Wanasayansi wagundua sukari katika anga za mbali

.

Chanzo cha picha, NASA/Universal History Archive/Universal Images Group via Getty Images

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Wanasayansi wamegundua chembechembe za sukari katika anga za kati kwa mara ya kwanza.

Kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa wiki hii katika jarida la Nature Astronomy, ugunduzi huo unadokeza jinsi ambavyo chembechembe zinaweza kuwa muhimu kwa uelewa wetu wa asili ya molekuli hizi duniani na asiloi ya uhai katika sayari yetu.

Timu ya kimataifa, ikiongozwa na wanaastronomia kutoka Kituo cha Astrobiolojia nchini Uhispania, imegundua uwepo wa chembe chembe za kisukari zinazoitwa erytherythrulose katika anga za kati, eneo kati ya nyota, ambalo linajumuisha zaidi gesi na vumbi.

Erythrulose imeundwa na atomi nne za kaboni, atomi nane za hidrojeni na atomi nne za oksijeni na Duniani tunaweza kuipata kwa kiasi kidogo katika matunda kama vile raspberries na bidhaa zinazojiongezea rangi.

Kwa mujibu wa wataalamu, ugunduzi wa sukari hii katika nebula karibu na katikati ya galaski ya Milky Way unaonyesha kwamba chembe chembe, tata muhimu kwa uhai zinaweza kuundwa hapo, licha ya hali yake ya joto kali.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Wanasayansi wanakadiria kuwa mamilioni ya tani za sukari hii huenda zilifika Duniani kupitia tukio linalojulikana kama nadharia ya 'Late Intense Bombardment' kumaanisha kipindi cha makabiliano makali ya vitu angani, ambapo asteroidi na nyota zenye mikia ziliigonga sayari hii kati ya miaka 4,100 na 3,800 iliyopita, na hivyo kuchukua nafasi muhimu katika kuundwa kwa molekuli za kwanza muhimu kwa uhai.

"Hii ndiyo sukari ya kwanza kugunduliwa katika anga la nje (kati ya nyota) na ni muhimu kwa sababu inatuonyesha kuwa sukari za aina hii zinapatikana kwa wingi zaidi kuliko tulivyodhani," alisema Dkt. Izaskun Jiménez-Serra, kutoka Kituo cha Uhispania cha Astrobiolojia, ambaye alikuwa mmoja wa watafiti wakuu katika utafiti huo.

"Hii inafungua uwezekano wa uhai kuibuka katika ulimwengu mwingine kwa namna inayofanana na jinsi ulivyotokea Duniani," aliongeza.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kulingana na waandishi wa utafiti huo, kabla ya ugunduzi huu, wanasayansi walikuwa tayari wamegundua sukari kama vile ribosi au glukosi kwenye vimondo na asteroidi, jambo linaloashiria kuwa chanzo cha sukari duniani kinaweza kuwa ni kutoka nje ya sayari hii.

Hata hivyo, sukari haikuwahi kugunduliwa katika anga la nje (eneo lililo katikati ya nyota) na haikuthibitishwa kuwa erythrulose, hasa, inaweza kutengenezwa kiasili angani.

Timu za utafiti zilitumia michanganuo ambayo ni nyeti zaidi na ya ukanda mpana, kwa kutumia darubini mbili zenye nguvu za kipenyo cha mita 30 na 40.

Kwa njia hii, walikusanya data kuhusu masafa ya redio kutoka nafasi ya nyota na kubaini ulinganifu na wigo wa mzunguko wa erythrulose.

Asili ya sukari duniani ni mojawapo ya maswali ambayo kwa kiasi kikubwa yameangaziwa sana na wanasayansi wanaosoma hatua ya prebiotic, yaani kabla ya maisha.

Inaaminika kuwa sukari lazima itengenezwe mapema sana kwa sababu ni muhimu kwa malezi na kukuwa kwa viumbe hai vya kwanza.

Shida, hadi sasa, ilikuwa kwamba majaribio ya maabara ya kuunda tena hali za kemikali kabla ya maisha yalishindwa mara kwa mara, kwa mujibu wa watafiti.

.

Chanzo cha picha, Ashley Barnes/Izaskun Jiménez-Serra/Juan García de la Concepción

"Haisuluhishi tatizo la asili ya maisha"

Ugunduzi huo ulipokelewa vyema na ulimwengu wa kisayansi.

Wataalamu wanaangazia mchango wa "ajabu" na "muhimu" ambao utafiti unaweza kumaanisha kwa sayansi.

Hata hivyo, baadhi ya wanazuoni pia wameonya kuhusu mapungufu yake.

César Menor Salván, mwanajimu na profesa wa Biokemia katika Chuo Kikuu cha Alcala, alisema kulingana na Kituo cha Vyombo vya Habari vya Sayansi cha Uhispania kwamba "jambo la kwanza kusema ni kwamba kazi hii haisuluhishi tatizo la asili ya uhai au asili ya molekuli kama vile DNA au RNA."

Mtaalamu huyo alisisitiza kwamba kugunduliwa kwa sukari angani "kunaweza kuunga mkono dhana kwamba molekuli hizi, zilizokusanywa na kuhifadhiwa kwenye barafu, zinaweza kutoa sukari hizi katika mazingira yanayofaa kwa asili ya maisha, kama vile asili ya dunia."

Na alielezea kuwa "Inaonyesha kwamba erythrulose iko katika wingu la molekuli angani, si kwamba inafika duniani au mahali pengine ambapo uhai unaweza kutokea, si kwamba chembe chembe hizo zinaweza kusalia hai katika safari hiyo, wala kufikia viwango vinavyofaa au kwamba inashiriki katika usanisi wa prebiotic."

Kwa upande wake, Andrés de la Escosura Navazo, mtafiti katika Taasisi ya Utafiti wa Kina katika Sayansi ya Kemikali (IAdChem), alifichua kwamba "kuna njia ndefu sana ya kuelewa jambo lolote tatanishi" asili na chimbuko la uhai.

"Kupata baadhi ya vipengele hivi vya msingi vya Masi katika anga ni hatua muhimu katika mwelekeo huo," aliongeza.