Tume ya vurugu za uchaguzi Tanzania yakataa madai ya kuingiliwa, yasema iko huru

Chanzo cha picha, TUME
Mwenyekiti wa Tume ya kuchunguza vurugu za uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, Jaji Othman Chande, amesema tume hiyo iko huru na haiikingiliwa na mamlaka yoyote, akikanusha madai kuwa muda wa kazi yake umeongezwa ili kuruhusu kuhaririwa kwa ripoti yake.
Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam leo, Jaji Chande alisema kuwa tume hiyo ina mamlaka kamili ya mwisho juu ya ripoti yake na haitoi nafasi kwa mtu yeyote kuingilia kazi yake.
"Tume inajitegemea kwa kila kitu. Tume yenyewe ndiyo mhariri, na mamlaka iliyotupa jukumu tutakutana nayo wakati wa kukabidhi ripoti ya mwisho, hatuna mtu yoyote katikati, hatuna dalali," alisisitiza.
Kumekuwa na madai kutoka kwa baadhi ya wadau hasa wanaharakati mitandaoni nchini Tanzania wanaoona kwamba kuongezwa kwa muda wa tume hiyo mara mbili kunalenga kutoa nafasi kwa mamlaka fulani 'kuchakachua' yaliyomo kwenye ripoti hiyo.
Hata hivyo, Jaji Chande alieleza kuwa sababu kuu ya kuongeza muda ni kupanuka kwa wigo wa kazi pamoja na ongezeko la ushahidi unaokusanywa.
"Awali tulipanga kutembelea mikoa sita, lakini baadaye tukapanua na kufikia mikoa 11 na wilaya 22," alisema.
Aliongeza kuwa tume imepokea ushahidi mwingi kutoka kwa wananchi na wadau mbalimbali, pamoja na ushauri wa kitaalamu ambao unahitaji kuchambuliwa kwa kina kabla ya kukamilisha ripoti.
"Tunachambua ushahidi kwa kina ili kuhakikisha ripoti yetu inakuwa na ubora unaotakiwa, na pia itatolewa kwa lugha ya Kiswahili na tafsiri ya Kiingereza," alifafanua.
Jaji Chande aliwahakikishia watanzania kuwa hawapaswi kuwa na hofu kuhusu uadilifu wa ripoti hiyo, akisisitiza kuwa tume hiyo inafanya kazi kwa uhuru bila shinikizo la nje.
Tume hiyo iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan novemba 20, 2025 kuchunguza matukio yaliyojitokeza wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, imeongezewa muda mara mbili.
Awali ilipewa siku 90 kabla ya kuongezea siku 42 na wiki hii ikaongezewa siku nyingine 21, ambapo sasa itakamilisha kazi yake April 24, 2026.
Moja ya majukumu ya tume hiyo ni kuchunguza kiini cha vurugu za uchaguzi huo zilizosababisha vifo vya watu kadhaa na uharibu mkubwa wa mali zikiwemo ofisi za umma, vituo vya mafuta na vituo vya Polisi.














