Kushiriki mapenzi kwa kuridhiana kati ya vijana si hatia, mahakama ya Kenya yasema
Mahakama moja nchini Kenya imetoa uamuzi kuwa baadhi ya vifungu vya sheria ya makosa ya unyanyasaji wa kingono nchini humo haviwezi kutumika kwa watoto wanaopatikana wameshiriki mapenzi kwa kuridhiana.
Watetezi wa haki wamesema uamuzi huo utasaidia kupunguza kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa vijana wenye chini ya umri wa miaka 18 wanaojihusiha kimapenzi kwa kuridhiana na msichana pia aliyechini ya umri wa miaka 18.
Uamuzi huo unatarajiwa kuleta mageuzi katika utendaji wa idara ya polisi ikija katika kuwaajibisha wanaoshtakiwa na kosa la unyanyasaji wa kingono pamoja na mageuzi katika utoaji wa huduma za afya ya uzazi kwa vijana.
Uamuzi huo wa mahakama ya Kenya unasema kuwa, vijana waliobaleghe (mvulana na msichana) ambao umri wao unakaribiana hawafai kuchukuliwa hatua za kisheria moja kwa moja iwapo watapatikana wameshiriki mapenzi.
Uamuzi huu unatokana na kesi mbili zilizokuwa katika mahakama, ambapo kijana mmoja alishtakiwa kumbaka msichana wa umri wa miaka 16, na nyingine kijana wa miaka 17 alishtakiwa kumpa uja uzito msichana mwenye umri sawa.
Kulingana na sheria za Kenya, mtu aliye chini ya umri wa miaka 18, hana uwezo wa kujifanyia maamuzi ya kisheria.