Makumi ya watu wameuawa kwa kupigwa risasi katika vijiji viwili vilivyoko katika jimbo la Kwara, nchini Nigeria.
Washambuliaji hao pia walichoma maduka na makazi ya watu, na kuwalazimisha wakaazi wa vijiji vya Woro na Nuku, kukimbia makwao, mbunge na kiongozi wa vijiji hivyo aliiambia BBC Idhaa ya Hausa.
Mamlaka nchini Nigeria zinasema shambulio dhidiu ya jimbo la Kwara lilitokana na itikadi kali, wala si uhalifu, huku kikosi cha wanajeshi kikitumwa jimbo la Kwara kudhibiti hali.
Gavana wa jimbo hilo AbdulRahman AbdulRazaq, aliyezuru vijiji vya Woro na Nuku vilivyoathiriwa na shambulio hilo jana usiku, akiwa na viongozi wengine alisema kuwa watu 75 ambao ni Waumini wa dini ya Kiislamu waliuawa.
Afisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu huko Kwara, Babaomo Ayodeji, aliliambia shirika la AFP kwamba “ripoti zinaonyesha idadi ya vifo sasa imefikia 162, huku oparesheni ya kutafuta miili zaidi ikiendelea.”
Wakati huo huo, Amnesty International ilisema katika taarifa yake kwamba zaidi ya watu 170 wamefariki dunia, ikibainisha kuwa baadhi yao walipigwa risasi na wengine kuchomwa moto wakiwa hai.
Akizungumza na wanahabari, gavana huyo alisema shambulio hilo lilitokana na jimbo hilo kukakataa kufuata maadili Kiislamu.
“Kulingana na taarifa nilizopokea, kijiji hiki kilikataa kufuata maelekezo potovu ya dini ya kiislamu.”
Aliongezea kuwa wakaazi wa vijiji hivyo walikataa kufuata kanuni na mafundisho tofauti ya dini ndio maana walishambuliwa na kuuawa.
“Ni tofauti na kile tumezoea kushuhudia ambapo wanawateka watu na kuitisha fidia”.
Msemaji wa polisi katika jimbo la Kwara Adetoun Ejire-Adeyemi, aliiambia BBC kuwa shambulio hilo huenda lilitekelezwa na wahalifu wa eneo hilo ila uchunguzi bado unaendelea.
Aidha gavana wa jimbo hilo alisema kuwa rais wa Nigeria Bola Tinibu, ameidhinisha jeshi kupelekwa katika eneo hiloili kudumisha usalama.
Eneo la kaskazini mwa Nigeria limekuwa likikabiliwa na ukosefu wa usalama kwa muda, tukio la hivi karibuni likiwa la watu kutekwa nyara wakiwa kanisani.