Je, Israel inatambua vipi maeneo ya kushambulia nchini Iran?

Picha ya setilaiti ya Israel ya makao makuu ya televisheni ya Iran kabla ya kulipuliwa tarehe 2 Machi.

Chanzo cha picha, Israeli source

Maelezo ya picha, Picha ya setilaiti ya Israel ya makao makuu ya televisheni ya Iran kabla ya kulipuliwa tarehe 2 Machi.
    • Author, Muhannad Tutunji
    • Nafasi, BBC News Arabic Reporting from,Jerusalem
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Israel inategemea kwa kiwango kikubwa teknolojia za kisasa za upelelezi, ufuatiliaji na uchambuzi wa taarifa ili kubaini malengo yake ya kijeshi katika vita inayotekeleza kwa kushirikiana na Marekani dhidi ya Iran. Kwa mujibu wa chanzo cha kijasusi cha Israel kilichozungumza na BBC, hatua hii imeiwezesha kutekeleza operesheni za angani baada ya kufanya zaidi ya mashambulizi 8,500 ndani ya Iran kwa kutumia zaidi ya makombora 15,000.

Teknolojia hizo zinajumuisha satelaiti zinazoendeshwa na kitengo cha ujasusi wa kijeshi, mifumo ya uchambuzi wa data, ndege za kivita, ndege zisizo na rubani (droni) pamoja na sensa za hali ya juu.

Chanzo hicho kilielezea BBC kuwa satelaiti hizo huruhusu Israel kufuatilia kwa wakati halisi maeneo ya kurushia makombora ndani ya Tehran, na hivyo kuyaainisha na kuyashambulia kabla Israel haijashambuliwa.

Kwa mujibu wa chanzo hicho ambacho hakikutaka kutajwa, uwezo wa ufuatiliaji wa anga umegeuka kuwa nguzo kuu ya juhudi za kijasusi, huku satelaiti zikifuatilia mji mkuu wa Iran saa 24 kwa siku na kutoa taarifa kwa haraka kwa viongozi wa Israel wanaotoa maamuzi.

Tathmini ya ujasusi wa kijeshi wa Israel inaeleza kuwa operesheni dhidi ya Iran iliyopewa jina la "Lion's Roar" imesababisha uharibifu mkubwa kwa uwezo wa kijeshi wa Iran.

Katika shambulizi la mwanzo, inadaiwa kuwa maafisa waandamizi wa Iran wapatao 40 waliuawa ndani ya sekunde 40, pamoja na kulenga vituo vitatu vya amri ya Walinzi wa Mapinduzi IRGC, ikiwa ni pamoja na maeneo yaliyounganishwa na Kiongozi Mkuu, Baraza Kuu la Usalama wa Taifa, na serikali. Hali iliyosababisha mkanganyiko katika mfumo wa maamuzi wa Iran.


Picha ya setilaiti ya Israel ya makao makuu ya televisheni ya Iran baada ya kulipuliwa.

Chanzo cha picha, Israeli source

Maelezo ya picha, Picha ya setilaiti ya Israel ya makao makuu ya televisheni ya Iran baada ya kulipuliwa.

Ingawa Iran imethibitisha vifo vya baadhi ya viongozi wake, BBC imeshindwa kubainisha kwa uhuru idadi ya mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Israel dhidi ya Iran.

Tangu kuanza kwa vita tarehe 28 Februari, viongozi kadhaa wa ngazi za juu, akiwemo Kiongozi Mkuu Ali Khamenei na maafisa wa juu wa kijeshi, wameripotiwa kuuawa, huku Mojtaba Khamenei akichukua nafasi ya uongozi.

Kwa upande wake, Iran imejibu kwa mashambulizi ya makombora na droni dhidi ya Israel na kambi za Marekani katika eneo la Ghuba, pamoja na kudhibiti Mlango-Bahari wa Hormuz kwa kuruhusu upitishaji wa meli kwa masharti maalum.

Chanzo hicho kinaeleza kuwa mfumo wa uchambuzi wa kijasusi hufuatilia kwa wakati halisi mabadiliko ya uwanjani, ikiwemo ujenzi mpya, ukarabati wa vituo vya kijeshi na usafirishaji wa silaha. "IDF ilitumia uwezo huu wakati wa mashambulizi ya awali ya operesheni ili kufuatilia mienendo ya adui, kuhakikisha kuwa mashambulio hayo yalitekelezwa kama ilivyopangwa, na kutathmini athari katika uwanja wa vita''.

Malengo makuu: nyuklia na makombora ya balistiki

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa mujibu wa chanzo hicho, Jeshi la Anga la Israel limefanikiwa kwa muda mfupi kupata udhibiti mkubwa wa anga, hali iliyowezesha mashambulizi ya kimfumo dhidi ya miundombinu ya kijeshi ya Iran hasa mifumo ya makombora ya balistiki kwa kulenga majukwaa ya kurushia na kupunguza uwezo wake.

Mashambulizi hayo pia yalilenga viwanda vya kijeshi vinavyohusiana na utengenezaji wa makombora na droni, pamoja na miundombinu ya mpango wa nyuklia wa Iran, kwa lengo la kudhoofisha uwezo wake wa kujiendeleza.

Chanzo hicho cha kijasusi kilieleza kuwa operesheni hiyo inaendeshwa kwa mujibu wa mpango uliopangwa kwa umakini, ukitumia udhibiti wa anga kufuatilia kwa wakati halisi majukwaa ya kurushia makombora na vikundi vya operesheni uwanjani. Kilibainisha kuwa mashambulizi ya mfululizo yamesababisha kudhoofika kwa kiasi kikubwa kwa uwezo wa Iran wa kuitishia Israel na nchi nyingine za eneo hilo yaani Mashariki ya kati.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Israel, takriban Waisraeli 5,229 wamejeruhiwa kutokana na mashambulizi ya makombora na droni kutoka Iran katika maeneo mbalimbali ndani ya nchi hiyo.

Moja ya makombora hayo lililenga maeneo ya Arad na Dimona, ambako inaaminika kuwa kuna kinu cha nyuklia cha Israel kilicho umbali wa chini ya kilomita 20.

Chanzo cha kijasusi kinasema kuwa Israel imefanikiwa kuharibu au kuzima takriban asilimia 70 ya maeneo ya kurushia makombora na karibu asilimia 80 ya mifumo ya ulinzi wa anga ya Iran. Aidha, zaidi ya maeneo 700 ya kijeshi yanayohusiana na mfumo wa makombora yameshambuliwa, huku maelfu ya wanajeshi wa Walinzi wa Mapinduzi IRGC na vikosi vya utawala huo wakiripotiwa kuuawa.

Hata hivyo, mashambulizi ya Iran yanaendelea kusababisha uharibifu wa mali na vifo ndani ya Israel na baadhi ya nchi za Ghuba, huku maafisa wa Iran wakidai bado hawajatumia uwezo wao wote wa kijeshi.

Bendera ya Iran inapepea juu ya vifusi mjini Tehran.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Bendera ya Iran inapepea juu ya vifusi mjini Tehran.

Gharama za kibinadamu na kiuchumi

Chanzo cha kijeshi cha Israel kinasema mipango ya mashambulizi huzingatia kupunguza madhara kwa raia kwa kuchagua aina ya silaha, muda na mbinu za utekelezaji, na wakati mwingine kutoa tahadhari mapema. Kila shambulizi hupimwa ili kuhakikisha madhara yake hayazidi faida ya kijeshi inayotarajiwa.

Maafisa wa Iran wameishutumu Marekani na Israel kwa mashambulizi yaliyosababisha vifo vya watu 168 katika shule moja kusini mwa Iran siku ya kwanza ya vita.

Hata hivyo, hakuna nchi kati ya hizo mbili iliyokubali kuwajibika, ingawa Waziri wa Ulinzi wa Marekani amesema uchunguzi wa kijeshi unaendelea. Hii inafuatia ripoti na uchambuzi wa vyombo vya habari vya Marekani, hususan CNN na The New York Times, unaoashiria uwezekano mkubwa kuwa tukio hilo lilisababishwa na makombora ya Marekani aina ya Tomahawk.

Ikitoa maoni kuhusu shambulizi hilo la shule ya Menab, Israel imesema haikuwa na ufahamu wa operesheni yoyote katika eneo hilo.

Kukatika kwa huduma za intaneti nchini Iran kumezuia uthibitisho huru wa maelezo ya tukio hilo pamoja na idadi kamili ya waliouawa na kujeruhiwa. Hata hivyo, shirika la Amnesty International limetoa wito wa kuwawajibisha waliopanga na kutekeleza shambulizi hilo, likilitaja kuwa "kinyume cha sheria," dhidi ya shule ya Minab ambayo iliripotiwa kuwa na zaidi ya watoto 100 miongoni mwa waathiriwa.

Chanzo hicho kilithibitisha kuwa jeshi la Israel "linajutia mauaji yoyote ya raia," na kusisitiza kuwa juhudi zinafanywa ili kupunguza vifo hivyo, na kufafanua kuwa operesheni zake zinalenga utawala wa Iran, na sio idadi ya watu.

Israel inasisitiza kuwa inalenga utawala wa Iran na si raia, huku Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu akiwahimiza wananchi wa Iran kuchukua hatua dhidi ya uongozi wao, akisema hali iliyopo ni "fursa ya kipekee ya kurejesha uhuru."

Moshi mwingi unafuka juu ya matangi ya kuhifadhia mafuta yaliyolengwa katika shambulio la anga la pamoja la Israel na Marekani kwenye kituo kaskazini magharibi mwa Tehran. Machi 8, 2026.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Moshi mwingi unafuka juu ya matangi ya kuhifadhia mafuta yaliyolengwa katika shambulio la anga la pamoja la Israel na Marekani kwenye kituo kaskazini magharibi mwa Tehran. Machi 8, 2026.

Kwa upande wa gharama za kiuchumi, operesheni hiyo inakadiriwa kugharimu mabilioni ya dola kwa siku, ingawa haijabainishwa kama inajumuisha athari kwa uchumi wa Israel kwa ujumla.

Akijibu swali la BBC kuhusu ongezeko la vifo vya raia vinavyotokana na mashambulizi ya Israel kama ilivyoripotiwa na mashirika ya haki za binadamu na Wizara ya Afya ya Iran chanzo cha kijeshi cha Israel kilisema kuwa jeshi la nchi hiyo linaendesha operesheni zake kwa kuzingatia sheria za kimataifa, kikisisitiza kuwa kinacholengwa ni kile kinachoitwa "utawala" na si raia.

Shirika la Habari la Wanaharakati wa Haki za Binadamu (HRANA), linalojishughulisha na masuala ya Iran, limesema limeripoti vifo vya angalau raia 1,400 wa Iran tangu kuanza kwa vita, wakiwemo watoto 214.

Limeeleza kuwa takwimu zake zinatokana na ushahidi uliothibitishwa kutoka maeneo mbalimbali nchini humo, ikiwemo taarifa za vyanzo vya uwanjani, video na picha za kuaminika.

HRANA, ambalo ni shirika lisilo la kiserikali lililosajiliwa nchini Marekani, limekuwa likifuatilia ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Iran kwa takriban muongo mmoja kupitia watafiti na wanaharakati wake.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid