Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Iran yasema itajilinda dhidi ya vitisho vya Marekani
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Iran, Waziri wa masuala ya kigeni Abbas Araghchi amesema hali ya sasa ya ukosefu wa usalama katika Mlango wa Hormuz ni matokeo ya moja kwa moja ya kile alichodai kuwa Marekani ilikiuka ahadi zake.
Muhtasari
- Ufaransa na Uhispania zatangaza hali ya dharura kutokana na moto mkubwa wa nyika
- Madagascar yatangaza siku ya maombolezo ya kitaifa baada ya watu sita kuuawa na 200 kutoweka
- Marekani yasema meli iliyokiuka vikwazo dhidi ya Iran ililengwa kwa risasi kwenye injini
- Trump: Utawala wenye nguvu umeondolewa, sasa unaongozwa na kiongozi wa jinsia moja
- Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC Karim Khan aondolewa madarakani
- Ujumbe wa Oman wawasili Iran kujadili kuhusu mgogoro wa Mlango wa Hormuz
- Harry Kane afanya mazungumzo ya kuongeza mkataba Bayern Munich
- Rufaa ya Senegal kupokonywa ubingwa wa AFCON kusikilizwa
- Saudi Arabia yashambulia ngome za Wahouthi Hodeidah
- Trump azitaka China na Urusi kutoingilia vita dhidi ya Iran
- Trump asema Iran bado haiko tayari kufikia makubaliano na Marekani
Moja kwa moja
Na Mariam Mjahid
Umoja wa Mataifa waeleza wasiwasi kuhusu hali ya usalama nchini Syria
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amesema hali ya usalama katika eneo la Golan heights nchini Syria "haikubaliki kabisa," huku akitoa wito wa kuheshimiwa kwa makubaliano ya kimataifa yanayosimamia eneo hilo.
Akizungumza jijini Damascus akiwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, Asad Shaibani, Guterres alisema kinachoendelea katika eneo linalosimamiwa na Umoja wa Mataifa ni jambo lisilokubalika.
Kwa upande wake, Shaibani ameitaka Israel kuyaondoa mara moja na bila masharti majeshi yake kutoka ukanda wa mpito unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa, ambako yaliingia mwaka 2024.
Kauli hizo zinakuja wakati mvutano ukiendelea kuongezeka katika eneo la Golan heights, huku Syria ikiendelea kushinikiza kurejeshwa kwa udhibiti kamili wa eneo hilo na kuheshimiwa kwa mipaka iliyowekwa chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa.
Heche adai viongozi 51 wa CHADEMA wamekamatwa, awataka mawakili kujiandaa
Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, John Heche, amedai kuwa jumla ya viongozi 51 wa chama hicho wamekamatwa katika kanda mbalimbali nchini na baadhi yao wanakabiliwa na mashtaka ya uhaini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza leo Julai 25, 2026, Heche amesema kati ya waliokamatwa, viongozi 23 wanatoka Kanda ya Victoria, 17 Kanda ya Serengeti na 11 Kanda ya Nyasa.
“Viongozi wa CHADEMA kwa Kanda tatu, Kanda ya Victoria wamekamatwa watu 23, Kanda ya Serengeti watu 17 na Kanda ya Nyasa watu 11, jumla kuna viongozi wa CHADEMA 51 wamekamatwa na kubambikizwa kesi kubwa ya uhaini, hapo ni mbali na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma,” alisema Heche.
Katika mkutano huo, Heche aliwataka mawakili wa chama hicho kujiandaa kuwapa msaada wa kisheria viongozi wanaoshikiliwa, akisisitiza kuwa CHADEMA itatumia njia zote za kisheria kuhakikisha wanaachiliwa.
“Hata makande tutakula ili watoke,” alisema.
Mamlaka za serikali hazikuwa zimetoa tamko kuhusu madai ya kukamatwa kwa viongozi 51 wa CHADEMA au tuhuma za kubambikiziwa kesi kufikia wakati wa kuchapishwa kwa taarifa hii.
Kauli za Heche zinaakisi msimamo wa chama hicho na madai hayo hayajathibitishwa na upande wa serikali.
Zelensky: Ukraine yashambulia meli za Urusi zilizokuwa zikisafirisha vifaa vya kijeshi vya Iran
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amesema vikosi vya nchi yake vimeshambulia meli za Urusi katika Bahari ya Kaspia zilizokuwa zikisafirisha vifaa vya kijeshi vinavyohusishwa na Iran.
Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X, Zelensky amesema kuwa meli ya kivita ya Urusi ilikuwa miongoni mwa malengo ya mashambulizi hayo ya masafa marefu yaliyofanyika katika eneo la Bahari ya Kaspia.
Hata hivyo, hakutoa maelezo zaidi kuhusu ukubwa wa mashambulizi hayo au kiwango cha uharibifu uliosababishwa.
Zelensky amesema vikosi vya Ukraine pia vilishambulia kiwanda cha silaha katika mji wa Kirov, ulioko takribani kilomita 1,200 kutoka mpaka wa Ukraine na Urusi. Kwa mujibu wake, kiwanda hicho huzalisha sehemu za silaha zinazotumiwa na Urusi katika vita dhidi ya Ukraine.
Ameongeza kuwa mashambulizi hayo yalilenga pia kiwanda cha kusafisha mafuta mjini Tyumen, kituo cha usafirishaji na usimamizi wa vifaa mjini Yekaterinburg, pamoja na ghala la kuhifadhi mafuta katika mji wa Rostov on Don, yote yakiwa ndani ya Urusi.
Madai hayo ya Zelensky hayajathibitishwa kwa kujitegemea, na Urusi haijatoa tamko rasmi kuhusu mashambulizi hayo.
Soma zaidi;
Iran yasema itajilinda dhidi ya vitisho vya Marekani
Iran imesema iko tayari kulinda maslahi na usalama wake wa taifa dhidi ya kile ilichokitaja kuwa vitisho vya Marekani, huku ikisisitiza haitaruhusu Mlango wa Hormuz kutumiwa kuhatarisha usalama wake.
"Tutalinda maslahi ya wananchi wa Iran, tutalinda haki zao, na tutalinda haki za Iran katika Mlango wa Hormuz na Ghuba ya Uajemi. Haya ni sehemu ya misingi na malengo yetu, na hatumuogopi yeyote," amesema Araghchi.
Ameongeza kuwa Iran haitaacha msimamo wake kwa muda ambao maslahi na haki za wananchi wake zitaendelea kuheshimiwa, akisisitiza kuwa taifa hilo litaendelea kutetea maslahi yake ya kitaifa dhidi ya tishio lolote.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, wakati wa mkutano na mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov, kandokando ya mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Shirika la Ushirikiano la Shanghai unaofanyika nchini Kyrgyzstan.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Iran, Araghchi amesema hali ya sasa ya ukosefu wa usalama katika Mlango wa Hormuz ni matokeo ya moja kwa moja ya kile alichodai kuwa Marekani ilikiuka ahadi zake.
Amesema Iran imeonyesha umuhimu wa diplomasia katika kushughulikia masuala ya kimataifa, lakini wakati huo huo itaendelea kulinda maslahi yake na usalama wa taifa dhidi ya tishio lolote.
Wakati huohuo, Araghchi pia alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na mawaziri wa mambo ya nje wa Misri na Oman kuhusu masuala ya kikanda.
Soma pia:
Ufaransa na Uhispania zatangaza hali ya dharura kutokana na moto mkubwa wa nyika
Zaidi ya watu 220,000 wamelazimika kuhama makazi yao huku moto mkubwa wa nyika ukiendelea kusambaa kusini magharibi mwa Ufaransa na katikati mwa Uhispania, hali iliyosababisha mamlaka za nchi hizo kuchukua hatua za dharura.
Nchini Ufaransa, mamlaka zimeamuru watu karibu 60,000 kuhama maeneo yaliyo karibu na mji wa Bordeaux, na kufanya idadi ya waliohamishwa nchini humo kufikia takribani 200,000 katika maeneo ya Gironde na Landes.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameagiza jeshi kushiriki katika operesheni za uokoaji na kuzima moto huku vikosi vya zimamoto vikikabiliana na moto unaoendelea kusambaa.
Nchini Uhispania, serikali imetangaza hali ya dharura ya kitaifa baada ya moto mkubwa karibu na jiji la Madrid kuzidi uwezo wa vikosi vya zimamoto kuudhibiti. Moto huo ulitokana na kuungana kwa mioto mitatu iliyokuwa ikiwaka magharibi mwa mji mkuu.
Mamlaka zimewaamuru watu 25,000 kuhama makazi yao, huku wengine karibu 40,000 wakitakiwa kubaki ndani ya nyumba zao kwa sababu za usalama.
Rais wa serikali ya jimbo la Madrid, Isabel Díaz Ayuso, amesema huu ni moto mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika eneo hilo. Amesema hali hiyo imesababishwa na mchanganyiko wa joto kali, upepo mkali unaovuma kwa muda mrefu na moto kusambaa kutoka pande mbalimbali kwa wakati mmoja.
Huduma za dharura za Uhispania zimesema moto unaendelea kuelekea maeneo ya Robledo de Chavela na Fresnedillas de la Oliva, yaliyoko takribani kilomita 50 kutoka Madrid.
Mkuu wa idara ya dharura ya jimbo la Madrid, Carlos Novillo, amesema moto huo umefikia kiwango chake cha juu na kwa sasa hauwezi kudhibitiwa moja kwa moja katika baadhi ya maeneo.
"Kwa sasa haiwezekani kupambana moja kwa moja na moto katika baadhi ya maeneo, hivyo tunalenga hatua za kujihami ili kuzuia usiendelee kusambaa," amesema Novillo.
Soma Pia:
Madagascar yatangaza siku ya maombolezo ya kitaifa baada ya watu sita kuuawa na 200 kutoweka
Serikali ya Madagascar imetenga siku ya maombolezo ya kitaifa na mapumziko ya kulipwa kufuatia ongezeko la matukio ya utekaji na kutoweka kwa watu yaliyoitikisa nchi hiyo.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya watu sita waliokuwa wametekwa kuuawa, tukio lililozua hofu kubwa na kufufua wasiwasi kuhusu hali ya usalama nchini.
"Leo ni siku ya kitaifa ya maombolezo na tutaitumia kuombea taifa. Kwa kuwa ni ibada ya kidini na nchi inapitia kipindi kigumu kutokana na matukio yanayoendelea, nitaitikia wito huo. Ninatoa mwito kwa ndugu zangu wote wa harakati za Uamsho wa Kikristo kufika katika Uwanja wa Analakely wakiwa wamevaa mavazi meupe," amesema Rais Randrianirina.
Maombolezo hayo yanawalenga hasa waathiriwa vijana wa visa vya utekaji vilivyogeuka mauaji katika wiki za hivi karibuni.
Serikali imeahidi kuimarisha hatua za usalama huku Rais Kanali Michaël Randrianirina akidai matukio hayo ni jaribio la kuvuruga utulivu wa kisiasa nchini.
Katika siku ya maombolezo, bendera zote zimeshushwa nusu mlingoti, shughuli za burudani zimepigwa marufuku, pamoja na uuzaji wa vileo.
Aidha, Baraza la Makanisa ya Kikristo nchini humo limeandaa ibada ya pamoja katika Uwanja wa Analakely, mbele ya Jengo la Manispaa ya mji mkuu, Antananarivo.
Kwa mujibu wa Waziri Msaidizi anayesimamia Jeshi la Polisi la Kijeshi, Jenerali Bama Marima, jumla ya visa 200 vya watu kutoweka vimeripotiwa katika kipindi cha miezi sita iliyopita, huku sita kati ya hivyo vikihusisha watu waliopatikana wamefariki dunia.
Alisema baadhi ya vifo hivyo vilihusishwa na imani za kishirikina, vingine vilitokana na kulipiza kisasi, kujiua, pamoja na mashambulizi ya uhalifu.
Maafisa wa serikali wanasema sehemu kubwa ya watu walioripotiwa kutoweka walirejea nyumbani salama, huku wengine wakielezwa kuwa walikuwa wameondoka wenyewe au taarifa zao ziliripotiwa mapema kabla ya kuthibitishwa.
Hata hivyo, visa vya watu waliotoweka na baadaye kupatikana wameuawa vimezua hofu kubwa miongoni mwa wananchi, hali iliyowafanya baadhi ya wazazi kuwazuia watoto wao kutoka nje wakati huu wa likizo.
Marekani yasema meli iliyokiuka vikwazo dhidi ya Iran ililengwa kwa risasi kwenye injini
Jeshi la Marekani limetoa maelezo zaidi kuhusu shambulio dhidi ya meli ya kubeba mafuta katika Bahari ya Oman, likisema wafanyakazi wa meli hiyo walijaribu angalau mara nne kukiuka vikwazo vinavyozuia safari kuelekea bandari za Iran kabla ya kulengwa.
Msemaji wa Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM), Tim Hawkins, ameiambia AFP kuwa wafanyakazi wa meli hiyo walionywa mara kadhaa, lakini walipuuza maagizo ya kusimama.
Alisema kuwa baada ya onyo hizo kupuuzwa, wanajeshi wa Marekani walifyatua risasi kulenga sehemu ya injini ya meli ili kuizuia kuendelea na safari.
Hawkins aliongeza kuwa meli hiyo haikuwa tena ikielekea Iran.
Awali, afisa mmoja wa Marekani aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa vikosi vya Marekani viliilenga meli ya mafuta MT Lavin baada ya kudaiwa kujaribu kukwepa vikwazo vilivyowekwa katika bandari za Iran.
Soma Pia:
Trump: Utawala wenye nguvu umeondolewa, sasa unaongozwa na kiongozi wa jinsia moja
Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa wakati wa uongozi wake, "utawala ambao zamani ulikuwa wa kutisha, wenye nguvu na uliokuwa ukiishambulia Marekani bila kukoma uliondolewa madarakani," ingawa hakuitaja Iran moja kwa moja.
Akizungumza katika hafla ya Chama cha Waandishi wa Habari wa Ikulu ya White House, Trump alisema viongozi wa zamani wa utawala huo waliondolewa na sasa nchi hiyo inaongozwa na "dikteta ambaye anashiriki mahusiano ya jinsia moja anayekabiliwa na migogoro ya ndani."
Kauli za Trump zinaonekana kuirejelea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Mojtaba Khamenei.
Hata hivyo, hakutoa ushahidi wa kuunga mkono madai hayo, na hapo awali pia amewahi kutoa madai yanayofanana kuhusu kiongozi wa Iran.
Unaweza kusoma;
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC Karim Khan aondolewa madarakani
Nchi wanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, zimepiga kura kumwondoa Karim Khan katika wadhifa wa Mwendesha Mashtaka Mkuu kufuatia tuhuma za utovu wa nidhamu wa kingono.
Uamuzi huo ulipitishwa Ijumaa kwa kura 82 za kuunga mkono kuondolewa kwake.
Khan, ambaye alichaguliwa kuwa mwendesha mashtaka wa tatu wa ICC mwaka 2021, alikuwa amesimamishwa kazi mwezi uliopita wakati uchunguzi ukiendelea.
Mnamo Juni, chombo cha usimamizi wa mahakama hiyo kilihitimisha kuwa Khan alifanya ukiukaji mkubwa wa majukumu yake na utovu mkubwa wa nidhamu kwa kuhusishwa na uhusiano wa kingono usiofaa na mfanyakazi wa ngazi ya chini wa ICC.
Pia alidaiwa kujaribu kumzuia mfanyakazi huyo kuwasilisha malalamiko dhidi yake.
Hata hivyo, Khan amekanusha mara kwa mara tuhuma zote zinazomkabili.
Mawakili wake wameeleza kuwa kusimamishwa kwake kulikuwa kinyume cha sheria, hakukufuata taratibu za haki na hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuunga mkono madai hayo.
Kuondolewa kwa Khan kunakuja wakati ICC ikikabiliwa na changamoto kubwa zinazotishia mustakabali wake.
Uchunguzi dhidi yake umeiweka mahakama hiyo chini ya uangalizi mkali, umeongeza migawanyiko ya ndani na umeendelea sambamba na kile kinachoelezwa kuwa juhudi zisizo za kawaida za kuidhoofisha au hata kuivunja mahakama hiyo.
Wafuasi wa ICC wanaonya kuwa mgogoro huo unaweza kuidhoofisha mahakama hiyo na kupunguza uwezo wake wa kushughulikia uhalifu mkubwa wa kimataifa, ikiwemo uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.
Soma Pia:
Ujumbe wa Oman wawasili Iran kujadili kuhusu mgogoro wa Mlango wa Hormuz
Ujumbe kutoka Oman umewasili mjini Tehran kwa mazungumzo yanayohusu usimamizi wa usafiri wa meli katika Mlango wa Hormuz, kwa mujibu wa Shirika rasmi la Habari la Iran, IRNA.
IRNA ilisema lengo la ziara hiyo ni “kuandaa utaratibu unaofaa wa kusimamia harakati za meli katika Mlango wa Hormuz.”
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na mwenzake wa Oman, Badr al Busaidi, Ijumaa jioni.
Hata hivyo, maelezo ya mazungumzo hayo hayajawekwa wazi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Iran inalenga kuratibu kwa karibu na Oman kuhusu masuala yanayohusu Mlango wa Hormuz, ambao ni njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta na bidhaa duniani.
Ziara ya ujumbe wa Oman mjini Tehran inafanyika wakati vita kati ya Marekani na Iran vikiendelea, huku kukiwa na juhudi mpya za kufufua mazungumzo kati ya mataifa hayo mawili.
Soma Pia:
Harry Kane afanya mazungumzo ya kuongeza mkataba Bayern Munich
Nahodha wa England, Harry Kane, yuko katika mazungumzo na Bayern Munich kuhusu kuongeza mkataba wake na mabingwa hao wa Ujerumani.
Mkataba wa Kane unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu ujao, lakini Bayern Munich ina nia ya kumbakisha mshambuliaji huyo kwa muda mrefu zaidi.
Kane pia anafahamu kuwa uongozi wa klabu hiyo unataka asaini mkataba mpya, huku taarifa zikieleza kuwa makubaliano yanaweza kukamilika katika wiki zijazo.
Mshambuliaji huyo alijiunga na Bayern Munich mwaka 2023 akitokea Tottenham Hotspur kwa ada ya pauni milioni 86.
Tangu kuwasili kwake, Kane ameisaidia Bayern kutwaa mataji mawili ya Bundesliga na Kombe moja la Ujerumani.
Pia alikuwa na mchango mkubwa kwa England katika Kombe la Dunia, akifunga mabao sita, huku akiwa ameifungia Bayern Munich jumla ya mabao 146 katika mechi 134 tangu ajiunge na klabu hiyo.
Hata hivyo, ripoti zinaeleza kuwa Barcelona inaendelea kufuatilia hali yake, wakati baadhi ya klabu za Saudi Arabia zikisubiri fursa ya kumsajili pindi mkataba wake utakapomalizika.
Soma Zaidi:
Rufaa ya Senegal kupokonywa ubingwa wa AFCON kusikilizwa
Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo imepanga Oktoba 8 kuwa tarehe ya kusikiliza rufaa ya Senegal dhidi ya uamuzi wa kupokonywa ubingwa wa Mataifa ya Afrika wa mwaka 2025.
Shirikisho la Soka Afrika lilibatilisha ushindi wa Senegal na kutangaza Morocco kuwa mabingwa wa mashindano hayo yaliyomalizika Januari, licha ya Senegal kushinda mchezo huo kwa bao 1 kwa 0.
Mzozo ulizuka mwishoni mwa mchezo wakati Morocco ilipopewa penalti huku matokeo yakiwa bado 0 kwa 0.
Wachezaji wa Senegal walitoka uwanjani kupinga uamuzi huo.
Baada ya mchezo kusimama kwa dakika 17, wachezaji wa Senegal walirejea uwanjani, na Brahim Diaz akaifungia Morocco penalti waliyopewa.
Mnamo Machi 25, Senegal iliwasilisha rufaa katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo ikitaka uamuzi wa CAF ubatilishwe na kombe la ubingwa lirejeshwe kwao.
Katika uamuzi wake, CAF ilitangaza Morocco kuwa washindi kwa mabao 3 kwa 0 dhidi ya Senegal.
Sasa Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo itasikiliza rufaa hiyo Oktoba 8 kabla ya kutoa uamuzi wa mwisho kuhusu nani anayestahili kutambuliwa rasmi kama bingwa wa AFCON 2025.
Soma Zaidi:
Saudi Arabia yashambulia ngome za Wahouthi Hodeidah
Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia umetangaza kuwa operesheni yake dhidi ya Wahouthi imekamilika baada ya kushambulia kambi za kijeshi za kundi hilo kufuatia mashambulizi dhidi ya meli za kibiashara katika Bahari ya Shamu.
Msemaji wa muungano huo, Turki al Maliki, alisema kupitia taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X kuwa Wahouthi walilenga meli za kibiashara katika Bahari ya Shamu, jambo lililochochea muungano kujibu kwa kile alichokiita “jibu kali na la kuamua.” Kwa mujibu wa Al Maliki, mashambulizi hayo yalilenga maeneo yaliyokuwa
Kwa mujibu wa chanzo cha kiusalama kilichozungumza na AFP, mashambulizi hayo yalilenga maeneo ya kijeshi na ngome zinazotumiwa na Wahouthi.
Runinga ya Al Masirah inayomilikiwa na Wahouthi ilisema maeneo kadhaa katika mkoa wa Hodeidah yalishambuliwa, huku wakazi wa eneo hilo wakithibitisha kusikia milipuko mikubwa.
Kundi la Wahouthi wa Yemen limetishia kulipiza kisasi dhidi ya Saudi Arabia siku ya Jumamosi, likiishutumu nchi hiyo kwa kulenga miundombinu ya kiraia. Hatua hiyo inaashiria kuongezeka kwa mivutano katika vita vinavyoendelea katika eneo hilo.
Aidha, kundi hilo limetishia kulenga njia kuu za usafiri wa baharini za Saudi Arabia.
Mashambulizi hayo yanajiri wakati mvutano wa usalama katika eneo hilo ukiendelea kuongezeka.
Hivi karibuni Wahouthi walitangaza kuanzisha mzingiro wa baharini dhidi ya Saudi Arabia na kudai kulenga meli zinazohusishwa na taifa hilo.
Soma Zaidi:
Trump azitaka China na Urusi kutoingilia vita dhidi ya Iran
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema marais wa China na Urusi wamemhakikishia kuwa hawataiuzia Iran silaha.
Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa Truth Social, Trump alisema Rais wa China, Xi Jinping, alimweleza wakati wa mkutano wao wa hivi karibuni mjini Beijing kuwa China haitatoa wala kuuza silaha kwa Iran kwa hali yoyote.
“Katika mkutano wetu wa hivi karibuni mjini Beijing, Rais Xi aliniambia kwamba hatatoa wala kuuza silaha kwa Iran kwa hali yoyote. Hilo linajumuisha pia kampuni za China,” aliandika Trump.
Trump aliongeza kuwa Rais wa Urusi, Vladimir Putin, pia alimpa ahadi kama hiyo.
Akizungumzia msaada wa kijeshi kwa Ukraine, Trump alisema: “Watu wanafikiri siuzi silaha kwa Ukraine. Ninaziuza kwa nchi za NATO. Wanalipa bei kamili kwa silaha hizo na sijui wanazifanyia nini baadaye.”
Trump pia alisema haamini kuwa China na Urusi zinahusika moja kwa moja katika vita dhidi ya Iran.
“Mataifa hayo mawili makubwa ambayo mara nyingi hutajwa kuhusishwa na Iran, sidhani kama yanahusika. Kama yangekuwa yanahusika, hakika isingekuwa kwa maslahi yao wenyewe,” alisema.
Hata hivyo, China na Urusi hazijatoa tamko rasmi kuthibitisha kauli za Trump kuhusu madai hayo.
Soma Pia
Trump asema Iran bado haiko tayari kufikia makubaliano na Marekani
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema Marekani na Iran zinaendelea na mazungumzo ya kutafuta suluhisho la mgogoro kati ya mataifa hayo mawili, lakini akasisitiza kuwa Tehran bado haiko tayari kufikia makubaliano.
Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu ya White House siku ya Ijumaa, Trump alisema: “Tunazungumza nao. Nafikiri wana nia ya dhati, na wako makini zaidi kuliko wakati mwingine wowote, lakini hilo halimaanishi tutafikia makubaliano. Tutaona kitakachotokea.”
Kuhusu makubaliano ya ushirikiano wa nyuklia wa kiraia kati ya Marekani na Saudi Arabia, Trump alisema hatasonga mbele na utekelezaji wa makubaliano hayo hadi Saudi Arabia itakapokubali kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel kwa kujiunga na Makubaliano ya Abraham.
Kauli hiyo inajiri siku chache baada ya Marekani na Saudi Arabia kutangaza makubaliano yatakayoiruhusu Riyadh kurutubisha urani na kujenga mitambo ya nyuklia kwa kutumia teknolojia ya Marekani, bila kufuata utaratibu wa ukaguzi wa haraka wa Umoja wa Mataifa ambao Washington imekuwa ikisisitiza utekelezwe kwa Iran.
Hadi sasa, Saudi Arabia haijakubali kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Israel, jambo linalobaki kuwa moja ya vikwazo vikuu katika mazungumzo kati ya pande hizo.
Unaweza kusoma;
Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya tarehe 25/07/2026.