Mahakama ya Uganda imepinga agizo la Chama cha Wanasheria Uganda (Uganda Law Society - ULS) lililowaelekeza wanachama wake kuacha kuwaita majaji kwa vyeo vya heshima kama "My Lord" na "My Lady", pamoja na kusitisha utamaduni wa kuwainamia wanapoingia mahakamani.
Katika agizo hilo, ULS ilisema kuwa vyeo hivyo ni mabaki ya mfumo wa kikoloni ambao huwapa majaji hadhi ya juu kuliko raia, ilhali wananchi ndio waajiri wao kupitia mamlaka ya dola.
Hata hivyo, msemaji wa Mahakama ya Uganda, James Ereemye, aliiambia BBC kuwa ULS haina mamlaka ya kuwaelekeza majaji jinsi ya kuendesha mahakama au namna ya kuheshimiwa. Alisisitiza kuwa mahakama itaendelea kudai maadili na heshima za kawaida kutoka kwa mawakili.
Kama ilivyo kwa nchi nyingi zilizokuwa makoloni ya Uingereza, Uganda ilirithi mfumo wake wa sheria pamoja na mila nyingi za mahakama kutoka Uingereza.
ULS imesema mfumo huo wa kikoloni na taratibu zake za zamani umechangia kudhoofika kwa mfumo wa utoaji haki nchini Uganda.
Chama hicho pia kilieleza kuwa desturi za kuwainamia majaji na kutumia vyeo vya heshima zinawalazimisha Waganda kujidhalilisha mbele ya wenye mamlaka.
Katika taarifa iliyotiwa saini na rais wa ULS, Isaac Ssemakadde, chama hicho kilipiga marufuku wanachama wake kuwainamia maafisa wa mahakama na kuwataka waache kutumia vyeo kama "My Lord", "Your Lordship", "My Lady" na "Your Worship", kama sehemu ya juhudi za kuondoa athari za ukoloni katika mfumo wa haki na kurejesha heshima kwa wananchi.
Badala yake, Chama cha Wanasheria Uganda (ULS) kimewataka mawakili kutumia namna rahisi za kuwahutubia maafisa wa mahakama kama vile "Bw. Jaji", "Bi. Jaji", "Bw. Hakimu", "Bi. Hakimu", au kutumia majina yao ya ukoo pale inapofaa.
ULS pia ilisema kuwa mawakili na washtaki na washtakiwa wote wanaofika mbele ya mahakama au vyombo vya utoaji haki wanapaswa kusimama wima na kuzungumza kama raia huru, bila kuonesha ishara zozote za unyenyekevu wa lazima.
Akijibu agizo hilo, msemaji wa Mahakama ya Uganda, James Ereemye, alisema mahakama ni mhimili huru wa serikali na haiwezi kupewa maelekezo na chombo chochote cha nje kuhusu namna ya kuendesha shughuli zake.
Aliipuuza ULS akisema ni "kikundi cha vijana ambao hawajaelewa misingi ya kuweka ajenda katika usimamizi na utawala."
Ereemye aliongeza kuwa ikiwa kuna hoja kuhusu mabadiliko ya taratibu za mahakama, zinapaswa kuwasilishwa kupitia vikao rasmi vya majadiliano ili zikikubalika, ziwe sehemu ya sera au miongozo rasmi ya mahakama.