Watu 31 wauawa katika mlipuko msikitini nchini Pakistan

Kwa mujibu wa polisi, angalau watu 24 walipoteza maisha papo hapo, huku wengine wasiopungua 100 wakijeruhiwa katika mlipuko huo.

Moja kwa moja

Na Asha Juma, Beldeen Waliaula & Mariam Mjahid

  1. Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa yahitaji ufadhili wa haraka ili kufanya kazi mwaka 2026

    Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk
    Maelezo ya picha, Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk

    Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, ameomba dola milioni 400 kufadhili shughuli za ofisi yake hadi mwaka 2026, akionya kuwa tayari shirika lake linafanya kazi kwa “usalama wa kiwango cha chini kabisa.”

    Kiasi hicho kinachotakiwa ni kidogo kuliko cha mwaka uliopita, baada ya shughuli kupunguzwa kwa zaidi ya nusu kufuatia kupungua kwa michango kutoka Marekani na nchi nyingine.

    Türk alisema kuwa ofisi yake hapo awali ilichangia kuwawajibisha wahalifu wa vita.

    Hata hivyo, ameonya kuwa upungufu wa bajeti umeacha wahalifu katika sehemu mbalimbali za dunia wakiwa na uhuru mkubwa wa kufanya wanachotaka bila hofu ya kuwajibishwa.

    Soma Pia:

  2. Mujahid asema hakuna "kundi la kigeni au la kidhalimu" nchini Afghanistan

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Msemaji wa serikali ya Taliban Zabihullah Mujahid ametaja wasiwasi uliotolewa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu usalama nchini Afghanistan na kuwepo kwa makundi yenye silaha nchini humo kuwa "hakuna msingi."

    "Tunawahakikishia kuwa Afghanistan iko salama, hakuna vikundi vya kigeni au vya kidhalimu hapa," aliandika katika ujumbe kwenye X mnamo Alhamisi.

    Aliongeza, "Jambo la ISIS, ambalo lilishindwa nchini Afghanistan, kwa bahati mbaya limezua hali mbaya katika ujirani wetu." "Tunaposema kwamba udongo wa Afghanistan hautatumika dhidi ya mtu yeyote, ina maana kwamba hakuna mtu anayejali," anasema Bw. Mujahid.

    Haya yanajiri wakati Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililokutana Jumatano (Februari 4) kuhusu vitisho vinavyoibuka kutoka kwa kundi la Islamic State (IS) kote duniani na njia za kuvizuia, likiibua wasiwasi kuhusu kuwepo kwa ISIS-K na makundi mengine ya kigeni yenye silaha nchini Afghanistan.

    Soma Pia:

  3. Iran yaelezea kuhusu meli za mafuta zilizokamatwa

    Walinzi wa Pwani ya Iran

    Chanzo cha picha, mehrnews

    Maelezo ya picha, Walinzi wa Pwani ya Iran

    Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran IRGC limetangaza kuwa limekamata meli mbili zilizokuwa zimebeba "mafuta haramu" katika Ghuba ya Uajemi.

    Afisa kutoka kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ameiambia Redio ya Iran kwamba meli hiyo ilikamatwa kwa amri ya mahakama karibu na Rasi ya Farsi na kisha kuhamishiwa Bushehr.

    Kulingana na afisa huyo, "zaidi ya lita milioni moja za mafuta ya dizeli haramu" zilipatikana kwenye meli hizo na kukabidhiwa kwa Kampuni ya Kitaifa ya Mafuta na Usambazaji.

    Aliongeza kuwa "wafanyakazi 15 wa kigeni" kwenye meli hizi pia walikamatwa na kuhamishiwa kwa mamlaka ya mahakama.

    Kukamatwa kwa meli hizo kumekuja wakati ambapo mvutano unaongezeka kati ya Tehran na Washington na kuwepo kwa Jeshi la Wanamaji la Marekani katika eneo hilo.

    Maelezo zaidi:

  4. Starmer azungumzia juu ya uwezekano wa kuenguliwa na chama chake

    Keir Starmer

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Keir Starmer

    Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer aliulizwa ikiwa angepinga ikiwa chama chake kitajaribu kumwondoa afisini.

    Aliulizwa na Mhariri wa kisiasa wa ITV, Robert Peston, baada ya kukiri kuwa alijua nalozi Mandelson alikuwa na ukaribu na Jeffrey Epstein.

    Starmer alijibu kwa kusema anabadilisha nchi kuwa bora, akitaja mfumuko mdogo wa bei, viwango vya chini vya riba na kazi ya chama chake kukabiliana na umaskini wa watoto.

    "Je, si jambo la kukatisha tamaa kwamba mwelekeo hauko katika masuala hayo na mengine, bali ni tabia mbaya na udanganyifu wa watu wengine? Bila shaka mimi," alisema na kuongeza kuwa ataendelea kuzingatia kazi ya serikali, ambayo anatumai "itaathiri mamilioni ya maisha."

  5. Wito watolewa kwa Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer kujiuzulu

    d

    Chanzo cha picha, PA Media

    Mbunge wa chama cha Labour amemtaka waziri mkuu wa Uingereza Keir Starmer kujiuzulu kutokana na kashfa ya Lord Mandelson.

    Rachael Maskell, anayewakilisha York Central, anasema angeweza kusikia "mshtuko wa kweli wa kila mtu katika chumba hicho" kwa ukweli kwamba Starmer alijua uhusiano kati ya Mandelson na Jeffrey Epstein kwa "miezi".

    "Tunahitaji tu kusoma nchi inavyotamauka ili kutambua kwamba msimamo wake sasa haukubaliki," anaiambia BBC Radio York.

    "Nadhani sote tumeshtushwa na kushangazwa na kile ambacho kimezinduliwa jana lakini tunahitaji sasa kusonga mbele kama chama ili kuhakikisha kwamba tunaweza kupata uungwaji mkono huo.

    "Siamini kuwa tunaweza kuwa na waziri mkuu, kwa hivyo nadhani ni jambo lisiloepukika kwamba Waziri Mkuu atalazimika kuachia ngazi," anasema Maskell.

    Waziri starmer alipoulizwa na mwanahabari kama atakubali kujivua madaraka iwapo atashinikizwa baada ya kukiri kuwa alijua balozi huyo Mandelson alikuwa na ukuruba na Jeffrey Epstein alijibu kuwa analenga kubadilisha nchi kuwa bora.

  6. Starmer aomba msamaha kwa waathiriwa wa Epstein kwa kumteua Mandelson na "kuamini uwongo wake"

    Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer

    Waziri mkuu wa Uingereza Keir Starmer amekiri kuwa ilikuwa inajulikana hadharani kuwa Peter Mandelson alikuwa na uhusiano na Jeffrey Epstein.

    “Lakini hakuna kati yetu aliyejua kina na giza la uhusiano huo,” anasema Starmer.

    Waziri Mkuu anaongeza kuwa taarifa zilizoibuka sasa hazikujulikana wakati wa uteuzi wake kama balozi.

    Starmer anasema Mandelson aliulizwa moja kwa moja kuhusu uhusiano wao, ikiwemo kama alikuwa amekaa na Epstein baada ya hukumu yake.

    Anaongeza: "Nimeomba msamaha kwa ukweli kwamba nilimteua kwanza".

    Baadaye Starmer anasema Mandelson aliulizwa pia kama alikuwa amepokea zawadi kutoka kwa Epstein na kama alikuwa wazi kuhusu uhusiano wao.

    Mandelson “aliwasilisha Epstein kama mtu aliyejaribu kumfahamu kidogo sana,” anaongeza Waziri Mkuu, na anasema aliposalia wazi kuwa hiyo si kweli, Mandelson alifutwa kazi.

    Hakuna mtu anayepaswa kushikilia nafasi ya umma ikiwa hawezi kufikia “jaribio la msingi la uaminifu,” anasema.

    Starmer anasema waathirika wa Epstein wameishi “na maumivu ambayo wengi wetu hatuwezi kuyafahamu” na kuona uwajibikaji “ukicheleweshwa na mara nyingi kukanushwa.”

    “Ninaomba radhi,” anasema kwa waathirika. “Radhi kwa kuamini uongo wa Mandelson na kumteua.”

    Baada ya kuomba msamaha kwa waathirika wa Jeffrey Epstein, Waziri Mkuu ameongeza kuwa atafanya kila liwezekanalo kuhakikisha uwajibikaji unatekelezwa.

    Soma pia:

  7. Waumini wote waliotekwa nyara waachiliwa katika jimbo la Kaduna nchini Nigeria

    Sarah Peter bado anasumbuliwa na kiwewe baada ya kuachiliwa huru
    Maelezo ya picha, Sarah Peter bado anasumbuliwa na kiwewe baada ya kuachiliwa huru

    Waumini waliosalia waliotekwa nyara na watu wenye silaha katika kijiji cha Kurmin Wali katika jimbo la Kaduna kaskazini mwa Nigeria wameachiliwa huru, zaidi ya wiki mbili baada ya kutekwa nyara, kiongozi wa jamii ameiambia BBC.

    Mkuu wa kijiji, Ishaku Dan’azumi, alisema siku ya Alhamisi kwamba polisi wa kijasusi wa Nigeria walimjulisha kwamba wote waliokuwa bado wanazuiliwa wameachiliwa huru.

    Alisema kwa sasa amesafiri hadi katika nyumba ya serikali ya jimbo la Kaduna kuwapokea.

    Kuachiliwa huko kunafuatia kutoroka mapema wiki hii kwa waumini 80, waliofanikiwa kukimbia muda mfupi baada ya kutekwa nyara lakini wakajificha katika vijiji jirani kwa hofu ya kukamatwa tena.

    Jumla ya watu 177 walikamatwa mwezi uliopita wakati wa mashambulizi dhidi ya makanisa matatu katika kijiji cha mbali.

    Bw Dan’azumi hakutoa maelezo kuhusu jinsi waumini waliosalia waliachiliwa.

    Mchungaji John Hayab, rais wa Jumuiya ya Kikristo ya Nigeria (Can) Kaskazini mwa Nigeria, pia alithibitisha BBC kuwa wako huru.

    "Kufikia sasa, nadhani wako katika hali nzuri," alisema, akiongeza kuwa mipango inafanywa kuwapeleka kwa serikali ya jimbo ili waweze kuunganishwa na familia zao.

    Pia unaweza kusoma:

  8. Uingereza yawawekea vikwazo wanaochochea vita Sudan

    Baadhi ya nchi ambazo hazihusiki moja kwa moja na vita zimegeuka kuwa masoko ya silaha na vyanzo vya wapiganaji wa kulipwa.

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Baadhi ya nchi ambazo hazihusiki moja kwa moja na vita zimegeuka kuwa masoko ya silaha na vyanzo vya wapiganaji wa kulipwa.

    Serikali ya Uingereza imeweka vikwazo dhidi ya watu sita muhimu ambao inadai wanachochea vita vya Sudan.

    Hatua hizo zilitangazwa na Katibu wa Mambo ya Nje, Yvette Cooper, baada ya ziara yake kwenye mpaka wa Sudan na Chad wiki hii, ambapo alikutana na wakimbizi waliokimbia vurugu.

    Katibu wa Mambo ya Nje wa Uingereza alisema katika taarifa yake kuwa anatumai vikwazo hivi ‘vitasambaratisha vita vya wale wanaoendesha au kufaidika na ghasia za kikatili nchini Sudan," na kutuma ujumbe kwa wale waliohusika na uhalifu kuwa watachukuliwa hatua.

    Watu walio chini ya vikwazo ni pamoja na maafisa wakuu wa Jeshi la Sudan na wanamgambo wa (RSF), pamoja na raia watatu wa kigeni wanaodaiwa kuwa na jukumu la kuajiri mashujaa wa Colombia kupigania RSF.

    Yvette Cooper alitembelea wakimbizi walioko nchi jirani, Chad, wiki hii, wakiwemo wanawake na wasichana waliokuwa wahanga wa mashambulizi ya kingono yanayofanywa na makundi yanayopigana.

    Vita nchini Sudan vimekuwa vikidumu takriban miaka mitatu, na ni mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu duniani, kulingana na Umoja wa Mataifa.

    Zaidi ya milioni 13 za watu wamehamishwa makwao kutokana na mzozo huu, na zaidi ya milioni 21 kwa sasa wanateseka kutokana na uhaba mkali wa chakula.

    Soma pia:

  9. Pombe, Sigara vinachangia ongezeko la saratani Kenya- Utafiti

    Bakteria na fungi pia huishi katika tumors.

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Bakteria na fungi pia huishi katika tumors.

    Vidonda vya tumbo, uvutaji wa sigara, na matumizi ya pombe vinachangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa ugonjwa wa saratani nchini Kenya, haya ni kwa mujibu wa Shirika la habari za afya la Willow.

    Takwimu mpya za kimataifa zinaonyesha kuwa kesi nyingi zinazohusiana na Helicobacter pylori (H. pylori), maambukizi ya Human Papillomavirus (HPV), na matumizi ya tumbaku zinaweza kuzuilika, kielezo kilichotolewa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO).

    Uchambuzi wa kimataifa uliofanywa na Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Saratani (IARC), uliopewa jina Global and Regional Cancer Burden Attributable to Modifiable Risk Factors to Inform Prevention, ulibaini kuwa karibu visa vinne kati ya kumi vya saratani duniani zinatokana na sababu zinazoweza kuzuilika. Hali hii inahusisha Kenya, ambapo saratani za tumbo, shingo ya kizazi, na mapafu bado ndizo zinazochangia zaidi kwa maradhi na vifo.

    “Uchambuzi huu ni wa kwanza kuonyesha ni kiasi gani cha hatari ya saratani kinatokana na sababu tunazoweza kuzizuia,” alisema Dk. Andrew Ilbawi, Kiongozi wa Timu ya Udhibiti wa Saratani wa WHO na mwandishi wa utafiti. “Kwa kuchunguza mifumo ya nchi na makundi ya watu, tunaweza kuwapa serikali na wananchi taarifa za kina zaidi, zinazoweza kusaidia kuzuia visa vingi vya saratani kabla havijaanza.”

    ''Mwaka wa 2022 pekee, takriban milioni 7.1 kati ya visa vipya vya saratani milioni 18.7 vilivyogunduliwa kati ya watu wazima vilichangiwa na sababu hizi 30 za hatari ambazo tulichunguza," Dk Isabelle Soerjomataram, Naibu Mkuu wa Kitengo cha Uchunguzi wa Saratani ya IARC na mwandishi mkuu wa utafiti huo.

    "Hii inawakilisha asilimia 37.8 ya mzigo wote wa saratani, sehemu kubwa sana."

    Kwa kufafanua takwimu hizo zaidi, uvutaji sigara ulichangia takriban visa milioni 3.3 duniani kote, maambukizi kwa visa milioni 2.2 na pombe kwa takriban visa 700,000.

    "Mambo haya matatu pekee yanawakilisha wingi wa mzigo unaoweza kuzuilika wa saratani duniani, ikionyesha ni wapi juhudi za kuzuia zinaweza kuwa na athari kubwa," Dk Soerjomataram alisema.

    Takriban watu 102,152 wamekuwa wakiishi na saratani nchini Kenya katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

    Soma Pia:

  10. Nchi ya kwanza ya Afrika kupokea droni za kisasa za Urusi

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wiki iliyopita, Ethiopia iliandaa hafla ya kuadhimisha miaka 90 tangu kuanzishwa kwa Jeshi lake la Anga, ambapo ilionesha uwezo wake wa kijeshi.

    Maonesho hayo, mbali na kuhusisha ndege za kivita, pia yalijumuisha ndege zisizo na rubani za kivita zilizotengenezwa na nchi mbalimbali na kuoneshwa nchini Ethiopia.

    Miongoni mwa ndege hizo kulikuwa na droni ya Urusi aina ya Orion-E UAV, ambayo ni droni ya ukubwa wa kati.

    Hatua hii inaifanya Ethiopia kuwa nchi ya kwanza nje ya Urusi kupokea rasmi droni hiyo.

    Picha za droni hiyo zilichapishwa wakati wa maonesho ya Aviation Expo 2026 yaliyofanyika mjini Bishoftu.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia pia ilithibitisha kuwa nchi hiyo imepokea droni hiyo ya Urusi.

    Vivyo hivyo, gazeti la kijeshi la Ukraine, Defense Express, liliripoti tarehe 27 Januari kwamba Urusi imeipatia Ethiopia ndege sita za kivita aina ya Yak-130 pamoja na droni moja ya Orion.

    Soma Pia:

  11. Mazungumzo ya kusitisha vita kati ya Urusi na Ukraine, yaingia siku ya pili

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Ukraine,Urusi na Marekani wanaendeleza mazungumzo ya kusitisha vita vya Urusi nchini Ukraine, mjini Abu Dhabi kwa siku ya pili sasa.

    Wapatanishi wa Urusi, Ukraine na Marekani wamerejelea mazungumzo hayo ya kutafuta suluhu ya kumaliza vita hivyo ambavyo vimedumu kwa miaka minne.

    Moscow imekuwa ikisistiza lazima Ukraine iiachie eneo lake la mashariki la Donbas, suala ambalo Kyiv haijaridhia.

    Wakati mazungumzo hayo yakiendelea Urusi, imekuwa ikitekeleza mashambulizi nchini Ukraine na kulenga vituo vya nishati, na kuwaacha wengi bila umeme msimu huu wa baridi kali.

    Hapo jana mazungumzo hayo yaliripotiwa kupiga hatua ila hakuna kilichoafikiwa.

    Soma zaidi:

  12. Guterres: Mkataba wa nyuklia kati ya Urusi na Marekani umemalizika wakati mbaya

    Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres,

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres,

    Mkataba wa mwisho uliosalia wa kudhibiti silaha za nyuklia kati ya Marekani na Urusi unamalizika leo Alhamisi, Februari 5, 2026, hatua ambayo inazua hofu ya mashindano mapya ya silaha.

    Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ameonya ikiwa makubaliano ya kudhibiti silaha kati ya Marekani na Urusi hayataafikiwa hivi karibuni basi itakuwa ‘'wakati mgumu kwa amani na usalama duniani’'

    Guterres ametoa wito kwa mataifa hayo mawili kujadili mkataba mpya wa kudhibiti silaha.

    “Kwa mara ya kwanza katika zaidi ya nusu karne, tunakabiliwa na ulimwengu usio na mipaka yoyote ya kisheria inayodhibiti silaha za nyuklia kati ya mataifa mawili yanayomiliki akiba kubwa ya silaha za nyuklia dunia,” alisema Guterres.

    Aliongezea kuwa mkataba wa awali uliofahamika kama '‘New START’' ulisaidia pakubwa kuimarisha usalama na maisha ya watu.“

    Kumalizika kwa mkataba huu umekuja wakati mbaya, na kuna hatari ya silaha za nyuklia kutumika kwa mara ya kwanza baada ya miongo kadhaa.”

    Urusi na Marekani wanamiliki zaidi ya 80% ya silaha za nyuklia duniani.

    Guterres sasa anayataka mataifa hayo kureja katika meza ya mazungumzo na kuafikia makubaliano ya kudhibiti matumizi ya silaha hizo.

  13. Bei ya mafuta yashuka baada ya Marekani na Iran kukubali kufanya mazungumzo

    Trump na Khamenei

    Chanzo cha picha, Reuters / Getty Images

    Ikulu ya White House imetangaza kuwa itashiriki mazungumzo na Iran hapo kesho Ijumaa, nchini Oman.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi, pia alidhibitisha mkutano huo, utakao jadili mpango wa silaha za nyuklia katika taifa lake.

    Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Marco Rubio, alisema hapo jana kuwa iwapo watakutana na Iran, lazima taifa hilo likubali kujadili kuhusu makombora yake ya masafa marefu pamoja na masuala mengine.

    Hukuu hayo yakijiri bei ya mafuta imeshuka kwa 2% Alhamisi baada ya Marekani kukubaliana na Iran kufanya mazungumzo.

    Hatua hiyo imepuguza wasiwasi uliokuwepo wa uwezekano wa Marekani kuishambulia kijeshi Iran na kuharibu usambazaji wa mafuta kutoka mashariki ya kati.

    Bei ya mafuta ghafi ilishuka kwa $1.44 au 2.07%, na kufikia $68.02 kwa pipa moja la mafuta.

    Mashariki mwa jimbo la Texas bei ya mafuta ilishuka hadi $63.80 kwa pipa moja.

    Bei ya mafuta ilipanda kwa 3% hapo jana baada ya ripoti kutoka vyombo vya habari kuashiria kuwa mazungumzo kati ya Marekani na Iran yameporomoka.

    Ila baadaye maafisa wa mataifa hayo mawili walikubaliana kufanya mazungumzo hayo hapo kesho.

    Ila bado pande hizo mbili hazijakubalina ni vipingele vipi vya kuzungumziwa katika mkutano huo.

    Iran iko wazi kujadili mpango wake wa nyuklia ikiwemo madini ya urani huku Marekani ikitaka kujadili makombora ya kibalistiki ya Iran, na taifa hilo kuunga mkono makundi yaliyojihami mashariki ya kati.

    Iran ni taifa la nne duniani, ambalo huzalisha mafuta mengi.

    Kwa hivyo iwapo Trump ataishambulia taifa hilo, itaathiri uzalishaji na usambazaji wa mafuta haswa kwa mataifa ya ghuba.

    Maelezo zaidi:

  14. Marekani lazima iwe makini inapotoa silaha kwa Taiwan, Xi amwambia Trump

    Trump na Xi last walikutana Oktoba mwaka jana pembezoni mwa kongamano la Kiuchumi la Asia-Pacific nchini Korea Kusini

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Trump na Xi last walikutana Oktoba mwaka jana pembezoni mwa kongamano la Kiuchumi la Asia-Pacific nchini Korea Kusini

    Rais wa China Xi Jinping amesema Taiwan ni ''suala muhimu’' katika uhusiano wao na Marekani, baada ya kuzungumza na rais Trump kwa njia ya simu hapo jana.

    Xi alimuambia Trump kuwa ''makini'' anapoipa Taiwan silaha za kijeshi na kuongeza kuwa uhusiano wao na Marekani una umuhimu mkubwa na anatumai watasuluhisha tofauti walizonazo.

    Trump alisema mazungumzo hayo yalikuwa ''mazuri, ndefu na ya kina.''

    Maongezi kati ya wawili hao yanajiri siku chache tu baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer kukamilisha ziara yake nchini China.

    Ziara hiyo iliyokuwa ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya Uingereza na China.

    Trump ambaye anatarajiwa kuzuru China mwezi Aprili mwaka huu, alisema kuwa Beijing inapania kununua tani millioni 20 ya maharagwe ya soya kutoka Marekani.

    "Uhusiano wetu na China, pamoja na mahusiano yangu binafsi na rais Xi, ni mazuri, na sote tunajua umuhimu wa kuhakikisha inasalia hivyo," Trump alisema katika ujumbe kwenye mtandao wake wa Truth Social.

    Trump na Xi pia walizungumzia vita vya Ukraine na Urusi, hali ya sasa nchini Iran, na China kununua mafuta na gesi kutoka Marekani.

    Aidha Beijing ilionya kuwa yeyote atakayedhubutu kuunga mkono Taiwan kuwa taifa huru atakabiliwa vikali, wakidai bado ni sehemu ya himaya ya China.

    Soma pia:

  15. Makumi ya watu wauwa katika shambulio kaskazini mwa Nigeria

    Nigeria inakabiliwa na changamoto za kiusalama kote nchini

    Chanzo cha picha, AFP/Getty Images

    Maelezo ya picha, Nigeria inakabiliwa na changamoto za kiusalama kote nchini

    Makumi ya watu wameuawa kwa kupigwa risasi katika vijiji viwili vilivyoko katika jimbo la Kwara, nchini Nigeria.

    Washambuliaji hao pia walichoma maduka na makazi ya watu, na kuwalazimisha wakaazi wa vijiji vya Woro na Nuku, kukimbia makwao, mbunge na kiongozi wa vijiji hivyo aliiambia BBC Idhaa ya Hausa.

    Mamlaka nchini Nigeria zinasema shambulio dhidiu ya jimbo la Kwara lilitokana na itikadi kali, wala si uhalifu, huku kikosi cha wanajeshi kikitumwa jimbo la Kwara kudhibiti hali.

    Gavana wa jimbo hilo AbdulRahman AbdulRazaq, aliyezuru vijiji vya Woro na Nuku vilivyoathiriwa na shambulio hilo jana usiku, akiwa na viongozi wengine alisema kuwa watu 75 ambao ni Waumini wa dini ya Kiislamu waliuawa.

    Afisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu huko Kwara, Babaomo Ayodeji, aliliambia shirika la AFP kwamba “ripoti zinaonyesha idadi ya vifo sasa imefikia 162, huku oparesheni ya kutafuta miili zaidi ikiendelea.”

    Wakati huo huo, Amnesty International ilisema katika taarifa yake kwamba zaidi ya watu 170 wamefariki dunia, ikibainisha kuwa baadhi yao walipigwa risasi na wengine kuchomwa moto wakiwa hai.

    Akizungumza na wanahabari, gavana huyo alisema shambulio hilo lilitokana na jimbo hilo kukakataa kufuata maadili Kiislamu.

    “Kulingana na taarifa nilizopokea, kijiji hiki kilikataa kufuata maelekezo potovu ya dini ya kiislamu.”

    Aliongezea kuwa wakaazi wa vijiji hivyo walikataa kufuata kanuni na mafundisho tofauti ya dini ndio maana walishambuliwa na kuuawa. “Ni tofauti na kile tumezoea kushuhudia ambapo wanawateka watu na kuitisha fidia”.

    Msemaji wa polisi katika jimbo la Kwara Adetoun Ejire-Adeyemi, aliiambia BBC kuwa shambulio hilo huenda lilitekelezwa na wahalifu wa eneo hilo ila uchunguzi bado unaendelea.

    Aidha gavana wa jimbo hilo alisema kuwa rais wa Nigeria Bola Tinibu, ameidhinisha jeshi kupelekwa katika eneo hiloili kudumisha usalama.

    Eneo la kaskazini mwa Nigeria limekuwa likikabiliwa na ukosefu wa usalama kwa muda, tukio la hivi karibuni likiwa la watu kutekwa nyara wakiwa kanisani.

    Maelezo zaidi:

  16. Waendesha mashtaka wa Libya waanzisha uchunguzi kuhusu mauaji ya mwanawe Gaddafi

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waendesha mashtaka wa Libya wanasema wanachunguza mauaji ya Saif al-Islam Gaddafi, mwana wa kiongozi wa muda mrefu wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi.

    Ofisi yake ilisema katika taarifa kwamba al-Islam Gaddafi mwenye umri wa miaka 53, ambaye hapo awali alionekana kama mrithi wa baba yake, aliuawa wakati wa "makabiliano ya moja kwa moja" na watu wanne wasiojulikana wenye bunduki waliovamia nyumba yake katika jiji la Zintan.

    "Mwathiriwa alifariki kutokana na majeraha ya risasi," waendesha mashtaka wa Libya walisema Jumatano, wakiongeza kuwa juhudi zinaendelea kuwatambua watu hao wenye silaha.

    Katika toleo tofauti la tukio hilo, dada yake aliambia televisheni ya Libya kwamba alifariki karibu na mpaka wa nchi hiyo na Algeria.

    Wakati huo huo, wakili wa Saif al-Islam aliambia shirika la habari la AFP kwamba kikosi cha "makomandoo wanne" kilifanya mauaji nyumbani kwake katika jiji la Zintan, ingawa haikuwa wazi ni nani aliyehusika na shambulio hilo.

    Ofisi ya mwendesha mashtaka wa umma ilisema wataalamu wa uchunguzi wa jinai wametumwa Zintan kaskazini magharibi mwa Libya kufanya uchunguzi.

    Saif al-Islam kwa muda mrefu alionekana kama mtu mwenye ushawishi mkubwa na kuogopwa zaidi nchini baada ya baba yake, ambaye alitawala Libya kuanzia 1969 hadi alipoondolewa madarakani na kuuawa wakati wa uasi mwaka 2011.

    Soma zaidi:

  17. Rais wa zamani wa Zimbabwe Mugabe atajwa katika faili za Epstein

    .

    Chanzo cha picha, AFP/Getty Images

    Rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe huenda alikuwa na uhusiano wa kifedha na Jeffrey Epstein, kulingana na kundi la hivi karibuni la faili za Epstein zinazohusiana na mhalifu huyo kingono wa Marekani aliyefariki dunia.

    Katika mawasiliano ya barua pepe ya mwaka 2015 na mjasiriamali wa Kijapani Joi Ito, Epstein alipendekeza waende kwa Rais Mugabe wakati huo ili kuipa Zimbabwe sarafu mpya baada ya dola ya ndani kuporomoka kutokana na mfumuko wa bei uliokithiri.

    Nyaraka za FBI za mwaka 2017 pia zilitoa ushahidi usiothibitishwa kutoka kwa "chanzo cha siri ambaye ni mwanadamu", kikidai Epstein alikuwa meneja wa utajiri wa Rais wa Urusi Vladimir Putin na alitoa huduma hiyo hiyo kwa Mugabe.

    Kutajwa miongoni mwa faili za Epstein si dalili ya kufanya makosa.

    BBC imeiomba familia ya Mugabe kutoa maoni yake.

    Robert Mugabe, kiongozi wa zamani wa Zimbabwe wakati inapata uhuru na rais wa muda mrefu, alifariki mnamo mwezi Septemba 2019 akiwa na umri wa miaka 95 - miaka miwili baada ya kuondolewa madarakani katika mapinduzi.

    Epstein, mfadhili anayejulikana sana wa Marekani na aliyehukumiwa kuwa mhalifu wa kingono, alipatikana amekufa gerezani kwa kujiua wakati akisubiri kesi yake kuhusu mashtaka ya biashara haramu ya ngono mnamo Agosti mwaka 2019.

    Soma zaidi:

  18. Ahukumiwa kifungo cha maisha jela kwa jaribio la kumuua Trump

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Ryan Routh amehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kujaribu kumuua Rais Donald Trump kwenye uwanja wa gofu wa Florida mnamo Septemba 2024.

    Routh, mwenye umri wa miaka 59, alipatikana na hatia mwaka jana ya kujaribu kumuua Trump, ambaye wakati huo alikuwa mgombea urais, katika Klabu ya Gofu ya Kimataifa ya Trump huko West Palm Beach.

    Afisa wa Jeshi la Marekani katika eneo hilo aliona mtutu wa bunduki ikichomoza kutoka kwenye kichaka na kumpiga risasi Routh, ambaye kisha alitoroka eneo la tukio na kukamatwa eneo la karibu.

    Katika hati ya hukumu, Jaji Aileen Cannon alisema uhalifu wa Routh "bila shaka unastahili kifungo cha maisha".

    "[A]lichukua hatua kwa miezi kadhaa kumuua mgombea mkuu wa Urais, alionyesha nia ya kumuua mtu yeyote aliyemzuia, na tangu wakati huo hajaonyesha majuto wala kuhuzunishwa kwa waathiriwa wake," aliandika.

    Wakili wa Routh, Martin Ross, alisema watakata rufaa dhidi ya kesi hiyo.

    Routh alikanusha kuwa na hatia na akachagua kujiwakilisha mwenyewe wakati wa kesi hiyo, iliyoanza tarehe 8 Septemba.

    Pia unaweza kusoma:

  19. Faili za Epstein: Barua pepe yathibitisha picha ya aliyekuwa mwanamfalme na Virginia Giuffre ni ya kweli

    .

    Chanzo cha picha, US Department of Justice via Press Association

    Barua pepe inayoonekana kutoka kwa Ghislaine Maxwell inaonekana kuthibitisha kwamba picha ya Andrew Mountbatten-Windsor akiwa amemkumbatia Virginia Giuffre, ambaye alimtuhumu kwa unyanyasaji wa kingono, ni ya ukweli.

    Mwanamfalme huyo wa zamani, ambaye amekuwa akikanusha kufanya makosa yoyote, hapo awali alisema kuwa picha hiyo imefanyiwa ukarabati na kudai kuwa hajawahi kukutana na Giuffre.

    Lakini katika ujumbe, uliotolewa kama sehemu ya kundi la hivi karibuni la faili za Epstein, wenye kichwa "rasimu ya taarifa" iliyotumwa na "G Maxwell" kwa Jeffrey Epstein mnamo mwaka 2015, aliandika: "Mnamo 2001 nilikuwa London wakati…nilikutana na marafiki zangu kadhaa akiwemo Prince Andrew. Picha ilipigwa kwani nadhani alitaka kuionyesha kwa marafiki na familia."

    Familia ya Giuffre, ambaye alifariki mwaka wa 2025, iliambia kipindi cha Newsnight cha BBC kwamba barua pepe hiyo ilionyesha kuwa alikuwa "akisema ukweli".

    "Kwa kweli hii inamtetea Virginia... hakuwa akidanganya wakati huu wote", kaka yake Guiffre, Sky Roberts, alisema.

    "Ni wakati ambapo tunajivunia sana dada yetu," aliongeza.

    Barua pepe hiyo, iliyotolewa na Idara ya Sheria ya Marekani (DoJ), inaongeza kwamba "G Maxwell" hakujua kuwa kuna "jambo lolote lisilofaa" linaloendelea nyumbani kwake.

    Jina la mtu huyo limeondolewa kwenye toleo lililochapishwa la taarifa hiyo, lakini maelezo yanaonyesha kwamba ni Maxwell aliyekuwa akimzungumzia Giuffre.

    Giuffre - mshtaki maarufu wa Epstein na Maxwell - inadaiwa kuwa Mountbatten-Windsor alifanya naye mapenzi mara tatu akiwa kijana.

    Daima amekuwa akikanusha dai hilo na kufikia makubaliano ya nje ya mahakama na Giuffre mwaka wa 2022. Hayakuwa na kukiri kuwajibika au kuomba msamaha.

    BBC News imewasiliana na wawakilishi wa Mountbatten-Windsor kwa ajili ya kutoa maoni yao.

    Soma zaidi:

  20. Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara ya tarehe 05/02/2026.