Mambo 7 muhimu kuhusu kesi ya uhaini ya Lissu
Tundu Lissu, Mwenyekiti wa CHADEMA, anakabiliwa na kesi ya uhaini Tanzania. Usikilizwaji wa kesi hiyo unaendelea Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, huku upande wa Jamhuri ukiendelea kuwasilisha mashahidi wake. Kufikia jana, mashahidi 16 walikuwa wamefika kutoa ushahidi katika kesi hiyo.
1. Kesi ya Lissu inahusu nini?
Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, anakabiliwa na shtaka la uhaini nchini Tanzania.
Kesi hiyo inasikilizwa katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, na imekuwa ikiendelea kwa awamu huku upande wa Jamhuri ukiwasilisha ushahidi wake.
2. Lissu alikamatwa lini?
Lissu alikamatwa 8 Aprili 2025, na siku moja baadaye akafikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, ambako alisomewa shtaka la uhaini kama Mahakama ya ukabidhi.
Hapo ndipo mchakato wa kesi ulipoanzia kabla shauri hilo kuendelea kusikilizwa katika Mahakama Kuu.
3. Kesi ilifikaje Mahakama Kuu?
Baada ya hatua za awali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kesi ya uhaini iliendelea katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.
Huko, upande wa Jamhuri ulianza kuwasilisha ushahidi na mashahidi wake katika kuunga mkono mashtaka dhidi ya Lissu. Na Mpaka sasa Mashahidi 16 wametoa ushahidi wao mpaka Agosti 12, 2026.
4. Kwa nini kesi ilisimama kwa miezi mitano?
Hili ni moja ya mambo muhimu katika historia ya kesi hiyo.
Februari 2026, Jamhuri iliwasilisha notisi ya kutaka kuongeza ushahidi mpya katika kesi hiyo.
Lissu alipinga hatua hiyo, na Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam ikatupilia mbali notisi ya Jamhuri ya kuwasilisha ushahidi huo mpya.
Jamhuri haikukubaliana na uamuzi huo. Ilipeleka suala hilo Mahakama ya Rufani, ikiomba mapitio ya uamuzi wa Mahakama Kuu.
Kutokana na shauri hilo, Mahakama Kuu ilisimamisha usikilizwaji wa kesi ya uhaini hadi Mahakama ya Rufani itakapotoa uamuzi.
Hivyo, kesi hiyo ilisimama kwa takribani miezi mitano kuanzia Februari 2026.
5. Nini kilitokea Mahakama ya Rufani?
Baada ya suala hilo kufikishwa Mahakama ya Rufani, mahakama hiyo ilitoa uamuzi kuhusu hoja iliyokuwa imewasilishwa na Jamhuri.
Lissu alishinda katika suala hilo, na hivyo kuondoa kikwazo cha kisheria kilichokuwa kimesababisha usikilizwaji wa kesi kusimama.
Baada ya uamuzi huo, kesi ilirejea Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji wake.
6. Kesi ilianza tena lini?
Baada ya kusimama kwa takribani miezi mitano, usikilizwaji wa kesi ulianza tena Agosti 10, 2026.
Tangu kurejea kwake Mahakama Kuu, upande wa Jamhuri umeendelea na uwasilishaji wa ushahidi.
Kufikia Agosti 12, shahidi wa 16 wa upande wa Jamhuri, ACP Amin Mahamba, alikuwa amemaliza kutoa ushahidi wake na kuhojiwa na Lissu. Akitumia siku 3 Mahakamani
7. Nini kimejitokeza katika ushahidi wa mashahidi?
Katika hatua ya sasa ya kesi, Lissu amekuwa akiwahoji mashahidi wa Jamhuri kuhusu ushahidi waliowasilisha na taarifa walizowahi kutoa katika hatua za uchunguzi.
Katika ushahidi wa Agosti 12, kwa mfano, Lissu alimuuliza shahidi kuhusu tofauti kati ya maelezo aliyowahi kutoa wa maandishi na majibu ya mdomo aliyoyatoa mahakamani. Shahidi alisema hakuwa ameeleza sababu ya tofauti hiyo kwa maandishi, lakini akiongozwa na wakili wa Serikali alisema , alikuwa akijibu maswali kwa namna alivyoulizwa na mshitakiwa.
Lissu pia aliuliza kuhusu video zilizotumika katika uchunguzi. Shahidi alisema polisi walitazama video iliyokuwa mtandaoni, lakini hawakuangalia video iliyokuwa kwenye memory card na flash disk zilizotajwa mahakamani.
Jana, Agosti 12, shahidi wa 16 wa Jamhuri alimaliza kutoa ushahidi. Baada ya hapo, upande wa Jamhuri uliomba kesi iahirishwe kwa kuwa haukuwa umejiandaa na shahidi mwingine, na Jaji Dunstan Ndunguru akaahirisha kesi hadi leo, Agosti 13.
Kwa hiyo, leo macho yanaelekezwa Mahakamani kujua hatua inayofuata katika ushahidi wa upande wa Jamhuri.