Mashirika ya kutetea haki za binadamu yaitaka ICC kuichunguza serikali ya Tanzania

Muungano wa kimataifa wa wanasheria na makundi ya haki za binadamu umeiomba rasmi Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kumchunguza rais wa Tanzania, na serikali yake kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Mashirika ya kutetea haki za binadamu yaitaka ICC kuichunguza serikali ya Tanzania

    Rais Samia

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Muungano wa kimataifa wa wanasheria na makundi ya haki za binadamu umeiomba rasmi Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kumchunguza rais wa Tanzania, na serikali yake kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu unaodaiwa kufanywa wakati wa uchaguzi Mkuu wa hivi karibuni.

    Waraka wa Ombi kwa ICC linamtuhumu Rais Samia Suhulu Hassan na maafisa wengine wa ngazi za juu kwa kuhusishwa moja kwa moja na vifo vya raia wakati wa maandamano ya baada ya uchaguzi.

    Juma lililopita Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alizindua tume ya uchunguzi kuhusu vurugu hizo baada ya kuwatuhumu wapinzani na mashirika yasiyo ya kiserikali kwa kusababisha machafuko.

    Ombi la kuchunguza ukatili unaodaiwa kufanywa na serikali ya Tanzania liliwasilishwa rasmi kwa ofisi ya mwendesha mashtaka wa ICC mnamo Novemba 13 lakini limetangazwa hadharani leo tu.

    Hati hiyo yenye kurasa 82 pia inaelezea kile ilichokiita ukiukwaji wa kimfumo na unaoendelea, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita ikiwa ni pamoja na utekaji nyara, mateso kwa watu waliopotezwa na mauaji ya wapinzani kinyume cha sheria.

    ICC bado haijathibitisha kama itafanya uchunguzi. Tanzania ni mwanachama wa chombo hicho.

    Rais Samia alishinda zaidi ya asilimia 97 ya kura katika uchaguzi uliowazuia wagombea wakuu wa upinzani kugombea. Maandamano ya baada ya uchaguzi yalisababisha kufungwa kwa intaneti, amri ya kutotoka nje na vifo na kukamatwa kwa mamia ya watu. Makundi ya waangalizi wa kikanda na kimataifa yalielezea uchaguzi huo kama usio wa kidemokrasia.

  2. Watu tisa wakamatwa nchini India baada ya polisi kudhibiti wizi wa dola 800,000

    Maafisa wa polisi katika mkutano na wanahabari

    Chanzo cha picha, Imran Qureshi

    Watu tisa wamekamatwa nchini India baada ya wizi wa rupia milioni 70 ($800,000) ambapo wanaume wenye silaha waliojifanya maafisa wa benki kuu waliiba gari la pesa la ATM.

    Siku ya Jumatatu, polisi katika mji wa kusini wa Bengaluru walisema walikuwa wamewakamata watu wengine wawili, pamoja na saba hapo awali, na kupata rupia milioni 68.5, pesa zilizoibwa wiki iliyopita.

    "Hatuwezi kusema ni wangapi zaidi watakaokamatwa tunapoendelea kuchunguza kesi hiyo," Lokesh Jagalasar, Naibu Kamishna wa polisi wa Bengaluru Kusini, aliiambia BBC. Wezi hao walikuwa wamejifanya maafisa wa Benki Kuu ya India.

    Walisimamisha gari la usafiri wakisema walipaswa kuangalia nyaraka hizo za kiasi kikubwa cha pesa.

    Mwangalizi wa pesa taslimu wa gari hilo na walinzi wawili waliagizwa kuingia kwenye gari aina ya SUV, huku mmoja wa wafuasi wa genge hilo akichukua akidhibiti gari hilo, polisi walisema.

    Polisi walisema genge hilo lilikuwa limebadilisha magari, lilitumia nambari bandia za usajili na maeneo yaliyochaguliwa yenye ulinzi mdogo wa CCTV kuhamisha masanduku ya pesa taslimu.

    Msako mkubwa ulianzishwa Jumatano, huku zaidi ya maafisa 200 wa polisi wakipelekwa katika jimbo la Karnataka na majimbo jirani ya Kerala, Tamil Nadu, Telangana, Andhra Pradesh na Goa.

  3. Trump asema atatembelea China mwezi Aprili baada ya mazungumzo na Xi

    Xi na Trump

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais Donald Trump amesema alikubali kutembelea Beijing mwezi Aprili na kumwalika Rais wa China Xi Jinping kwa ziara ya kiserikali baadaye mwaka ujao, kufuatia mazungumzo ya simu kati ya viongozi hao wawili.

    Trump na Xi, ambao walikutana karibu mwezi mmoja uliopita nchini Korea Kusini, walijadili masuala mbalimbali ikiwemo biashara, uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine, fentanyl na Taiwan, kulingana na rais na wizara ya mambo ya nje ya China.

    "Uhusiano wetu na China ni imara sana!" Trump aliandika katika chapisho la Truth Social. Shirika jipya la serikali ya China lilitoa taarifa iliyosema nchi zote mbili zinapaswa "kuendelea na kasi, kuendelea kusonga mbele katika mwelekeo sahihi kwa msingi wa usawa, heshima na manufaa ya pande zote".

    Viongozi hao walikutana Busan, Korea Kusini mnamo Oktoba, baada ya hapo walikubaliana kusitisha ushuru.

    Unaweza kusoma;

  4. Shirika la misaada ya Kibinadamu la Gaza linaloungwa mkono na Marekani lasitisha za misaada

    GHF tayari ilikuwa imesimamisha maeneo yake ya usambazaji wa misaada huko Gaza baada ya kusitisha mapigano kuanza kutumika mwezi uliopita.

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mfuko tata wa Kibinadamu wa Gaza (GHF) unaoungwa mkono na Marekani na Israel unasema unasitisha shughuli zake za misaada katika eneo la Palestina, baada ya karibu miezi sita.

    Shirika hilo tayari lilikuwa limesimamisha maeneo yake matatu ya usambazaji wa chakula huko Gaza baada ya kusitisha mapigano kati ya Hamas na Israel kuanza kutumika wiki sita zilizopita.

    GHF ililenga kuipita Umoja wa Mataifa kama mtoaji mkuu wa misaada kwa watu wa Gaza. Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya misaada yalikataa kushirikiana na mfumo wake, ukisema haukuwa wa kimaadili na si salama.

    Mamia ya Wapalestina waliuawa walipokuwa wakitafuta chakula huku kukiwa na matukio ya vurugu karibu na maeneo ya GHF, hasa kutokana na mashambulizi ya Israel, kulingana na Umoja wa Mataifa. Israel ilisema wanajeshi wake walifyatua risasi za onyo.

    GHF ilisema Jumatatu kwamba inasitisha shughuli sasa kwa sababu ya "kukamilika kwa mafanikio kwa misheni yake ya dharura", huku jumla ya vifurushi milioni tatu vikiwa na sawa na zaidi ya milo milioni 187 iliyowasilishwa kwa Wapalestina.

    Mkurugenzi mtendaji wa GHF, Jon Acree, pia alisema Kituo cha Uratibu wa Kijeshi na Kiraia (CMCC) kinachoongozwa na Marekani - ambacho kimeanzishwa kusaidia kutekeleza mpango wa amani wa Rais wa Marekani Donald Trump wa Gaza, "kitakuwa kikipitisha na kupanua mfumo wa majaribio wa GHF". Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Tommy Piggott aliandika kwenye X: "Mfumo wa GHF, ambapo Hamas haikuweza tena kupora na kufaidika kutokana na kuiba misaada, ulichangia pakubwa katika kuifikisha Hamas mezani na kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano."

    Hamas, ambayo inakanusha kuiba misaada, ilikaribisha kufungwa kwa GHF, Reuters iliripoti.

    Unaweza kusoma;

  5. Maafisa wa Marekani na Urusi kukutana Abu Dhabi

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Afisa wa Marekani amethibitisha kwa BBC kwamba watakutana na wawakilishi wa Urusi mjini Abu Dhabi ikiwa ni juhudi za hivi karibuni za utawala wa Rais Donald Trump kufanikisha makubaliano ya amani kati ya Urusi na Ukraine.

    Hatua hii inafuatia mazungumzo ya Geneva kati ya Marekani na Ukraine kuhusu rasimu ya mpango wa amani.

    Mkutano huo unafanyika baada ya maafisa wa Marekani na Ukraine kutaka kupunguza kasoro zilizopo kwenye mpango wa kumaliza vita huko Ukraine, wakikubali kurekebisha pendekezo la Marekani ambalo Kyiv na washirika wake wa Ulaya walilichukulia kama lenye kupendelea Urusi.

    Ilisemekana kuwa mkutano utafanyika leo Jumanne lakini haikuwa wazi ni nani angehudhuria katika ujumbe wa Urusi.

    Ikulu ya White House haikujibu mara moja ombi la Reuters la kutoa maoni.

    Pendekezo la hivi punde la amani la Marekani, mpango wenye vipengele 28, liliwavutia watu wengi katika serikali ya Marekani, Kyiv na Ulaya na kuzua wasiwasi mpya kwamba utawala wa Trump unaweza kuwa tayari kuishinikiza Ukraine kutia saini makubaliano ya amani ambayo yameegemea upande mmoja.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Mwanamke wa Thailand apatikana akiwa hai ndani ya jeneza

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mwanamke mmoja nchini Thailand aliwashangaza wafanyikazi wa hekalu alipoanza kusogea akiwa ndani ya jeneza lake baada ya kuletwa kama maiti kwa ajili ya kuchomwa.

    Wat Rat Prakhong Tham, hekalu la Wabuddha katika jimbo la Nonthaburi nje kidogo ya Bangkok, ilichapisha video kwenye ukurasa wake wa Facebook, ikimuonyesha mwanamke akiwa amelala kwenye jeneza jeupe nyuma ya lori, akisogeza mikono na kichwa kidogo, na kuwaacha wafanyakazi wa hekalu wakiwa wamechanganyikiwa.

    Pairat Soodthoop, meneja mkuu na masuala ya fedha wa hekalu hilo, aliambia The Associated Press siku ya Jumatatu kwamba kaka yake mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 65 alimsafirisha kutoka mkoa wa Phitsanulok kwa ajili ya kuchomwa moto.

    Alisema walisikia mlio kwa mbali ukitoka kwenye jeneza.

    "Nilishangaa kidogo, kwa hiyo niliwaomba wafungue jeneza, na kila mtu alishtuka," alisema. "Nilimwona akifungua macho yake kidogo na kugonga kando ya jeneza. Lazima alikuwa amegonga kwa muda mrefu."

    Kwa mujibu wa Pairat, kaka huyo alisema dada yake alikuwa amelazwa kwa takribani miaka miwili, hali yake ya afya ilidhoofika na kuonekana kufariki dunia baada ya kuacha kupumua siku mbili zilizopita.

    Kisha ndugu huyo alimweka ndani ya jeneza na kufunga safari ya kilomita 500 hadi hospitali moja huko Bangkok, ambako mwanamke huyo alikuwa ameeleza kwamba angependa kutoa viungo vyake kusaidia wengine.

  7. Wawili wafariki katika shambulizi la usiku kucha huko Kyiv, wanasema maafisa

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mji mkuu wa Ukraine, Kyiv umeshambuliwa na makombora na ndege zisizo na rubani za Urusi usiku kucha, huku maafisa wakisema takriban vyumba viwili vya makazi vilishambuliwa.

    Ikiandika kwenye mtandao wa Telegram, Huduma ya Dharura ya Jimbo la Ukraine inasema watu wawili wamefariki dunia na sita kujeruhiwa.

    Tymur Tkachenko, mkuu wa utawala wa kijeshi wa mji mkuu huo, anasema mmoja aliuawa wakati jengo la makazi la urefu wa juu lilishambuliwa katika wilaya kwenye ukingo wa mashariki wa Mto Dnipro.

    Huduma za dharura zilisema jengo la juu pia lilishambuliwa katika wilaya ya Pechersk katikati mwa jiji, huku moto ukisababisha uharibifu kwenye orofa tatu kabla ya kudhibitiwa.

    "Lazima tufahamu kwamba Urusi haitapunguza shinikizo lake kwa Ukraine," Rais Volodymyr Zelensky alisema hapo awali, wakati jeshi lake la anga lilipotoa onyo la kombora nchi nzima.

    Soma zaidi:

  8. Afrika yaongoza kwa mauaji ya wanawake – Ripoti ya UN

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Takwimu zilizotolewa na Umoja wa Mataifa zaonyesha kwamba mwaka jana wanawake na wasichana elfu hamsini ulimwenguni pote waliuawa na watu wa karibu au wanafamilia familia - sawa na mtu mmoja kufa karibu kila dakika 10 (kumi).

    Kulingana na data kutoka nchi 117 takriban wanawake na wasichana 50,000 waliuawa na wapenzi wa karibu au wanafamilia mnamo 2024, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Madawa ya Kulevya na Uhalifu na Wanawake ilisema katika ripoti iliyotolewa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake.

    Ripoti hiyo iliongeza kuwa asilimia 60 ya wanawake waliuawa duniani kote na wenzi au jamaa kama vile baba, wajomba, mama na ndugu.

    Ripoti ya Umoja wa Mataifa inasema chakusikitisha zaidi ni kwamba hakuna dalili ya hali hii kubadilika na "nyumbani kunaendelea kuwa mahali hatari kwa wanawake na wasichana katika suala la hatari ya kuuawa."

    Idadi hiyo ni ndogo kuliko takwimu iliyoripotiwa mnamo 2023, ingawa haionyeshi kupungua katika uhalisia, kulingana na ripoti, kwani inatokana na tofauti za upatikanaji wa data kutoka nchi hadi nchi.

    Hakuna eneo duniani lililokosa visa vya mauaji ya wanawake, lakini Afrika ilikuwa na idadi kubwa zaidi mwaka jana ikiwa na karibu 22,000, ripoti hiyo ilisema.

    "Mauaji ya wanawake sio kuwa ni tukio moja moja. Mara nyingi huwa ni kwenye mfululizo wa unyanyasaji ambao unaweza kuanza na kudhibiti tabia, vitisho, na unyanyasaji - ikiwa ni pamoja na mtandaoni," Sarah Hendricks, Mkurugenzi wa Kitengo cha Sera za Wanawake wa Umoja wa Mataifa, alisema katika taarifa.

    Ripoti hiyo ilisema maendeleo ya kiteknolojia yamezidisha aina fulani za unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana na kuunda zingine, kama vile kushirikisha picha bila ridhaa, utafutaji taarifa mitandaoni na video za uwongo.

    "Tunahitaji utekelezaji wa sheria zinazotambua jinsi unyanyasaji unavyojitokeza katika maisha ya wanawake na wasichana, mtandaoni na nje ya mtandao, na kuwawajibisha wahalifu kabla haujawa mbaya," alisema Hendricks.

    Soma zaidi:

  9. Watoto tisa wauawa katika shambulizi la Pakistan, Taliban inasema

    /

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Takriban watoto tisa na mwanamke mmoja wameuawa baada ya vikosi vya Pakistan kushambulia kwa bomu nyumba ya mkazi wa eneo hilo katika mkoa wa Khost nchini Afghanistan, msemaji wa Taliban wa Afghanistan Zabihullah Mujahid alisema Jumanne.

    Mujahid alisema Pakistan pia ilifanya uvamizi katika majimbo ya Kunar na Paktika, na kuwajeruhi raia wanne.

    "Jana usiku saa 12 katika wilaya ya Gerbzwo mkoa wa Khawst, wanajeshi wavamizi wa Pakistani walishambulia kwa mabomu nyumba ya mkazi wa eneo hilo Wilayat Khan, ambayo iliua watoto 9 (wavulana 5 na wasichana 4) na mwanamke mmoja, na kuharibu nyumba yao," Mujahid alisema katika chapisho kwenye X, iliyoambatana na picha za waliokufa.

    Jeshi la Pakistani na wizara ya mambo ya nje haikuweza kupatikana kwa ajili ya kutoa maoni nje ya saa za kazi.

    Uvamizi huo umefanyika siku moja baada ya milipuko miwili ya kujitoa mhanga kuwaua wanajeshi watatu huko Peshawar nchini Pakistan.

    Wanajeshi wa Pakistan na Afghanistan walipigana mnamo mwezi Oktoba, na kuua makumi ya watu, katika ghasia mbaya zaidi tangu Taliban kurejea madarakani nchini Afghanistan mwaka 2021.

    Pande zote mbili zilitia saini makubaliano ya kusitisha mapigano mjini Doha mwezi Oktoba, lakini mazungumzo ya amani nchini Uturuki yalisambaratika bila ya makubaliano ya muda mrefu kutokana na kutoelewana kuhusu makundi ya wapiganaji wanaoipinga Pakistan ambayo yanaendesha harakati zake ndani ya Afghanistan.

    Soma zaidi:

  10. RSF yasema itaingia katika makubaliano ya kusitisha mapigano

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mkuu wa Kikosi cha Rapid Support Forces nchini Sudan amesema siku ya Jumatatu kwamba wanamgambo wake wataingia mara moja katika mapatano ya kusitisha vita ya miezi mitatu, baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kusema wiki iliyopita kwamba angeingilia kati kutafuta kukomesha vita ambavyo vimeitumbukiza nchi hiyo katika baa la njaa.

    Marekani, Umoja wa Falme za Kiarabu, Misri na Saudi Arabia - inayojulikana kama Quad - mapema mwezi huu ilipendekeza mpango wa makubaliano ya miezi mitatu na kufuatiwa na mazungumzo ya amani. RSF ilijibu kwa kusema imekubali mpango huo, lakini mara tu baada ya kushambulia eneo la jeshi kwa mfululizo wa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani.

    Taarifa ya Jumatatu ilionekana kutangaza kusitisha mapigano kwa upande mmoja. Taarifa hiyo imetolewa siku moja baada ya mkuu wa jeshi la Sudan kukataa mapendekezo ya Quad, na kukosoa kujumuishwa kwa Umoja wa Falme za Kiarabu, ambayo imekuwa ikishutumiwa sana kwa kuipatia silaha RSF, kama mpatanishi.

    Taifa hilo la Ghuba limekanusha shutuma hizo na kusema kuwa linalenga kusitisha vita.

    "Katika kukabiliana na juhudi za kimataifa, hasa zile za Rais wa Marekani Donald Trump ... natangaza usitishaji mapigano ikiwa ni pamoja na kusitishwa kwa uhasama kwa miezi mitatu," Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo wa RSF alisema katika hotuba yake Jumatatu.

    "Tunatumai nchi za Quad zitatekeleza jukumu lao katika kushinikiza upande mwingine kufikia hatua hii," aliongeza.

    Maoni yake yanajitokeza wakati ambapo RSF imekuwa ikishutumiwa kwa mashambulizi ya kikatili dhidi ya raia baada ya kuchukua mji wa El Fasher mwishoni mwa Oktoba.

    Unyakuzi huo uliimarisha udhibiti wake wa eneo la Darfur, na kikosi hicho hatimaye kimeongeza mashambulizi katika eneo la Kordofan katika jitihada za kuchukua udhibiti wa nchi.

    Mkuu wa jeshi la Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, katika hotuba yake siku ya Jumapili alishutumu pendekezo la Marekani kwa lengo la kudhoofisha jeshi la Sudan huku likiruhusu RSF kudumisha eneo ambalo imeteka.

    Soma zaidi:

  11. Zelensky aunga mkono marekebisho ya mpango wa amani unaopendekezwa

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amekaribisha mabadiliko yaliyopendekezwa kwenye mpango wa amani wenye vipengele 28 wenye utata wa kumaliza vita na Urusi.

    Inaonekana washirika wa Ukraine wa Ulaya walitoa toleo lililorekebishwa la mpango huo baada ya kukataa sehemu ambazo zilipendelea malengo ya Urusi.

    "Sasa orodha ya hatua muhimu za kumaliza vita inaweza kufikiwa ..." Zelensky alisema kwenye mtandao wa Telegraph. "Vipengele vingi sahihi vimejumuishwa katika mfumo huu."

    Akizungumzia mpango huo, Zelensky alisema Jumatatu jioni kwamba kurekebishwa kwake ndio "njia sahihi".

    "Masuala nyeti, mambo nyeti zaidi, nitajadili na Rais Trump," aliongeza, bila kusema ni lini.

    Kulingana na afisa katika ofisi ya Zelensky, mpango huo wenye vipengele 28 uliovuja siku ya Ijumaa umebadilishwa.

    Urusi imekuwa ikiitaka Ukraine ijitoe kikamilifu kutoka eneo lote la mashariki mwa Donbas, linaloundwa na mikoa ya Donetsk na Luhansk. Pia inadhibiti eneo la Crimea na sehemu kubwa za mikoa mingine miwili, Kherson na Zaporizhzhia.

    Makumi ya maelfu ya wanajeshi na raia wameuawa au kujeruhiwa, na mamilioni ya watu wamekimbia makazi yao, tangu uvamizi kamili wa Urusi uanze karibu miaka minne iliyopita.

    Soma zaidi: