Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Trump asema ana “habari njema” kuhusu Iran, licha ya hatma ya makubaliano ya amani kuwa gizani

Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuna “habari njema” kuhusu Iran, akionyesha matumaini juu ya mazungumzo ya amani ya kumaliza vita, ikiwa zimesalia siku nne kabla ya wiki mbili za kusitisha vita kumalizika

Moja kwa moja

Na Yusuph Mazimu

  1. Kundi la kwanza la wahamiaji lawasili DRC kutoka Marekani chini ya makubaliano mapya

    Kundi la kwanza la wahamiaji waliorejeshwa kutoka Marekani chini ya makubaliano mapya ya pande mbili limewasili mapema Ijumaa nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), reuters inaripoti.

    Ndege iliyobeba wahamiaji kutoka Colombia, Peru na Ecuador ilitua mjini Kinshasa majira ya saa 1:00 usiku. Mwanamke mmoja kutoka Colombia alisema kulikuwa na wahamiaji 16, wanaume tisa na wanawake saba, ingawa chanzo kimoja kutoka uwanja wa ndege kilitaja idadi ya wahamiaji 15. Mamlaka za serikali ya Congo hazikutoa tamko mara moja kuhusu tukio hilo.

    Ripoti zilieleza kuwa zaidi ya wahamiaji 30 walitarajiwa kuwasili DRC wiki hii, lakini wakili mmoja wa Marekani alisema idadi hiyo ndogo huenda imesababishwa na maamuzi ya dakika za mwisho ya majaji wanaoshughulikia uhamisho huo.

    Mmoja wa wahamiaji alisema safari hiyo ilikuwa ndefu sana, ikichukua takribani saa 26 hadi 27, lakini walihudumiwa vizuri ndani ya ndege. Taarifa za safari zinaonyesha ndege ilianzia Alexandria, Louisiana, na kupita Dakar, Senegal pamoja na Accra, Ghana kabla ya kufika Kinshasa.

    Huu ni uhamisho wa kwanza wa wahamiaji wa nchi nchingine kupelekwa DRC, taifa linalokabiliwa na changamoto za usalama, wakimbizi wa ndani na mfumo dhaifu wa hifadhi ya wakimbizi. Makubaliano hayo pia yanakwenda sambamba na juhudi za Marekani kusukuma makubaliano ya amani kati ya DRC na Rwanda ili kumaliza mapigano mashariki mwa nchi.

  2. Trump asema Xi Jinping “ana furaha” kufunguliwa kwa Hormuz

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa Rais wa China, Xi Jinping, “ana furaha sana” kuhusu hali ya kufunguliwa kwa mlango bahari wa Hormuz, huku akieleza matarajio makubwa ya mkutano wao ujao nchini China.

    Kupitia mtandao wake wa Truth Social, Trump alisema kuwa Xi ameridhishwa na hatua ya kufunguliwa kwa njia hiyo muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani.

    Aliongeza kuwa mkutano wao ujao nchini China utakuwa wa kipekee na huenda ukawa wa kihistoria, akisisitiza kuwa mambo mengi yanatarajiwa kufikiwa kupitia mazungumzo hayo.

    Kwa mujibu wa taarifa hizo, Xi Jinping anatarajiwa kukutana na Trump katikati ya mwezi ujao, ambapo ajenda kuu itajumuisha masuala ya amani katika eneo la Mashariki ya Kati, hasa katika muktadha wa mvutano unaoendelea kuhusisha Iran na washirika wake.

    China amekuwa mdau mkubwa wa mafuta kupitia njia hiyo ya muhimu ya kupitisha mafuta duniani - Hormuz.

  3. Trump asema ana “habari njema” kuhusu Iran, licha ya hatma ya makubaliano ya amani kuwa gizani

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuna “habari njema” kuhusu Iran, akionyesha matumaini juu ya mazungumzo ya amani ya kumaliza vita.

    Pamoja na hayo Trump amesisitiza kuwa huenda usitishwaji wa mapigano wa wiki mbili usiongezwe muda wake hata kama hakutakuwa na kufikiwa kwa makubaliano ifikapo Jumatano. Kauli hiyo imekuja wakati hali ikiendelea kubaki tete katika eneo la Mashariki ya Kati.

    Mapema, Iran ilifungua kwa muda mlango bahari wa Hormuz kufuatia makubaliano tofauti ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Marekani kati ya Israel na Lebanon. Hata hivyo, kauli zilizofuata kutoka pande zote zimeacha sintofahamu kuhusu ni kwa kasi gani usafirishaji wa meli utarejea katika hali ya kawaida kwenye njia hiyo muhimu ya mafuta duniani. Trump, akizungumza akiwa ndani ya ndege ya rais (Air Force One), alikataa kufafanua zaidi kuhusu hicho alichokisema cha “habari njema” alizozitaja.

    Vita kati ya Marekani, Israel na Iran vilivyoanza Februari 28 vimesababisha vifo vya maelfu ya watu na kupanda kwa bei za mafuta duniani kutokana na kufungwa kwa mlango bahari wa Hormuz, ambao hubeba karibu theluthi moja ya biashara ya mafuta duniani.