Mjumbe wa Rais wa Marekani ambaye pia ni Mkwe wa Rais Donald Trump Jared Kushner amesema hatua za kuwapokonya sialaha wanamgambo wa Hamas zinasonga mbele na huenda zikaanza kutekelezeka katika kipindi cha mwezi mmoja ujao kuambatana na makubaliano ya amani kuhusu Gaza.
Baada ya kufanya mazungumzo na Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini Tel Aviv hapo jana Jumatatu, Bwana Kushner amesema huenda wakaanza kuona matokeo ya yaliyofikiwa katika siku thelathini zijazo na kuwa hilo litaanza kwa kuondolewa kwa silaha Gaza.
'Ikiwa Hamas watasalimisha silaha na mahandaki yao kwa hiari yao katika muda wa siku 60 hadi 90 zijazo, bila shaka hilo litakuwa ni kuondolewa kwa tishio kubwa la kiusalama kwa Israel, mafanikio makubwa ambayo huenda hayakutarajiwa. Na iwapo hawatatimiza ahadi yao sasa, kila mtu ataona kwamba hawana nia ya dhati kuhusu amani, na kisha Israel itapata uungwaji mkono mkubwa zaidi kutoka Marekani na wengine kwenda na kumaliza kazi hiyo kwa njia inayofaa'.
Kauli hiyo inakuja baada ya Kushner na Netanyahu kukubaliana kuwa Jenerali wa Jeshi la Marekani ndiye atakahakiki kuwa wanamgambo wa Hamas wanaweka chini silaha zote huku Bwana Netanyahu akisisitiza kuwa majeshi ya Israel hayataondoka katika ukanda wa Gaza hadi pale Hamas itakaposalimisha silaha zake zote.
Waziri huyo Mkuu wa Israel amekuwa akisita kuridhia makubaliano yaliyosimamiwa na Marekani kuhusu kupatikana amani Gaza, akikabiliwa na shinikizo la kisiasa nchini mwake kutolegeza kamba dhidi ya Hamas.
Siku ya Jumapili, Bwana Kushner ambaye pia ni rafiki wa muda mrefu wa Netanyahu, alifanya mazungumzo ya ana kwa ana na kiongozi mpya wa Hamas Khalil al-Hayya nchini Misri. Hamas imeahidi kukabidhi silaha zake kwa uongozi mpya wa Palestina utakaosimamia Gaza.
Netanyahu, waziri mkuu wa Israeli aliyedumu kwa muda mrefu zaidi ambaye hatma yake kisiasa iko mashakani katika uchaguzi unaotarajiwa mwezi Oktoba mwaka huu, anaonekana kuzidi kupinga mitizamo ya mshirika wake wa karibu Rais Trump.
Waziri mkuu huyo pia ameweka wazi kutoridhishwa kwake na uamuzi wa Trump wa kusitisha vita vya Marekani na Israeli dhidi ya Iran vilivyoanzishwa mwishoni mwa Februari na badala yake kufuata njia ya kutafuta makubaliano na viongozi wa wa Iran.
Katika mahojiano yaliyoibua hisia kubwa miongoni mwa nchi za Kiarabu, Itamar Ben Gvir, waziri wa usalama wa taifa wa Israel mwenye msimamo mkali wa mrengo wa kulia hivi karibuni alisema kuwa Israeli inapaswa kuua watu 30 hadi 40 kila usiku huko Gaza.
Kwa upande wake,Rais wa Israel Isaac Herzog, alipokutana na Kushner hapo jana, alisifu juhudi za Bodi ya Amani iliyoanzishwa na Rais Trump kwa kuhakikisha mustakabali mzuri na salama zaidi kwa Israel, Gaza na kanda ya Mashariki ya Kati kwa jumla.
Operesheni za kijeshi za Israel zimewaua takriban Wapalestina 1,265 tangu makubaliano ya kusitisha vita yalipofikiwa mwezi Oktoba mwaka jana.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amemueleza Rais Trump kuwa Israel inawashambulia Wapalestina wa Gaza wakati ambapo awamu ya pili ya makubaliano ya kusitisha vita inapaswa kuwa inatakelezwa.