Nchi gani za kiarabu zina uhusiano wa karibu na Israel?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Wawakilishi kutoka Israel na Lebanon wamekutana tena mjini Washington nchini Marekani kwa duru nyingine ya mazungumzo.

Hii ni baada ya kukutana na Rais Trump wa Marekani mwezi Aprili.

Hata baada ya Marekani kusimamia usitishaji mapigano yaliyoafikiwa tarehe 16 mwezi Aprili, Israel na kundi la Hezbollah wamekuwa wakiendelea kupigana kusini mwa Lebanon.

Israel ilimuua kamanda wa Hezbollah tarehe 6 mwezi Mei, mjini Beirut.

Usitishaji mapigano ulikuwa udumu kwa siku 10 ila muda huo ukaongezwa hadi wiki tatu, na ilikuwa ikamilike tarehe 17 mwezi Mei.

Tulifikaje hapa?

Hii ni duru ya tatu ya mazungumzo yanayofanyika nchini Marekani.

Baada ya Rais Trump kutangaza usitishaji mapigano, alisema kuwa anapanga kukutana na Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Rais wa Lebanon Joseph Aoun mjini Washington.

Ila mkutano huo na viongozi hao, bado haujafanyika, kwani Aoun alisema lazima Israel isitishe mashambulizi kabla ya pande hizo mbili kukutana.

Mwezi Aprili tarehe 14, wawakilishi wa Lebanon na Israel walikutana kwa mara kwanza baada ya miaka 30 ya mvutano.

Balozi wa Israel nchini Marekani, Yechiel Leiter, na mwenzake wa Lebanon, Nada Hamadeh Moawad, walikutana mjini Washington katika mkutano uliosimamiwa na Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Marco Rubio.

Je, Kuhusu Hezbollah?

Kundi la Hezbollah liliundwa mwaka wa 1982, na inajumuisha waislamu wa Kishiite, kusini mwa Beirut.

Baadhi ya viongozi wa kundi hilo wapo katika serikali ya Lebanon, huku uhusiano kati ya serikali ya Lebanon na Hezbollah ukizidi kudorora.

Israel bado inaendelea kuishambulia kundi hilo na kulenga makazi ya watu kusini mwa Lebanon, huku Hezbollah ikijibu kwa kurusha makombora.

Usitishaji mapigano ulipoafikiwa mwezi Aprili, Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema, kuwapokonya Hezbollah silaha ndiyo jambo muhimu kwa sasa.

Hezbollah walikataa kusalimisha silaha zao, na kusema watajadili suala la silaha baada ya vita kuisha.

Iran kwa upande mwingine imetaka amani ya kudumu nchini Lebanon, kabla ya kutia saini mkataba wowote na Marekani.

Zaidi ya watu 2,896 wamefariki tangu vita kuanza, huku zaidi ya watu million 1.2 wakikimbia makazi yao.

Israel nayo imesema wanajeshi wake 18 na raia 4 wameuawa.

Mbona Israel na Lebanon hawana uhusiano wa kidiplomasia?

Israel na Lebanon zimekuwa katika hali ya vita tangu mwaka wa 1948 wakati Lebanon ilipojiunga na mataifa ya Kiarabu yaliyopinga kuundwa kwa taifa la Israel.

Hawana uhusiano wa kidiplomasia kwa sababu ya:

Kutokuwepo kwa mkataba wa amani: Tofauti na Misri na Jordan, Lebanon haijawahi kusaini mkataba wa amani na Israel.

Vita na uungaji mkono wa makundi yaliyojihami: Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Lebanon pamoja na uingiliaji wa Israel vilizorotesha zaidi uhusiano kati ya nchi hizo mbili. Israel ilidhibiti kusini mwa Lebanon kuanzia mwaka 1982 hadi 2000.

Nafasi ya Hezbollah: Tangu miaka ya 1980, Hezbollah imekuwa kundi lenye nguvu linaloweza kuikabili Israel kutoka Lebanon. Israel inaliona kundi hilo kama adui wake mkuu, huku Hezbollah ikikataa uwepo wa Israel nchini Lebanon.

Sheria na msimamo rasmi: Lebanon imeitangaza rasmi Israel kuwa adui, na Israel nayo imekuwa ikishambuliwa kusini mwa Lebanon karibu na mpaka wan chi hizo mbili.

Nchi gani za Kiarabu zina uhusiano na Israel na zipi hazina?

Kufikia mwezi Mei mwaka wa 2026, nchi sita za Kiarabu zina uhusiano wa kidiplomasia na Israel:

  • Misri (1979)
  • Jordan (1994)
  • Falme za Kiarabu (UAE) (2020)
  • Bahrain (2020)
  • Morocco (2020)
  • Sudan (2020)

Nchi hizi ambazo zilitia saini mkataba wa Abraham Accord hazikuondoka kwenye makubaliano hayo baada ya kuanza kwa vita vya Gaza mwezi Oktoba mwaka 2023, ingawa baadhi yao zilionyesha kuunga mkono Wapalestina.

Nchi za Kiarabu ambazo hazina uhusiano na Israel

Nchi nyingi za Kiarabu bado hazina uhusiano mzuri na Israel. Nazo ni:

  • Lebanon
  • Syria
  • Saudi Arabia
  • Kuwait
  • Iraq
  • Qatar
  • Algeria
  • Libya
  • Yemen

Oman (imekuwa katika mazungumzo na Israel, lakini hakuna uhusiano rasmi ulioafikiwa)

Nchi nyingi za Kiarabu zimetaja kuunga mkono Palestina na kupinga uvamizi wa Israel huko Gaza kama sababu za kutokuwa na uhusiano wa kidiplomasia na Israel.

Saudi Arabia ilianza juhudi zake za kufikia makubaliano na Israel muda mfupi kabla ya vita vya Gaza kuanza, huku ikisema itaendelea na juhudi hizo, baada ya kuafikiwa kwa makubaliano ya kuitambua rasmi eneo la Palestina kama taifa.