'Wakuue au ujiue': Manusura waelezea eneo la genge la Mexico ambako mabaki ya binadamu yalipatikana

Chanzo cha picha, Getty Images
Mara ya kwanza dunia kushuhudia kilichokuwa ndani ya Rancho Izaguirre ilikuwa kupitia matangazo ya moja kwa moja ya Facebook yaliyofanywa na wazazi wa vijana waliopotea katika magharibi mwa Mexico. Baada ya kupata taarifa kuhusu uwezekano wa kuwepo kwa kaburi la watu wengi, kundi hilo lilikwenda kwenye ranchi hiyo likitumaini kupata dalili yoyote ya wapendwa wao waliopotea.
Walichokikuta kilikuwa mamia ya jozi za viatu, nguo, masanduku ya kusafiria na mabegi ya mgongoni, vikiwa vimetupwa baada ya wamiliki wake kudhaniwa kuuawa. Ranchi hiyo ilionekana kuwa kituo cha uajiri cha genge la uhalifu la Jalisco New Generation Cartel (CJNG), ambapo mauaji yalikuwa yakifanyika kwa utaratibu. Ugunduzi wake mwezi Machi 2025 uliishtua Mexico na kuvutia umakini wa kimataifa.
"Ilikuwa kana kwamba ni kituo cha kazi ya bei nafuu kwa ajili ya genge hilo," anasema Sandra Romandía, ambaye alizungumza na manusura kwa ajili ya kitabu chake Witnesses to Horror: The Truth They Tried to Hide at Rancho Izaguirre.
"Jambo la kwanza [genge] walilofanya ni kuwapa kazi ya aina fulani. Inaweza kuwa kama mhandisi wa kompyuta, mlinzi, dereva au mfanyakazi wa kawaida,kila mara wakiahidi mshahara mzuri. Hii ilifanywa kupitia WhatsApp, Facebook na mitandao mingine ya kijamii," Romandía aliiambia BBC News Mundo.
"Vijana walipitia majaribio fulani kwa simu au kwa ujumbe, na mtu alipochaguliwa waliambiwa: 'Tutakutumia tiketi ya basi kwenda kituo cha mabasi cha Tlaquepaque (Guadalajara),' ambacho ni muhimu sana, ni miongoni mwa vituo vikubwa zaidi katika jimbo la Jalisco.
"Walipofika huko, walichukuliwa na Uber au teksi kuwapeleka kwenye 'ofisi za kampuni'.
"Nini kilitokea? Gari hilo lililodaiwa kuwa Uber,ambalo kwa kweli lilikuwa gari la kawaida tu, lilipowasili, walitekwa nyara, kutishwa kwa silaha, kunyang'anywa simu zao, na kusafirishwa kwenda Rancho Izaguirre au ranchi nyingine kwa ajili ya kulazimishwa kufundishwa.
"Mtu yeyote aliyepinga aliuawa papo hapo."

Chanzo cha picha, GBJ
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Manusura walielezea hali ya kikatili sana katika ranchi hiyo, ikiwa ni pamoja na kulazimishwa kupigana wao kwa wao au kutesana huku wengine wakitazama.
"Walilazimika kuua watu wengine, kukata viungo vya miili ya watu, kuchoma miili, kula nyama ya binadamu, na kuishi wakiwa wamefungwa minyororo," anasema Romandía.
"Walipaswa kufuata amri kikamilifu: muda wa kwenda chooni, kuvaa suruali, kuvua nguo. Kama waliambiwa wafanye push-up 50, walipaswa kufanya, vinginevyo walijua wangepigwa au hata kuuawa. Wanasimulia jinsi, ghafla, wao wenyewe walivyogeuka kuwa burudani kwa viongozi wa genge hilo."
Ushuhuda wa wanaume na wanawake wanaodai kuwa walikuwepo Rancho Izaguirre unaeleza wazi kuwa mauaji na kutoweka kwa miili ya vijana wengi waliodanganywa kwenda huko kwa ahadi ya kazi rasmi vilifanyika huko.
"Kuna njia mbili tu za kutoka hapa: ama wakuue au ujiue," anasema mmoja wa waliochangia katika kitabu cha Romandía, akielezea jinsi vijana waliokwenda huko walivyofikishwa kwenye hali ya mbaya kabisa.
Mwingine anaelezea hali za kinyama na zinazodhalilisha utu, jinsi walivyoajiriwa kwa hila na kulazimishwa, kutekwa nyara na kuteswa, akiongeza kuwa anaamini kati ya watu 100 waliokuwa kwenye kundi lake, ni takriban 30 tu waliokoka.
Baadaye anaelezea jinsi alivyoshuhudia kundi jipya likifika, naye alikuwa na silaha, na akasema:
"Ningeweza kufanya jambo la kuwatetea, lakini sikufanya chochote kwa sababu nilijua naweza pia kupigwa kama ningewasaidia."
"Hivyo alijifanya kama ni mfuasi mwingine tu wa genge hilo la kikatili ili kuishi," Romandía anaeleza, "lakini kwa ndani alikuwa anafikiria: 'Ninawezaje kuwaokoa watu hawa?'"

Chanzo cha picha, Getty Images
Raúl Servín, mmoja wa wazazi katika kundi linaloitwa Guerreros Buscadores de Jalisco (GBJ) , yaani "Watafutaji Mashujaa wa Jalisco", aliiambia BBC Mundo wakati eneo hilo lilipogunduliwa kuwa walipata maganda ya risasi na magazini za bunduki, pamoja na makaburi yaliyofichwa na dalili za matumizi ya moto.
Hata hivyo, Ofisi ya mwanasheria mkuu, ambayo ilichukua jukumu la uchunguzi huo, imekanusha vikali kuwepo kwa ushahidi wa "tanuri za kuchomea miili" au aina yoyote ya uteketezaji mkubwa wa mabaki ya binadamu.
"Uchunguzi umebaini wazi na bila shaka kwamba eneo hilo lilitumika kama kambi ya mafunzo," FGR ilisema tarehe 5 Machi mwaka uliopita.
Tangu wakati huo, watu 47 wanaohusishwa na ranchi hiyo wamekamatwa, na washtakiwa 10 wamehukumiwa kifungo cha miaka 141 kila mmoja jela kwa kutoweka na mauaji ya watu watatu katika ranchi hiyo.
Meya wa Teuchitlán, pia amekamatwa na anashutumiwa kuwa mshirika wa uhalifu wa kupangwa.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Inaonekana kana kwamba mamlaka zinajaribu kudhibiti simulizi ya kile kilichotokea," anasema Romandía.
"Daima kulikuwa na ahadi kutoka kwa Ofisi ya mwanasheria mkuu, kufafanua kesi hii, lakini bila kutaka kuthibitisha au kusema kama kweli kulikuwa na tanuri za kuchomea miili au mabaki ya mifupa ya binadamu iliyochomwa , wakidai ili kutoathiri uchunguzi.
"Tatizo ni kwamba hawakuwahi kuweka wazi hadharani. Na wakati fulani, mwendesha mashtaka Alejandro Gertz Manero alikiri kuwa kulikuwa na mwili mmoja ulioteketezwa, ilhali kwa picha tulizoona kulikuwa na vipande vingi vilivyochomwa ambavyo vinaweza kabisa kuwa vya binadamu.
"Baadhi ya wataalamu wa kisayansi wanasema kuwa uchomaji wa miili huenda ulikuwa ukifanyika hapo kwa zaidi ya miaka 10."
BBC Mundo iliomba mahojiano na ofisi ya mwanasheria mkuu, kuhusu kesi hiyo, lakini haikuwa imepata majibu kufikia wakati makala haya yalipochapishwa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Zaidi ya watu 130,000 wameripotiwa kutoweka nchini Mexico. Karibu matukio yote ya kutoweka yamejitokeza tangu mwaka 2007, wakati rais wa wakati huo Felipe Calderón alipoanzisha kile kilichoitwa "vita dhidi ya dawa za kulevya".
Katika matukio mengi ya waliopotea hulazimishwa kujiunga na magenge ya dawa za kulevya au huuawa wanapokataa.
Romandía anaamini kuwa maeneo mengi zaidi ya mbali katika Jalisco yanapaswa kuchunguzwa baada ya ushuhuda kutaja uwepo wa kambi na ranchi nyingine.
"Vijana wanaendelea kupotea," anasema Romandía. "Hivyo sioni kama jambo hili limebadilisha chochote.
"Kuna unyanyapaa, ambao unaumiza sana na lazima ukome nchini Mexico, kwamba wale wanaopotea ni kwa sababu walikuwa na madeni kwa wanamgambo wa dawa za kulevya, au walihusika na magenge au biashara ya dawa za kulevya.
"Lakini tunaona visa vinavyoongezeka, katika miaka ya hivi karibuni, vya vijana na watoto, hata wale walio chini ya umri wa utu uzima, pamoja na watu wazima, wanaolazimishwa kujiunga.
"Baadhi yao huchukuliwa kwa sababu ya ujuzi wao, kama wanajua uhandisi, ujenzi, tiba n.k., wengine kwa sababu wanaweza kulazimishwa kuwa wauaji wa kukodiwa."















