Moja kwa moja, Marekani yasema inaweza kuendelea na zuio la majini dhidi ya Iran bila ukomo
Kauli hiyo inakuja wakati mazungumzo ya kusitisha vita yakikwama, huku usafirishaji wa mafuta duniani ukiathiriwa na mzozo unaoendelea katika eneo la Mlango wa Hormuz.
Muhtasari
Wazambia wasubiri matokeo ya uchaguzi huku rais akiwania muhula wa pili
Marekani inasema nchi nyingi ziliisaidia China kukwepa ushuru wa Trump
Mvua kubwa nchini Japan yaua watu sita
Misri na Bahrain zalaani shambulio dhidi ya meli mbili za mafuta za Imarati katika Mlango-Bahari wa Hormuz
CENTCOM: Tunaanzisha kikosi kazi cha kwanza cha kimataifa cha ndege zisizo na rubani za mashambulizi
Bodi ya Dawa yaonya Wakenya kuhusu vidonge vya P2 bandia vilivyoingia sokoni
Wazambia wasubiri matokeo ya uchaguzi huku rais akiwania muhula wa pili
Chanzo cha picha, Reuters
Zoezi la
kuhesabu kura linaendelea nchini Zambia baada ya upigaji kura kuhitimishwa siku
ya Alhamisi katika uchaguzi mkuu, ambapo Rais Hakainde Hichilema alikuwa
akiwania muhula wa pili wa miaka mitano.
Licha ya
kuiongoza Zambia katika kipindi cha kufufuka kwa uchumi, Hichilema alikabiliwa
na changamoto kwani watu wengi wamesema hali zao za maisha hazijaboreka.
Mpinzani
wake mkuu, Brian Mundubile, alitarajia kutumia hali hiyo ya kutoridhika kwa
wananchi kwa faida yake ya kisiasa.
Ukosefu wa
ajira na kupanda kwa gharama za maisha vilikuwa masuala muhimu kwa wapiga kura.
Ili mgombea
urais ashinde moja kwa moja katika duru ya kwanza, anahitaji kupata zaidi ya
nusu ya kura zilizopigwa; vinginevyo, uchaguzi wa marudio hufanyika.
Tume ya
uchaguzi ina muda hadi mwisho wa siku ya Jumapili kutangaza matokeo.
Siku ya
upigaji kura ilikuwa ya amani kwa kiasi kikubwa, huku kukiwa na ripoti za
foleni katika maeneo mengi na ucheleweshaji wa hapa na pale tu.
Mbali na
kumchagua rais, wapiga kura zaidi ya milioni nane waliojiandikisha walipata
fursa ya kuchagua bunge jipya na mabaraza ya serikali za mitaa.
Upigaji kura wa Alhamisi ulionekana kuwa kipimo
cha sifa ya Zambia kama mojawapo ya nchi zenye demokrasia
Marekani inasema nchi nyingi ziliisaidia China kukwepa ushuru wa Trump
Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Ikulu ya
White House ilisema katika ripoti siku ya Alhamisi kwamba zaidi ya nchi 40
zimeisaidia China kuepuka ushuru wa Marekani kwa kuhamisha mauzo ya nje kupitia
mataifa ambayo yanakabiliwa na ushuru mdogo wa uagizaji wa Marekani.
Nchi
zilizotajwa ni pamoja na Canada, India, Mexico, Japan na Korea Kusini, ambazo
Ikulu ya White House ilisema zimeisaidia China kukwepa makumi ya mabilioni ya
dola katika ushuru, ambao hutozwa kwa makampuni yanayoagiza bidhaa.
Mshauri wa
biashara wa Ikulu ya White House, Peter Navarro, alisema imegharimu "kazi
za Marekani na mabilioni ya mapato".
Msemaji wa
ubalozi wa China huko Washington alisema "vita vya biashara havina
washindi" na kwamba inapinga hatua za ushuru wa Marekani na matumizi ya
nguvu za serikali kulenga makampuni ya China.
"Vitendo
au makubaliano yoyote ya upande mmoja kuhusu bidhaa zilizohamishwa hayapaswi
kulenga au kudhuru maslahi ya wahusika wengine," msemaji huyo aliongeza.
BBC
imewasiliana na balozi za Marekani za Canada, India, Mexico, Japani, Korea
Kusini na washirika wengine wa biashara walioorodheshwa katika ripoti hiyo kwa
maoni.
Ripoti hiyo
inafuatia wimbi la vikwazo kati ya Marekani na China na inakuja wiki chache
kabla ya Rais wa Marekani Donald Trump kukutana na kiongozi wa China Xi Jinping
huko Washington.
Kati ya dola
bilioni 30 (£22bn) na takriban dola bilioni 300 katika bidhaa zimehamishwa
kutoka nchi zenye ushuru mkubwa kupitia zile zenye viwango vya chini, kulingana
na makadirio ya serikali na sekta binafsi yaliyonukuliwa na Ikulu ya White
House.
Mvua kubwa nchini Japan yaua watu sita
Chanzo cha picha, Reuters
Angalau watu
sita wamefariki dunia na wengine watano kujeruhiwa mashariki mwa Japan baada ya
mvua kubwa kunyesha katika eneo la Chiba, karibu na mji mkuu wa Tokyo.
Mvua hizo,
ambazo mamlaka zimezitaja kuwa "zisizo na kifani", zilisababisha
kukatika kwa umeme katika kaya zaidi ya 20,000, huku wasafiri 7,000 wakikwama
usiku kucha katika uwanja wa ndege wa Narita jijini Tokyo.
Mamlaka za
eneo hilo zilitoa onyo la dharura la kiwango cha tano, kiwango cha juu zaidi cha
tahadhari—siku ya Alhamisi. Ingawa kiwango hicho kilishushwa hadi cha nne
kufikia Ijumaa asubuhi, mamlaka zinaendelea kutoa tahadhari kuhusu hatari ya
maporomoko ya ardhi na mafuriko.
Mvua hizi
kubwa zimefuatia mfululizo wa dhoruba zilizokumba Japan na nchi jirani wiki
hii, katika msimu ambao umetabiriwa kuwa na dhoruba kali (typhoon) nyingi
kuliko kawaida..
Habari za hivi punde, Misri na Bahrain zalaani shambulio dhidi ya meli mbili za mafuta za Imarati katika Mlango-Bahari wa Hormuz
Misri na
Bahrain zililaani kitendo cha kushambuliwa kwa meli mbili za Imarati wakati
zikipita katika Mlango-Bahari wa Hormuz.
Kwa mujibu
wa Kampuni ya Kitaifa ya Mafuta ya Abu Dhabi, ambayo ndiyo mmiliki wa meli
hizo, meli hizo zililengwa na kushambuliwa jioni ya Alhamisi.
Katika
taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri ilielezea shambulio hilo kama
"kitendo cha uchokozi" ambacho "kinatishia usalama wa
usafirishaji na uhuru wa meli kupita katika mojawapo ya njia muhimu zaidi za
majini duniani."
Misri pia
ilisisitiza "umuhimu wa kuzingatia sheria za kimataifa kwa namna
inayosaidia kupunguza mivutano na kudumisha usalama na utulivu katika eneo
hilo."
Wizara ya
Mambo ya Nje ya Bahrain nayo ililaani "shambulio la Iran" dhidi ya
meli hizo mbili za mafuta za Imarati kupitia ujumbe kwenye mtandao wa kijamii
wa X.
Bahrain
ililaani vikali mashambulizi hayo, ikiyaita ya "kigaidi" na kusema
kuwa "shambulio hili ni tishio kubwa kwa usalama na utulivu wa eneo hilo
pamoja na usalama wa usafiri wa baharini, na ni ukiukaji wa wazi wa sheria za
kimataifa."
Wizara ya
Mambo ya Nje ya Bahrain pia ilitoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa
Mataifa kuchukua "hatua madhubuti na za kuzuia" dhidi ya mashambulizi
hayo na "kuilazimisha" Iran kusitisha mara moja vitendo vyote vya
"uchokozi."
Kampuni ya Kitaifa ya Mafuta ya Abu Dhabi
inasema kuwa zaidi ya meli zake kumi na mbili zimeshambuliwa katika wiki chache
zilizopita
CENTCOM: Tunaanzisha kikosi kazi cha kwanza cha kimataifa cha ndege zisizo na rubani za mashambulizi
Chanzo cha picha, US Central Command via Getty Images
Maelezo ya picha, Picha ya vifaa vya Marekani kwenye meli ya USS Abraham Lincoln mwanzoni mwa vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Kamandi Kuu
ya Marekani (CENTCOM) imetangaza juhudi zake za kuunda "kikosi kazi cha
kwanza cha kimataifa cha ndege zisizo na rubani za mashambulizi zenye uwezo wa
kufanya kazi katika maeneo mbalimbali" huko Mashariki ya Kati.
Marekani
inasema kuwa imeanza mchakato wa kushauriana na washirika wa kikanda na
kuwaalika rasmi kushiriki.
Habari hii
imetolewa wakati huo huo na ziara ya Kamanda wa CENTCOM, Brad Cooper, katika
baadhi ya nchi za eneo hilo, ikiwemo Saudi Arabia.
CENTCOM
inasema kuwa kikosi hicho, kilichopewa jina la "Falcon Strike Task
Force", kitajumuisha ndege zisizo na rubani za mashambulizi zenye injini
moja, zenye uwezo wa kufanya kazi juu ya bahari, juu ya uso wa bahari, na hata
chini ya maji.
CENTCOM
inasema kuwa Marekani na washirika wake wa kikanda wataendesha kikosi hiki; kwa
hakika, ni mwendelezo na upanuzi wa mpango wa awali wa Marekani uitwao
"Scorpion Strike", ambao ulianzishwa miezi tisa iliyopita kwa kutumia
ndege zisizo na rubani za mashambulizi.
Marekani
inasema ilitumia ndege zisizo na rubani kutoka Kundi la Operesheni Maalum la
"Scorpion Strike" katika mashambulizi dhidi ya bandari za kusini mwa
Iran, na wafanyakazi hao hao sasa wataendesha Kundi la "Falcon
Strike" kwa kushirikiana na nchi za eneo hilo."
Bodi ya Dawa yaonya Wakenya kuhusu vidonge vya P2 bandia vilivyoingia sokoni
Chanzo cha picha, Getty Images
Bodi ya Famasi na Sumu nchini Kenya imewaonya Wakenya kuhusu uwepo wa dawa bandia ya kuzuia mimba Postinor 2, maarufu kama P2, ambayo tayari imeingia sokoni.
Katika tahadhari ya umma iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Dkt Ahmed Mohamed, imesema dawa hiyo bandia ni vidonge vya Levonorgestrel vyenye miligramu 0.75, kutoka kundi lenye namba T34197R.
Wauzaji wa dawa hiyo walidai kuwa kundi hilo lilitengenezwa na kampuni ya kimataifa ya dawa kutoka Ulaya, Gedeon Richter.
Hata hivyo, Bodi ya Famasi na Sumu ilifanya uchambuzi wa kulinganisha dawa hiyo bandia na Postinor 2 halisi inayotengenezwa na Gedeon Richter Plc, na kubaini tofauti kadhaa.
Miongoni mwa tofauti hizo ni namna namba ya kundi ilivyochapishwa kwenye kifungashio, ambayo haikulingana na mfumo unaotumiwa kwenye bidhaa halisi za Gedeon Richter.
Bodi hiyo pia ilibaini kuwa kijikaratasi chenye maelekezo kwa mtumiaji kilikuwa na makosa kadhaa ya uchapishaji na tahajia, jambo lililoashiria kuwa dawa hiyo ni bandia.
Postinor 2 ni dawa ya dharura ya kuzuia mimba inayotumiwa baada ya kujamiiana bila kinga au pale ambapo njia ya kawaida ya uzazi wa mpango imeshindwa. Inapaswa kutumiwa ndani ya saa 72 baada ya kujamiiana.
Haaland athibitishwa kuwa anashikilia rekodi saba za Guinness
Chanzo cha picha, Guiness World Records
Mshambuliaji wa Manchester City, Erling Haaland, ametunukiwa vyeti vinne vya Guinness World Records kutokana na mafanikio yake ya kipekee katika ufungaji mabao kwenye soka la ndani na kimataifa.
Raia huyo wa Norway mwenye umri wa miaka 26 ametambuliwa kwa kuweka rekodi mbalimbali katika Ligi Kuu ya England, Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ligi ya Mataifa ya UEFA, kabla ya kuanza kwa msimu mpya.
Haaland sasa ametunukiwa rasmi vyeti vinne vya Guinness World Records, ikiwa ni kutambua mafanikio yake ya kipekee akiwa na Manchester City na timu ya taifa ya Norway.
Mafanikio hayo yanajumuisha kuwa mchezaji aliyefikisha mabao 100 ya Ligi Kuu ya England kwa haraka zaidi, kufunga mabao mengi zaidi katika msimu mmoja wa ligi hiyo, kuwa kinara wa muda wote wa mabao katika Ligi ya Mataifa ya UEFA na kufunga idadi inayolingana na rekodi ya mabao mengi zaidi katika mchezo mmoja wa Ligi ya Mabingwa.
Miongoni mwa rekodi zake kubwa ni kufikisha mabao 100 ya Ligi Kuu ya England katika mechi 111 pekee.
Haaland alifikisha idadi hiyo kupitia mkwaju wa penalti dhidi ya Fulham, Desemba 2, 2025, na hivyo kuweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyefikisha mabao 100 kwa haraka zaidi katika historia ya ligi hiyo.
Katika kipindi cha zaidi ya miaka mitatu tangu alipojiunga na Manchester City msimu wa 2022/23, Haaland amegeuka kutoka kuwa mmoja wa washambuliaji chipukizi waliokuwa wakiahidi zaidi barani Ulaya hadi kuwa mmoja wa wafungaji bora zaidi katika historia ya Ligi Kuu ya England.
Zambia yamkamata Mkenya kwa tuhuma za kuhujumu mfumo wa uchaguzi
Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Mamlaka nchini Zambia zimemkamata raia wa Kenya mwenye umri wa miaka 56, Michael Njuka, anayefahamika pia kama Michael Juga, kwa tuhuma za kuhusika katika njama ya kutekeleza mashambulizi ya kimtandao dhidi ya serikali na kulenga miundombinu ya uchaguzi nchini humo.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Ndani na Usalama wa Ndani ya Zambia, Dickson Matembo, Njuka alikamatwa Jumatano katika operesheni ya pamoja iliyofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama, siku chache kabla ya uchaguzi mkuu wa Zambia wa Agosti 13, 2026.
Akizungumza kuhusu kukamatwa kwa Njuka, Matembo alisema: “Katika tukio linalohusiana na hili, serikali imemkamata raia wa Kenya aliyetambuliwa kama Michael Njuka, mwenye umri wa miaka 56, ambaye anadaiwa kuwa amepewa kandarasi ya kutekeleza uhalifu wa kimtandao unaolenga serikali.”
Kwa mujibu wa chombo cha habari cha Kenya NTV, mamlaka zinasema Njuka na washukiwa wengine wawili walikuwa wamepewa kandarasi ya kutekeleza uhalifu wa kimtandao dhidi ya serikali, kwa lengo la kuhujumu miundombinu ya uchaguzi.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Matembo alisema, “Baada ya operesheni iliyofanikiwa, serikali imewakamata maafisa watatu wa zamani wa ngazi za juu serikalini kwa madai ya kutoa huduma za kiufundi zilizolenga kuvuruga mfumo wa uchaguzi. Watatu hao kwa sasa wanashikiliwa chini ya ulinzi halali wa serikali.”
Maafisa hao ni Japhern Mwakalombe, Mwila Kakana na Sensho Banda, ambao wizara imesema wanasaidia katika uchunguzi unaoendelea.
Kwa mujibu wa mamlaka, washukiwa hao walikutwa wakiwa na dola za Marekani 387,500.
Hata hivyo, mamlaka hazijaeleza chanzo cha fedha hizo wala madhumuni yaliyokusudiwa.
Matembo pia alisema uchunguzi umebaini kuwepo kwa taarifa nyeti za kijeshi katika baadhi ya vifaa vya kielektroniki vilivyokamatwa kutoka kwa washukiwa, hali iliyozua wasiwasi kuhusu uwezekano wa watu wasioidhinishwa kupata taarifa zinazolindwa.
Kuhusu kukamatwa kwa Njuka, Matembo alisema raia huyo wa Kenya anadaiwa kupewa kandarasi ya kutekeleza uhalifu wa kimtandao uliolenga serikali.
Mamlaka za ulinzi na usalama nchini Zambia zimesema zimeongeza tahadhari ili kulinda mchakato wa uchaguzi na usalama wa taifa dhidi ya hujuma za kimtandao au za kimwili.
Rais wa Zambia na kiongozi wa chama tawala cha United Party for National Development, Hakainde Hichilema, alikuwa akiwania muhula mwingine akisisitiza ajenda ya kufufua uchumi, kuboresha huduma za umma na kuongeza ajira kwa vijana.
Hichilema anashindana na wagombea wengine 13 katika uchaguzi huo, uliokuwa muhimu kwa Zambia inayojulikana kwa historia ya chaguzi zinazochukuliwa kuwa za amani na za kuaminika.
Wapalestina waamriwa kuondoka majumbani mwao katika operesheni ya kuwaondoa walowezi wa Israel
Chanzo cha picha, EPA
Takriban familia 12 za Wapalestina zinazoishi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel zimeamriwa kuondoka katika nyumba na mali zao, huku vikosi vya Israel vikiendelea kuwaondoa walowezi wa Israel katika eneo hilo.
Tangu Jumapili, vikosi vya Israel vilikuwa vimezingira familia hizo zilizokuwa zikiishi katika nyumba tatu, huku vikikata huduma za umeme na maji.
Msemaji wa Israel aliiambia BBC kuwa hatua zilizochukuliwa na wanajeshi hao ni za aibu na hazikubaliki, akiongeza kuwa serikali itachunguza tukio hilo na kuwakamata waliohusika.
Katika eneo la Qusra, wakazi waliiambia BBC kuwa familia zilizokuwa zimezingirwa katika nyumba zao ziliamriwa kuondoka siku ya Alhamisi. Baada ya kuondolewa, baadhi yao walipata hifadhi katika nyumba nyingine.
Familia hizo si pekee zilizoathirika. Katika maeneo mengine ya kijiji cha Qusra, familia nyingine 11 zilizoishi katika nyumba tofauti pia ziliamriwa na jeshi kuondoka katika makazi yao.
Video zilizosambazwa usiku wa kuamkia Alhamisi zilionyesha magari kadhaa ya usalama ya Israel, likiwemo tingatinga lililotumika katika operesheni hiyo.
Picha nyingine zilizopigwa wakati wa mchana zilionyesha safu ndefu ya wanajeshi na maafisa wa usalama wa Israel kwenye barabara inayoelekea katika kijiji hicho cha Wapalestina.
Jeshi la Ulinzi la Israel lilisema lilikuwa limebomoa vituo viwili vilivyojengwa kinyume cha sheria na Waisraeli waliokuwa wamekalia eneo hilo.
Baada ya takriban saa 10, baadhi ya familia ziliruhusiwa kurejea katika nyumba zao. Hata hivyo, zilisema zilikuta vitu vyao vimetapakaa kila mahali.
Mkazi mmoja aliiambia BBC kuwa wanajeshi walitupa chakula chote kilichokuwa kwenye jokofu na hata kuchukua dola 1,500, sawa na takriban faranga milioni mbili za Rwanda, kutoka kwake.
BBC iliwasiliana na Jeshi la Ulinzi la Israel kuhusu madai hayo, lakini jeshi hilo halikutoa maelezo.
Tanzania yashindwa mtihani wa uwazi wa fedha wa Marekani, Kenya yapita
Chanzo cha picha, MWANANCHI
Kenya imetimiza viwango vya Marekani kuhusu uwazi katika matumizi na usimamizi wa fedha za umma, huku Tanzania ikishindwa kufikia viwango hivyo.
Hayo yamebainishwa katika Ripoti ya Uwazi wa Fedha ya 2026 iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.
Ripoti hiyo inaangalia iwapo serikali zinaweka wazi kwa wananchi taarifa kuhusu zinavyokusanya na kutumia fedha za umma, pamoja na namna zinavyosimamia madeni, bajeti, manunuzi ya serikali na rasilimali za nchi.
Kenya ni miongoni mwa nchi 73 zilizofikia viwango vilivyowekwa na Marekani, pamoja na Uganda, Rwanda, Afrika Kusini, Ghana na Mauritius.
Tanzania, kwa upande mwingine, ni miongoni mwa nchi 67 ambazo hazikufikia viwango hivyo. Hata hivyo, Marekani imesema Tanzania imepiga hatua kubwa kuelekea kutimiza viwango hivyo.
Ripoti hiyo pia imeeleza kuwa kushindwa kufikia viwango vya uwazi wa fedha hakumaanishi moja kwa moja kuwa serikali husika ina kiwango kikubwa cha ufisadi.
Katika Afrika Mashariki, Kenya, Uganda na Rwanda ndizo zilizotimiza viwango vya chini vya uwazi wa fedha za umma.
Kwa ujumla, serikali na taasisi 140 zilitathminiwa. Kati yao, 73 zilifikia viwango vya uwazi vilivyowekwa, huku 67 zikishindwa.
Wabunge wa Marekani waeleza wasiwasi kuhusu hali ya meli ya kivita ya USS Abraham
Chanzo cha picha, Reuters
Wabunge wa chama cha Democratic nchini Marekani wameeleza wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya meli ya kubeba ndege za kivita ya Marekani, USS Abraham Lincoln, ambayo imekuwa ikifanya shughuli katika Mashariki ya Kati kwa muda mrefu.
Wamesema taarifa za upungufu wa mahitaji muhimu, hitilafu katika mabomba ya maji na matatizo mengine ndani ya meli hiyo hazikubaliki.
Aidha, wameeleza wasiwasi kuhusu uchovu uliokithiri na msongo wa mawazo miongoni mwa wanajeshi, huku kukiwa na taarifa kwamba baadhi yao walijaribu kujirusha baharini.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, hata hivyo amesema taarifa kuhusu hali ya USS Abraham Lincoln zimewasilishwa kwa njia isiyo sahihi.
Meli hiyo imekuwa baharini tangu Novemba mwaka jana.
Watu wanne wafariki dunia huku mvua kubwa ikisababisha maporomoko Japan
Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Mvua kubwa isiyokuwa ya kawaida katika Mkoa wa Chiba nchini Japan imesababisha vifo vya watu wanne na kuwaacha maelfu ya wasafiri wakikwama usiku kucha katika Uwanja wa Ndege wa Narita jijini Tokyo.
Mkoa huo, unaopakana na jiji la Tokyo, umerekodi zaidi ya milimita 100 za mvua kwa saa tangu Alhamisi alasiri, kwa mujibu wa mamlaka.
Kiasi hicho ni takriban mara tatu ya wastani wa mvua inayonyesha nchini Japan mwezi Agosti na ndicho kikubwa zaidi kuwahi kurekodiwa nchini humo.
Mvua hiyo kubwa ilisababisha kusitishwa kwa huduma za treni, mabasi na teksi, huku zaidi ya kaya 20,000 katika Chiba zikikosa umeme.
Mamlaka za Japan zimeeleza mvua hiyo kuwa tukio lisilo na mfano.
Gavana wa Chiba, Toshihito Kumagai, amesema tukio hilo lilikuwa la kipekee hata kwa viwango vya hali ya hewa vya kihistoria nchini Japan.
“Nimekabiliana na majanga mengi hapo awali, lakini sijawahi kukumbana na hali kama hii,” amesema.
Ameongeza kuwa serikali itaweka kipaumbele katika kuokoa maisha na kuendelea na shughuli za uokoaji na kurejesha hali ya kawaida.
Mkazi mmoja wa jiji la Ichikawa, Chiba, ameiambia NHK kuwa mvua hiyo ilianza ghafla na kumshangaza.
Mvua hiyo ilisababisha Shirika la Hali ya Hewa la Japan kutoa onyo la dharura la kiwango cha tano, ambacho ndicho kiwango cha juu zaidi.
Onyo hilo lilishushwa hadi kiwango cha nne Ijumaa asubuhi, lakini mamlaka zimeendelea kuwaonya wakazi kuwa waangalifu kutokana na hatari ya maporomoko ya ardhi, mafuriko na kujaa kwa mito.
Takriban watu 7,000 walikwama usiku kucha katika Uwanja wa Ndege wa Narita, mmoja wa viwanja viwili vikuu vya ndege vya Tokyo, baada ya mvua kusababisha kukatika kwa huduma za usafiri zinazounganisha uwanja huo na maeneo mengine.
Trump atangaza ushuru wa hadi asilimia 100 kwa ndege zisizo na rubani zinazoagizwa kutoka nje
Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza ushuru wa hadi asilimia 100 kwa ndege zisizo na rubani zinazoagizwa kutoka nje pamoja na baadhi ya vipuri vyake.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, ndege kubwa zisizo na rubani zenye uzito wa zaidi ya kilo 25 na zilizo na teknolojia zinazohusishwa na usalama wa taifa, ikiwemo kamera za joto na vituo vya kuziendeshea, zitatozwa ushuru wa asilimia 100.
Ndege ndogo zisizo na rubani zitatozwa ushuru wa asilimia 25, huku ushuru huo ukitarajiwa kuanza kutekelezwa Septemba 3.
Utawala wa Trump unasema hatua hiyo inalenga kuhamasisha uzalishaji wa ndege hizo na vipuri vyake nchini Marekani, pamoja na kupunguza utegemezi wa minyororo ya ugavi ya nje, hususan China.
Mamlaka za Marekani zimeeleza kuwa ndege zisizo na rubani zina matumizi ya kibiashara, lakini pia zinaweza kutumika katika shughuli za kijeshi na kiusalama, ikiwemo ufuatiliaji, ukusanyaji wa taarifa nyeti na mashambulizi.
Hatua hiyo huenda ikaongeza gharama kwa waagizaji, watumiaji na kampuni zinazotegemea ndege hizo pamoja na vipuri vinavyotengenezwa nje ya Marekani.
Marekani yasema inaweza kuendelea na zuio la majini dhidi ya Iran bila ukomo
Chanzo cha picha, Getty Images
Marekani imesema inaweza kuendelea na mzingiro wake wa kijeshi dhidi ya Iran kwa muda usiojulikana, huku ikiendelea kuongeza shinikizo la kiuchumi kwa Tehran.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, amesema jeshi la Marekani lina uwezo wa kuendeleza mzingiro huo kwa muda wowote unaohitajika kwa kubadilisha meli za kivita zinazopelekwa katika eneo hilo.
Kauli hiyo inakuja wakati mazungumzo ya kusitisha vita yakikwama, huku usafirishaji wa mafuta duniani ukiathiriwa na mzozo unaoendelea katika eneo la Mlango wa Hormuz.
Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, amesema malengo makuu ya Washington katika mzozo huo ni kuhakikisha bei za nishati zinabaki katika viwango vinavyoweza kumudu Wamarekani, kuzuia Iran kupata silaha za nyuklia na kuhakikisha Marekani inakuwa katika nafasi imara zaidi kimkakati.
Rais Donald Trump amekuwa akisisitiza kuwa Marekani inadhibiti kikamilifu Mlango wa Hormuz, wakati Iran ikisema njia hiyo itaendelea kufungwa hadi masharti yake yatimizwe.
Waziri wa Hazina wa Marekani, Scott Bessent, amesema Washington iko tayari kuchukua hatua za kiuchumi dhidi ya Iran ambazo hazijawahi kutekelezwa katika historia ya kuitenga nchi kiuchumi.
Bessent amesema Marekani itatangaza hatua zaidi wiki ijayo, huku ikilenga kuongeza shinikizo la kiuchumi kwa Tehran.