Washirika wa NATO watangaza pauni bilioni 37 kwa mradi mpya wa makombora

Chanzo cha picha, EPA
Mataifa kumi na mawili, yakiwemo Uingereza, yanatarajiwa kutumia zaidi ya pauni bilioni 37 sawa na dola bilioni 50 za Marekani katika kipindi cha miaka 10 ijayo kutengeneza kombora jipya la masafa marefu kwa ajili ya kuimarisha ulinzi wa Ulaya.
Mradi huo unaojulikana kama Deep Precision Strike umetangazwa rasmi na Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza na unatarajiwa kujadiliwa baadaye Jumatano katika mkutano wa NATO unaofanyika mjini Ankara, Uturuki.
Waziri Mkuu wa Uingereza, Sir Keir Starmer, anahudhuria mkutano huo ambao unatarajiwa kuwa wa mwisho kwake akiwa waziri mkuu.
Anatarajiwa kukosolewa na Rais wa Marekani, Donald Trump, kwa kushindwa kuweka mpango wa kufikia lengo la kutumia asilimia 3.5 ya Pato la Taifa (GDP) kwa matumizi ya ulinzi ifikapo mwaka 2035, ambalo lilikubaliwa na karibu wanachama wote wa NATO mwaka uliopita.
Hata hivyo, Jumatano Sir Keir ataongoza mkutano wa viongozi wapatao 12 kujadili mpango huo mpya wa utengenezaji wa kombora.
Kombora la Deep Precision Strike linaelezwa kuwa miongoni mwa silaha za kisasa zaidi za NATO, likiwa na uwezo wa kushambulia malengo yaliyo umbali wa karibu kilomita 300 kwa usahihi mkubwa, huku uwezo wake ukitarajiwa kuongezwa hadi kufikia kilomita 2,000.
Sir Keir alisema mpango huo unaoongozwa na Uingereza "utasaidia kuwaunganisha washirika wa Ulaya na kuimarisha usalama wa NATO kwa miaka mingi ijayo."
Hata hivyo, kama ilivyo kwa miradi mingine mingi ya kijeshi inayopangwa, kombora la Deep Precision Strike halitarajiwi kuwa tayari kutumika hadi katika miaka ya 2030.
Mnamo Juni, Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, alitangaza mapitio ya miezi sita kuhusu uwepo wa majeshi ya Marekani barani Ulaya.























