Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Makubaliano ya awali ya kukomesha vita na Marekani ni Israel iondoke Lebanon - Iran

Mkataba huo, ambao ni kati ya Marekani na Iran, haujawekwa wazi, na wakati mwingine maafisa wametoa tafsiri zinazokinzana za kile kilichomo ndani yake.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Waathiriwa wa Ebola Afrika wanapendelea waganga wa kienyeji kuliko hospitali

    Kila mara kunapokuwa na mlipuko wa Ebola, baadhi ya walioathiriwa huchagua njia ya kwenda hospitali iliyo karibu. Wengine hufuata njia ya kuelekea kwenye madhabahu ya mganga wa kienyeji, na thari zake huwa mbaya zaidi.

    Wengi wanaona mwanzo wa homa ya kutokwa na damu kama ugonjwa wa kiroho na hutafuta dawa za mitishamba na maombi badala ya kwenda hospitalini.

    Hivi ndivyo ilivyo sasa nchini Kongo, ambayo inakabiliwa na mlipuko wake wa kumi na saba wa Ebola tangu 1976, wakati virusi hivyo kugunduliwa kwa mara ya kwanza katika mfumo ikolojia tajiri wa Bonde la Congo.

    Miongo mitano baadaye, virusi hivyo vinaendelea kuwachanganya wagonjwa wengi barani Afrika ambapo wengine wanageukia viongozi wa kidini kuwa wahudumu.

    Waathiriwa wa mlipuko wa sasa ni pamoja na wafanyakazi wa afya bila vifaa vya kujikinga pamoja na wachungaji na waumini waliokusanyika wakati Ebola ikienea, kulingana na wafanyakazi wa kibinadamu na wengine waliozungumza na The Associated Press.

    Ebola huenea kupitia kugusana kwa karibu na majimaji ya mwili ya wagonjwa au waliofariki.

    Mlipuko wa sasa unatia wasiwasi hasa katika eneo ambalo wengi hawaamini wafanyakazi wa afya na wanakataa kutafuta huduma ya matibabu.

    Soma zaidi:

  2. Upinzani Congo walaani muswada mpya unatoa fursa kwa Tshisekedi kugombea muhula wa tatu

    Upinzani wa Congo siku ya Jumanne umelaani kupitishwa kwa muswada ambao unaweza kutoa fursa kwa Rais Félix Tshisekedi kugombea muhula wa tatu, ukishutumu kile wanachosema ni unyakuzi wa madaraka.

    Muswada huo, uliopitishwa na Seneti Jumatatu, utawezesha kura ya maoni kuhusu katiba mpya ambayo mihula ya awali ya Tshisekedi haitahesabiwa. Tayari umepitishwa na Bunge la Kitaifa na sasa unasubiri saini ya rais.

    Tshisekedi, mwenye umri wa miaka 62, amekuwa madarakani tangu mwak 2019. Amesema kwamba atagombea muhula wa tatu, ikiwa wapiga kura wataukubali kupitia kura ya maoni. Lakini hakuna tarehe iliyowekwa.

    Katiba ya Congo inakataza waziwazi marekebisho yoyote ya mipaka ya mihula ya urais. Muswada huo unaruhusu rais kurekebisha katiba iwapo kutatokea "hitilafu kubwa" inayoathiri taasisi za serikali.

    Soma zaidi:

  3. Taiwan yaishutumu Kenya kwa kuzuia wajumbe wake

    Serikali ya Taiwan siku ya Jumanne imesema kuwa inajiondoa katika Kongamano la masuala ya Bahari Yetu (OAC) linalofanyika huko Mombasa baada ya wajumbe wawili kuzuiwa kuingia na kukamatwa na mamlaka ya uhamiaji ya Kenya kutokana na shinikizo la China.

    Kulingana na Wizara ya Mambo ya Nje (MOFA) na Baraza la Masuala ya Bahari waandaaji wa tukio la kabla ya mkutano walikataa kutoa idhini kwa wajumbe kwa sababu hawakutambua pasipoti ya Taiwan.

    Baadaye, wajumbe wawili walikamatwa kwa nguvu na mamlaka ya uhamiaji ya Kenya kwa saa 20, ambapo pasipoti na simu zao za mkononi zilichukuliwa, na kurejeshewa kwao baada ya mamlaka kuwaruhusu kupanda ndege karibu siku moja baadaye.

    Kwa mujibu wa gazeti la Taipei Times, mamlaka za Kenya zilikataa kutambua pasi zao za kusafiria za Jamhuri ya China (Taiwan) na kwamba juhudi za serikali ya Taiwan kushughulikia suala hilo hazikufaulu.

    Soma zaidi:

  4. Makubaliano ya awali ya kukomesha vita na Marekani ni Israel iondoke Lebanon - Iran

    Mwanadiplomasia mkuu wa Iran amesema siku ya Jumanne kwamba makubaliano ya awali ya kukomesha vita na Marekani yanailazimisha Israeli kujiondoa kutoka Lebanon — sharti ambalo Israeli tayari imekataa na ambalo linaweza kusambaratisha makubaliano hayo, na kusababisha kuanza tena kwa vita vya jumla.

    Mkataba huo, ambao ni kati ya Marekani na Iran, haujawekwa wazi, na wakati mwingine maafisa wametoa tafsiri zinazokinzana za kile kilichomo ndani yake.

    Ingawa Israeli si mshiriki wa makubaliano hayo, ni sehemu ya vita baada ya kujiunga na Marekani katika kushambulia Iran mnamo Februari 28.

    Israeli pia imepigana na kundi la wanamgambo wa Hezbollah linaloungwa mkono na Iran nchini Lebanon na kuteka maeneo makubwa ya nchi hiyo.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi alisema kuendelea kwa Israel kukalia eneo la kusini mwa Lebanon kunakiuka makubaliano hayo.

    "Bila ya kuondolewa kwa vikosi vya Israeli kutoka maeneo waliyoyachukua wakati wa vita hivi, vita havijafikia mwisho kamilifu," Araghchi alisema.

    Soma zaidi:

  5. Mgogoro wa Gaza waangaziwa kwenye Mkutano wa G7

    Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi, amehutubia mkutano wa kilele wa G7 na kuitaka Israel kuachana na mpango wake wa kudhibiti asilimia 70 ya Ukanda wa Gaza. Rais Sisi amesisitiza kuwa:

    • Hatua hiyo inakiuka makubaliano tete ya Oktoba.
    • Jeshi la Israel (IDF) linapaswa kuacha mara moja kusonga mbele zaidi ya 'mstari wa njano' uliokubaliwa.
    • Suluhisho la mataifa mawili ndilo pekee litakalohakikisha amani ya kudumu.

    Tangu kusainiwa kwa makubaliano ya usitishaji mapigano yaliyosimamiwa na Marekani, zaidi ya Wapalestina 900 wameuawa.

    Israel inatetea hatua zake kwa kuishutumu Hamas kwa kukataa kuweka chini silaha.

    Wakati huo huo, shinikizo la kisiasa la ndani nchini Israel linaonekana kuchochea moto wa mzozo, ambapo Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amewahi kuashiria kuungwa mkono na baadhi ya makundi ya walowezi wanaotaka udhibiti wa asilimia 100 ya Gaza.

    Hali hii inaashiria kupanuka kwa ufa wa kidiplomasia kati ya Israel na washirika wake wa karibu, huku mustakabali wa amani katika ukanda huu ukizidi kuwa na utata.

    Soma zaidi:

  6. Haaland mchezaji bora wa mechi huku Norway ikiishinda Iraq

    Erling Haaland ameongoza viwango vya wachezaji katika mchezo wa ufunguzi wa Kombe la Dunia wa Norway dhidi ya Iraq.

    Mshambuliaji huyo wa Manchester City alifunga mabao mawili katika mechi yake ya kwanza ya mashindano huku Norway ikishinda 4-1 na kupata pointi 7.9 kati ya 10.

    Aymen Hussein wa Iraq - ambaye alifikisha matokeo ya 1-1 kwa kufunga bao la pili pekee la nchi yake katika Kombe la Dunia - alikuwa wa pili, akiwa na pointi 7.78.

    Haaland aligusa mpira mara chache katika kipindi cha kwanza kuliko mchezaji mwingine yeyote, 11 pekee, lakini ushawishi wake ulikuwa mkubwa zaidi alipoteleza na kupiga krosi ya David Moller Wolfe kutoka kushoto muda mfupi kabla ya nusu saa - bao la kwanza la Norway katika fainali za Kombe la Dunia. La mwisho, lilipatikana mnamo mwaka 1998, lilifungwa siku 759 kabla Haaland hajazaliwa.

    Akizungumza kwenye BBC One, mchambuzi mwenza wa michezo Stephen Warnock alisema: "Jambo moja unalojua ni kwamba jamaa huyo Haaland atapata anachokitaka, atafanya kila awezalo kufikia lengo lake."

    Soma zaidi:

  7. Mtoto mwenye Ebola atekwa nyara kutoka kituo cha matibabu DR Congo

    Mamlaka za afya nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo zimo katika hali ya taharuki baada ya msichana wa miaka sita aliyekuwa akipatiwa matibabu ya Ebola, kutekwa nyara kutoka kituo cha afya mashariki mwa nchi hiyo.

    Watu wenye silaha walivamia kliniki moja karibu na mji wa Butembo, jimbo la Kivu Kaskazini, na kumchukua mtoto huyo pamoja na mama yake, hatua ambayo wataalamu wa afya wameitaja kuwa ni tishio kubwa kwa usalama wa jamii.

    Wataalamu wameonya kuwa mtoto huyo na mama yake wanaweza kueneza virusi hivyo kwa kasi kubwa ikiwa wataendelea kubaki nje ya uangalizi wa kitabibu.

    Dkt. Lubambo Maboko Gaston, meneja wa kukabiliana na mlipuko wa Ebola katika jimbo hilo, ametoa wito wa dharura kwa watekaji na familia hiyo.

    "Hadi sasa bado hatujawapata watu hao wawili. Tunatoa wito rasmi kwao kwenda haraka iwezekanavyo katika kituo cha matibabu ya Ebola," Dkt. Gaston aliliambia shirika la habari la Reuters.

    Tukio hili linatokea wakati nchi hiyo ikikabiliana na mlipuko wa kirusi cha aina ya Bundibugyo. Kwa mujibu wa data za Wizara ya Afya kufikia Juni 15:

    • Jumla ya maambukizi: 837
    • Idadi ya vifo: 196 (Kiwango cha vifo ni 23.4%)
    • Waliopona: 49
    • Wanaofuatiliwa: 376

    Jimbo la Ituri linaendelea kuwa kitovu cha maambukizi hayo, likifuatiwa na Kivu Kaskazini.

    Wakati huo huo, timu za kukabiliana na janga hilo kutoka Shirikisho la Kimataifa la Msalaba Mwekundu zinasema changamoto kubwa inayozikabili ni ugumu wa kufuatilia watu waliokaribiana na wagonjwa.

    Serikali ya DR Congo bado haijatoa tamko rasmi kuhusiana na tukio hili la utekaji nyara hadi kufikia wakati wa kuchapishwa kwa taarifa hii.

    Pia unaweza kusoma:

  8. Mbappe aweka rekodi ya mfungaji bora Ufaransa

    Ufaransa imekuwa na idadi kubwa ya wachezaji mahiri wa kushambulia kwa miaka mingi lakini hakuna bora zaidi katika ufungaji magoli kuliko Kylian Mbappe baada ya kufunga mabao yake katika mchezo wa ufunguzi wa Kombe la Dunia dhidi ya Senegal.

    Mshambuliaji huyo wa Real Madrid amekuwa mfungaji bora wa muda wote wa Ufaransa, akimpita Giroud katika rekodi ya mabao aliyofungia Les Bleus ikiwa ni bao lake la 58 akiwa na umri wa miaka 27 tu.

    "Hongera Kylian," Giroud alisema kwenye BBC One, akiwa kama mchambuzi wa mchezo wa Ufaransa dhidi ya Senegal. "Ninamfurahia."

    "Inaeleweka, ilitarajiwa. Atavunja rekodi zote - idadi ya mechi na mabao. Nadhani anaweza kufikia mabao 100 kwa urahisi na labda [kuvunja] rekodi ya Miroslav Klose ya Kombe la Dunia. Amekuwa na matokeo mazuri katika Kombe la Dunia na michezo mikubwa."

    Mabao ya Jumanne yalimfanya afikishe mabao 14 katika Kombe la Dunia - mawili tu nyuma ya Klose wa Ujerumani, ambaye anashikilia rekodi hiyo akiwa na mabao 16 ambayo nayo pia sasa imefikiwa na Lionel Messi.

    "Anajua anakotaka kwenda, ni kiongozi na hilo lilionekana tangu akiwa mdogo. Ni mchezaji mwenye kipaji cha ajabu na nadhani ni kiongozi mzuri ndani na nje ya uwanja."

    Soma zaidi:

  9. Kombe la dunia 2026: Messi afunga magoli matatu yake ya kwanza huku wakiipa Algeria kichapo

    Lionel Messi amekuwa mfungaji bora wa muda wote wa Kombe la Dunia kwa kufunga mabao 3 huku mabingwa watetezi Argentina wakianza kwa kupata ushindi dhidi ya Algeria.

    Messi akicheza mechi yake ya 200 kwa nchi yake alitengeneza historia, kwani mshindi huyo mara nane wa Ballon d'Or alifikisha jumla ya mabao yake ya fainali za Kombe la Dunia hadi 16 - na kumfanya awe sawa na Miroslav Klose wa Ujerumani kama mfungaji bora wa wakati wote katika historia ya mashindao hayo.

    Mabingwa hao mara tatu wa dunia walilazimishwa kutafuta ushindi kwa bidii ili wawe kifua mbele katika Uwanja wa Kansas City huku wakilenga kuwa taifa la tatu pekee kutetea Kombe la Dunia kwa mafanikio.

    Ilikuwa mara ya kwanza kwa Argentina kushinda mechi yao ya ufunguzi kwenye Kombe la Dunia kama mabingwa watetezi, baada ya kushindwa mwaka 1982 na 1990.

    Hilo lilitokana na weledi wa Messi, ambaye alifunga bao la ufunguzi la kuvutia dakika ya 17.

    Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 38 alipokea mpira kutoka kwa mchezaji mwenzake wa Inter Miami, Rodrigo De Paul, kabla ya kumchenga Luca Zidane - mtoto wa gwiji wa Ufaransa, Zinedine Zidane - katika mechi yake ya 27 ya Kombe la Dunia.

    Bao lake lilifungwa dakika 12 baada ya juhudi za awali kukataliwa wakati wa mwanzo mgumu, huku Algeria pia ikipata shuti lililokataliwa dakika tatu baadaye huku mchezo ukianza kwa kasi tangu mwanzo.

    Lakini usiku ambao alikuwa mchezaji wa kwanza kucheza Kombe la Dunia kwa mara ya sita, Messi alikuwa na bahati ya kuepuka adhabu kwa kumchezea vibaya Aissa Mandi wa Algeria katikati ya kipindi cha kwanza.

    Bao la pili la Argentina lilifungwa kwa karibu sana katika dakika ya mwisho wakati Messi alipomrukia Zidane kimakosa, kabla ya kufunga mabao matatu ya kwanza ya Kombe la Dunia katika dakika ya 76 kwa shuti kali kutoka ukingoni mwa eneo la hatari baada ya kuchukua mpira kutoka kwa Nicolas Gonzalez.

    Baada ya kuanza kwa ushindi katika Kundi J, Argentina itakabiliana na Austria na Jordan.

    Soma zaidi:

  10. Iran na Marekani zaonya Israel dhidi ya kushambulia Lebanon

    Iran imeitaka Israel kusitisha mara moja mashambulizi yake kusini mwa Lebanon, ikitishia kutoa "kujibu vikali" iwapo uvunjifu wa makubaliano ya kusitisha mapigano utaendelea.

    Makao makuu ya jeshi mjini Tehran yamesema Israel imekiuka makubaliano hayo mara 84 katika kipindi cha siku mbili zilizopita.

    Kwa upande mwingine, Rais wa Marekani Donald Trump ametoa kauli nzito akikosoa mbinu za kivita za Israel dhidi ya Hezbollah.

    Rais Trump ameeleza kutoridhishwa na kitendo cha Israel kubomoa majengo ya ghorofa kwa ajili ya kutafuta mtu mmoja, akisisitiza kuwa raia wengi wanaopoteza maisha si wapiganaji wa Hezbollah.

    "Ikiwa Israel haiwezi kufanya operesheni yake bila kuua kila mtu, basi Syria itafanya kazi hiyo," Trump alisema.

    Katika pendekezo la kushangaza, Rais Trump amedokeza kuwa ni bora kuiachia Syria jukumu la kushughulikia kundi la Hezbollah, akiamini kuwa inaweza kufanya kazi hiyo kwa ufanisi zaidi bila kusababisha vifo vingi vya raia.

    Shinikizo la kimataifa dhidi ya operesheni za kijeshi za Israel limefikia kilele huku kukiwa na mgogoro wa kidiplomasia kuhusu hatua za kijeshi nchini Lebanon na Gaza.

    Soma zaidi:

  11. Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara. Tarehe ni 17/06/2026.