ya OpenAI yakiri roboti zake kuingilia tovuti za serikali ya Marekani
- Klabu za EPL zatafuta fidia dhidi ya Man City
- Iran yatoa masharti ya kufunguliwa kwa Mlango wa Bahari wa Hormuz
Moja kwa moja
Na Asha Juma
Umati mkubwa wamlaki Papa Leo Paris wakati wa Misa ya wazi
Mamia ya maelfu ya watu wamemlaki Papa Leo XIV katikati mwa jiji la Paris wakati wa Misa kubwa iliyofanyika uwanjani.
Umati huo ulishangilia huku kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki akipita katika Barabara ya Champs-Élysées chini ya Mnara wa Arc de Triomphe, akiwapungia mkono waumini akiwa kwenye gari maalum la kipapa.
Papa alibariki watoto kadhaa wachanga alipokuwa akisalimia waumini katika vituo mbalimbali kando ya barabara hiyo, huku sauti za watu wakipaza, "Leo, Leo", zikisikika kila upande.
Zaidi ya watu nusu milioni wanatarajiwa kushiriki hafla hiyo iliyofanyika katikati ya mji mkuu wa Ufaransa siku ya Jumamosi. Madhabahu maalum pia imejengwa katika eneo la Place de la Concorde kwa ajili ya ibada hiyo.
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, ambaye alikutana na Papa Leo kwa mazungumzo ya saa moja siku ya Ijumaa, hatashiriki misa yoyote wakati wa ziara ya siku nne ya Papa nchini humo. Hatua hiyo inalenga kuepuka kukiuka kanuni kali za Ufaransa za kutenganisha dini na serikali.
Hata hivyo, Misa iliyofanyika Champs-Élysées itahudhuriwa na mke wa rais, Brigitte Macron, pamoja na Waziri Mkuu Sébastien Lecornu.
Baadhi ya wagombea wa uchaguzi wa urais wa mwaka ujao pia wanatarajiwa kuhudhuria hafla hiyo.
Watu 11 wauawa katika shambulio la bomu Pakistan
Polisi nchini Pakistan wamesema watu wasiopungua 11 wameuawa na wengine 30 kujeruhiwa kufuatia mlipuko wa bomu katika eneo la Dera Ismail Khan, kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa polisi, gari lililokuwa limebeba vilipuzi liligonga kituo cha ukaguzi wa usalama.
Miongoni mwa waliouawa ni wanajeshi wawili wanawake na mtoto mmoja.
Hadi sasa hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo.
Wanamgambo wa Tehreek-e-Taliban Pakistan (TTP) wamewahi kutekeleza mashambulizi kama hayo dhidi ya vikosi vya usalama huko nyuma.
Tukio hilo limetokea siku mbili baada ya Pakistan kutangaza kuwa ilifanya mashambulizi ya anga dhidi ya wanamgambo wanaoshukiwa kuwa na makazi nchini Afghanistan na ambao walikuwa wakilenga vikosi vyake katika maeneo ya mpakani.
Rais wa Iran: Marekani inataka kuipindua serikali ya Iran
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesema Marekani inalenga kuipindua serikali ya Iran na si kutafuta suluhisho la mzozo uliopo, akisisitiza kuwa Tehran bado haina imani na Washington.
"Nia ya Marekani si kutatua tatizo hili, bali kuipindua serikali yetu. Waziri Mkuu wa Israel amekuwa akisema wazi katika hotuba zake kwamba lengo lake ni kuiondoa serikali hii madarakani, si kufanya mazungumzo. Tuko tayari kufanya mazungumzo kwa moyo wote, lakini hatutakubali vitisho wala shinikizo, na hatutakubali kulazimishwa kujisalimisha," amesema Pezeshkian katika mahojiano na CBS.
Akijibu swali kuhusu uwezekano wa kukutana na Donald Trump, Pezeshkian alisema:
"Kwa sasa kuna hali kubwa ya kutokuaminiana kati ya Iran na Marekani. Sababu yake ni kwamba tumefanya mazungumzo na Marekani mara kadhaa, na tulifikia makubaliano kupitia JCPOA. Hata hivyo, baada ya miezi kadhaa ya mazungumzo na makubaliano hayo kufikiwa, rais wa Marekani aliyekuwa madarakani wakati huo alijiondoa katika makubaliano hayo."
Pezeshkian aliongeza: "Kwanza kabisa, hali hii ya kutokuaminiana iliyojengeka lazima ivunjwe. Hilo linaweza kufikiwa kwa kutekeleza yale tuliyokubaliana na kuyaandika. Marekani lazima ionyeshe kwa vitendo kwamba haina mpango wa kuipindua serikali yetu na mfumo wetu wa utawala."
Rouhani: Mafanikio ya vita si kuzuia mashambulizi pekee
Rais wa zamani wa Iran, Hassan Rouhani, amesema kuwa mafanikio ya vita hayapaswi kuishia katika kuzuia mashambulizi pekee, bali yanapaswa kuleta usalama wa kudumu, kupunguza uwezekano wa kushambuliwa tena na kuirejesha nchi kwenye mkondo wa maendeleo.
Rouhani alitoa kauli hiyo kujibu maandamano yaliyoibuka hivi karibuni kufuatia matamshi yake kuhusu mikusanyiko ya watu inayofanyika nyakati za usiku.
Amesema mjadala wake ulikuwa unahusu umuhimu wa malengo ya kitaifa kuungwa mkono na wananchi, na si kuhusu kuitisha kura ya maoni kuhusiana na kujilinda dhidi ya mashambulizi.
Rouhani alisisitiza kuwa kauli zake zilipotoshwa, akisema: "Sikutaja neno kura ya maoni wala kura ya maamuzi."
Aliongeza kuwa Iran haikuanza vita, na inaposhambuliwa ina wajibu wa kujilinda.
"Hiyo ni mojawapo ya kanuni za msingi," alisema.
Rais huyo wa zamani alisema hoja yake ilikuwa kwamba malengo ya muda mrefu ya taifa yanahitaji kuungwa mkono kwa mapana na jamii ili kuimarisha nguvu, ustawi, amani, umoja wa kitaifa na hadhi ya Iran.
Hivi karibuni Rouhani alitoa wito wa kufikiwa kwa "mwisho wa vita wenye heshima", akisema kuwa inaonekana baadhi ya watu hawapendi mazungumzo.
"Tunapaswa, kwa kuzingatia matakwa ya walio wengi, kumaliza vita kwa heshima ili tuweze kuijenga upya nchi na kufidia hasara zilizosababishwa," alisema.
Baada ya matamshi hayo, wafuasi wa serikali waliandaa maandamano ya usiku katika maeneo mbalimbali, huku baadhi yao wakikusanyika mbele ya nyumba ya Rouhani katika siku za karibuni wakitaka afikishwe mahakamani.
Soma Zaidi Hapa:
CNN yazuiwa kusafiri na Trump ndani ya ndege ya Air Force One
Shirika la utangazaji la Marekani, CNN, limezuiwa kusafiri pamoja na Rais Donald Trump ndani ya ndege ya rais ya Air Force One wakati wa safari yake kuelekea jimbo la Tennessee siku ya Jumamosi.
Hatua hiyo ni ya hivi karibuni katika mvutano unaoendelea kati ya Ikulu ya Marekani na vyombo vya habari, baada ya White House kulazimika kuondoa marufuku iliyokuwa imeweka dhidi ya baadhi ya taasisi za habari.
CNN ilikuwa imepangwa kuandamana na Trump katika safari yake ya Tennessee kuhudhuria mechi ya mpira wa miguu wa vyuo vikuu nchini Marekani. Hata hivyo, ratiba ya vyombo vya habari iliyotolewa na White House usiku wa Ijumaa haikuonyesha jina la CNN.
BBC imeiomba White House kutoa maoni kuhusu uamuzi huo.
CNN imeripoti kuwa hakuna chombo kingine cha habari kilichotajwa kuchukua nafasi yake katika ratiba ya muda ya rais.
Wiki iliyopita, Trump aliwapiga marufuku waandishi wa habari wa CNN, Politico na MS NOW kuingia White House, akiwatuhumu kuchapisha "taarifa za kubuni au uongo" kuhusu utawala wake.
Vyombo hivyo vitatu vya habari vilisema vinachukua hatua za kisheria dhidi ya uamuzi huo na kumtuhumu Trump kwa kukiuka haki zao za kikatiba za uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari.
Wakati huo huo, mitandao minne ya televisheni ambayo hushiriki kwa zamu kuripoti shughuli za White House pamoja na CNN, yaani ABC, CBS, Fox News na NBC, ilisimamisha kwa muda matangazo ya shughuli za rais kama ishara ya mshikamano na vyombo vilivyowekewa marufuku.
Iran yatoa onyo jipya kwa Marekani
Makao Makuu ya Kijeshi ya Iran ya Khatam al-Anbiya yameionya Marekani kwamba iwapo Washington itafanya "kosa lolote" dhidi ya Iran, kambi zote za kijeshi za Marekani, majeshi yake na maslahi yake katika eneo hilo yatakuwa shabaha ya mashambulizi.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Mehr, ambalo lina uhusiano na serikali ya Iran, onyo hilo limetolewa wakati Tehran ikisubiri jibu la Marekani kuhusu pendekezo lake la mpango wa siku saba unaolenga kufunguliwa tena kwa Mlango Bahari wa Hormuz.
Shirika hilo limesema eneo la Mashariki ya Kati kwa sasa linakabiliwa na hali nyeti ya kiusalama, huku harakati za kijeshi za Marekani zikizua hofu ya kuongezeka kwa mvutano. Wakati huo huo, juhudi za kidiplomasia na upatanishi zinaendelea kutafuta suluhu ya mgogoro huo.
Kwa mujibu wa Mehr, msimamo wa Tehran ni kwamba "Iran haitaanzisha vita, lakini ikiwa adui ataanzisha vita, Iran iko tayari kikamilifu kulinda usalama wake na mipaka yake."
Kauli hiyo inaongeza mvutano wa maneno kati ya Iran na Marekani wakati juhudi za kidiplomasia zikiendelea kuhusu mustakabali wa Mlango Bahari wa Hormuz, mojawapo ya njia muhimu zaidi duniani ya usafirishaji wa mafuta.
Soma Zaidi:
Iraq yataka Marekani iruhusu kurejea kwa ndege za Iran
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Iraq imesema kuwa ipo katika mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani ikitaka kuondolewa kwa baadhi ya viwanja vya ndege vya Iraq vikwazo vipya vinavyolenga mashirika ya ndege ya Iran.
Katika duru ya hivi karibuni ya vikwazo, Marekani imetishia kuviwekea vikwazo viwanja vya ndege vinavyopokea au kutoa huduma kwa ndege za Iran. Kutokana na hali hiyo, safari nyingi za ndege za Iran kuelekea nchi jirani, ikiwemo Iraq, zimesitishwa katika siku za karibuni.
Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi, Ofisi ya Waziri Mkuu wa Iraq ilisema mazungumzo hayo yanalenga kupata msamaha utakaoruhusu kurejea kwa safari za ndege kwa madhumuni ya kibinadamu, ikiwa ni pamoja na matibabu, elimu, hija za kidini na masuala mengine yanayowahusu raia.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa serikali ya Iraq inaendelea kufanya juhudi za kupunguza mvutano katika eneo hilo, ikisisitiza kuwa kuendelea kwa migogoro kutazidi kuifanya hali kuwa ngumu zaidi.
Iraq pia imezitaka pande zote husika kutafuta suluhisho la kumaliza mgogoro na mivutano ya sasa kupitia mazungumzo na diplomasia.
“Suluhisho litakalopatikana linapaswa kuzingatia maslahi ya nchi na wananchi wa eneo hili,” ilisema taarifa hiyo.
Polisi: Mwanamke aliyepatikana amening'inia mtini alikuwa amefariki tayari
Tahadhari: Habari hii ina maelezo yanayoweza kusumbua.
Polisi katika jimbo la Mississippi nchini Marekani wamesema wanaamini kuwa mwanamke Mweusi aliyepatikana amening'inizwa kwenye mti alikuwa tayari amefariki kabla mwili wake "kuandaliwa" na kutundikwa kwenye mti huo.
Taarifa hiyo ilitolewa mahakamani siku ya Ijumaa na mmoja wa wapelelezi wa kesi hiyo, ambaye pia alisema wanaamini kuwa Tasia Fortune, mama wa watoto wanne, aliuawa kufuatia mgogoro uliokuwa unahusiana na dawa za kulevya.
Mwili wa mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 29 ulipatikana ukining'inia kwenye mti katika nyumba iliyotelekezwa mjini Jackson mwezi Agosti.
Ugunduzi huo ulizua hofu kubwa katika mji huo wenye wakazi wengi Weusi, kutokana na historia ndefu ya Mississippi ya ukatili wa kibaguzi na vitendo vya kunyonga watu.
Baada ya wiki kadhaa za uvumi na shinikizo la kutaka maelezo zaidi, polisi walifanya ukamataji wa watu kadhaa kuhusiana na tukio hilo.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, polisi walisema kuwa daktari wa uchunguzi wa maiti alibaini kwamba kifo cha Fortune kilikuwa mauaji, na kwamba eneo la tukio pamoja na kitendo cha kuning'iniza mwili wake "vilipangwa ili kuonekana kama tukio la kujinyonga."
Maafisa hawajabainisha chanzo halisi cha kifo hicho wala kueleza kwa nini wanaamini mwili huo ulitundikwa baada ya marehemu kufariki.
Mama wa marehemu, ambaye alizungumza na BBC, alisema anakumbuka daktari wa uchunguzi wa maiti akimwambia:
"Hatulishughulikii tukio hili kama kujinyonga halisi."
Alisema pia aliambiwa kwamba binti yake alikuwa tayari amefariki kabla ya kuwekwa kwenye mti huo.
Mama huyo alikumbuka polisi wakimweleza kuwa tukio hilo lilihusishwa na dawa za kulevya.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Makao Makuu ya Polisi ya Jackson siku ya Ijumaa, alisema anaamini binti yake alipambana hadi dakika za mwisho za maisha yake.
"Najua alipambana. Namjua binti yangu," alisema.
Fortune ameacha watoto wanne wenye umri wa miaka 7, 5, 4 na 1.
Akiwa amevaa fulana yenye maandishi "Justice for Tasia Fortune" (Haki kwa Tasia Fortune), mama huyo alisema hataki kuona watu wasio na hatia wakifungwa gerezani.
"Natumaini tu wamewakamata watu sahihi," alisema.
Watu watatu wamekamatwa hadi sasa kuhusiana na kesi hiyo, wote wakiwa ni Weusi.
Miongoni mwao ni Jarques Ratliff, mwenye umri wa miaka 51, ambaye amekana mashtaka dhidi yake na anaendelea kuzuiliwa bila dhamana.
Mtu mwingine, Earnest Lloyd Jr, mwenye umri wa miaka 25, alikamatwa wiki hii.
Mtuhumiwa wa tatu, Eric Clark, mwenye umri wa miaka 45, alijisalimisha kwa mamlaka siku ya Ijumaa na kushtakiwa kwa mauaji. Anatarajiwa kufikishwa mahakamani siku ya Jumatatu.
Kifo cha Fortune ni miongoni mwa visa kadhaa vya watu Weusi kupatikana wakiwa wamening'inizwa ambavyo katika miaka ya hivi karibuni vimechochea wito wa kutaka Idara ya Haki ya Marekani na FBI kuchunguza kwa kina vifo vyote vya aina hiyo nchini humo.
Mbunge Ayanna Pressley wa chama cha Democratic amesema kulikuwa na angalau matukio 10 yaliyorekodiwa ya aina hiyo, kwa mujibu wa barua aliyoiwasilisha bungeni mwezi Septemba ikiwa imeungwa mkono na wabunge zaidi ya 50.
Tukio la karibuni zaidi lilitokea katika Kaunti ya Prince George's, karibu na Washington DC, ambapo kifo cha mtu Mweusi aliyepatikana amening'inia kilihitimishwa kuwa kujiua.
Kampuni ya OpenAI yakiri roboti zake kuingilia tovuti za serikali ya Marekani
Kampuni ya OpenAI imekiri kuwa iliyashtua mashirika kadhaa duniani kwamba huenda tovuti zao ziliingiliwa isivyofaa na roboti zake za akili bandia (AI).
OpenAI ilisema mawakala wake wa AI walijaribu kupata taarifa kutoka kwa "serikali, vyuo vikuu, mashirika ya umma na taasisi nyingine", zikiwemo Tume ya Usalama wa Mitaji ya Marekani (SEC), Ofisi ya Sensa ya Marekani (Census Bureau) na Idara ya Elimu ya Marekani.
Ufichuzi huo unakuja siku chache baada ya Waziri Mkuu wa Australia, Anthony Albanese, kutangaza kuwa mawakala wa OpenAI walikuwa wameingia kwenye faili ambazo hazikuwa za umma katika tovuti ya mpango wa huduma za afya unaoendeshwa na serikali.
Tangu mwezi Agosti, hofu imeongezeka kuhusu uwezekano wa zana za akili bandia kufanya kazi nje ya udhibiti wa binadamu, hali ambayo inaweza kuwa na athari kubwa au hata kuhatarisha maisha.
OpenAI ilisema baadhi ya taarifa hizo zilifikiwa na mawakala wa AI, ambao ni roboti zilizoundwa kufanya kazi kwa kiwango fulani cha kujitegemea na zilikuwa zikitafuta "vyanzo vinavyoaminika vya taarifa za umma".
Hata hivyo, kampuni hiyo ilikiri kuwa baadhi ya roboti hizo zilivuka mipaka na kujaribu kukwepa hatua za usalama zilizowekwa kwenye tovuti mbalimbali.
Kwa mfano, wakati wa kujaribu kupata taarifa kutoka Ofisi ya Sensa ya Marekani, mawakala hao wa AI walitumia zana zinazotumika na watengenezaji wa programu ili kupata ufikiaji wa taarifa hizo.
OpenAI imesisitiza kuwa taarifa zote za serikali zilizofikiwa na roboti zake zilikuwa tayari zinapatikana kwa umma na hakukuwa na data ya siri iliyofikiwa.
Klabu za EPL zatafuta fidia dhidi ya Man City
Vilabu vya Ligi Kuu ya England (Premier League) vimeanza kutafuta ushauri wa kisheria ili kubaini kama vinaweza kudai fidia kufuatia kesi ya mashtaka dhidi ya Manchester City.
Baada ya kusubiri kwa muda mrefu matokeo ya kesi hiyo, Manchester City imepatikana na hatia ya kukiuka sehemu kubwa ya kanuni za kifedha ambazo ilikuwa inatuhumiwa kuvunja.
BBC Sport pia imeelezwa kuwa klabu hiyo inapanga kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.
Imebainika kuwa hata kabla ya taarifa za Ijumaa kuibuka, baadhi ya vilabu vya Premier League vilikuwa tayari vimeanza kutafuta ushauri wa kisheria kuhusu uwezekano wa kudai fidia ya kifedha kutokana na ukiukaji unaodaiwa kufanywa na City.
Soma Zaidi:
Trump akataa mpango wa amani, Iran yasubiri hatua ya Marekani
Iran siku ya Jumamosi ilikuwa ikisubiri jibu rasmi kutoka Marekani kuhusu pendekezo lake la kufungua tena Mlango Bahari wa Hormuz na kumaliza mapigano katika vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati, baada ya gazeti la Wall Street Journal kuripoti kwamba Rais wa Marekani Donald Trump alikuwa amelikataa pendekezo hilo.
Iran iliwasilisha mpango huo wa kidiplomasia katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) mjini New York, ikisema kuwa uliwasilishwa kwa Marekani kupitia wapatanishi wa Qatar. Kwa mujibu wa Iran, mpango huo ungeweza kufungua tena njia hiyo muhimu ya majini na kumaliza uhasama katika eneo hilo ndani ya siku saba.
Iran pia ilifanya mazungumzo na hasimu wake wa muda mrefu, Saudi Arabia, kuhusu Mlango wa Bahari wa Hormuz, jambo linaloonyesha uzito wa mzozo huo wa miezi saba ambao umeathiri mtiririko wa mafuta kupitia mojawapo ya njia muhimu zaidi za usafirishaji wa majini duniani na kuathiri uchumi wa dunia.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, aliwaambia waandishi wa habari katika Umoja wa Mataifa siku ya Ijumaa kwamba makubaliano hayo yangeanzisha kipindi cha siku saba kuelekea kufunguliwa tena kwa Mlango Bahari wa Hormuz na kusitishwa kwa mapigano katika eneo hilo.
"Ikiwa upande wa Marekani una dhamira ya kweli ya kufikia makubaliano na kufungua tena Mlango wa Bahari wa Hormuz, kila kitu sasa kiko tayari," Araghchi alisema.
Araghchi alisema kuwa iwapo Marekani itakubali pendekezo hilo, pande zinazohusika katika mzozo huo zinaweza kuanza mazungumzo mapana zaidi kuhusu "masuala yatakayokubaliwa kwa pamoja."
Soma Zaidi Hapa:
Hujambo. Karibu katika matangazo yetu mubashara ya tarehe 26/09/2026.