Moja kwa moja, Iran yasema inapendelea mazungumzo, lakini iko tayari kwa vita pia

Mpatanishi mkuu wa upande wa Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf, ameeleza katika mahojiano na televisheni ya taifa ya nchi hiyo kuwa Tehran haitaacha kujilinda iwapo mazungumzo na Marekani hayatatoa matokeo.

Skip Video and continue reading
  • Lungu
  • xx
  • xx
  • d
  • s
  • a
  • Sonko
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx
  • Dangote
  • xx
  • Lydia Wanjiku

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Iran yatangaza likizo ya umma ili kujiandaa kwa mazishi ya Khamenei

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Serikali ya Iran imetangaza Jumanne, Julai 6, kuwa siku ya mapumziko ya umma mjini Tehran.

    Msemaji wa serikali ya Iran, Fatima Mohajerani, amesema hatua hiyo inalenga kuwezesha waombolezaji wa kiongozi wa zamani wa Iran kurejea kutoka mji mkuu.

    Pia amesema siku ya maombolezo ya kitaifa itaadhimishwa nchini Iran siku ya Alhamisi, huku mazishi ya Ali Khamenei yakitarajiwa kufanyika mjini Mashhad Julai 8.

    Kwa mujibu wa ratiba rasmi, sala za mazishi na shughuli za kuaga mwili wa Khamenei zitafanyika kati ya Julai 4 na 8 katika miji ya Tehran, Qom na Mashhad. Hafla za kutoa pole pia zitafanyika katika miji ya Baghdad, Kazmin, Karbala na Najaf nchini Iraq.

    Inakumbukwa kuwa Ali Khamenei aliuawa katika mashambulizi ya anga ya Marekani na Israel dhidi ya Iran yaliyolenga makazi na ofisi yake, maarufu kama Nyumba ya Uongozi, lakini hadi sasa bado hajazikwa.

    Unaweza kusoma;

  2. Mvulana wa miaka mitatu aokolewa akiwa hai siku sita baada ya tetemeko la ardhi Venezuela

    m

    Chanzo cha picha, Jordan Public Security via Reuters

    Mvulana mwenye umri wa miaka mitatu ameokolewa akiwa hai kutoka chini ya vifusi siku sita baada ya matetemeko makubwa ya ardhi yaliyolikumba Venezuela, timu ya uokoaji kutoka Jordan imesema.

    Mtoto huyo, aliyetambuliwa kwa jina la Klieber Morán, aliokolewa kutoka kwenye vifusi katika jimbo la La Guaira, kwa mujibu wa Rais wa mpito wa Venezuela, Delcy Rodríguez, ambaye alieleza uokoaji huo kuwa "chanzo cha matumaini kwa watu wetu."

    Tukio hilo limejiri huku Umoja wa Mataifa ukionya kwamba makumi ya maelfu ya watu wanahitaji kwa dharura chakula na makazi.

    Idadi ya vifo kutokana na matetemeko ya ardhi ya wiki iliyopita, yaliyokuwa na ukubwa wa 7.2 na 7.5, imefikia watu 1,943, huku zaidi ya watu 10,000 wakijeruhiwa na makumi ya maelfu wengine wakiwa hawajulikani waliko.

    Kwa mujibu wa tathmini ya awali ya data za satelaiti za NASA, matetemeko hayo huenda yaliharibu au kubomoa majengo 58,870.

    Idara ya Ulinzi wa Raia ya Jordan ilisema Klieber alipatiwa huduma ya kwanza, akapelekwa hospitalini na hali yake ilikuwa nzuri. Anaendelea kupatiwa matibabu katika mji mkuu, Caracas.

    Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) lilisema upungufu wa chakula umeenea, huduma za msingi zimevurugika na mawasiliano mengi yamekatika katika jimbo la La Guaira.

    "Mvutano ndani ya jamii unaongezeka huku upatikanaji wa misaada ukiendelea kuwa mgumu," UNHCR ilisema katika taarifa yake.

  3. Bilionea wa China ahukumiwa miaka 30 jela Marekani kwa ulaghai wa dola bilioni moja

    d

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Guo Wengui, ambaye wakati mmoja aliaminika kuwa miongoni mwa watu matajiri zaidi nchini China, amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela nchini Marekani kwa kuendesha ulaghai wa zaidi ya dola bilioni moja.

    Bilionea huyo wa zamani wa sekta ya mali isiyohamishika alikimbilia Marekani mwaka 2017, ambako alijijenga upya kama mkosoaji wa Chama cha Kikomunisti cha China na kupata wafuasi wengi mtandaoni.

    Hata hivyo, baadaye alipatikana na hatia ya makosa ya uhalifu wa kupangwa, ulaghai na utakatishaji fedha.

    Jaji wa New York, Analisa Torres, alisema Guo aliwalaghai watu waliokuwa wakitafuta kuleta demokrasia nchini China na kutumia fedha zao kugharimia maisha yake ya anasa.

    Wakili wake, Melinda Sarafa, alisema hukumu hiyo ni kali kupita kiasi na haikuzingatia maelfu ya wawekezaji wake ambao wanasema hawakulaghaiwa.

    Guo amesisitiza kuwa hana hatia na atakata rufaa dhidi ya hukumu na adhabu hiyo.

    Mwanasheria wa serikali ya Marekani, Sean Buckley, amesema:

    "Hukumu ya leo inaonyesha kuwa umaarufu na utajiri haviweki mtu juu ya sheria, na walaghai wanaowaathiri wengine ili kujinufaisha watakabiliwa na madhara makubwa."

    Kabla ya kuondoka China, Guo alijijengea utajiri mkubwa kupitia biashara za mali isiyohamishika na alikuwa na uhusiano mzuri na serikali ya China.

    Hata hivyo, aliomba hifadhi nchini Marekani baada ya kutuhumiwa na maafisa waandamizi wa China kwa ufisadi.

  4. Iran yasema inapendelea mazungumzo, lakini iko tayari kwa vita pia

    .

    Chanzo cha picha, CBS

    Mazungumzo ya kidiplomasia kati ya Iran na Marekani yanaendelea huku Iran ikisisitiza kuwa, pamoja na kuipa kipaumbele njia ya mazungumzo, bado iko tayari kurejea vitani ikiwa juhudi hizo zitashindwa.

    Hayo yameelezwa na mpatanishi mkuu wa upande wa Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf, ambaye alisema katika mahojiano na televisheni ya taifa kuwa Tehran haitaacha kujilinda iwapo mazungumzo hayatatoa matokeo.

    "Tunafuata njia ya mazungumzo, lakini ikiwa mazungumzo hayatatekelezwa, pia tuko tayari kwa vita na tutajibu ipasavyo," alisema Ghalibaf.

    Kauli hiyo ilitolewa wakati wajumbe wa Iran na Marekani walipokuwa wakitarajiwa kufanya mazungumzo mengine mjini Doha, yakilenga kupunguza mvutano na kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro uliodumu kwa miezi kadhaa.

    Mvutano huo uliongezeka mwezi Juni 2026, baada ya mashambulizi ya kijeshi kati ya Iran na Israel, yaliyohusisha pia mashambulizi ya Marekani dhidi ya baadhi ya maeneo ya nyuklia ya Iran. Baada ya siku kadhaa za mapigano, pande husika zilikubaliana kusitisha mapigano kwa muda ili kutoa nafasi kwa juhudi za kidiplomasia.

    Ingawa mapigano yamesitishwa kwa sasa, bado hakuna makubaliano ya kudumu yaliyofikiwa.

  5. Kombe la Dunia: Ivory Coast yaaga, Afrika yasalia na timu saba

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Ivory Coast imekuwa timu ya pili ya Afrika kuondolewa katika hatua ya 32 bora ya Kombe la Dunia baada ya kufungwa mabao 2-1 na Norway, na kuziacha timu saba za bara hilo zikiendelea na harakati za kutinga hatua ya 16 bora.

    Kuondolewa kwa Ivory Coast kunaiunganisha na Afrika Kusini, ambayo iliaga hatua hiyo mapema, huku Tunisia ikiwa ilitolewa katika hatua ya makundi.

    Katika mechi nyingine zilizochezwa usiku wa kuamkia leo, Ufaransa ilitinga hatua ya 16 bora baada ya kuichapa Sweden mabao 3-0, wakati Mexico nayo ilifuzu kwa kuishinda Ecuador mabao 2-0, asubuhi hii.

    Sasa matumaini ya Afrika yapo kwa timu saba zilizobaki kwenye mashindano hayo.

    Usiku wa leo saa moja usiku, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) itavaana na England, huku saa tano usiku Senegal ikikabiliana na Ubelgiji kuwania nafasi ya kutinga hatua ya 16 bora.

    Ratiba ya Ijumaa inaonyesha Algeria ikicheza dhidi ya Uswisi, wakati Misri itavaana na Australia.

    Maelezo zaidi:

  6. Marekani yaombwa kuangalia upya uhusiano wake na Uganda

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Baada ya kufungwa kwa vyombo vya habari Seneta wa Marekani, Jim Risch, ametaka kufanyika kwa mapitio ya uhusiano wa kiusalama kati ya Washington na Uganda.

    Risch, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti ya Marekani inayoshughulikia Masuala ya Nje, amesema Uganda huenda isiwe mshirika anayefaa kufuatia kufungwa kwa baadhi ya vyombo vya habari hivi karibuni kwa agizo lililoidhinishwa na Mkuu wa Majeshi ya Uganda, Muhoozi Kainerugaba.

    “Marekani inahitaji kupitia upya uhusiano wake wa kiusalama na Uganda. Mashambulizi ya Jenerali Muhoozi Kainerugaba dhidi ya uhuru wa kujieleza, yakiwemo ya kufunga taasisi kubwa za habari mwishoni mwa wiki hii, yanamfanya yeye pamoja na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda kuwa washirika wasiofaa.''

    Tunapaswa kushirikiana tu na wale wanaoimarisha usalama wa kikanda, si wanaoudhoofisha,” Risch aliandika kwenye ujumbe wake katika mtandao wa X almaarufu Twitter.

    Soma zaidi:

  7. Trump aingiza zaidi ya dola bilioni moja kutokana na sarafu za kidijitali tangu arejee madarakani

    f

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Marekani Donald Trump aliingiza zaidi ya dola bilioni moja kupitia shughuli zinazohusiana na sarafu za kidijitali mwaka jana, kwa mujibu wa ripoti yake ya lazima ya mwaka 2025 ya kutangaza mali zake.

    Katika ripoti hiyo yenye kurasa 927, Trump amesema alipata dola milioni 635 kutokana na mrabaha wa sarafu ya kidijitali ya Trump meme coin, ambayo thamani yake imeshuka kwa kiasi kikubwa tangu ilipozinduliwa siku tatu kabla ya kuapishwa kwake.

    Pia amesema alipata zaidi ya dola milioni 500 kutoka World Liberty Financial, kampuni ya sarafu za kidijitali iliyoanzishwa na wanawe pamoja na watoto wa mjumbe wake maalum wa Mashariki ya Kati, Steve Witkoff.

    Mbali na hilo, Trump alipata mamilioni ya dola kupitia biashara za mali isiyohamishika na bidhaa zinazobeba jina la Trump.

    Hata hivyo, Ikulu ya White House imekanusha kuwa Trump ananufaika kifedha kutokana na urais wake.

    Mapato yaliyoorodheshwa katika ripoti hii mpya ni makubwa zaidi kuliko yale aliyotangaza mwaka 2024, aliposema alikuwa ameingiza zaidi ya dola milioni 600.

    White House pia ilikanusha kuwapo kwa mgongano wa maslahi, ikisema Trump alihamishia biashara zake kwenye mfuko wa amana unaosimamiwa na wanawe.

    Naibu msemaji wa White House, Anna Kelly, amesema rais huyo ameifanya Marekani kuwa "kitovu cha dunia cha sarafu za kidijitali."

  8. Hujambo natumai umzima.