Chris Brown aamriwa kumlipa mfanyakazi wake wa nyumbani dola milioni 13 baada ya kushambuliwa na mbwa
Mwimbaji wa Marekani Chris Brown amepatikana na hatia na kutakiwa kuwajibika kisheria kwa shambulio la mbwa lililomjeruhi vibaya na kumwacha mfanyakazi wake wa nyumbani akiwa na ulemavu wa kudumu nyumbani kwake mwaka 2020.
Baada ya kesi iliyodumu kwa wiki mbili mjini Los Angeles, jopo la majaji lilitoa uamuzi kwa manufaa ya Maria Avila, ambaye alishambuliwa na mbwa aina ya Caucasian Shepherd mwenye uzito wa takriban kilo 90, anayemilikiwa na Brown, alipokuwa akimwaga taka nyumbani kwake eneo la Tarzana.
Brown pamoja na kampuni yake, Black Pyramid LLC, sasa wanatakiwa kumlipa Avila fidia ya dola za Marekani milioni 12.9 kutokana na uzembe, kwa mujibu wa chapisho la Marekani Billboard.
BBC News imewasiliana na wawakilishi wa Brown ili kupata maoni yao kuhusu uamuzi huo.
Avila alisema mbwa huyo, anayeitwa Hades, alimnyofoa vipande vikubwa vya ngozi yake, jambo lililosababisha uharibifu wa kudumu wa uso, makovu, kupoteza uwezo wa kuona kwa kiwango fulani na kuharibika kwa mishipa ya fahamu.
Brown alidai kuwa mbwa huyo alikuwa akifugwa kwa madhumuni ya ulinzi wa nyumba na hakuwa mnyama wake wa kufugwa binafsi.
Wakati wa kesi hiyo, mahakama ilisikia ushahidi ulioonesha kuwa badala ya kupiga simu kwa huduma za dharura au kumsaidia Avila mwenyewe baada ya shambulio, Brown aliondoka eneo la tukio, kwa mujibu wa Rolling Stone.
Majaji pia walielezwa kuwa Brown aliwaacha wafanyakazi wake wamuhudumie Avila, akisema aliogopa kuwapo kwake au sauti yake kusikika kwenye simu ya dharura ya 911 kungesababisha "msisimko mkubwa wa vyombo vya habari" polisi walipowasili.
Chris Brown alisema alikuwa anajiandaa kuoga alipomsikia mbwa akinguruma, ndipo akashuka chini na kumkuta Maria Avila akiwa amelala bila kutikisika na akiwa ametapakaa damu nyingi.
"Kuona damu nyingi kulinishtua sana," alisema, akiongeza kuwa alikuwa katika hali ya mshtuko alipoamua kufuata ushauri wa meneja wake wa kuondoka eneo la tukio kabla ya wahudumu wa dharura kufika.
Brown alikiri kuwa alikuwa na sehemu ya kuwajibika kabla ya kesi kuanza, lakini alipinga kiwango cha majeraha aliyopata Avila na kudai kuwa Avila pia alikuwa na mchango katika kutokea kwa tukio hilo.
Mwimbaji huyo alisema alikuwa amewaonya dada hao wawili waliokuwa wafanyakazi wa nyumbani kuwa mbwa hao "hawakuwa kabisa wa kirafiki", na aliwaambia watoke nje ya nyumba tu pale walinzi walipokuwa wamefika.
Hata hivyo, wafanyakazi hao wawili walikanusha kuwa kuliwahi kufanyika mazungumzo kati yao na Brown, wakisema pia kuwa tofauti ya lugha ilifanya mazungumzo ya aina hiyo kuwa kutofanyika kwa urahisi.