Rais wa
Marekani Donald Trump ametishia kuiangamiza Iran "ndani ya usiku
mmoja" ikiwa itashindwa kufikia makubaliano kabla ya tarehe ya mwisho
aliyoiweka kwa Tehran kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji
duniani.
Tarehe ya
mwisho ya Trump ya kufikiwa kwa "makubaliano" - ambayo yanajumuisha usafirishaji
huru wa mafuta kupitia Ghuba - imewekwa saa 20:00, saa za Washington DC siku ya
Jumanne (00:00 GMT Jumatano).
Akizungumza
katika Ikulu ya White House, Trump alisema kwamba anaamini viongozi "wenye
busara" nchini Iran walikuwa wakijadiliana kwa "nia njema",
lakini matokeo yake yamesalia kuwa yasio na uhakika.
Iran
imekataa mapendekezo ya kusitisha mapigano kwa muda, badala yake imetoa wito wa
kukomeshwa kabisa kwa vita na kuondolewa kwa vikwazo.
Mkutano wa
Trump na waandishi wa habari uliofanyika pamoja na Jenerali Dan Caine,
mwenyekiti wa Wakuu wa Majeshi na waziri wa ulinzi Pete Hegseth umefanyika siku
chache baada ya vikosi vya Marekani kuwapata marubani wawili wa ndege ya kivita
ya F-15 iliyodunguliwa kusini mwa Iran.
Ingawa
sehemu kubwa ya matamshi ya Trump yaliangazia kile alichokielezea kama uokoaji
wa "kishujaa" wa marubani, alirudia tena onyo lake kwamba Marekani
inaweza kuanzisha mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati na usafiri ya
Iran ikiwa Mlango-Bahari wa Hormuz hautafunguliwa tena kufikia tarehe ya ukomo
ya Jumanne.
"Nchi
nzima inaweza kuangamizwa kwa usiku mmoja - na usiku huo unaweza kuwa kesho
usiku," alisema Jumatatu, akimaanisha leo usiku.
Mara tu
tarehe ya mwisho itakapopita, Trump aliongeza, Iran itarudishwa ksiku za "Enzi
ya Mawe".
"Hawatakuwa
na madaraja," alisema. "Hawatakuwa na viwanda vya umeme."
Licha ya
Iran kukataa matakwa ya Marekani hapo awali, Trump aliendelea kuonyesha
matumaini kwamba Iran ilikuwa ikijadiliana kwa nia njema baada ya safu ya mfululizo
za uongozi wa Iran kuuawa katika mashambulizi ya Marekani na Israel.
Maendeleo
yenye tija katika mazungumzo yoyote hayawezekani kufanyika bila kusitisha
mapigano kwanza, kulingana na afisa wa kikanda anayefahamu majadiliano hayo.
Afisa huyo -
ambaye aliomba kutotajwa jina kutokana na jinsi mazungumzo yalivyo nyeti -
alisema kwamba majadiliano yalikuwa magumu kwa sababu ya changamoto ya mawasiliano
kutoka kwa maafisa wa Iran kutokana na hatua ya kuminywa kwa intaneti.
"Ili
kufikisha ujumbe kwa Iran, kupata jibu kwa wakati unaofaa ni jambo
lisilowezekana," afisa huyo alisema. "Wastani wa muda wa kutoa majibu
umekuwa siku moja hivi."
Pakistani,
Uturuki na Misri zote zinahusika katika juhudi za upatanishi.