Nchi na mashirika ya kimataifa zaitaka DRC na Rwanda kuharakisha utekelezaji wa makubaliano ya amani
Wadau wanaohusika katika mchakato wa amani wa Ukanda wa Maziwa Makuu wanazitaka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Rwanda kutekeleza kwa haraka ahadi zao chini ya makubaliano ya amani, huku juhudi zikiendelea kwa lengo la kurejesha utulivu na kutatua suala la makundi yenye silaha mashariki mwa DRC.
Wito huo ulitolewa wakati wa mkutano wa sita wa Mfumo wa Pamoja wa Usalama na Uratibu (JSCM), ambao hufuatilia utekelezaji wa makubaliano ya amani kati ya DRC na Rwanda. Mkutano huo uliwakutanisha wawakilishi wa nchi hizo, pamoja na wawakilishi kutoka Marekani, Qatar, Togo -kama mpatanishi wa Kiafrika-, na Umoja wa Afrika {AU}.
Katika mkutano huo uliofanyika Geneva nchini Uswizi, tarehe 12 na 13 Agosti, DRC na Rwanda zilikubaliana kuendeleza miradi miwili inayolenga kuendelea kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa Makubaliano ya Washington.
Washiriki kwenye mchakato huo wa amani pia walijadili mpango wa DRC wa kuwapokonya silaha na kuwarejesha katika maisha ya kawaida wapiganaji wa kundi la FDLR.
Kundi linalofuatilia mchakato huo kutoka Ulaya na Marekani (ICG) limepokea vyema jinsi utekelezaji wa Makubaliano ya Washington unavyoendelea.
Katika taarifa yake, kundi hilo ambalo linajumuisha Marekani, Ubelgiji, Canada, Denmark, Umoja wa Ulaya, Ufaransa, Ujerumani, Uholanzi, Uswizi, Uswidi na Uingereza lilikaribisha makubaliano yaliyotiwa saini tarehe 28 Julai na kundi la waasi la FDLR (Vikosi vya Kidemokrasia vya Ukombozi wa Rwanda), ambalo lilikubali kuweka chini silaha, kuvunja vikosi vyake na kuwarejesha wapiganaji wake katika jamii.
ICG inazitaka mamlaka za DRC kuandaa mpango madhubuti na ratiba iliyo wazi kwa ajili ya kuliondoa kabisa kundi la FDLR, kwa mujibu wa makubaliano ya amani yaliyopo.
Kundi hilo linasisitiza kuwa serikali ya Kinshasa inapaswa kueleza wazi jinsi wale waliofanya uhalifu watakavyowajibishwa, na kushirikiana kwa karibu na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo (MONUSCO).
Aidha, Linakumbusha kuwa kushirikiana kwa namna yoyote ile na wapiganaji wa FDLR hakulingani na ahadi za DRC chini ya Makubaliano ya Washington.
Hayo yakijiri, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imefungua kesi dhidi ya Rwanda katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki mjini The Hague, ikiitaka mahakama hiyo kuiwajibisha Rwanda kwa madai ya ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa.
Hadi sasa, mamlaka za Rwanda hazijatoa tamko kuhusu kesi hiyo. Hata hivyo, wachambuzi wa sheria za kimataifa wanasema kesi hiyo inaweza kukabiliwa na changamoto za kisheria kuhusu mamlaka ya mahakama kuisikiliza bila ridhaa ya Rwanda au msingi mwingine wa kisheria unaoifunga nchi hiyo. Soma Zaidi: