Moja kwa moja, Trump: Mazungumzo na Iran yako katika hatua za mwisho, tutawashambulia iwapo hawataafikia makubaliano

Rais wa Marekani Donald Trump amesema Marekani ipo tayari kutekeleza mashambulizi dhidi ya Iran, iwapo hawataafikia makubaliano ya kusitisha vita, na kusema kuwa Washington itasubiri kwa siku chache ili kupata majibu sahihi kutoka Tehran.

Muhtasari

Trump: Mazungumzo na Iran yako katika hatua za mwisho, na tutawashambulia iwapo hawataafikia makubaliano.

Moja kwa moja

Na Beldeen Waliaula

  1. Marekani imemfungulia mashtaka kiongozi wa zamani wa Cuba Raul Castro

    Picha ya Raul Castro

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Picha ya Raul Castro

    Marekani imemshtaki kiongozi wa zamani wa Cuba, Raul Castro, kwa kupanga kuwaua raia wa Marekani na makosa mengine yaliyotokana na kuangushwa kwa ndege mbili zilizokuwa zikifanya safari kutoka eneo la Florida hadi Cuba.

    Kesi hiyo inamshtumu Castro na watu wengine watano kwa kuhusika kuzifyatulia risasi ndege hizo, zilizokuwa zinamilikiwa na kundi la Cuba-America Group Brothers, na kuwauwa watu wanne, watatu wakiwa raia wa Marekani.

    Castro, kwa sasa ana umri wa miaka 94, na wakati huo alikuwa mkuu wa majeshi ya Cuba na alikashifiwa vikali kimataifa baada ya tukio hilo.

    Wakati Marekani inaendelea kuongeza shinikizo dhidi ya utawala wa kikomunisti wa Cuba, Rais Miguel Díaz-Canel ameelezea mashtaka hayo kama “shinikizo la kisiasa, usio na msingi wa kisheria.”

    Akizungumza katika jengo la Freedom Tower mjini Miami, Mwanasheria Mkuu wa Marekani Todd Blanche, alitangaza kuwa taifa lake litamfungulia Castro mashtaka ya uharibifu wa ndege na makosa manne ya mauaji .

    “Marekani, na Rais Trump, haisahau wala haitasahau raia wake,” Blanche alisema.

    Mashtaka hayo yatasikizwa katika mahakama za Marekani, na kila shtaka la mauaji linaweza kuwa na adhabu ya kifo au kifungo cha maisha.

    Pia unaweza kusoma:

  2. Trump asema atazungumza na kiongozi wa Taiwan, hatua inayovunja utaratibu wa kidiplomasia

    Picha ya Donald Trump

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Picha ya Donald Trump

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema atazungumza na kiongozi wa Taiwan, Lai Ching-te, kuhusu uwezekano wa kuiuzia Taiwan silaha, hatua ambayo ni mabadiliko makubwa kutoka utamaduni wa kidiplomasia uliodumu kwa miaka mingi katika kisiwa hicho na Marekani.

    Viongozi wa Marekani na Taiwan hawajawahi kuzungumza moja kwa moja tangu mwaka wa 1979, wakati Washington ilipositisha rasmi uhusiano wake na Taiwan ili kuitambua serikali ya Beijing kama serikali halali ya China.

    Beijing inaichukulia Taiwan kama sehemu ya himaya yake na haijaondoa uwezekano wa kuitwaa kwa nguvu za kijeshi.

    Lai, aliingia madarakani mwaka wa 2024, na ameongoza moja ya juhudi kubwa zaidi katika miaka ya hivi karibuni za kuimarisha ulinzi wa kisiwa hicho.

    Marekani kwa muda mrefu imekuwa ikiunga mkono Taiwan na kuipatia silaha za kujilinda, lakini imekuwa ikijaribu kudumisha uhusiano wa kidiplomasia na China.

    Alipoulizwa na wanahabari iwapo anapanga kuzungumza na Lai, kuhusu kuiuzia Taiwan silaha, Trump alisema, “nitazungumza naye. Nazungumza na kila mtu tutalifanyia kazi hilo, tatizo la Taiwan.”

    Katika ziara yake ya hivi karibuni nchini Taiwan, Rais Xi Jinping wa China alitaka Marekani kusitisha uuzaji wa silaha kwa Taiwan.

    Mwaka wa 1979, Marekani ilipitisha Sheria ya Mahusiano na Taiwan inayoruhusu Marekani kuipatia Taiwan silaha za kujilinda, sheria ambayo inatumika kuiuzia Taiwan silaha hadi leo.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Chanjo ya Ebola huenda ikachukua miezi tisa, WHO yaonya

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema huenda ikachukua hadi miezi tisa kabla ya chanjo dhidi ya aina ya Ebola inayosambaa kwa sasa kuwa tayari.

    Chanjo mbili ambazo zinazoweza kutumika dhidi ya ebola ya Bundibugyo zinatengenezwa, lakini hakuna hata moja ambayo imefanyiwa majaribio ya kitabibu kufikia sasa,hii ni kulingana na msahuri wa shirika la WHO, Dkt Vasee Moorthy.

    Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom, alisema kumekuwa na visa 600 vya Ebola na vifo 139 kutokana na ugonjwa huo, huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka.

    WHO ilitangaza hali ya dharura ya afya ya umma ya kimataifa, lakini ikasema hali hiyo bado haijafikia kiwango cha kuwa janga la dunia.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Trump: Mazungumzo na Iran yako katika hatua za mwisho, tutawashambulia iwapo hawataafikia makubaliano

    Picha ya Donald Trump

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Picha ya Donald Trump

    Rais wa Marekani Donald Trump, amesema kuwa wapo katika hatua za mwisho za mazungumzo ya kupatikana kwa amani na Iran, na wasipo afikia makubaliano, wataanzisha wimbi jipya la mashambulizi.

    Wiki sita sasa tangu kusitisha oparesheni ya “epic fury” mazungumzo ya kumaliza vita hivyo hayajapiga hatua kubwa.

    Trump alisema wiki hii karibu atoe agizo la kutekeleza mashambulizi zaidi, ila aliombwa asifanye hivyo na mataifa ya Ghuba ili kutoa nafasi kwa mazungumzo kufanyika.

    “Tuko katika hatua za mwisho za mazungumzo na Iran. Tutaona kile ambacho kitatokea baadaye. Tutaafikina makubaliano au tutafanya vitu ambavyo si vizuri, ila nadhani hatutafika huko” Trump aliwaambia wanahabari.

    Rais huyo aliongezea kuwa “tunawapa nafasi, sina haraka. Ni heri watu wachache kuuawa kuliko watu wengi. Mkondo wowote unaweza kuchukuliwa”

    Serikali ya Iran nayo imemkosoa vikali Trump kwa kutaka kuanzisha tena vita hivyo na kusema kuwa wako tayari kuanzisha mashambulizi yatakayokwenda nje ya eneo la Mashariki ya Kati.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja Alhamisi ya leo.