Wanawake: Kutoka waathirika wakuu hadi vinara wa mapinduzi ya nishati safi Tanzania

Chanzo cha picha, REA/DIRA MAKINI
- Author, Yusuph Mazimu
- Akiripoti kutoka, BBC Dar es Salaam
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Kwa miongo na miongo, mwanamke wa Kitanzania amekuwa mhimili wa mfumo wa nishati ya kupikia majumbani. Kila siku, maelfu ya wanawake huamka mapema kabla ya jua kuchomoza, wakianza safari ya kutafuta kuni au kuandaa mkaa kwa ajili ya kupika chakula cha familia.
Katika maeneo mengi hasa ya vijijini, shughuli hii ya kusaka kuni ni safari ya saa nne hadi sita msituni. Muda huo, ambao ungeweza kutumika katika biashara, kilimo au elimu, hupotea kabisa kwenye kazi ya kuhakikisha familia inapata chakula.
Kwa muktadha huu, changamoto ya nishati ya kupikia si suala la chakula pekee, bali ni kikwazo cha moja kwa moja cha maendeleo ya kiuchumi ya wanawake na familia zao.
"Lazima tuwakomboe wanawake wa Tanzania kutoka kwenye moshi na kukata kuni ili apate muda wa kufanya mambo mengine ya maendeleo," anasema Dk Gertrude Mongella, mmoja wa wanawake wenye ushawishi ndani na nje ya Tanzania, aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali ikiwemo Spika wa Bunge la Afrika.
Takwimu za sekta ya nishati zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya kaya Tanzania bado hutegemea kuni na mkaa, huku wanawake wakiwa ndio wanaobeba mzigo mkubwa wa matumizi hayo ya kila siku.
Kwa upande wa afya, Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa karibu watu milioni 3.7 hufariki kila mwaka duniani kutokana na uchafuzi wa hewa wa majumbani, ambapo asilimia kubwa ni wanawake na watoto. Kwa Tanzania pekee, takwimu zinaashiria takriban vifo 33,000 kwa mwaka vinavyohusishwa na matumizi ya nishati zisizo safi.
Huu ndio ukweli unaoonesha ukubwa wa changamoto ambayo sasa Tanzania inaikabili kupitia mapinduzi ya nishati safi ya kupikia, mapinduzi ambayo mwanamke anaonekana kuwa na sehemu yake.
Mwanamke kiini cha mabadiliko

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika viunga vya Dar es Salaam, Siwatu Mugibu anakumbuka maisha yake ya zamani kwa hisia mchanganyiko, uchungu na mabadiliko.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Nikiwa kijijini kwetu, nilikuwa naamka asubuhi, naenda msituni kutafuta kuni. Kurudi ni jioni. Nilikuwa sina muda wa biashara wala hata kupumzika," anasema.
Leo, Siwatu ni miongoni mwa wanawake waliobadilisha maisha yao kupitia matumizi ya nishati safi ya kupikia, na sasa anahamasisha wanawake wengine kuingia kwenye biashara ya usambazaji wa majiko safi na utengenezaji wa mkaa mbadala.
"Kwangu nishati safi ni fursa. Nimeweza kujifunza kutengeneza mkaa mbadala na sasa naendesha shughuli inayonisaidia kusomesha watoto wangu vizuri kuliko zamani."
Utafiti wa UN Women Tanzania (2023) unaonesha kuwa wanawake wa vijijini walikuwa wakitumia saa 3 hadi 4 kila siku kukusanya kuni na kupika, lakini matumizi ya majiko yenye ufanisi yamepunguza muda huo hadi chini ya saa moja. Muda uliookolewa unatumika sasa katika shughuli za kiuchumi na kijamii.
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, anasema: "Tunahimiza nishati safi ya kupikia kwa sababu inalinda mazingira, inalinda afya zetu, na inamuwezesha mwanamke asikae jikoni kwa muda mrefu."
Anaongeza:
"Tusimuache mwanamke wa Kitanzania akaendelea kuteketea kwa kutumia nishati isiyo safi. Lengo letu ni kuhakikisha ifikapo 2030, zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia."
Wanawake Injini ya soko la nishati safi?

Chanzo cha picha, Mwananchi
Kadiri matumizi ya nishati safi yanavyoongezeka nchini Tanzania, wanawake wanazidi kuwa sehemu muhimu ya soko hili jipya la kiuchumi. Katika majiji ya Dar es Salaam, Dodoma na Arusha, wanawake sasa wanauza mitungi ya gesi na vifaa vya jikoni, ni mawakala wa usambazaji wa nishati safi, na wengine wameajiriwa katika kampuni za LPG na majiko banifu.
Lakini zaidi ya biashara za kawaida, kuna wanawake wabunifu wanaobadilisha sekta yenyewe. Hanny Mbaria wa Arusha, kupitia kampuni yake ya majiko banifu na mkaa mbadala unaotokana na mabaki ya miwa na mchele, ameajiri wanawake wengi katika uzalishaji.
Mmoja wa wafanyakazi wake, Martha Mwashinga, anasema: "Naendesha mashine. Mwanzoni tulizoea kuona ni kazi ya wanaume, lakini hapa karibu wote ni wanawake."
Rehema Mema, mchambuzi anasema hiyo inaonyesha mabadiliko ya msingi kwamba wanawake wanatoka kuwa watumiaji wa nishati na waathirika kwenda kuwa wazalishaji, wasambazaji wa nishati safi na waokoaji wa athari zitokanazo na matumizi ya kuni na mkaa.
Waziri wa zamani wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, aliwahi kusisitiza kuwa: "Wanawake ni msingi wa familia na jamii, hivyo mchango wao katika kusukuma ajenda ya nishati safi ya kupikia ni wa muhimu sana."
Juhudi zote hizi za kumtanguliza mwanamke ni kwa sababu nishati ya kupikia ina athari pana zaidi ya jikoni, inaingia kwenye elimu, usalama na mustakabali wa mtoto wa kike. Hata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amewahi kueleza:
"Wasichana wadogo wanaokwenda umbali mrefu kutafuta kuni, yanayowakuta huko, mengine hayaelezeki, wasichana wengine wanapata ujauzito wakiwa kwenye hizo safari za kutafuta kuni, ujauzito ule unamkatishia masomo yake, kwa maana hiyo kutafuta kuni kumemuharibia maisha yake yote, atafukuzwa shule, atapata mtoto mapema, na uwezo hana".
Mapinduzi ya nishati safi Tanzania

Chanzo cha picha, URT
Mapinduzi haya hayawezi kueleweka bila sera na uongozi wa taifa. Mema anasema Rais Samia kujitokeza mbele kama mwanamke na kuonyesha njia, kumeongeza msukuma mkubwa kuhusu nishati safi Tanzania.
Ingawa Tanzania imeanza kwa kasi ya hivi karibuni ukilinganisha na baadhi ya nchi jirani, sasa imeweka ajenda ya nishati safi ya kupikia kama kipaumbele cha kitaifa na anayeiweka mbele ni rais wa nchi.
Serikali imeweka lengo la kuhakikisha zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2030, ikianzisha mradi maalumu kusambaza nishati safi ya kupikia katika taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100.
Mradi huo ni sehemu ya mpango mkubwa wa kuunganisha miundombinu ya nishati safi ya kupikia katika taasisi 453 wenye thamani ya Shilingi bilioni 25.8, ambapo gharama zote zinagharamiwa kwa asilimia 100 na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Wakati huo huo, taasisi za kimataifa kama UNDP kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania na washirika wengine, zimeanzisha programu mbalimbali za kuwajengea uwezo wanawake katika sekta ya nishati safi. Takriban wanawake 45 sasa wamepitia mafunzo ya kuwa viongozi na wabunifu katika sekta hii chini ya UNDP.
Mwakilishi wa UNDP, Shigeki Komatsubara, anasema: "Nyinyi ni viongozi. Ni muhimu kubeba maono ya wengi na kufanya kazi kwa bidii ili wengine wajifunze kutoka kwenu."
Wachambuzi wa maendeleo wanaeleza kuwa ushiriki wa wanawake ambao ni asilimia 51% ya watanzania wote, katika kila ngazi ya mnyororo wa nishati safi kutoka sera, biashara hadi matumizi ya kaya ndio unaoharakisha mafanikio ya taifa kufikia malengo yake ya nishati safi lakini pia kuonyesha mabadiliko ya nafasi ya mwanamke katika uchumi na maendeleo ya taifa.
Na mwishowe, huenda historia itakumbuka kwamba mojawapo ya mafanikio makubwa ya Tanzania si tu kuanzisha ajenda ya nishati safi, bali jinsi wanawake walivyogeuka kutoka waathirika wakuu hadi vinara wa mapinduzi hayo.












