Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Vita vya Iran: Trump asema 'mashambulizi ya mabomu' yatarejea iwapo makubaliano hayataafikiwa

Kauli hiyo imekuja wakati ambapo bado kuna sintofahamu kuhusu uwezekano wa kufanyika kwa mazungumzo mapya ya kumaliza vita kati ya pande hizo mbili huko Pakistan.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Martha Saranga & Mariam Mjahid

  1. Tume ya vurugu za uchaguzi Tanzania yapokea ushahidi

    Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Jaji Chande, amesema tume hiyo imepokea ushahidi kutoka kwa Watanzania 63,603 kupitia njia mbalimbali.

    Amesema ushahidi huo umetolewa kupitia mahojiano ya ana kwa ana ya watu 1,323, mashahidi wa viapo (affidavits) 553, madodoso yasiyo na majina ya watu 4,891, mikutano na makundi 202, pamoja na simu na ujumbe mfupi kutoka kwa watu 56,445.

    Kulingana na Jaji Chande, wote hao wametoa taarifa kuhusu matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea katika kipindi hicho.

    Kumekuwa na madai kutoka kwa baadhi ya wadau hasa wanaharakati mitandaoni nchini Tanzania wanaoona kwamba kuongezwa kwa muda wa tume hiyo mara mbili kunalenga kutoa nafasi kwa mamlaka fulani 'kuchakachua' yaliyomo kwenye ripoti hiyo.

    Hata hivyo, Jaji Chande alieleza kuwa sababu kuu ya kuongeza muda ni kupanuka kwa wigo wa kazi pamoja na ongezeko la ushahidi unaokusanywa.

    Ripoti kamili ya uchunguzi huo inatarajiwa kuwasilishwa tarehe 23 Aprili 2026.

  2. Vita vya Iran: Trump asema 'mashambulizi ya mabomu' yatarejea iwapo makubaliano hayataafikiwa

    Rais Donald Trump amesema Iran "haina chaguo ila kutuma" wajumbe kwenda Pakistan kwa mazungumzo na Marekani.

    Katika mahojiano na CNBC, rais amesema ana uhakika Marekani "itaishia na mpango mkubwa".

    Anasema kwamba Marekani "haishughulikii watu wazuri zaidi" lakini inafanya hivyo "kwa mafanikio", kabla ya kuitaja kizuizi cha wanamaji cha Marekani "mafanikio makubwa".

    Alipoulizwa kama angerefusha muda wa usitishaji mapigano iwapo mazungumzo yanaonekana kuwa yanaendelea, rais wa Marekani anasema: "Sitaki kufanya hivyo".

    Trump baadaye anasema: "Natarajia kushambulia kwa sababu huo ungekuwa mtazamo bora zaidi."

    Anasema hakuna "muda mwingi" wa kufikia makubaliano, na kwamba Iran inaweza kujipatia "hali nzuri sana" ikiwa itafikia makubaliano na Marekani.

  3. Donald Trump aishutumu Iran kwa kukiuka usitishaji mapigano 'mara kadhaa'

    Rais wa Marekani Donald Trump ameishutumu Iran kwa kukiuka makubaliano ya usitishaji mapigano “mara kadhaa.”

    Tuhuma hiyo ilitolewa kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa Truth Social muda mfupi uliopita, bila kutoa maelezo zaidi kuhusu alichomaanisha.

    Haya yanajiri kufuatia hali ya ati ati ya iwapo mazungumzo ya Marekani na Iran yatafanyika leo huko Islamad au la.

  4. Iran yaweka masharti mazito kabla ya kushiriki Kombe la Dunia

    Kuhusu suala la kuipeleka timu ya taifa ya soka kwenye Kombe la Dunia, ambalo Marekani ni miongoni mwa wenyeji wake watatu, Waziri wa Michezo wa Iran amesema uamuzi wa mwisho uko mikononi mwa serikali au Baraza Kuu la Usalama wa Taifa.

    Ahmad Donyamali amesema: “Inawezekana uamuzi ukawa kutoshiriki Kombe la Dunia,” lakini hakutoa msimamo wa mwisho.

    Kombe la Dunia linatarajiwa kuanza chini ya miezi miwili ijayo.

    Aidha, waziri huyo alisema: “Kambi ya timu ya taifa imepangwa kufanyika katika wiki ya tatu ya Mei katika nchi jirani na itadumu takriban wiki moja. Ikiwa hali ya usalama itakuwa nzuri kwa wachezaji na mwenyeji (Marekani) ataacha vitendo vya uchokozi na hatari, basi uamuzi mwafaka utafanywa.”

    Rais wa FIFA, Gianni Infantino, alisema Jumatano iliyopita kuwa Iran “hakika” itashiriki Kombe la Dunia la 2026: “Iran itakuja bila shaka. Tunatumaini kufikia wakati huo kutakuwa na hali ya amani, jambo litakalosaidia kwa kiasi kikubwa.”

    Aliongeza: “Iran inapaswa kushiriki. Wanaiwakilisha nchi yao, wamefuzu na wachezaji wanataka kucheza.”

    Soma zaidi:

  5. Jeshi la Iran lasema meli yake yavuka kizuizi cha majini cha Marekani

    Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limesema kuwa meli ya mafuta ya Iran imefanikiwa kuvuka kizuizi cha majini kilichowekwa na Marekani na kuingia katika bandari moja kusini mwa nchi hiyo.

    Katika taarifa yake, jeshi hilo lilisema: “Licha ya maonyo na vitisho vingi kutoka kwa jeshi la wanamaji la Marekani, meli ya mafuta ya Iran iitwayo Silica City, kwa msaada wa operesheni wa wanamaji wa jeshi na kwa usalama kamili, iliingia katika maji ya Iran jana usiku baada ya kupita katika Bahari ya Arabia, na kwa sasa imeegeshwa katika moja ya bandari za kusini za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa saa kadhaa.”

    Marekani haijatoa tamko lolote kuhusu madai hayo.

    Hata hivyo, kamandi ya kijeshi ya Marekani katika eneo hilo, CENTCOM, ilisema katika taarifa fupi jana kuwa tangu kuanza kwa mzingiro wa baharini dhidi ya Iran, “majeshi ya Marekani yamelazimisha meli 27 kubadili njia au kurejea katika bandari za Iran.”

    Soma Zaidi:

  6. Vyombo vya habari vya Iran vyakanusha kuwepo kwa ujumbe wa mazungumzo kuelekea Islamabad

    Shirika la habari la taifa la Iran, kupitia taarifa iliyotolewa kwenye kituo chake cha Telegram, limekanusha ripoti zilizodai kuwa ujumbe wa Iran umeondoka kuelekea Islamabad.

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hakuna ujumbe wowote uliotoka Iran hadi sasa.

    Taarifa hiyo imeeleza kuwa habari zinazosambaa katika vyombo vya kimataifa na vya kanda kuhusu kuondoka, kuwasili au muda wa kutarajiwa kwa ujumbe huo ni uvumi tu.

    Aidha, imesisitiza msimamo wa maafisa wa Iran, akiwemo Spika wa Bunge na mkuu wa majadiliano Mohammad Baqer Qalibaf.

    Amesema Tehran “haikubali aina yoyote ya mazungumzo chini ya kivuli cha vitisho.”

    Wakati huo huo, Balozi wa Iran nchini Pakistan, Reza Amiri Moqadam, asema kwamba Iran haitafanya mazungumzo chini ya vitisho au shinikizo lolote.

    Katika ujumbe wake kwenye X, aliandika kwamba “ni ukweli unaokubalika ulimwenguni kuwa nchi yenye ustaarabu wa kale kama huu haitafanya mazungumzo chini ya vitisho au shinikizo.”

    Akaongeza tena: “Hii ni kanuni thabiti ya Kiislamu na kidini. Natamani Marekani ingeielewa.”

    Soma zaidi:

  7. Utajiri wa mbunge wa Minnesota Ilhan Omar wawekwa wazi

    Jumla ya mali za mbunge wa Marekani Ilhan Omar na mumewe zimewekwa wazi.

    Kituo cha habari cha Fox News kiliripoti kuwa kulikuwa na hitilafu katika makadirio ya mali za kifedha za Ilham, ambazo zilikuwa zimetajwa kuwa dola milioni 30.

    Gazeti hilo, likinukuu ripoti mpya iliyotolewa na ofisi ya Ilhan, lilisema kuwa mali ya pamoja ya yeye na mumewe inafikia dola elfu 95 pekee.

    Ripoti hiyo iliyorekebishwa ilitolewa baada ya Ofisi ya Maadili ya Bunge kuomba maelezo zaidi kuhusu mali zinazodhaniwa za mbunge huyo wa Minnesota mapema mwaka huu.

    Soma zaidi:

  8. Trump ni 'muongo' - Iran

    Shirika la habari la Fars lenye mafungamano na kikosi cha walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC) limechapisha nukuu kwenye mtandao wa Telegram kutoka kwa kamanda katika makao makuu ya kijeshi ya Iran. Nukuu inayomkosoa Rais wa Marekani, Donald Trump, kwamba amekuwa akisema uongo.

    Akiandika kwa Kiajemi, Meja Jenerali Abdullahi anasema kwamba IRGC imefanikiwa kuisukuma Israel na Marekani hadi kufikia hali ya kukata tamaa na uchovu,na kuwalazimu kuomba kwa dharura kusitishwa mapigano, kwa mujibu wa Fars.

    Anasema vikosi vya kijeshi visingemruhusu "rais wa Marekani muongo na mdanganyifu" "kutunga maelezo ya uongo kuhusu hali ilivyo katika uwanja wa vita haswa kuhusu Mlango Bahari wa Hormuz.

    Bado haijulikani wazi ikiwa ujumbe wa Iran utaelekea Islamabad kwa duru ya pili ya mazungumzo ya amani na Marekani.

    Trump hakupatanikana mara moja kuelekeza hilo, lakini mara kadhaa amekanusha kuhusu tuhuma za kudanganya, akisimamia msimamo wa Marekani kwenye mzozo huo wa Mashariki ya Kati.

    BC Asia Kusini anaeleza, kuna mvutano wa kisiasa nyuma ya pazia nchini Iran, huku watu wenye msimamo mkali wakiweka shinikizo kwa wapatanishi kuchagua mzozo badala ya diplomasia.

    Unaweza kusoma pia:

  9. Pakistan iko kwenye nafasi ya kipekee kuandaa mazungumzo, huku ikikabiliwa na hatari

    Pakistan iko katika nafasi ya kipekee ya kuwa mwenyeji wa mazungumzo ya amani, lakini hatua hiyo inaambatana na hatari kubwa kwa nchi hiyo.

    Wakati Pakistan ikijiandaa kwa duru ya pili ya mazungumzo hayo ingawa bado kuna mashaka ikiwa yatafanyika usalama unaimarishwa sana mjini Islamabad.

    Aidha, mabango yenye ujumbe wa “Mazungumzo ya Islamabad” yanaonekana kote katika mitaa ya mji mkuu huo.

    Nchi hiyo ina nafasi maalum kwa sababu inaaminika na mataifa mbalimbali yenye ushawishi mkubwa kama Marekani, Iran na nchi za Ghuba.

    Hali hii inaifanya Pakistan kuwa kiunganishi muhimu katika juhudi za kidiplomasia zinazolenga kupunguza mvutano katika eneo hilo lenye migogoro ya mara kwa mara.

    Hata hivyo, uhusiano wa karibu wa Pakistan na Marekani haukuizuia kulaani rasmi mashambulizi ya awali ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

    Ikiwa mazungumzo yatavunjika, Pakistan inaweza kujikuta ikipigana na jirani yake Iran.

    Pakistan ilisaini mkataba wa ulinzi wa pande zote na Saudi Arabia mwaka jana, moja ya nchi za Ghuba ambazo zimeathiriwa na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Iran kabla ya usitishaji mapigano wa sasa, ambao unatarajiwa kuisha kesho.

  10. Safari za meli kupitia Mlango Bahari wa Hormuz zinapaswa kuendelea - Xi Jinping

    Rais wa China Xi Jinping anasema "safari za kawaida za meli kupitia Mlango Bahari wa Hormuz "zinapaswa kuendelea".

    Alitoa kauli hiyo wakati wa mazungumzo kwa njia ya simu na Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman siku ya Jumatatu.

    Xi alisema kuwa njia hiyo muhimu ya baharini inapaswa kubaki wazi kwa matumizi ya kawaida, kwa sababu ni kwa manufaa ya nchi za eneo hilo pamoja na jamii ya kimataifa kwa ujumla.

    Kwa upande mwingine rais wa Marekani Donald Trump na Xi wanatarajiwa kukutana nchini China mwezi Mei, baada ya safari hiyo kuahirishwa awali kutokana na vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

    Unaweza kusoma pia:

  11. Iran yasema ina 'karata mpya' vita vikirejea, mazungumzo yakiwa shakani

    Kadiri muda wa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Marekani, Israel na Iran unavyokaribia kuisha, bado hakuna uthibitisho wa mazungumzo zaidi ya amani.

    Spika wa bunge la Iran aliandika kwenye mtandao wa X akisema kwamba Iran imekuwa "ikiandaa mkakati mpya kwa ajili ya uwanja wa vita" katika wiki mbili zilizopita na "haitakubali mazungumzo chini ya kivuli cha vitisho".

    Wakati huo huo, Rais Donald Trump amekanusha kwamba yuko chini ya shinikizo la kufanya makubaliano, huku vyombo vya habari vya Marekani vikiripoti kwamba makamu wa rais JD Vance atasafiri kwenda Pakistan Jumanne kwa mazungumzo.

    Katika Ghuba, Marekani inaendelea kuzuia Mlango wa Hormuz baada ya kukamata meli ya mizigo yenye bendera ya Iran siku ya Jumapili na pande zote mbili zinashutumiana kwa ukiukaji wa mapigano.

    Kwingineko, duru ya pili ya mazungumzo kati ya Israeli na Lebanon inatarajiwa kufanyika Alhamisi kwa mujibu wa afisa wa Marekani.

  12. Wachimbaji haramu 42 wanaswa Nigeria baada ya kiongozi wa jadi kutekwa

    Polisi katika jimbo la Kwara nchini Nigeria wamewakamata washukiwa 42 wa uchimbaji haramu kufuatia kutekwa nyara kwa kiongozi wa jadi, huku hofu ya usalama ikizidi kuongezeka katika eneo hilo.

    Mfalme Oba Salman Olatunji Aweda, wa jamii ya Olayinka katika eneo la serikali ya mtaa ya Ifelodun, alitekwa nyara Jumamosi jioni baada ya watu wenye silaha kuvamia ikulu yake.

    Akizungumza na waandishi wa habari Jumatatu, kamishna wa Polisi wa Jimbo la Kwara, Adekimi Ojo, alisema kukamatwa kwao ni sehemu ya uchunguzi unaoendelea kuhusu utekaji nyara huo.

    Hata hivyo, alisisitiza kwamba haijabainika ikiwa walihusika moja kwa moja katika shambulio hilo.

    Kwa mujibu wa polisi, takriban wanaume kumi wenye silaha nzito walivamia ikulu muda mfupi baada ya wachimbaji wanaofanya kazi katika eneo hilo kumtembelea mfalme mapema siku hiyo.

    Washambuliaji hao wanaripotiwa kudai pesa kwa kiongozi huyo wa kitamaduni kabla ya kumtoa chumbani kwake.

    Bw. Ojo alisema mfalme alikabidhi pesa hizo lakini bado alichukuliwa pamoja na kaka yake.

  13. Raia wa Canada auawa kwa risasi katika eneo la kale nchini Mexico

    Mwanamke mmoja raia wa Canada ameuawa huku wengine kadhaa wakijeruhiwa baada ya mtu aliyejihami kwa silaha kufyatua risasi katika eneo la kihistoria nchini Mexico, kwa mujibu wa maafisa wa nchi hiyo.

    Tukio hilo limeibua hofu na maswali kuhusu usalama katika maeneo maarufu ya utalii. Shambulio hilo lilitokea katika eneo la kumbukumbu ya kale la Teotihuacán lililopo kaskazini mwa Mexico City siku ya Jumatatu.

    Serikali ya Mexico ilisema mshambuliaji huyo alijiua baada ya kutekeleza tukio hilo.

    Polisi walipofika eneo la tukio walikuta bunduki, silaha yenye makali pamoja na risasi ambazo hazikutumika.

    Rais wa Mexico Claudia Sheinbaum alisema "Kilichotokea leo huko Teotihuacán kinatuumiza sana. Ninatuma salamu za pole na rambirambi kwa waathiriwa na familia zao," aliandika kwa Kihispania.

    Piramidi na magofu ya kale ya Teotihuacán ni eneo la urithi wa dunia lililotambuliwa na UNESCO, ni miongoni mwa vivutio vikubwa vya watalii nchini Mexico.

    Tukio hilo linaweza kuathiri taswira ya usalama katika maeneo hayo muhimu ya kihistoria.

    Waziri wa mambo ya nje wa Canada Anita Anand alithibitisha kuwa raia mmoja wa Canada aliuawa na mwingine kujeruhiwa

  14. Tahadhari ya ujio wa tetemeko yatangazwa Japan baada ya kuondoa onyo la Tsunami

    Maafisa nchini Japani wameonya kuhusu tetemeko la ardhi "kubwa" linalotarajiwa katika wiki ijayo baada ya tetemeko la ukubwa wa richa 7.7 kutokea pwani ya kaskazini-mashariki, na kusababisha amri ya kuhama na maonyo ya mawimbi ya tsunami ya mita 3 (futi 10).

    Maelfu ya watu waliamuriwa kuondoka katika maeneo ya pwani kwenda kwenye maeneo ya juu baada ya tetemeko hilo katika karibu na mkoa wa Iwate, kilomita 530 (maili 330) kaskazini mwa mji mkuu Tokyo.

    Mawimbi makubwa zaidi ya tsunami yalikuwa na urefu wa sentimita 80. Onyo la ujio wa Tsunami liliondolewa saa chache baada ya tetemeko hilo Jumatatu.

    Lakini shirika la hali ya hewa la Japan limeonya kwamba matetemeko "yanayosababisha tetemeko kubwa zaidi" yanaweza kutokea katika wiki ijayo, na kusababisha mawimbi makubwa zaidi.

    Mamlaka ilisema kuna uwezekano wa kutokea tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa richa 8.0 au zaidi kuliko wakati wa kawaida.

    Japan ina kumbukumbu za tetemeko kubwa la ardhi lililotokea mwaka 2011 lililosababisha tsunami iliyogharimu maisha ya zaidi ya watu 18,000 na kusababisha kuyeyuka kwa kinu cha nyuklia cha Fukushima.

  15. Marekani haitaondoa kizuizi cha kijeshi Hormuz hadi makubaliano na Iran yafikiwe - Trump

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa nchi yake haitaondoa kizuizi ilichoweka kwenye bandari za Iran hadi pale makubaliano rasmi yatakapofikiwa na Tehran.

    Kauli hiyo imekuja wakati ambapo bado kuna sintofahamu kuhusu uwezekano wa kufanyika kwa mazungumzo mapya ya kumaliza vita kati ya pande hizo mbili.

    Kizuizi hicho, ambacho kilianza wiki moja iliyopita, "kinaiangamiza Iran kabisa", Trump aliandika kwenye ukurasa wake wa mitandao ya kijamii wa Truth Social, akiongeza kuwa nchi yake ilikuwa ikishinda mzozo huo "kwa kiasi kikubwa".

    Maoni yake yanaambatana na makubaliano ya muda ya kusitisha mapigano kati ya Marekani na Iran yanayotarajiwa kukamilika Jumatano, lakini bado hakuna uhakika ikiwa awamu ya pili ya mazungumzo ya amani itaendelea nchini Pakistan.

    Usalama umeimarishwa katika mji mkuu wa Pakistan kufuatia mkutano huo. Hata hivyo makamu wa rais wa Marekani JD Vance anayetarajiwa kuongoza ujumbe wa Marekani bado hajaondoka Washington, huku Iran ikisema bado haijaamua kuhudhuria.

  16. Karibu katika habari zetu za moja kwa moja leo Aprili 21, 2026