Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Israel inasema imepata miili sita ya raia wake waliotekwa na Hamas Gaza

Israel inasema vikosi vyake vimefanikiwa kupata miili sita ya mateka wanaoshikiliwa na Hamas katika Ukanda wa Gaza.

Muhtasari

  • Miili 17 yapatikana kufuatia ajali ya helikopta ya watalii Urusi
  • Urusi kubadilisha sera yake ya nyuklia - Naibu Waziri wa Mambo ya Nje
  • "Ni Man City pekee ndio wameshinda zaidi ya timu yangu" - Erik Ten Hag
  • Mrembo aliyepigwa vita kutoka Afrika Kusini ashinda mashindano ya malkia wa urembo Nigeria
  • Msanii wa muziki wa Rap kutoka Marekani, Fatman Scoop, afariki baada ya kuanguka jukwaani
  • Moto wazuka katika mitambo ya umeme ya Urusi kufuatia mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Ukraine
  • Katika picha: Maelfu ya watoto wa Palestina waanza kupanga foleni ili kupata chanjo ya polio
  • Israel yasema polisi wake watatu wameuawa katika Ukingo wa Magharibi
  • Israel inasema imepata miili sita ya raia wake waliotekwa na Hamas Gaza

Moja kwa moja

Abdalla Seif Dzungu

  1. Waziri wa ulinzi wa Israel amuhimiza Netanyahu kujadili makubaliano ya kusitisha mapigano

    Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant amemtaka Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kufanya mazungumzo ya kusitisha mapigano na Hamas ili kuwarudisha nyumbani mateka waliosalia kutoka Gaza.

    Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X uliojulikana kama Twitter zamani, Gallant amesema "Muda umeisha kwa watu waliotekwa na kuawa bila hatia yoyote.”

    "Lazima mateka ambao bado wanashikiliwa na kundi la Hamas warudishwe nyumbani."

    Ombi lake linakuja baada ya miili sita ya mateka kupatikana katika handaki la chini ya ardhi huko Rafah kusini mwa Gaza.

  2. Muungano wa wafanyakazi wa Israel watangaza mgomo wa siku moja

    Muungano wa wafanyakazi wa Israel watangaza mgomo wa siku moja

    Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa shirikisho la vyama vya wafanyakazi nchini Israel - Histadrut – litafanya mgomo siku ya Jumatatu.

    Vyombo vya habari nchini Israel vinasema Mwenyekiti wa Shirikisho la Wafanyakazi Arnon Bar-David alipanga kukutana na familia za mateka saa 16:00PM saa za Israel (14:00 BST) kwenye makao makuu ya shirika lake huko Tel Aviv.

    Jukwaa la Mateka na Familia zilizotoweka awali lilikuwa limetaka muungano wenye nguvu zaidi nchini humo kushiriki katika mgomo huo baada ya kutoa wito kwa umma kwa ujumla "kujiunga na maandamano hayo makubwa".

    Je, tunafahamu nini kuhusu mgomo wa Muungano wa wafanyakazi nchini Israel had hadi sasa?

    Histadrut - moja ya vyama vya wafanyakazi vyenye nguvu zaidi nchini Israel - sasa inataka mgomo mkubwa ufanyike kesho siku ya Jumatatu huku kukiwa na wito kwa serikali kufikia makubaliano ya kuwarudisha mateka ambao bado wanashikiliwa na kundi la Hamas huko Gaza.

    Mkuu wa muungano huo, Arnon Bar-David, anasema kuwa Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion utafungwa kuanzia saa 08:00 AM saa za Israel (06:00 AM BST).

    Mgomo wenyewe umepangwa kuanza saa 06:00AM kwa saa za Israel (04:00AM BST) na utadumu kwa siku moja.

    Shirika la habari la taifa la Israel, Kan, linaripoti juu ya maelezo yaliyotolewa kutoka kwa taarifa ya hivi karibuni ya Bar-David, ikiwa ni pamoja na kauli yake anayosema kuwa "kutelekezwa" kwa mateka lazima kukomeshwe.

  3. Habari za hivi punde, Miili 17 yapatikana kufuatia ajali ya helikopta ya watalii Urusi

    Waokoaji katika eneo la mashariki mwa Urusi Urusi hawakupata mtu yeyote aliyenusurika kwenye mabaki ya helikopta iliyotoweka ikiwa imebeba watu 22 wengi wao wakiwa watalii.

    Ndege hiyo ilitoweka siku ya Jumamosi baada ya kupaa kutoka kambi moja karibu na volcano ya Vachkazhets katika rasi ya Kamchatka.

    Maafisa wanasema miili 17 ilikuwa imepatikana kufikia sasa.

    Eneo hilo, ambalo ni kivutio maarufu cha watalii, ni maarufu kwa volkano zake .

    Chanzo cha ajali hiyo hakijafahamika.

    Ajali kama hizo hutokea mara kwa mara katika eneo la mashariki mwa Urusi, ambalo lina watu wachache na linakabiliwa na hali mbaya ya hewa.

    Miaka mitatu iliyopita watu wanane waliuawa wakati helikopta ya watalii ilipoanguka katika ziwa huko Kamchatka.

    Helikopta ya Mi-8T iliyotoweka kwenye rada siku ya Jumamosi ilikuwa na watalii 19 na wafanyakazi watatu.

    Mabaki hayo yalipatikana Jumapili asubuhi katika eneo lenye milima, Gavana wa Kamchatka Vladimir Solodov alisema kwenye Telegram.

    Picha zilizochapishwa kwa programu ya ujumbe na wizara ya dharura ya Urusi zilionyesha vifusi vya helikopta vikiwa karibu na mteremko karibu na kilima kikubwa chenye miti.

    Maafisa walisema mabaki hayo yalipatikana karibu na eneo ambapo helikopta hiyo ilipotea katika rada.

    Afisa wa wizara ya dharura, Ivan Lemikhov, anasema miili 17 imepatikana hadi sasa na utafutaji wa wale ambao bado hawajapatikana umesitishwa, na unaotarajiwa kuendelea alfajiri siku ya Jumatatu.

    Shirika la habari la Interfax la Urusi liliripoti kwamba hitilafu, huenda ilisababishwa na ukungu.

    Awali, maafisa walisema kuwa ukungu mzito ulikuwa unatatiza juhudi za waokoaji.

    Ndege hiyo ilimilikiwa na Vityaz-Aero, kampuni ya Kamchatka ambayo hupanga safari za watalii.

    Ikiwa imeundwa wakati wa enzi ya Soviet, helikopta hiyo ya Mi-8 bado inatumika sana nchini Urusi.

  4. Urusi kubadilisha sera yake ya nyuklia - Naibu Waziri wa Mambo ya Nje

    Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Ryabkov aliambia shirika la habari la TASS kwamba seraya nyuklia la Urusi itabadilishwa.

    Ryabkov hakufafanua ni nini hasa kitabadilika katika sera hiyo ya kijeshi. Alitangaza mabadiliko hayo yatafanyika mwisho wa Juni.

    "Kama tulivyosema mara kwa mara, kazi hiyo iko katika hatua za juu na kuna mwelekeo wa wazi kufanya marekebisho, ambayo pia yanatokana na utafiti na uchambuzi wa migogoro katika miaka ya hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na, bila shaka kila kitu kinachohusiana na uchokozi wa wapinzani wetu wa Magharibi kuhusiana na SVO," TASS inamnukuu Ryabkov akisema (SVO ni "operesheni maalum ya kijeshi" - kuhusu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine).

  5. "Ni Man City pekee ndio wameshinda zaidi ya timu yangu" - Erik Ten Hag

    Erik ten Hag anasema ana uhakika wa kushinda mataji tena akiwa na Manchester United - kwa sababu ni Manchester City pekee ndio walionyanyua zaidi ya timu yake katika miaka miwili iliyopita.

    Akiongea kabla ya mechi ya Jumapili ya Old Trafford inayosubiriwa kwa hamu dhidi ya Liverpool, meneja Ten Hag alisisitiza mara mbili kwamba ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza City ambao wamemapata mataji zaidi ya mawili tangu aanze kuinoa United 2022.

    United iliilaza Newcastle na kushinda Kombe la Carabao mwaka wa 2023, na hivyo kuhitimisha kusubiri kwa miaka sita kwa klabu hiyo kupata kombe, na kisha kunyakua Kombe la FA mwezi Mei baada ya ushindi wa kushtukiza wa fainali dhidi ya Manchester City kwenye uwanja wa Wembley.

    Sir Alex Ferguson ndiye meneja pekee wa United kushinda mataji katika misimu mitatu mfululizo."Katika miaka miwili iliyopita tulishinda, nyuma ya City, mataji mengi zaidi katika soka ya England," Ten Hag alisema.

    "Huo ndio ukweli. Ni ukweli."Mwaka huu tunataka kushinda. Tunataka kushinda mataji. Nina imani kabisa tutafanya hivyo."

  6. Mrembo aliyepigwa vita kutoka Afrika Kusini ashinda mashindano ya malkia wa urembo Nigeria

    Baada ya kuandamwa juu ya uraia wake na kulazimishwa kujiondoa kwenye shindano la Afrika Kusini, Chidimma Adetshina ametawazwa kuwa malkia wa urembo wa nchi tofauti kabisa.

    Bi Adetshina alilia machozi ya furaha alipotangazwa kuwa Miss Universe Nigeria siku ya Jumamosi.

    "Taji hili si la urembo tu; ni wito wa umoja," mwanafunzi huyo wa sheria mwenye umri wa miaka 23 alisema hayo baada ya wiki ya kusakamwa na vyombo vya habari.

    Alialikwa kushiriki Miss Universe Nigeria baada ya nafasi yake kama mshindi wa fainali katika shindano la Miss Afrika Kusini kuzua wimbi la ukosoaji.

    Baadhi ya watu nchini Afrika Kusini walikuwa wametilia shaka kustahili kwake kushiriki mashindano hayo kwa sababu licha ya kuwa ni raia wa Afrika Kusini, baba yake Bi Adetshina ana asili ya Nigeria huku mama yake akiwa na asili ya Msumbiji.

    Mzozo kuhusu uraia wake ulisababisha uchunguzi kufanyika huku waandaji wa Miss Afrika Kusini wakiitaka idara ya mambo ya ndani ya taifa hilo kuangalia kustahili kwake.

    Baada ya uchunguzi wa awali, idara ilitangaza kuwa mama yake Bibi Adetshina huenda alifanya "wizi wa utambulisho" ili aweze kuwa raia wa Afrika Kusini.

    Hata hivyo, taarifa hiyo iliongeza kuwa Bi Adetshina "hangeweza kushiriki katika madai ya vitendo vya kinyume cha sheria vya mama yake kwani alikuwa mtoto mchanga wakati huo".

    Baada ya kusikia yaliomkuta Bi Adetshina, waandaaji wa Miss Universe Nigeria walimwalika kushiriki katika shindano lao.

    Walisema ataweza "kuwakilisha nchi asili ya baba yake kwenye jukwaa la kimataifa".

    Baada ya kushinda shindano hilo siku ya Jumamosi, Bi Adetshina atawakilisha Nigeria katika shindano la Miss Universe linalotarajiwa kufanyika mwezi Novemba mwaka 2024.

    Mafanikio yake yamesherehekewa kwenye mitandao ya kijamii mbalimbali.

  7. Msanii wa muziki wa Rap kutoka Marekani, Fatman Scoop, afariki baada ya kuanguka jukwaani

    Msanii wa muziki wa Rap kutoka Marekani, Fatman Scoop, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 53 baada ya kuanguka kwenye tamasha lake siku ya Ijumaa huko Connecticut.

    Alikuwa katikati ya tamasha hilo katika eneo la Town Centre Park kwenye mji wa Hamden pale alipoanguka jukwaani.

    Meya wa eneo hilo, Lauren Garrett aliandika kupitia mtandao wa Facebook kuwa msanii huyo alipelekwa katika hospitali ya mtaa na gari la kubeba wagonjwa.

    Lakini shirika lake lililokuwa linasimamia shughuli zake za mziki, MN2S, lilithibitisha kifo chake kupitia taarifa kwa BBC, likisema kwamba "alama nzuri ya mzaliwa huyo wa New York itaendelea milele kupitia muziki wake".

    Scoop, ambaye jina lake rasmi ni Isaac Freeman III, ametambuliwa kama mtu mashuhuri katika eneo la muziki wa hip hop la New York City katika miaka ya 1990.

    Ameshiriki kwenye nyimbo maarufu ikiwa ni pamoja na Lose Control iliyoshinda tuzo ya Grammy ya Missy Elliott na It's Like That ya Mariah Carey.

    Katika taarifa yake kwenye mitandao ya kijamii, familia ya Scoop ilisema alikuwa "mtu mzuri sana, ambaye ni mfano bora kote jukwaani na katika maisha"

  8. Moto wazuka katika mitambo ya umeme ya Urusi kufuatia mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Ukraine

    Ukraine imeanzisha wimbi la mashambulizi ya usiku kucha kwa kutumia ndege zisizo na rubani dhidi ya Urusi, na kusababisha moto katika vituo viwili vya nishati vya Urusi.

    Kulingana na wizara ya ulinzi ya Urusi, zaidi ya ndege 158 zisizo na rubani za Ukraine zililenga maeneo 15 ya nchi hiyo, ukiwemo mji mkuu wa Moscow.

    Jeshi la Urusi lilidai kwamba ndege hizo zisizo na rubani zilinaswa na kuharibiwa.Lakini kutokana na shambulio hilo moto umezuka katika kiwanda cha kusafisha mafuta huko Moscow katika "chumba tofauti cha kiufundi", meya wa jiji hilo ameisema.

    Sergei Sobyanin aliripoti kuwa takriban ndege 11 zisizo na rubani zililenga mji mkuu na maeneo jirani.

    Wakati huo huo, maili 75 (km 120) kutoka mji mkuu wa Urusi, katika mkoa wa Tver, milipuko mikubwa ilisikika karibu na Kituo cha nishati cha Konakovo.

    Vyombo vya habari vya Urusi vinaripoti moto katika kituo hicho.

    Gavana wa eneo hilo, Igor Rudenya, amesema moto uliosababishwa na shambulio katika wilaya ya Konakovsky ulikuwa umedhibitiwa , bila kutoa maelezo ya kile kilichoshambuliwa.

    Maafisa wa eneo hilo pia walisema ndege zisizo na rubani zilijaribu kushambulia Kiwanda cha Nishati cha Kashira katika mkoa wa Moscow –ila hakukuwa na moto, uharibifu au majeruhi yalioshuhudiwa.

    Ukraine haijatoa tamko lolote kuhusu madai hayo. Vikosi vya Ukraine vimekuwa vikiongeza mashambulizi ya masafa marefu ndani ya Urusi katika miezi michache iliyopita, vikirusha ndege zisizo na rubani kwa wakati mmoja katika malengo ya kimkakati mara kadhaa kwa wiki.

    BBC imeambiwa kwamba teknolojia na fedha za nchi za Magharibi zinawasaidia kutekeleza mamia ya mashambuliziya masafa marefu ndani ya Urusi.

  9. Katika picha: Maelfu ya watoto wa Palestina waanza kupanga foleni ili kupata chanjo ya polio

    Tukirudi katika habari kuhusu chanjo ya polio, wizara ya afya ya Palestina huko Gaza imetoa picha mpya kutoka kwa mkoa wa kati.

    Maelfu ya watoto wa Kipalestina wameanza kupanga foleni ili kupata chanjo hiyo asubuhi ya leo, usambazaji unaotegemea msururu wa kusitishwa kwa mapigano kati ya vikosi vya Israel na wapiganaji wa Hamas.

  10. Israel yasema polisi wake watatu wameuawa katika Ukingo wa Magharibi

    Maafisa watatu wa polisi wa Israel - wanaume wawili na mwanamke mmoja - wameuawa baada ya gari lao kupigwa risasi karibu na mji wa Hebron katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa, mamlaka ya Israeli inasema.

    Akizungumza katika eneo la ufyatuaji risasi, kamishna wa polisi wa Israel Daniel Levy amesema maafisa hao watatu walikuwa wakihudumu katika wilaya ya Yudea na Samaria, ambalo ni neno la kibiblia linalotumika kuelezea Ukingo wa Magharibi.

    Maafisa wawili kati ya hao walitangazwa kufariki katika eneo la tukio karibu na kivuko cha Tarkumiya. Afisa wa tatu alipelekwa hospitalini kwa helikopta lakini baadaye alifariki.

    Maeneo ya Ukingo wa Magharibi - ambayo yamekuwa chini ya utawala wa Israel tangu vita vya Mashariki ya Kati vya 1967 - yamelengwa katika "operesheni ya kijeshi" iliyoratibiwa ya Israeli wiki hii, na kusababisha wito wa Umoja wa mataifa wa kusitisha vita.

  11. Israel inasema imepata miili sita ya raia wake waliotekwa na Hamas Gaza

    Israel inasema vikosi vyake vimefanikiwa kupata miili sita ya mateka wanaoshikiliwa na Hamas katika Ukanda wa Gaza.

    Katika taarifa, Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilisema miili hiyo ilipatikana siku ya Jumamosi kwenye handaki la chini ya ardhi katika eneo la Rafah.

    IDF iliwataja mateka hao kuwa ni Carmel Gat, Eden Yerushalmi, Hersh Goldberg-Polin, Alexander Lobanov, Almog Sarusi na Mwalimu Sgt Ori Danino.Rais wa Marekani Joe Biden alisema Bw Goldberg-Polin alikuwa raia wa Marekani.

    "Nimehuzunishwa na kughadhabishwa," Bw Biden alisema.Katika taarifa yake Jumapili asubuhi, IDF ilisema miili hiyo "imerejeshwa katika eneo la Israeli".

    "Wote walichukuliwa mateka tarehe 7 Oktoba [2023] na waliuawa na kundi la kigaidi la Hamas katika Ukanda wa Gaza."Taarifa hiyo iliongeza kuwa familia zao tayari zimearifiwa.

    Wakati huo huo, Rais Biden alisema katika taarifa yake kwamba "Hersh alikuwa miongoni mwa watu wasio na hatia walioshambuliwa kikatili alipokuwa akihudhuria tamasha la muziki la amani nchini Israel tarehe 7 Oktoba".

    "Alipoteza mkono wake akiwasaidia marafiki na wageni wakati wa mauaji ya kikatili ya Hamas.

    Alikuwa ametimiza umri wa miaka 23 tu. Alipanga kusafiri kote dunia."Nimewafahamu wazazi wake, Jon na Rachel.

    Wamekuwa wajasiri, wenye hekima, na imara, licha ya kustahimili mambo yasiyowezekana," Bw Biden alisema.

    Jeshi la Israel lilianzisha kampeni huko Gaza ya kuangamiza Hamas kujibu shambulio ambalo halijawahi kushuhudiwa kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba, ambapo takriban watu 1,200 waliuawa na wengine 251 kuchukuliwa mateka.

    Zaidi ya watu 40,530 wameuawa huko Gaza tangu wakati huo, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas.Wapatanishi wa Marekani, Misri na Qatar wanajaribu kusuluhisha makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo yatawezesha Hamas kuwaachilia mateka 97 ambao bado wanashikiliwa, wakiwemo takriban 27 wanaodhaniwa wamekufa, ili kubadilishana na wafungwa wa Kipalestina katika jela za Israel.

  12. Ni siku ya Jumapili na nadhani umeamka vyema