Polisi Tanzania imezuia pasipoti ya mpenzi wa Ashley na wanamhoji

Chanzo cha picha, social
Polisi nchini Tanzania imesema kuwa imezuia pasipoti ya Joseph Mccan huku wakiendelea kumhoji baada ya mpenzi wake mwanamitindo wa Marekani, Ashly Jenae mwenye umri wa miaka 31 kuripotiwa kufariki dunia.
Wamesema wanaendelea kufanya uchunguzi wakisubiria majibu kutoka kwa madaktari cha kubaini chanzo kifo cha mwanadada huyo raia wa Marekani.
Ashly na mpenzi wake Joseph Isaac Maccann mwenye umri wa miaka 45 waliwasili kisiwani Zanzibar tarehe 4 mwezi Aprili na walikuwa na malumbano ambapo hoteli waliokuwa wakikaa ikawatengenisha na kuwapa vyumba viwili kwa ajili ya usalama wao.
Katika mahojiano yao ya kwanza na chombo cha habari cha kitaifa, wazazi wa Ashly Robinson, mshawishi wa mitindo ya maisha wa Marekani mwenye umri wa miaka 31 aliyefariki chini ya mazingira yasiyoeleweka akiwa likizoni Zanzibar pamoja na mchumba wake, wanajaribu kufahamu kilichompata binti yao aliyekuwa akisherehekea siku yake ya kuzaliwa na uchumba wake.
"Alipaswa kuwa na furaha," mama yake, Yolanda Endres, aliiambia CBS News kupitia @iamthatreporterjd. "Kisha ghafla akawa hayupo."
Endres pamoja na baba wa Robinson, Harry Robinson, walisema walipokea taarifa mara moja tu kutoka kwa mchumba wa binti yao, Joe McCann, saa 11 baada ya tukio linalodaiwa kusababisha kifo chake. Baadaye walifahamishwa na hoteli waliokuwa wamekodisha kwamba Ashly alikuwa amefariki.
CBS News imewasiliana na kampuni ya McCann, Asymmetric, kuomba maoni, lakini haikupata majibu.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imethibitisha kwa CBS News kuwa raia wa Marekani amefariki Zanzibar, lakini haikutoa maelezo zaidi kwa sababu za faragha.

Chanzo cha picha, Ashly Jenae/Ig
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Awali Polisi Zanzibar walisema kuwa mwanamitindo anayeishi Marekani, Ashly Robinson maarufu kama Ashlee Jenae, alifariki kwa kujitoa uhai alipokuwa likizoni kisiwani humo pamoja na mchumba wake, Joe McCann.
Kisa hicho kimevutia umakini mkubwa kwenye mitandao ya kijamii katika siku tatu zilizopita, huku mamlaka zikisema zinasubiri matokeo ya uchunguzi wa maiti.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Benedict Mapujira, aliiambia BBC siku ya Jumatatu kuwa tukio hilo lilitokea Jumatano, Aprili 8, ambapo mwanamke huyo anadaiwa kujinyonga kwa kutumia kipande cha kitambaa.
Mapujira alisema wawili hao waliripotiwa kutoelewana, hali iliyosababisha uongozi wa hoteli kuwatenganisha na kuwapatia vyumba tofauti.
Alisema: "Mwanamke huyo alikuwa na mchumba wake, McCann, na walikuwa kisiwani kwa mapumziko... tunaambiwa walikuwa mzozano, na hoteli iliwapatia makazi tofauti; mwanamke alikuwa na chumba chake, na mwanaume pia alikuwa na chumba chake."
Polisi walisema tukio hilo liliripotiwa usiku katika kituo cha polisi cha karibu baada ya wafanyakazi wa hoteli kutoa taarifa kwamba kulikuwa na mgeni aliyeshukiwa kuwa katika hatari ya kujitoa uhai.
"Ashly alipelekwa hospitalini usiku huo kwa matibabu, lakini alifariki siku iliyofuata (Aprili 9)," polisi waliiambia BBC, wakiongeza kuwa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Kwa mujibu wa mamlaka, mwili wake bado uko Zanzibar ukisubiri uchunguzi zaidi kabla ya taratibu za kuusafirisha kurejeshwa nyumbani kufanyika.
Kwa mujibu wa taarifa zinazosambaa mitandaoni, mshauri huyo alisafiri kwenda Tanzania kusherehekea siku yake ya kuzaliwa Aprili 5, na alichapisha picha katika ukurasa wake wa Instagram siku hiyo, zikiwa zimepigwa katika hifadhi ya wanyama iliyoko mkoa wa Kilimanjaro.
Ujumbe kwenye akaunti ya Instagram ya Ashly umechanganya salamu za rambirambi pamoja na wito wa haki.
Kwa mujibu wa vyanzo, wakati wa safari hiyo, McCann pia alimshangaza kwa kumvisha pete ya uchumba, tukio lililoelezwa baadaye na familia yake kuwa la kukumbukwa.
Taarifa ya pamoja inayodaiwa kutoka kwa familia za Robinson na Endres, na kusambazwa sana mtandaoni, ilisomeka: "Wakati mmoja alikuwa akisherehekea upendo na maisha kwa namna yake ya kipekee, na muda mfupi baadaye, akawa hayupo tena."
Familia hizo zinasema zinaendelea kushirikiana na mamlaka za Zanzibar huku uchunguzi ukiendelea.
Katika mitandao ya kijamii kama X na Instagram, tukio hilo limeibua mjadala mkubwa, huku baadhi ya watumiaji wakitaka uchunguzi wa kina kuhusu kifo chake.
Wazazi wa Ashly wameripotiwa kuwa wanasafiri kuelekea Zanzibar kutathmini hali.












