Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Rais wa Urusi, Vladimir Putin, akutana na Rais wa China Xi Jinping

Rais wa Urusi, Vladimir Putin, amekutana na Rais wa China Xi Jinping siku chache tu baada ya ziara ya Rais wa Marekani, Donald Trump.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Beldeen Waliaula & Mariam Mjahid

  1. Wanandoa wa Uingereza waliofungwa Iran waanza kususia kula gerezani

    Familia ya wanandoa wa Uingereza waliofungwa nchini Iran baada ya kushutumiwa kwa ujasusi imesema wawili hao wameanza kususia kula.

    Lindsay Foreman na Craig Foreman walikamatwa walipokuwa wakivuka Iran kwa pikipiki mnamo Januari 2025, na baadaye walihukumiwa kifungo cha miaka kumi gerezani.

    Wakati huo huo, raia wa Iran mwenye ukaazi wa kudumu nchini Marekani ameachiwa huru na kurejea Marekani baada ya kuzuiliwa kwa miaka kumi nchini Iran.

    Shahab Dalili alikuwa ameshtakiwa kwa kushirikiana na serikali hasimu.

  2. Iran yaonya vita vitaenea nje ya Mashariki ya Kati iwapo itashambuliwa tena

    Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi la Iran IRGC limetoa taarifa likionya kuwa iwapo Marekani na Israel wataishambulia Iran tena, vita vitaenea nje ya eneo la Mashariki ya Kati.

    Taarifa hiyo ya kijeshi ya Iran imetolewa kujibu vitisho vya mashambulizi mapya vilivyotolewa na Rais wa Marekani Donald Trump pamoja na baadhi ya maafisa wa Israel, waliodai kuwa hatua mpya dhidi ya Iran inaweza kusababisha vita kuenea katika maeneo mengi duniani.

    Jeshi hilo limesema mashambulizi yoyote dhidi ya Iran yatakabiliwa na “majibu makali.”

    Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema kupitia mtandao wa X kuwa Iran imejifunza mengi kutokana na vita vya karibuni na sasa ina uwezo mkubwa zaidi wa kijeshi.

    “Marekani itashangazwa iwapo itaingia vitani nasi tena,” amesema Araghchi.

    Katika ujumbe wake mwingine, amesema Iran imefanikiwa kuangusha ndege ya kivita ya Marekani aina ya F 35, akidai hatua hiyo imeonyesha uwezo mpya wa vikosi vya Iran.

    “Kwa sababu ya mafunzo tuliyopata na maarifa tuliyojifunza, Marekani itakumbana na mshangao mwingine,” ameongeza.

    Kauli hiyo imejiri siku moja baada ya Rais Trump kusema alikuwa amesitisha mpango mkubwa wa mashambulizi dhidi ya Iran kufuatia ombi kutoka kwa viongozi wa Qatar, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Uingereza yaondoa vikwazo dhidi ya mafuta ya Urusi

    Serikali ya Uingereza imeondoa baadhi ya vikwazo dhidi ya mafuta ya Urusi,huku bei ya mafuta ikipanda nchini humo.

    Agizo hilo limeanza kutekelezwa hii leo, na inaashiria hofu inayoongezeka kuhusu upatikanaji wa mafuta kutokana na kuzuizi kilichowekwa katika Mlango bahari wa Hormuz tangu kuanza kwa vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

    Vikwazo dhidi usafirishaji wa gesi ya asili ya Urusi iliyoyeyushwa (LNG) pia vimeondolewa.

    Hatua kama hiyo iliyochukuliwa na Marekani hivi majuzi ilikosolewa vikali.

    Bei za mafuta ya ndege barani Ulaya zimeongezeka mara mbili Zaidi baada ya vita kuanza, huku bei ya mafuta katika vituo za mafuta zikipanda.

    Mashirika kadhaa ya ndege nchini Uingereza na duniani kote yamehairisha safari zake na kuongeza bei za tiketi kutokana na kupanda kwa bei mafuta ya ndege.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Meli za mafuta za China zapita katika Mlango Bahari wa Hormuz baada ya miezi miwili

    Meli mbili za mafuta za China zimeweza kupita katika Mlango bahari wa Hormuz hii leo, baada ya kuzuiliwa kwa Zaidi ya miezi miwili.

    Hii inaashiria dalili kuwa mkwamo katika mlango huo wa bahari umetatuliwa.

    Rais wa Marekani Donald Trump, hapo jana, alidokeza kuwa vita hivyo viko karibu kuisha na wako karibu kuafikia makubaliano

    Trump aidha alisema aliagiza kusitishwa kwa mashambulizi mapya dhidi ya Iran, baada ya kupokea ombi kutoka mataifa ya Ghuba.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Baada ya miaka 127, Bournemouth kucheza michuano ya Ulaya kwa mara ya kwanza

    Licha ya kutoka sare ushindi nyumbani dhidi ya Manchester City waliopata bao la kusawazisha la dakika za jioni kupitia Erling Haaland, Bournemouth bado wameandika historia kubwa kwa kufuzu michuano ya Ulaya kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo.

    Sare ya bao 1-1 dhidi ya City katika Uwanja wa Vitality usiku wa Jumanne imeihakikishia Bournemouth nafasi ya kushiriki michuano ya Europa League msimu ujao.

    Hata hivyo, bado kuna uwezekano kwa Bournemouth kufuzu hadi Ligi ya Mabingwa Ulaya kulingana na matokeo ya mechi za mwisho za msimu.

    Iwapo Aston Villa wataifunga Freiburg katika fainali ya Europa League itakayochezwa Jumatano usiku, Bournemouth kuna uwezekano ku kupata nafasi hiyo.

    Villa wakitwaa ubingwa huo na kumaliza nafasi ya tano kwenye msimamo wa EPL, watapata tiketi ya moja kwa moja ya Ligi ya mabingwa League kama mabingwa wa Europa League. Hivyo itafanya nafasi ya ziada ya timu ya Ligi kuu England (EPL) kwenda kwa timu itakayomaliza nafasi ya sita, jambo ambalo linaweza kuinufaisha Bournemouth.

    Ili hilo litokee, Aston Villa wanapaswa kupoteza dhidi ya Manchester City huku Liverpool wakishinda nyumbani dhidi ya Brentford. Kwa upande wa Bournemouth, watakuwa na uhakika wa kumaliza nafasi ya sita iwapo wataepuka kupoteza dhidi ya Nottingham Forest au Brighton wakashindwa kuifunga Manchester United.

    Bado kuna uwezekano mwingine mdogo wa Bournemouth kufuzu Ligi ya mabingwa Ulaya ikiwa Liverpool watapoteza kwa kipigo kikubwa katika mchezo wao wa mwisho huku Bournemouth wakishinda kwa mabao mengi.

    Kwa mfano, Liverpool wakifungwa mabao 3-0 na Bournemouth kushinda 4-0, tofauti ya mabao inaweza kuibeba Bournemouth. Pia njia ya kipekee zaidi inaweza kutokea ikiwa Liverpool wakifungwa 1-0 na Bournemouth kushinda 5-0.

    Katika mazingira hayo, timu hizo zinaweza kuwa sawa kwa kila kitu hadi kuhitaji mechi ya mchujo maalum ya mwisho wa msimu kuamua nani afuzu ligi ya mabingwa.

    Wakati Arsenal tayari wametwaa ubingwa wa EPL kwa mara ya kwanza baada ya miaka 22, bado kuna ushindani mkubwa katika michezo ya mwisho ya msimu huku nafasi za kufuzu mashindano ya Ulaya pamoja na vita vya kushuka daraja vikiwa bado havijaamuliwa.

    Katika vita vya kushuka daraja, West Ham wanahitaji ushindi dhidi ya Leeds United ili kujiweka kwenye nafasi ya kuendelea kubaki EPL.

    Tottenham pia wako kwenye presha kubwa huku wakihitaji ushindi dhidi ya Everton ili kuhakikisha hawashuki daraja.

    Chelsea, Brighton, Brentford na Sunderland nazo bado zinapambana kuwania nafasi za michuano ya Ulaya kabla ya pazia la msimu kufungwa rasmi Jumapili hii.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Beijing na Moscow zinafaa kushirikiana zaidi, Xi amwambia Putin

    Katika hotuba yake, Rais Xi Jinping wa China, amemwambia Rais wa Urusi Vladimir Putin, kwamba nchi hizo mbili zinapaswa kusaidiana katika maendeleo na kufufua uchumi wa mataifa hayo.

    Putin naye katika katika hotuba yake, amesema uhusiano kati ya Urusi na China ni wa viwango vya juu na unaonyesha “mwenendo mzuri” kati ya mataifa hayo mawili.

    Putin aliisifia taifa lake kuwa “muuzaji wa nishati anayeaminika” licha ya mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati.

    China na Urusi pia wameongeza muda wa miaka mitano kwa mkataba walionao wa kushirikiana kibiashara na kijeshi.

    Viongozi hao wawili pia wamejadili vita Mashariki ya Kati, Rais Xi akisema kuwa imefikia wakati muhimu wa kusitisha mashambulizi na kupatikana kwa amani.

    Putin amemwalika Rais Xi Jinping kutembelea Urusi mwaka ujao, akisisitiza kuwa uhusiano kati ya Beijing na Moscow ndiyo “unachangia utulivu wa dunia.”

    Xi alikuwa Urusi mara ya mwisho mwezi Mei mwaka uliopita.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Rais Trump atishia kuishambulia Iran, iwapo makubaliano hayataafikiwa

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa alikuwa amebakisha saa moja tu, kabla ya kuidhinisha shambulio jipya dhidi ya Iran, kisha akabadili uamuzi huo, baada ya kupokea ombi kutoka kwa mataifa ya Ghuba asitishe mashambulizi, huku akionya kuwa Marekani inaweza kuanzisha mashambulizi mapya dhidi ya Iran siku chache zijazo.

    Trump amesisitiza kuwa viongozi wa Iran “wanatakiwa kuafikia makubaliano kwa haraka,” na kuongezea kuwa shambulio jipya la Marekani linaweza kufanyika siku chache zijazo iwapo hakutakuwa na makubaliano yaliyoafikiwa.

    “Ninamaanisha ndani ya siku mbili au tatu, labda Ijumaa au Jumamosi au Jumapili, au mwanzoni mwa wiki ijayo, kwa sababu hatuwezi kuiruhusu Iran kuwa na silaha ya nyuklia.”

    Trump pia alisema kuwa Rais wa China Xi Jinping, aliahidi kutoipa jeshi la Iran silaha yoyote.

    Jeshi la Iran nalo limejibu semi za Trump na kusema pia wako tayari kurejea kutekeleza mashambulizi.

    Pia unaweza kusoma:

  8. Waziri wa Israel Bezalel Smotrich asema mwendesha mashtaka wa ICC anataka akamatwe

    Waziri wa Fedha kutoka mrengo wa kulia nchini Israel, Bezalel Smotrich, amesema amepewa taarifa kwamba waranti ya kukamatwa kwake imetolewa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC.

    Smotrich hakusema ni mashtaka gani anayokabiliwa nayo, lakini alieleza hatua hiyo kuwa “tangazo la vita” na kuinyooshea lawama mamlaka ya Palestina.

    Waranti ya mtu kukamatwa na mahakama ya ICC huwa suala la siri na lazima iidhinishwe na majaji wa mahakama hiyo.

    Mahakama hiyo aidha imekanusha kutoa waranti ya kukamatwa kwa viongozi watano wa Israel.

    Smotrich ambaye ana mamlaka makubwa juu ya sera za Israel katika eneo linalokaliwa kimambavu la Ukingo wa Magharibi, aliagiza kubomolewa kwa Kijiji maarufu cha Waaplestina cha Khan al-Ahmar karibu na Jericho.

    Afisa mmoja wa Mamlaka ya Palestina amelaani agizo hilo na kulitaja kama “hatua hatari ya kuongeza mvutano”.

    Mwaka 2018, Mahakama Kuu ya Israel iliidhinisha amri ya kuwafurusha wakazi wa Khan al-Ahmar, lakini amri hiyo haijatekelezwa baada ya mahakama ya ICC kutoa onyo kuwa ni ukiukwaji wa sheria za kimataifa.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Watu 19 wauawa katika mashambulizi ya anga Lebanon

    Mashambulizi ya angani yaliyotekelezwa na Israel, imewauwa takriban watu 19 kusini mwa Lebanon, kulingana na wizara ya afya ya taifa hilo.

    Kumi kati ya waliouawa ni watoto watatu na wanawake watatu ambao walifariki katika shambulio moja nyumbani kwao, katika mji wa Dier Qanoun.

    Lebanon ilianza kushambuliwa na Israel tarehe 2 mwezi Machi, baada ya kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran, kuishambulia Israel, kama hatua ya kulipiza kisasi kifo cha aliyekuwa kiongozi mkuu wa Iran Ali Khamenei.

    Mashambulizi haya yanajiri siku chache tu, baada ya mataifa hayo mawili kukubaliana kuongeza muda wa kusitisha mapigano kwa siku 45, ili kutoa muda kwa mazungumzo kufanyika.

    Licha ya makubaliano hayo ya kusitisha mapigano, Israel na kundi la Hezbollah wamekuwa wakishambuliana.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Ghana kuikabili Ivory Coast katika mechi za kufuzu Afcon 2027

    Ghana wamepangwa pamoja na Ivory Coast katika kundi ambalo linaonekana kuwa gumu kwenye mechi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027.

    Black Stars hawakuwa kwenye chungu cha kwanza cha timu zilizopanda daraja kwenye droo hiyo, baada ya kushuka kwenye viwango vya dunia kufuatia kushindwa kufuzu kwa mashindano yaliyopita yaliyofanyika Morocco mwezi Disemba na Januari.

    Mabingwa hao wawili wa Afrika Magharibi watakutana katika Kundi C, ambako pia watacheza dhidi ya Gambia, waliotikisa kwa kufika robo fainali ya Afcon 2021 kwenye ushiriki wao wa kwanza, pamoja na Somalia.

    “Kwa nini kila mara sisi? Hili ni kundi gumu,” alisema mchezaji wa zamani wa Ivory Coast, Max-Alain Gradel, ambaye aliisaidia timu ya Elephants kutwaa ubingwa nyumbani mwaka 2022 na alikuwa mmoja wa wasaidizi kwenye droo iliyofanyika Cairo.

    “Lakini tutafanya kila tuwezalo kufuzu. Nina imani na timu hivyo hakuna tatizo.”

    Kenya, Tanzania na Uganda zitakuwa wenyeji wa pamoja wa Afcon ijayo, itakayofanyika kuanzia tarehe 19 Juni hadi 17 Julai 2027.

    Timu 48 zinazowania kufuzu kwa fainali zimegawanywa katika makundi 12 yenye timu nne kila moja, ambapo timu mbili za juu kutoka kila kundi zitafuzu baada ya raundi sita za mechi.

    Hata hivyo, mambo yanakuwa magumu zaidi kwa sababu wenyeji watatu tayari wamehakikishiwa nafasi kwenye mashindano hayo, hivyo ni timu moja tu nyingine kutoka kwenye makundi yao itakayopata tiketi ya kufuzu.

    Nigeria, Afrika Kusini na Tunisia zina nafasi ndogo ya kufanya makosa baada ya kupangwa pamoja na mmoja wa wenyeji hao watatu. Kenya itacheza dhidi ya Eritrea, ambao wanarejea kwenye mechi za kufuzu Afcon kwa mara ya kwanza tangu mchujo wa mashindano ya 2008, pamoja na Guinea na Afrika Kusini katika Kundi A.

    Kwingineko, mabingwa wa kihistoria wa Afcon wenye mataji saba, Misri, wamepangwa pamoja na Angola, Malawi na Sudani Kusini.

    Raundi nne za kwanza za kufuzu zitachezwa mwezi Septemba, Oktoba na Novemba mwaka huu, huku mechi mbili za mwisho zikitarajiwa kuchezwa mwezi Machi mwaka ujao.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Rais Putin aanza ziara ya kitaifa nchini China

    Rais wa Urusi, Vladimir Putin, yuko mjini Beijing kwa ziara ya kitaifa ambapo anatarajiwa kufanya mazungumzo na Rais wa China, Xi Jinping, hii leo.

    Putin, aliwasili China usiku wa kuamkia leo, na anatarajiwa kujadili “masuala muhimu” yanayohusu Urusi na China,kulingana na taarifa iliyotolewa na ikulu ya Kremlin.

    Ziara ya Putin, ambayo ndiyo safari yake ya kwanza nje ya taifa lake mwaka huu wa 2026, imejiri siku chache tu baada ya ziara ya Rais wa Marekani, Donald Trump, nchini China, ambapo walijadili na Rais Xi masuala mbalimbali ya kibiashara ikiwemo vita vya Iran.

    Wizara ya Mambo ya Kigeni ya China imesema ziara ya Putin inalenga kuimarisha zaidi uhusiano wa mataifa hayo mawili.

    Pia unaweza kusoma:

  12. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja Jumatano ya leo