The Polygamist: Filamu ya Netflix iliyotokana na riwaya ilivyowatikisa wanawake walio kwenye ndoa Afrika

    • Author, Megha Mohan
    • Nafasi, BBC World Service
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Wakati Sue Nyathi alipowasilisha riwaya yake ya kwanza, The Polygamist, kwa wachapishaji, "walifikiri kwamba hakukuwa na soko la kitabu hicho," anasema. Kitabu hicho kinamhusu mwanaume wa Zimbabwe mwenye ndoa na wanawake anaowashawishi kimapenzi.

Kwa hiyo, mwandishi huyo wa Zimbabwe alimtafuta mhariri wake mwenyewe, mchapaji na msanii, na mwaka 2012 akachapisha nakala 500 kwa gharama zake.

Kinyume na utabiri wa wachapishaji, kitabu hicho kilipata mafanikio makubwa.

Sasa kimebadilishwa kuwa filamu ya Netflix na kimeingia katika orodha ya vipindi 10 vilivyotazamwa zaidi kwenye jukwaa hilo katika zaidi ya nchi 60, kikifikia nafasi ya pili nchini Marekani. Mwigizaji wa Hollywood, Taraji P. Henson, alisema mfululizo wa filamu hiyo ulimfanya asitoke kwenye skrini, kiasi kwamba alitazama vipindi vyote 22 ndani ya siku moja.

Nyathi anasisitiza kwamba huu si mfululizo unaohusu moja kwa moja suala la ndoa za wake wengi. Mila ya mitala si jambo geni kwake. Upande wa familia ya mama yake ilikuwa na desturi ya mitala kwa vizazi kadhaa.

Babu yake, aliyefariki mwaka 1979, alikuwa na wake watano, huku babu yake mkubwa akiwa na wake 11. Bibi yake, ambaye alikuwa mwanamke wa kwanza kuolewa na babu yake, alikuwa kiongozi wa familia kwenye shamba ambako wake hao waliishi pamoja, na mara nyingi hata alisaidia kuwachagua wanawake wapya waliojiunga na familia.

"Haikuwa na migogoro ya ndani, kwa sababu kila mtu alijua nafasi yake," anasema Nyathi.

Alipomuuliza bibi yake alielewaje jambo hilo alisema;

"Kila mtu anajua nani ni nani katika hii familia," Nyathi anaeleza.

Mitala inatambuliwa kisheria nchini Zimbabwe na Afrika Kusini ikiwa inafanywa kwa kufuata mila na desturi maalum zinazotambulika. Lakini jambo ambalo Nyathi alianza kuliona akiwa mwanamke kijana anayefanya kazi jijini Harare mwaka 2001 lilikuwa tofauti kabisa.

Wanaume waliodai kuwa katika ndoa za mke mmoja walikuwa, kwa uhalisia, wakiishi maisha ya mitala, wakiwa na wanawake wa siri na familia za siri. Hiyo ndiyo aina ya mitala inayozungumziwa katika riwaya yake, ambayo anaieleza kama "toleo la kisasa, au lililopotoshwa" la mitala, linalohusu udanganyifu badala ya ridhaa.

"Sipingi mitala," anasema Nyathi. "Ninachopinga ni kunyimwa uwezo wa mtu wa kufanya uamuzi kuhusu maisha yake. Si sahihi kubadilisha masharti baada ya mtu tayari kuwa ndani ya uhusiano."

Katika riwaya hiyo, mhusika mkuu wa kike, Joyce, anaamini kwamba ameolewa katika ndoa ya mtu mmoja na mwanamke mmoja. Hata hivyo, mume wake, Jonasi, anafunga ndoa na kuanzisha maisha na wanawake wengine watatu bila yeye kujua.

Hakuna kukiri wala kutangazwa kwa jambo hilo; Joyce anaishia kutambua, kadiri siri zinavyoongezeka na maisha ya wanawake hao yanavyoungana, kwamba wazo lake la kuwa katika ndoa ya mke mmoja limekuwa udanganyifu tangu mwanzo.

Swali la nani ana mamlaka ya kujadiliana na nani hana mamlaka hayo linapita katika hadithi nzima. Jonasi ni mfanyabiashara tajiri aliyejijenga mwenyewe, na katika jamii yenye mfumo dume, yeye ndiye anayefanya maamuzi kuhusu kila jambo.

Ingawa Joyce alimsaidia kujenga himaya yake ya biashara, hali yake ya kifedha inamtegemea yeye. Hali hiyo ni sawa na ya mke mwingine wa baadaye, Matipa, ambaye pia anamfanyia Jonasi kazi.

Kwa sababu hiyo, wanawake hao wana uhuru mdogo wa kujiamulia mambo yao, jambo linalowaweka katika mazingira hatarishi. Tofauti za umri zinaongeza zaidi ukosefu huo wa usawa, Nyathi anasema, hata katika maamuzi ya mambo ya faragha zaidi.

Kuna pia kisa kinachohusiana na HIV katika hadithi hiyo. Anasema, "ikiwa unajaribu kujadiliana kuhusu ngono salama, huwezi kuwa na sauti katika uhusiano wenye mienendo ya aina hiyo."

Kuna tofauti chache kati ya kitabu na mfululizo wa Netflix. Kwenye skrini, hadithi imehamishiwa Afrika Kusini, imerekodiwa kwa lugha ya Kizulu ikiwa na nukuu, na Jonasi ana wake wachache zaidi. Tofauti na toleo la televisheni, riwaya hiyo inasimuliwa kikamilifu kutoka kwa mtazamo wa wake wa Jonasi.

"Nilitaka kuangazia sauti za wanawake," anasema Nyathi, ili kumruhusu kila mwanamke kueleza kwa nini alijikuta katika uhusiano na mwanaume ambaye hakuwa mwaminifu kwake.

Anaongeza kwamba mada hizi zinawagusa wasomaji wengi. Wanawake humwandikia wakisema kwamba wanajiona katika maisha ya Joyce na wake wengine wa Jonasi. Baadhi yao huongeza kwamba wameolewa na mtu wa aina ya Jonasi na wanataka kuondoka katika mahusiano hayo.

Baada ya mfululizo huo kuoneshwa, Amnesty South Africa ilisambaza mwongozo kuhusu watu wenye tabia za unyanyasaji wa kihisia na hatua ambazo mwanamke anaweza kuchukua.

"Kwa baadhi ya watu, huu si mfululizo wa filamu tu," anasema Nyathi. "Ni maisha yao halisi. Unaonesha jamii kama ilivyo, kana kwamba ni kioo."

Hata hivyo, si kila mtu ameunga mkono tafakari hiyo.

Geoffrey Mosiria, mtumishi wa umma nchini Kenya, alitoa wito wa mfululizo huo kupigwa marufuku nchini Kenya, akidai kwamba unachanganya mitala na ukafiri, ulaghai na unyanyasaji. Nyathi hatikiswi na ukosoaji huo. Anasema utamaduni hubadilika, na desturi zinaweza kudhoofishwa au kupotoshwa; yeye anaonesha tu kile kilichotokea kwa desturi hiyo.

Anasema kwamba kwa kuwaweka Waafrika weusi wenye uwezo mkubwa wa kifedha kama wahusika wakuu, amefungua macho ya watu wengi. Anakumbuka msomaji mmoja wa Ulaya aliyemwambia kwamba hakuwahi kutambua kuwa Waafrika weusi matajiri wapo.

"Daima tumekuwa na mtazamo wa kijumla na wa dhana potofu kuhusu maana ya kuwa Mwafrika, na mara nyingi umehusishwa na umaskini," anasema Nyathi.

Filamu inaonesha hali tofauti na, kwa maoni yake, unakuwa na thamani zaidi kwa sababu umerekodiwa kwa lugha ya Kizulu: "Kiingereza hakibebi utajiri uleule wa kitamaduni ambao lugha zetu zinaubeba."

Ikiwa kuna hali ya kuchoshwa au kukatishwa tamaa ndani yake, hujitokeza hasa anapozungumzia suala la nani anapewa nafasi ya kuwa mwandishi. Nyathi alitamani kuwa mwandishi tangu utotoni, lakini wazazi wake walimsukuma kuelekea taaluma ya jadi na yenye uhakika zaidi.

Alifanya kazi katika sekta ya fedha kwa karibu miongo miwili, na anasema muda wake kama mchambuzi wa uwekezaji ulimfundisha kuuona uandishi kama ufundi na pia biashara.

Ingawa kazi yake ya kifedha ilimwezesha kulipa gharama za maisha, uandishi uliendelea kuwa shauku yake. Aliandika The Polygamist nyakati za jioni baada ya kumaliza kazi.

Aliacha maisha ya kampuni akiwa na umri wa miaka 40 ili kuandika kwa muda wote, miaka michache baada ya kuchapisha riwaya hiyo. Sasa ana miaka 48.

"Watu husema, 'Oh, umefanikiwa ghafla, kwa usiku mmoja.' Sivyo kabisa," anasema. "Kutambuliwa kumetokea ghafla, lakini kazi imefanywa kwa miaka mingi, na nimejitoa mara nyingi."

Anaongeza kwamba waandishi wengi hawawezi kujikimu kutokana na vitabu vyao, hasa barani Afrika. Anasema mara nyingi waandishi waliofanikiwa huwezeshwa na waume wenye uwezo mkubwa wa kifedha, ruzuku au programu za ukazi wa waandishi.

Lakini fursa hizo hazikuwepo kwake, akiwa mama asiye katika ndoa aliyelazimika kumsomesha mwanawe, alifanya kazi mbalimbali huku akiendelea kuandika.

"Kuna kipindi kirefu kati ya unapoanza kitabu na unapokimaliza. Kinaweza kuchukua miaka miwili, au hata miaka minane. Unaishije? Kwa upande wa maisha halisi, bili bado zinahitaji kulipwa," anasema. "Nimepitia safari hiyo na haina uhakika… bila shaka utalazimika kuendelea na ile kazi yako ya kawaida."

"Uandishi ni anasa ambayo watu wengi hawawezi kumudu," anasema, akiongeza kwamba gharama yake inapimwa pia kwa sauti ambazo mara nyingi hazisikiki.

Pia anaona kuna ukosefu wa usawa katika namna uandishi wa Kiafrika unavyosambaa duniani. "Ni rahisi zaidi kwa mwandishi Mwafrika aliyechapishwa nje ya Afrika kupata umaarufu. Vitabu kwa kawaida huuzwa kutoka juu kuja kwetu. Ni vigumu kwa kazi zetu kupenya kutoka kwetu kwenda juu."

Kile ambacho "athari ya Netflix" imempa ni hasa mwonekano na umaarufu ambao hakuwahi kuupata licha ya kuandika riwaya nne na kutumia zaidi ya muongo mmoja katika uandishi, mara nyingi akishughulikia mada zenye mwelekeo wa kisiasa.

Kwa sasa Nyathi anamalizia rasimu ya kwanza ya riwaya ya kihistoria ambayo amekuwa akiifanyia kazi kwa miaka miwili iliyopita, anasema mada zake zitawagusa watu wengi.

Kuhusu ufundi wa uandishi, anasema, "kila kitu huanzia kwenye hadithi." Anamshauri mwanamke yeyote anayehisi kwamba ana kitabu ndani yake lakini hana pesa, aanze kwa kalamu na karatasi, na akiandike kwa sababu ya upendo wa uandishi.

"Pesa haipaswi kamwe kuwa motisha. Upendo wa uandishi ndio utakaokupa nguvu wakati mambo yatakapokuwa magumu."