Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Urusi na Ukraine zaanza duru ya pili ya mazungumzo ya kumaliza vita

Wapatanishi wa Ukraine na Urusi wameanza duru ya pili ya mazungumzo yanayosimamiwa na Marekani siku ya Jumatano huko Abu Dhabi, wakiendeleza juhudi za kumaliza mzozo mkubwa zaidi barani Ulaya tangu Vita vya Pili vya Dunia.

Muhtasari

Moja kwa moja

Asha Juma, Beldeen Waliaula & Rashid Abdallah

  1. Kwaheri hadi kesho

  2. Idadi ya vifo katika shambulio huko Nigeria yaongezeka hadi 170

    Takribani watu 170 wameuawa katika shambulio lililofanywa na watu wenye silaha katika kijiji kimoja katika jimbo la Kwara katikati mwa Nigeria, mbunge mmoja wa eneo hilo ameiambia Reuters siku ya Jumatano.

    Wanajeshi wanaendelea kutafuta manusura katika maeneo ya vichaka yaliyo karibu katika jiji kilicho katika wilaya inayopakana na jimbo la Niger.

    Wanakijiji walikimbilia kwenye vichaka huku watu wenye silaha wakishambulia Kijiji cha Woro, mbunge Saidu Baba Ahmed ameiambia Reuters kwa simu.

    Ahmed alisema watu hao wenye silaha waliwakamata wakazi, wakawafunga mikono yao nyuma ya migongo yao na kuwaua. Mbunge huyo ameitumia Reuters picha za miili ya watu waliokufa, ambazo shirika hilo bado halijaweza kuzithibitisha.

    Washambuliaji hao pia walichoma nyumba na maduka wakati wa uvamizi siku ya Jumanne.

    "Ninapozungumza nanyi sasa, niko kijijini pamoja na wanajeshi, tukipanga maiti na kutafuta maeneo ya jirani," Ahmed alisema.

    Watu kadhaa bado wamepotea.

    Wakazi waliiambia Reuters kwamba watu hao wenye silaha, wanaodhaniwa kuwa wapiganaji wa jihadi ambao mara nyingi huhubiri katika kijiji hicho, waliwataka wenyeji kuacha utii wao kwa serikali ya Nigeria na kugeukia sheria za Kiislamu. Wanakijiji walipokataa, wanamgambo hao walifyatua risasi wakati wa mahubiri ya Jumanne.

    Msemaji wa polisi wa Kwara, Adetoun Ejire-Adeyem, amesema polisi na jeshi wamepelekwa katika eneo hilo kwa ajili ya operesheni ya utafutaji na uokoaji, lakini amekataa kutoa maelezo juu ya majeruhi.

  3. Mtuhumiwa wa usafirishaji dawa za kulevya raia wa Tanzania akamatwa Zambia

    Mfanyabiashara haramu wa dawa za kulevya kutoka Tanzania amekamatwa nchini Zambia wakati wa uvamizi, imetangaza Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya ya Zambia (DEC).

    Ahmed Muharram alikuwa miongoni mwa washukiwa kadhaa waliokamatwa katika mji mkuu wa Zambia, Lusaka, pamoja na kiasi kikubwa cha bangi na dawa ya kikohozi yenye kemikali ya codeine siku ya Jumanne, mamlaka hiyo imesema.

    "Mshukiwa anajulikana kama mlanguzi wa dawa za kulevya wa kimataifa," imesema DEC, na kuongeza kuwa mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 40 yupo kwenye orodha ya tume ya kupambana na dawa za kulevya kwa muda mrefu.

    Kukamatwa kwa Muharram, ambaye bado hajasema chochote, kulikuja baada ya mfululizo wa operesheni zilizoongozwa kijasusi, imesema tume hiyo.

    Chini ya sheria za Zambia, bangi imeorodheshwa kama dawa hatari na ni kinyume cha sheria kuimiliki.

    Usafirishaji, umiliki na matumizi ya dawa za kulevya haramu kama vile bangi unaadhibiwa kwa faini au kifungo jela.

    Nchi hiyo ya kusini mwa Afrika inapambana na matumizi mabaya ya dawa za kulevya na biashara haramu, hasa bangi na heroini.

    Wakati wa operesheni za Jumanne, DEC imesema, imekamata kilo 221.2 za bangi zilizofichwa kwenye lori katika eneo la Lilayi jijini Lusaka.

    Utafutaji huo uliendelea hadi kwenye makazi ya Muharram huko Lilayi, ambapo maafisa waligundua kilo 1,159.6 za ziada za bangi, na kufanya jumla kufikia kilo 1,380.8.

    Raia wa Zambia ambaye pia amekamatwa akiaminika kuwa mshiriki katika biashara hiyo haramu ya dawa za kulevya.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Muda wa makubaliano ya nyuklia kati ya Urusi na Marekani utafikia mwisho leo

    Mkataba wa mwisho wa nyuklia kati ya Urusi na Marekani unatarajiwa kuisha ndani ya saa chache zijazo, na kuongeza hatari ya mashindano mapya ya silaha hiyo ambapo China pia itakuwa na jukumu muhimu.

    Mkataba wa udhibiti wa nyuklia ulilenga kupunguza uwezekano wa vita vya vibaya ya nyuklia.

    Bila ya Washington na Moscow kufikia makubaliano, mataifa haya mawili makubwa zaidi ya nyuklia duniani yatakuwa huru bila mipaka kwa mara ya kwanza katika zaidi ya nusu karne wakati mkataba wa New START utakapoisha.

    Mkataba huo utakao malizika leo Jumatano usiku ulisainiwa mwaka 2010.

    Matt Korda, mkurugenzi msaidizi wa Mradi wa Taarifa za Nyuklia katika Shirikisho la Wanasayansi wa Marekani, amesema ikiwa hakutakuwa na makubaliano ya kuongeza muda, Urusi na Marekani hazitakuwa na kizuizi ikiwa zitataka kuongeza vichwa zaidi vya vyuklia.

    Rais wa Marekani Donald Trump alisema mwezi uliopita ikiwa mkataba huo utaisha, atafanya makubaliano bora zaidi.

    Vichwa vya nyuklia vimepungua na kufikia vichwa 12,000 mwaka wa 2025 kutoka vichwa 70,000 mwaka wa 1986, lakini Marekani na Urusi zinaboresha silaha zao na China imeongeza zaidi ya mara mbili ya silaha zake katika muongo mmoja uliopita.

    Mwaka jana, Trump alisema anataka China iwe sehemu ya mkataba mpya wa udhibiti wa silaha hizo na akahoji kwa nini Marekani na Urusi zizalishe silaha mpya za nyuklia ikizingatiwa kwamba zina silaha za kutosha kuangamiza dunia.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Urusi na Ukraine zaanza duru ya pili ya mazungumzo ya kumaliza vita

    Wapatanishi wa Ukraine na Urusi wameanza duru ya pili ya mazungumzo yanayosimamiwa na Marekani siku ya Jumatano huko Abu Dhabi, wakiendeleza juhudi za kumaliza mzozo mkubwa zaidi barani Ulaya tangu Vita vya Pili vya Dunia.

    Ni mazungumzo ya ya siku mbili.

    "Mchakato wa mazungumzo ulianza katika muundo wa pande tatu — Ukraine, Marekani, na Urusi," amesema afisa wa mkuu wa Ukraine, Rustem Umerov kwenye Telegram.

    Utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump umezisukuma Kyiv na Moscow kutafuta mwafaka wa kumaliza mgogoro wa miaka minne, uliosababishwa na uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine mwaka 2022.

    Masuala nyeti zaidi ni madai ya Moscow ya kuitaka Kyiv iachilie ardhi ambayo bado inaidhibiti na hatima ya kiwanda cha nyuklia cha Zaporizhzhia, kikubwa zaidi barani Ulaya, ambacho kiko katika eneo linalokaliwa na Urusi.

    Moscow inataka Kyiv iwaondoe wanajeshi wake kutoka eneo lote la mashariki mwa Donetsk, ikiwa ni pamoja na ukanda wa miji yenye ngome nyingi – ambazo ni ngomo imara kwa Ukraine, kama sharti la makubaliano yoyote.

    Ukraine imesema mzozo huo unapaswa kusita katika mstari wa mbele wa sasa na imekataa yeye pekee kuondoa vikosi vyake.

    Urusi kwa sasa inashikilia takriban 20% ya eneo la Ukraine, ikiwa ni pamoja na Crimea na sehemu za eneo la mashariki mwa Donbas zilizotekwa kabla ya uvamizi wa 2022.

    Wachambuzi wa kijeshi wamesema vikosi vya Urusi vimeongeza takriban 1.5% ya eneo la Ukraine tangu mwanzo wa 2024.

    Kura za maoni zinaonyesha Waukraine wengi wanapinga makubaliano yanayoipa Moscow ardhi.

    Duru ya kwanza ya mazungumzo ilifanyika UAE mwezi uliopita, ikafungua mazungumzo ya kwanza ya moja kwa moja ya umma kati ya Moscow na Kyiv.

  6. Watu wasiopungua 35 wameuawa Nigeria baada ya majambazi kuvamia kijiji

    Majambazi wamewaua watu wasiopungua 35 walipokuwa wakivamia kijiji katika jimbo la Kwara katikati mwa Nigeria, na kuchoma moto majengo na maduka Jumanne jioni, amesema mbunge mmoja wa jimbo hilo.

    Ni shambulio baya zaidi mwaka huu katika wilaya inayopakana na jimbo la Niger, eneo ambalo linazidi kulengwa na magenge yenye silaha

    Wanakijiji walikimbilia kwenye vichaka huku watu wenye silaha wakishambulia Kijiji cha Woro, Saidu Baba Ahmed ameiambia Reuters kwa simu.

    Amesema watu kadhaa bado wamepotea hadi kufikia Jumatano asubuhi.

    Ujambazi na mashambulizi ya kutumia silaha dhidi ya jamii za vijijini yameongezeka kaskazini magharibi na kaskazini-kati mwa Nigeria katika miaka ya hivi karibuni huku magenge yakivamia vijiji, kuwateka nyara wakazi na kupora mifugo.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Kocha wa Man City aapa kuwa ataendelea kuzungumzia migogoro ya kimataifa

    Pep Guardiola amesema anataka kutumia nafasi yake "kuzungumza na ulimwengu" alipozungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu "maumivu" anayohisi kwa waathiriwa wa migogoro ya kimataifa.

    Meneja huyo wa Manchester City ameyasema hayo siku moja baada ya kuzungumza kuhusu watoto wa Kipalestina katika tamasha la hisani katika mji wa Barcelona.

    Akizungumza kabla ya mchezo wa pili wa nusu fainali ya Kombe la Carabao dhidi ya Newcastle Jumatano, Guardiola alizungumza kuhusu watoto kuuawa na kujeruhiwa katika maeneo ya migogoro kote ulimwenguni, akisema video anazoziona "zinamuumiza."

    Amegusia migogoro huko Palestina, Ukraine, Sudan na hata mauaji ya hivi karibuni yaliyofanywa na afisa wa Uhamiaji na Forodha (ICE) nchini Marekani.

    Guardiola: "Inaniuma. Nitazungumza siku zote. Kuua maelfu ya watu wasio na hatia? Inaniuma."

    "Unapoona picha kila siku, baba, mama, watoto, yanayowatokea, maisha yao yakiharibiwa na watu hawawezi kuguswa hata kidogo? Samahani, siwezi kuacha kuguswa."

    Alipoulizwa kwa nini mambo haya yana umuhimu mkubwa kwake, Guardiola alijibu: "Nashukuru kwa sababu ni mara ya kwanza katika miaka 10 kwa mwandishi wa habari mmoja kuniuliza kuhusu hilo."

    "Inaonekana ninyi [vyombo vya habari] hamruhusiwi kuzungumza kwa sababu ya kazi yenu."

    Mhispania huyo amesema: "Hatujawahi katika historia ya binadamu, kuwa na taarifa mbele ya macho yetu tukizitazama kwa uwazi zaidi kuliko sasa - mauaji ya halaiki huko Palestina, yaliyotokea Ukraine, yaliyotokea kote ulimwenguni - huko Sudan, kila mahali."

    Israel inashutumiwa kwa kufanya mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina katika ripoti ya Umoja wa Mataifa mwaka jana, ingawa Israel inakataa vikali dai hilo. Hivi majuzi iliripotiwa kwamba maafisa wa Israel wamekubali kwamba kuna watu 70,000 waliouawa Gaza.

    Mwezi uliopita, raia wawili wa Marekani walipigwa risasi na kuuawa na maafisa wa serikali waliokuwa wakitekeleza msako mkali dhidi ya wahamiaji huko Minneapolis.

    Guardiola amesema: "Kwa mtazamo wangu, haki lazima izungumzwe. Tazama kilichotokea Marekani, Renee Good na Alex Pretti wameuawa. Niambie unawezaje kutetea hilo?

    "Hakuna jamii kamilifu, hakuna mahali palipo kamili, mimi si mkamilifu, tunapaswa kufanya kazi ili tuwe bora zaidi."

    Pia unaweza kusoma:

  8. China imewakamata waandishi wawili wa habari kwa kuripoti ufisadi

    Makundi ya haki za binadamu na wanaharakati wanalalamika kuhusu kukamatwa kwa waandishi wawili wa habari za uchunguzi kutoka China baada ya kuripotiwa kufichua ufisadi uliofanywa na afisa mkuu katika jimbo la Sichuan.

    Waandishi wa habari huru Liu Hu na Wu Yingjiao walikamatwa na polisi siku ya Jumapili baada ya kuchapisha uchunguzi wao, yanasema makundi ya haki za binadamu.

    Polisi wa Chengdu walisema Jumatatu wanaume wawili, waliotambuliwa kwa majina yao ya ukoo Liu na Wu, wenye umri wa miaka 50 na 34, wanachunguzwa kwa "kutoa shutuma za uongo" na "kufanya biashara haramu."

    Akijibu swali kuhusu kukamatwa kwa watu hao, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China amewaambia waandishi wa habari Jumatano kwamba mamlaka husika tayari zimetoa taarifa kuhusu kesi hiyo.

    "China ni nchi inayotawaliwa na sheria, na vyombo vya mahakama vya China hushughulikia kesi kulingana na sheria; kila mtu ni sawa mbele ya sheria," amesema msemaji huyo.

    Liu, mwandishi maarufu wa habari za uchunguzi nchini China, aliwahi kukamatwa mwaka 2013 kwa tuhuma za kashfa baada ya kumtuhumu afisa wa cheo cha juu kwa ufisadi.

    Baada ya kuachiliwa mwaka 2014, aliendelea na uchunguzi wake na kuchapisha ripoti zake kwenye mitandao ya kijamii.

    Kulingana na Watetezi wa Haki za Binadamu wa China, wanasema Liu alikuwa safarini katika treni kutoka mji wake wa Chongqing kuelekea mji mkuu wa Beijing siku ya Jumapili alipokamatwa.

    Wu alikamatwa na polisi katika jimbo la Hebei siku hiyo hiyo, kundi hilo linasema.

    Kulingana na makundi ya haki za binadamu, ripoti ya hivi karibuni ya wawili hao inafichua ufisadi wa afisa wa kaunti.

    Ripoti hiyo ambayo imeondolewa katika mtandao wa kijamii wa China wa WeChat - inataja biashara zilizofilisika kutokana na vitendo vya afisa huyo.

    Kwa mujibu wa Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka (RSF), kuna zaidi ya waandishi wa habari 120 waliokamatwa nchini China.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Shambulio la Israel lauwa watu 17 Gaza

    Wapalestina wasiopungua 17 wameuawa katika mashambulizi ya Israel huko Gaza kwa mujibu wa hospitali.

    Jeshi la Israeli limesema shambulio hilo limetokea baada ya "magaidi" kufyatua risasi kaskazini mwa Ukanda huo, na kumjeruhi vibaya mwanajeshi wakati wa operesheni karibu na Mstari wa Njano, ambao unaashiria mwanzo wa eneo linalodhibitiwa na Israeli chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano ya miezi mitatu na Hamas.

    IDF imesema vikosi vyake na ndege za kivita zimefanya mashambulizi katika eneo hilo kujibu kile ilichokiona kuwa ni "ukiukaji wa waziwazi" wa makubaliano ya kusitisha mapigano.

    Maafisa wa hospitali wanasema watoto sita ni miongoni mwa waliouawa katika maeneo ya Jiji la Gaza na Khan Younis.

    Hospitali ya Al-Shifa katika Jiji la Gaza imesema imepokea miili ya watu 13, wakiwemo watoto watano, ambao waliuawa wakati mahema na nyumba katika vitongoji vya mashariki mwa Zeitoun na Tuffah ziliposhambuliwa.

    Hospitali ya Nasser huko Khan Younis imesema watu wanne waliofariki, akiwemo mtoto mmoja, walifikishwa huko kufuatia mashambulizi katika mahema katika eneo la kusini mwa Qizan Rashwan.

    Israel na Hamas zote zinashutumiana kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha vita karibu kila siku tangu kusitishwa kwa mapigano kuanza tarehe 10 Oktoba.

    Wizara ya afya ya Gaza inayoongozwa na Hamas imesema watu 529 wameuawa na mashambulizi ya Israel, huku jeshi la Israel likisema wanajeshi wake wanne wameuawa katika mashambulizi ya Palestina.

    Vita hivyo vilichochewa na shambulio lililoongozwa na Hamas kusini mwa Israeli tarehe 7 Oktoba 2023, ambapo watu 1,200 waliuawa na wengine 251 walichukuliwa mateka.

    Israel ilijibu shambulio hilo kwa kuanzisha kampeni ya kijeshi huko Gaza, ambapo zaidi ya watu 71,800 wameuawa, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Elon Musk, mtu wa kwanza duniani kuwa na utajiri wa zaidi ya dola bilioni 800

    Elon Musk amekuwa mtu wa kwanza duniani kumiliki zaidi ya dolla billioni mia nane ($800) baada ya kampuni yake ya kutengeneza roketi Space X kununua kampuni ya akili mnemba xAI.

    Shirika la habari la Forbes linasema kuwa ununuzi wa kampuni hiyo ya xAI yenye thamani ya dola trillioni 1.25, iliongeza utajiri wa Musk kwa dola billioni 84, na kufikisha utajiri wake kuwa dola billioni 852.

    Kabla ya ununuzi huo, Musk alikuwa anamiliki 42% ya kampuni ya Space X ambayo thamani yake ni dola billioni 336, huku mwezi Desemba kampuni hiyo ilikadiriwa kuwa na thamani ya dola billioni 800.

    Musk pia alikuwa anamiliki 49% ya xAI ambayo thamani yake ni dola billioni 122, huku kampuni hiyo ikiwa na thamani ya dola billioni 250.

    Shirika la Forbes linasema kuwa Musk kwa sasa anamiliki 43% ya kampuni hiyo nzima ambayo ni dola billioni 542.

    Hii inamfanya Musk kuwa mtu Tajiri zaidi.

    Tajiri huyo pia anamiliki 12% ya kampuni ya kutengeneza magari ya kieletroniki ya Tesla ambayo thamani yake ni dola billioni 178, na yuko na hisa katika kampuni hiyo ya Tesla yenye thamani ya dola billioni 124.

    Kando na hayo, Musk pia alipokea malipo ya wadhamini wa kampuni ya Tesla mwezi Novemba ya dola trillioni 1 kabla ya ushuru kukatwa.

    Mwezi Machi mwaka uliopita Musk alitangaza kuwa kampuni ya xAI na mtandao wake wa kijamii wa X (twitter) zimejumuishwa katika makubaliano ya kibiashara yaliyogharimu xAI dola billioni 80 na X dola billioni 33.

    Suala la Musk kuwa muuzaji na mnunuzi wa kampuni hizi umezua maswali mengi kuhusu ukadiriaji wa thamani ya kampuni hizo.

    Soma zaidi:

  11. Urusi yaishambulia Ukraine na kuwaacha maelfu ya watu kwenye baridi kali

    Urusi imetumia makombora yenye masafa marefu kulenga vituo vya nishati vya Ukraine, amesema rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky.

    Makombora hayo pamoja na ndege zisizo na rubani zilishambulia kituo cha nishati mjini Kyiv pamoja na maeneo mengine.

    "Hili ni pigo kubwa sana kwetu mwaka huu" Kampuni ya nishati ya kibinafsi DTEK imesema.

    Shambulio hilo limetekelezwa wakati ambapo hali ya joto imeshuka na kufikia nyuzi joto -20C, na kuwaacha watu zaidi ya elfu moja mjini Kyiv, bila umeme na kwenye kibaridi kikali, huku kituo cha nishati cha Kharkiv kikiharibiwa kabisa.

    Zelensky amesema Urusi imeamua kutanua vita hivyo badala ya kutumia diplomasia kumaliza vita hivyo na kutaka mataifa washirika wa Ukraine kuiwekea Moscow ‘shinikizo la kutosha.’

    Shambulio hili linajiri wakati ambapo kulikuwa na ‘makubaliano ya nishati’ na rais wa Marekani Donald Trump na rais wa Urusi Vladimir Putin ambayo yalikamilika wikendi iliyopita.

    Katika makubaliano hayo, Urusi ilikuwa isitishe mashambulizi yake katika miundo mbinu ya nishati msimu huu wa baridi nchini Ukraine.

    Rais wa Ukraine anasema Urusi ilitumia kipindi hicho walichokubaliana kusitisha mashambulizi kuongeza akiba yake ya makombora ili kutekeleza mashambulizi zaidi.

    Shambulizi hili limetokea siku ambayo katibu mkuu wa jumuiya ya kujihami ya NATO Mark Rutte, alikuwa mjini Kyiv kukutana na rais Zelensky na pia kuhutubia bunge la Ukraine.

    Wawakilishi wa Urusi na Ukraine wanatarajiwa kukutana mjini Abu Dhabi kwa mazungumzo ya kusitisha vita baadaye wiki hii.

    Soma zaidi:

  12. Watimuliwa kwa uteuzi wa mtu aliyefariki Sudan Kusini

    Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir, amewafuta wafanyikazi wake wawili baada ya kumptosha kumteua mtu aliyefariki, kusimamia jopo la mazungumzo kuhusu uchaguzi utakao fanyika mwezi Desemba.

    Uteuzi wa Steward Soroba Budia ulitangazwa tarehe 30 Januari, ila vyombo vya habari vya taifa hilo vilitangaza kuwa Budia, ambaye alikuwa mwanachama wa chama cha upinzani cha United Democratic Party (UDP), alifariki miaka mitano iliyopita.

    Raia wa Sudan Kusini walikejeli uteuzi huo kwenye mitandao ya kijamii.

    Bila kutoa maelezo, taarifa kutoka kwa rais huyo kwa vyombo vya habari ilisema kuwa amewafuta kazi katibu wake wa mawasiliano David Amour Major na msimamizi wa ofisi ya rais Valentino Dhel Maluet.

    Siku ya Jumatatu, Amour alisema katika taarifa kwa vyombo vya habari kuwa ofisi ya rais ilitegemea “usahihi na uhakiki kikamilifu wa majina” yaliyowasilishwa na “washika dau” kwa ajili ya kujumuishwa katika jopo hilo.

    “Sasa imebainika kuwa uhakiki wa kina haukufanywa na mmoja wa washika wadau, jambo lililosababisha makosa haya yaliyotokea kwa bahati mbaya,” alisema Amour.

    Amour hakusema ni nani, na chama cha UDP pia hakijatoa tamko lolote kuhusu suala hilo.

    Haijulikani ikiwa taarifa hiyo ilisababisha kufutwa kazi kwa Amour ila kulikuwa na uvumi hapo awali kwamba angefutwa kazi.

    Kiir alikuwa ametengeneza jopo lililojumuisha wawakilishi kutoka vyama tofauti kujadili kuhusu uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika mwishoni mwa mwaka huu baada ya chaguzi za awali kuahirishwa.

    Mapigano bado yanashuhudia nchini humo, huku makamu wa rais wa taifa hilo Riek Machar, aliyesimamishwa kazi akiwa bado katika kifungo cha nyumbani na kukabiliwa na mashtaka ya mauaji, uhaini na uhalifu dhidi ya kibinadamu.

    Soma zaidi:

  13. Faili za Epstein zinaibua kumbukumbu ya 'nyakati za uchungu mwingi katika ndoa yangu' - Melinda Gates

    Bilionea Melinda French Gates amesema mumewe wa zamani, mwanzilishi mwenza wa Microsoft Bill Gates, aliyetajwa katika faili mpya zinazohusiana na marehemu Jeffrey Epstein, kunanikumbusha "nyakati za uchungu mwingi katika ndoa yangu".

    Aliambia kipindi cha NPR kwamba "amehuzunishwa sana" na madai ya Epstein na kwamba watu waliotajwa akiwemo mumewe wa zamani, wanahitaji kuwajibishwa.

    "Ninafurahi sana kuwa mbali na uchafu huu," alisema. Wanandoa hao walitalikiana mwaka wa 2021 baada ya miaka 27 ya ndoa.

    Rekodi zilizotolewa na idara ya sheria ya Marekani zinajumuisha madai ya Epstein kwamba Bill Gates aliambukizwa ugonjwa wa zinaa ambaye ameyaita madai hayo "upuuzi mkubwa".

    "Madai haya - kutoka kwa mwongo mkubwa na mwenye chuki - ni ya kipuuzi na ya uwongo kabisa," msemaji wa Bill Gates amejibu kuhusu madai hayo. BBC imewasiliana na wawakilishi wake kuhusu maoni ya mke wake wa zamani.

    Bill Gates hajashutumiwa kwa makosa na yeyote kati ya waathiriwa wa Epstein na jina lake kujumuishwa kwenye faili haimaanishi kuhusika kwa vyovyote na matendo ya uhalifu.

    Katika mahojiano na podikasti ya NPR ya Wild Card, Melinda French Gates alisema: "Kwangu mimi binafsi, ninakuwa hali ngumui kila maelezo ya namna hiyo yanapojitokeza, sivyo? Kwa sababu yanarudisha kumbukumbu za nyakati zenye uchungu mwingi katika ndoa yangu."

    Vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti kwamba kabla ya kutengana kwao, Melinda French Gates alikuwa amekasirika juu ya uhusiano wa mumewe na Epstein. Baada ya kutengana kwao kutangazwa, Bill Gates alikiri kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mfanyakazi wa Microsoft mnamo 2019.

    Madai hayo kuhusu Bill Gates yalijumuishwa katika zaidi ya hati milioni tatu zilizotolewa wiki iliyopita na Idara ya Sheria ya Marekani.

    Soma zaidi:

  14. Uhispania kuwazuia watoto chini ya miaka 16 kutumia mitandao ya kijamii

    Uhispania imekuwa taifa la hivi punde kutaka kupiga marufuku matumizi ya mitandao ya kijamii kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 16.

    "Tutawalinda dhidi ya mitandao ya magharibi" Waziri mkuu Pedro Sanchez alisema katika mkutano wa viongozi wa mataifa mjini Dubai.

    Marufuku hiyo lazima itapitishwa na bunge kabla ya kuwa sheria na ni sehemu ya mabadiliko ambayo ni pamoja na kufanya watendaji wa kampuni kuwajibika kwa "maudhui haramu au yenye madhara" kwenye majukwaa yao.

    Australia ilikuwa nchi ya kwanza duniani kuweka marufuku kama hiyo mwaka jana, huku wengine wakifuatilia mafanikio yake.

    Vilevile, Ufaransa, Denmark na Austria, pia wametangaza wataweka marufuku ya umri katika matumizi ya mitandao ya kijami.

    Serikali ya Uingereza bado inashauriana iwapo itatekeleza marufuku hiyo ya kuwazuia watoto chini ya umri wa 16, kutotumia mitandao ya kijami.

    Kampuni zinazomiliki mitandao ya kijami, zimepinga marufuku hiyo zikisema itakuwa vigumu kutekeleza, na huenda ikawatenga vijana wanaohitaji mitandao hiyo.

    Soma zaidi:

  15. Wahamiaji waaga dunia baada ya ajali ya boti pwani ya Ugiriki

    Takriban wahamiaji 14 wamefariki baada ya boti iliyokuwa imewabeba kugongana na meli ya polisi wa bahari karibu na kisiwa cha Chios Jumanne jioni.

    Mamlaka za Ugiriki zinasema boti hiyo ilikuwa ikiendeshwa vibaya wakati walikuwa wanawafuata kabla ya ajali hiyo kutokea karibu na kijiji cha Vrontades, kisiwa cha Chios.

    Watu 24 waliokolewa wengi wao wakiwa wamejuruhiwa, huku wengine wasijulikane waliko.

    Meli hiyo ya kushika doria bado haijafafanua jinsi ajali hiyo ilivyotokea.

    Shughuli ya kuwatafuta na kuwaokoa wahamiaji waliokuwa kwenye boti hiyo bado inaendelea.

    Shirika la habari la kitaifa la Ugiriki ERT, linaripoti kuwa waliojeruhiwa miongoni mwao ni watoto 7, mwanamke mmoja mjamzito na maafisa wawili wa polisi.

    Soma zaidi:

  16. Maelfu ya nyaraka za Epstein zaondolewa kwa umma baada ya waathiriwa kutambuliwa

    Idara ya sheria ya Marekani (DOJ) imeondoa nyaraka za Epstein kutoka kwenye tovuti zao, baada ya waathiriwa kulalamika kuwa hilo linahatarisha utambulisho wao.

    Mawakili wa waathiriwa wa Epstein walisema nyaraka zilizotolewa Ijumaa iliyopita, ziliharibu majina yao na kuhatarisha maisha ya zaidi ya waathiriwa 100.

    Anwani za barua pepe na picha za uchi ambazo majina na nyuso za waathiriwa ziliweza kutambuliwa zilijumuishwa kwenye toleo hilo.

    Waathiriwa hao walisema kuchapisha nyaraka hizo ni "kuwafedhehesha" na kusema hawataki "kutajwa, kuchunguzwa na kupewa kiwewe tena".

    Idara hiyo ya sheria imesema imeondoa nyaraka hizo zenye utata na kusema kuwa kasoro zilizokuwepo zimetokana na ‘makosa ya kibinadamu.’

    Katika barua iliyowasilishwa mbele ya jaji siku ya Jumatatu idara ya sheria ilisema kuwa "nyaraka zote ambazo waathiriwa au mawakili wao walitaka ziondolewe kufikia jana jioni, zimefutwa ili kuhaririwa" tena.

    "Idadi kubwa" ya nyaraka zilizotambuliwa kuwa na makosa pia zimeondolewa, iliongeza.

    Katika makubaliano ya kuchapisha nyaraka hizo baada ya Idara hiyo kutakiwa kufanya hivyo na Bunge, serikali iliitaka majina ya waathiriwa yafichwe ili kuwalinda.

    Msemaji wa DOJ aliambia mshirika wa habari wa BBC nchini Marekani, CBS kwamba "inachukulia ulinzi wa waathiriwa kwa uzito mkubwa na imeondoa maelfu ya majina ya waathiriwa katika mamilioni ya kurasa zilizochapishwa ili kuwalinda wasio na hatia".

    Mamilioni ya faili zinazohusiana na Epstein zimetolewa na DOJ tangu sheria ilipoamuru kutolewa kwake mwaka jana, ikiwa ni pamoja na kurasa milioni tatu, picha 180,000 na video 2,000 Ijumaa iliyopita.

    Mhalifu wa kingono Jeffrey Epstein, alifariki katika jela moja mjini Newyork tarehe 10 Agosti 2019 alipokuwa akisubiri kusikilizwa kwa kesi dhidi yake ya biashara haramu ya ngono.

    Soma zaidi:

  17. Kiongozi wa waasi adai kuhusika na shambulizi la ndege isiyo na rubani Congo

    Corneille Nangaa, kiongozi wa waasi wa AFC/M23 katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, amedai kuhusika na shambulizi la ndege isiyo na rubani iliyolenga uwanja wa ndege katika mji wa kimkakati kaskazini mashariki mwa Kisangani, akielezea kama onyo kwa serikali.

    Serikali ya mkoa wa Tshopo, katika eneo la Kisangani, ilisema katika taarifa Jumapili kwamba ndege nane zisizo na rubani zilizojaa vilipuzi zililenga uwanja wa ndege wa Kisangani. Ilisema ndege zote zisizo na rubani zilidunguliwa kabla ya kufika zilikoelekezwa.

    Uwanja wa ndege huo upo takriban kilomita 17 (maili 10) kutoka katikati mwa Kisangani, mamia ya kilomita kutoka eneo la vita katika majimbo ya Kaskazini na Kusini mwa Kivu, ambapo AFC/M23 imeteka maeneo makubwa tangu 2022, ikiwewemo miji muhimu ya Goma na Bukavu katika shambulizi la mwaka jana.

    Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X, kiongozi wa waasi Corneille Nangaa alisema operesheni ya Kisangani ilionyesha "ubora wa anga" wa vikosi vya jeshi vya Congo haupo tena na kuonya kwamba ndege yoyote itakayopaa juu ya maeneo yanayoshikiliwa na waasi iatashambuliwa.

    Pia unaweza kusoma:

  18. Marekani yathibitisha kutuma wanajeshi Nigeria

    Marekani imetuma kikosi kidogo cha wanajeshi nchini Nigeria, afisa mkuu wa jeshi la Marekani amethibitisha, ikiwa ni mara ya kwanza kukiri hadharani kuwepo kwa vikosi vya Marekani nchini humo tangu ilipofanya mashambulizi ya anga siku ya Krismasi.

    Mkuu wa Kamandi ya Marekani Afrika (Africom), Jenerali Dagvin RM Anderson, alisema alikutana na Rais wa Nigeria Bola Tinubu huko Roma, ambapo walijadili usalama wa kikanda na hitaji la ushirikiano wa karibu.

    Jenerali Anderson alisema nchi zote mbili zimekubaliana juu ya "njia ya kusonga mbele katika kanda".

    "Hiyo imesababisha kuongezeka kwa ushirikiano kati ya mataifa yetu, kujumuisha timu ndogo ambayo inaleta uwezo wa kipekee kutoka Marekani ili kuongeza kile ambacho Nigeria imekuwa ikifanya kwa miaka kadhaa" Jenerali Anderson alisema.

    Aliongeza kuwa kutumwa kwa wanajeshi nchini humo kulifanywa kwa ombi la Nigeria na kulenga msaada wa kijasusi.

    Hilo linatokea huku kukiwa na shinikizo kutoka Ikulu ya Marekani kwa serikali ya Nigeria kuboresha usalama na kufanya zaidi kulinda jumuiya za Kikristo.

    Rais Donald Trump hapo awali alidai kuwa kulikuwa na "mauaji ya Kimbari ya Kikristo" nchini Nigeria, akipendekeza kuwa viongozi walikuwa wakishindwa kuwalinda Wakristo dhidi ya mashambulizi ya wanajihadi.

    Serikali ya Nigeria imekanusha madai hayo, ikisema kuwa "Waislamu, Wakristo na wale wasio na imani sawa" wanalengwa na makundi yenye silaha.

    Krismasi iliyopita, Marekani ilifanya mashambulizi ya angani katika Jimbo la Sokoto nchini Nigeria, ikisema kuwa ilikuwa ikilenga kambi zinazotumiwa na makundi yenye uhusiano na Islamic State.

    Tangu wakati huo, Nigeria na Marekani zimeimarisha ushirikiano wa kiusalama, ikiwa ni pamoja na kushirikishana taarifa za kijasusi.

    Soma zaidi:

  19. Saif al-Islam Gaddafi, mwana wa kiongozi wa zamani wa Libya, aripotiwa kuuawa

    Saif al-Islam Gaddafi, mwana wa kiongozi wa zamani wa Libya Kanali Muammar Gaddafi, ameripotiwa kupigwa risasi na kuuawa.

    Kifo cha mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 53, ambaye hapo awali alionekana kuwa mrithi wa baba yake, kilithibitishwa na mkuu wa timu yake ya kisiasa siku ya Jumanne, kulingana na Shirika la habari la Libya.

    Wakili wake aliambia shirika la habari la AFP kwamba kikosi cha "makomandoo wanne" kilifanya mauaji nyumbani kwake katika jiji la Zintan, ingawa haikuwa wazi ni nani aliyehusika na shambulio hilo.

    Hata hivyo, dada yake alitoa taarifa zinazokinzana na hizo akiambia televisheni ya Libya kwamba alifariki karibu na mpaka wa nchi hiyo na Algeria.

    Saif al-Islam Gaddafi kwa muda mrefu alionekana kama mtu mwenye ushawishi mkubwa na anayeogopwa zaidi nchini baada ya baba yake, ambaye alitawala Libya kuanzia 1969 hadi alipoondolewa madarakani na kuuawa wakati wa uasi mwaka 2011.

    Alizaliwa mwaka wa 1972 na kuchukua jukumu muhimu katika uhusiano wa Libya na nchi za Magharibi kuanzia mwaka wa 2000 hadi kuanguka kwa utawala wa Gaddafi.

    Baada ya kuondolewa kwa baba yake, Saif al-Islam Gaddafi - ambaye alishutumiwa kwa kuchukua jukumu muhimu katika ukandamizaji wa kikatili wa maandamano ya kupinga serikali - alifungwa jela na wanamgambo wapinzani katika jiji la Zintan kwa karibu miaka sita.

    Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ilitaka kumshtaki kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu kwa madai ya jukumu lake katika kukandamiza maandamano ya upinzani mwaka wa 2011.

    Mnamo mwaka wa 2015, alipewa hukumu ya kifo bila kuwepo mahakamani na mahakama ya Libya kwa jukumu lake katika msako huo.

    Gaddafi alikuwa akikana kila mara kwamba alitaka kurithi madaraka kutoka kwa baba yake, akisema hatamu za madaraka hazikuwa "shamba la kurithi".

    Hata hivyo, mwaka wa 2021 alitangaza kwamba angegombea urais katika chaguzi ambazo baadaye ziliahirishwa kwa muda usiojulikana.

    Soma zaidi:

  20. Marekani yadungua ndege isiyo na rubani ya Iran

    Ndege isiyo na rubani ya Iran imedunguliwa ilipokaribia meli ya Marekani katika Bahari ya Arabia siku ya Jumanne, msemaji wa jeshi la Marekani amesema.

    Ndege ya kivita ya F-35C iliyopaa kutoka kwa meli ya kivita ya USS Abraham Lincoln imedungua ndege hiyo isiyo na rubani "ili kujilinda" na kulinda meli hiyo ya kubeba ndege na wafanyakazi wake, msemaji wa Jeshi Kuu la Marekani Kapteni Tim Hawkins alisema.

    Meli hiyo ilikuwa takriban maili 500 kutoka pwani ya Iran wakati ndege isiyo na rubani ilipoikaribia ikiwa na "nia isiyoeleweka".

    Hakuna vifaa vya Marekani vilivyoharibika na hakuna wanajeshi waliojeruhiwa.

    Hii inakuja huku Marekani ikiendelea kujenga uwepo wa kijeshi katika eneo hilo, huku mvutano ukiongezeka kati ya Washington na Tehran.

    Rais wa Marekani Donald Trump ametishia kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran ikiwa haitajadili makubaliano ya kuzuia mpango wake wa nyuklia.

    Hapo awali alizungumzia uwezekano wa kuingilia kati wakati wa msako mkali wa Tehran dhidi ya maandamano ya kupinga serikali.

    Akizungumza baada ya kuangushwa kwa ndege isiyo na rubani ya Iran, Katibu wa Habari wa Ikulu ya White House Karoline Leavitt aliambia Fox News kwamba mazungumzo kati ya Marekani na Iran bado yamepangwa kufanyika baadaye wiki hii.

    Alisema Trump "anaendelea kujitolea kufuata diplomasia kwanza kila wakati", lakini akaongeza kuwa "daima ana chaguzi mbalimbali mbele yake, na hiyo inajumuisha matumizi ya nguvu za kijeshi".

    Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei hapo awali alionya kwamba shambulio lolote dhidi ya nchi hiyo litasababisha "vita vya kikanda".

    Iran haijatoa maoni yoyote kuhusu tukio la ndege zisizo na rubani la Jumanne.

    Soma zaidi: