Je, shampoo hurekebisha nywele? Wataalamu waeleza hila 4 muhimu

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Sote tuna ndoto ya kuwa na nywele zenye afya na mvuto, iwe ziwe za mawimbi na zinazong'aa, zilizopinda au zilizonyooka.

Katika tasnia inayozalisha mamilioni ya dola ulimwenguni kote, bidhaa nyingi za TikTok, mitindo na vidokezo hutufanya tusahau kwa urahisi kile ambacho ni muhimu katika utunzaji wa nywele.

Kwa kweli, kuwa na nywele zenye afya hakutaki kutumia pesa nyingi au kufuata taratibu ngumu; cha muhimu ni kufanya mambo kwa urahisi na uangalifu.

Wataalamu wa trichology, Eva Proudman wa UK Hair Consultants na Tracey Walker wa Hair and Scalp Clinic, wanafafanua mambo manne yalioeleweka vibaya yanayohusu utunzaji wa nywele.

1. Maji baridi hayafanyi nywele zako kung'aa

Je, umewahi kutetemeka ukioga maji yenye barafu ili tu kupata nywele zinazong'aa?

Kwa bahati nzuri, unaweza kuacha kufanya hivyo na ufurahie kuoga kwa kutumia maji moto, kwa sababu Proudman anasema maji baridi hayaongezei nywele mwanga wa ziada.

"Hakuna haja ya kuosha nywele kwa maji baridi, haina maana," anasema. "Kile kilicho muhimu ni kulinda nywele kutokana na kemikali, joto na mazingira."

Aidha, si vyema kutumia maji moto sana kwani yanaunda hatari ya kuziparua nywele na kuchoma ngozi ya kichwa, kama vile maji moto yanavyoweza kuchoma ngozi.

2. Hakuna bidhaa inayoweza kurekebisha nywele zilizoharibika

Ikiwa unatarajia kurekebisha ncha zilizogawanyika bila kwenda saluni, utagundua kuwa suluhisho la pekee ni kukata nywele.

Proudman anaeleza: "Ncha zilizogawanyika ni kama shimo kwenye soksi iliyofumwa; haiwezi kurekebishwa."

Walker anafafanua: "Ukizichunguza nywele zilizokatika kwa kipimo cha hadubini, inaonekana kama zina pointi mbili au tatu za ziada."

Bidhaa sokoni hufanya kazi kama gundi linaloshikilia nywele kwa muonekano bora, lakini hizi ni suluhisho za muda tu.

Walker anaonya dhidi ya matumizi ya kupita kiasi kwenye bidhaa zinazoahidi suluhu.

Proudman pia anakemea madai kwamba kukata nywele kunaweza kuharakisha ukuaji wake:

"Haiwezekani kuharakisha ukuaji wa nywele; bidhaa yoyote inayodai hivyo ni uwongo."

3. Nywele zako hazijisafishi zenyewe

Huenda tayari umekutana na mtu ambaye anaapa kwamba anaacha nywele zao zijioshe, mara chache, ikiwa wameziosha.

Lakini, Proudman anasema hii si njia nzuri ya utunzaji nywele.

"Kichwa cha nywele kina tezi za mafuta 180,000 zinazokusanya uchafu ikiwa hazioshwi mara kwa mara."

Walker anakubaliana na nywele hazijisafishi, akilinganisha na vigumu kuondoa doa la mafuta kwenye nguo kwa maji tu; sabuni ya nguo pia inahitajika.

Kutoosha nywele mara kwa mara kunaweza kusababisha harufu mbaya na kuharakisha matatizo ya ngozi ya kichwa kama kuvimba au kupeleka.

Proudman anashauri kuosha nywele kila siku mbadala kwa wale wenye nywele zenye mafuta au wanaotumia bidhaa nyingi.

Laura Waters, profesa wa uchambuzi wa dawa katika Chuo Kikuu cha Huddersfield, Uingereza, anaeleza kuwa wale wenye nywele kavu wanaweza kutumia shampoo isiyo na haluli ya chumvi yaani salfeti ili kulinda mafuta asilia ya nywele.

4. Shampoo kavu sio mbadala ya kuosha.

Kupata wakati wa kuosha, kukausha na kuweka nywele zako mtindo sio rahisi.

Kwa hiyo, kati ya kazi, michezo, na kwenda nje, wengi wetu hugeuka kwenye shampoo kavu ili kuondoa mafuta na kufufua nywele zetu bila kuoga.

Proudman anadai kwamba shampoo kavu ni "kamilifu", lakini inapaswa kutumika mara moja tu kati ya kuosha.

Tatizo hutokea wakati unatumia shampoo kavu kwa siku kadhaa mfululizo bila kusuuza.

Kuzidi kutumia shampoo kavu kwa siku nyingi bila kuosha nywele kunachangia mkusanyiko wa mafuta na kuharibu ngozi ya kichwa, huku kuendesha uvimbe na kupeleka.

"Usipokuwa mwangalifu, una hatari ya kupata mwasho na ngozi kubambuka"

Proudman anashauri: "Tunza ngozi ya kichwa kwa njia ile ile unavyotunza uso wako: huwezi kujipaka vipodozi bila kwanza kuondoa vipodozi vyako na kuosha ngozi yako."

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid