Waokoaji katika eneo la
mashariki mwa Urusi Urusi hawakupata mtu yeyote aliyenusurika kwenye mabaki ya
helikopta iliyotoweka ikiwa imebeba watu 22 wengi wao wakiwa watalii.
Ndege hiyo ilitoweka
siku ya Jumamosi baada ya kupaa kutoka kambi moja karibu na volcano ya
Vachkazhets katika rasi ya Kamchatka.
Maafisa wanasema miili
17 ilikuwa imepatikana kufikia sasa.
Eneo hilo, ambalo ni kivutio
maarufu cha watalii, ni maarufu kwa volkano zake .
Chanzo cha ajali hiyo hakijafahamika.
Ajali kama hizo hutokea
mara kwa mara katika eneo la mashariki mwa Urusi, ambalo lina watu wachache na linakabiliwa na hali
mbaya ya hewa.
Miaka mitatu iliyopita
watu wanane waliuawa wakati helikopta ya watalii ilipoanguka katika ziwa huko
Kamchatka.
Helikopta ya Mi-8T
iliyotoweka kwenye rada siku ya Jumamosi ilikuwa na watalii 19 na wafanyakazi
watatu.
Mabaki hayo yalipatikana
Jumapili asubuhi katika eneo lenye milima, Gavana wa Kamchatka Vladimir Solodov
alisema kwenye Telegram.
Picha zilizochapishwa
kwa programu ya ujumbe na wizara ya dharura ya Urusi zilionyesha vifusi vya
helikopta vikiwa karibu na mteremko karibu na kilima kikubwa chenye miti.
Maafisa walisema mabaki
hayo yalipatikana karibu na eneo ambapo helikopta hiyo ilipotea katika rada.
Afisa wa wizara ya
dharura, Ivan Lemikhov, anasema miili 17 imepatikana hadi sasa na utafutaji wa
wale ambao bado hawajapatikana umesitishwa, na unaotarajiwa kuendelea alfajiri
siku ya Jumatatu.
Shirika la habari la
Interfax la Urusi liliripoti kwamba hitilafu, huenda ilisababishwa na ukungu.
Awali, maafisa walisema
kuwa ukungu mzito ulikuwa unatatiza juhudi za waokoaji.
Ndege hiyo ilimilikiwa
na Vityaz-Aero, kampuni ya Kamchatka ambayo hupanga safari za watalii.
Ikiwa imeundwa wakati wa enzi ya Soviet, helikopta hiyo ya
Mi-8 bado inatumika sana nchini Urusi.