Kikosi cha Artemis II kitarejea vipi duniani?

Chanzo cha picha, NASA
Baada ya kusafiri umbali mrefu zaidi kutoka duniani, hatari kubwa inayowakabili wanaanga wa kikosi cha Artemis II ni jinsi watakavyorejea duniani.
Chombo cha Orion kinatarajiwa kutua pwani ya San Diego saa tisa asubuhi saa za Afrika Mashariki na saa mbili usiku siku ya Ijumaa saa za Marekani.
Rubani wa Artemis II Victor Glover akizungumza na waandishi wa habari alisema "tangu tupewe misheni hiyo tarehe 3 mwezi Aprili mwaka 2023, nimekuwa nikifiria jinsi tutakavyorejea duniani"
Matayarisho
Katika siku yao ya mwisho angani, kikosi cha Artemis kilianza kujiandaa kurejea duniani.
Kando na kurejelea utaratibu wa kutua baharini, pia wamekuwa wakifanya majaribio ya nguo zao zenye uwezo wa kudhibiti kanieneo ambayo itawazuia kupata kizunguzungu wanaporejea duniani.

Chanzo cha picha, NASA
Chombo cha wafanyikazi wa Orion na chombo kinachotoa huduma, zitatengana dakika 20 kabla ya kufika katika anga za dunia. Chombo hicho kitatua kwa njia ambayo itakuwa inajikinga kutoka kwa miale ya jua na joto kali.
Chombo hicho cha anga kinahitaji kuingia kwenye anga ya dunia kwa njia ya iliyosahihi. Dkt. Chris James kutoka Kituo cha Utafiti cha Hypersonic katika Chuo Kikuu cha Queensland, Australia, anasema kuwa kiwango cha makosa kinachokubalika ni kidogo sana.
James anasema, "Wanapofikia eneo la kuingia duniani au entry interface, wanataka kuhakikisha kuwa hali zote za chombo hicho ziko kama zinavyotarajiwa."
"Entry interface" ni hatua ambayo chombo cha anga hupita kutoka angani kuingia kwenye anga ya dunia.
"Wakiingia kwa pembe isiyo sahihi, chombo kinaweza kuteketea kikiwa angani."
"Burudani inaanzia hapa"
Mkurugenzi wa safari ya ndege ya Artemis II, Rick Henfling, alisema katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumatano kwamba Orion itaingia tena kwenye anga kwa urefu wa takribani kilomita 122 kutoka usawa wa bahari.
Henfling alisema, "Na hapo ndipo burudani halisi inaanza."
Inapopita kwenye anga, ngao ya joto ya Orion itakumbana na halijoto ya takribani nyuzi joto 2,700. Hii ni karibu nusu ya joto la uso wa jua.
Ngao hiyo ya joto ilifanyiwa uchunguzi kwa umakini mkubwa kwa sababu ilipata uharibifu mkubwa wakati wa misheni ya kwanza ya Artemis ambayo haikuwa na rubani.
Hata hivyo, wahandisi wana uhakika kuwa wametatua tatizo hilo kwa kurekebisha pembe ya kuingia tena kwenye anga.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Henfling alisema kuwa muda wa kuingia kwenye anga ya dunia hadi kutua baharini ni dakika 13 tu.
Takribani sekunde 24 baada ya kuingia tena kwenye anga, chombo hicho kitapoteza kabisa mawasiliano na dunia, na hali hii itaendelea kwa dakika sita.
Kulingana na James, hii ni kwa sababu chombo kinaposafiri kwa kasi kubwa, hutoa joto jingi ambayo huondoa elektroni kutoka kwenye atomi za oksijeni na nitrojeni, na hivyo kuunda plazma yenye chaji ya umeme ambayo huathiri mawimbi ya redio.
Mkurugenzi huyo wa safari ya Artemis II alisema, "Katika hatua hiyo tutakuwa umbali wa maili kadhaa kutoka eneo la kutua. Kisha tutazingatia kufungua parachuti."
Kupunguza kasi
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Chombo hicho cha Orion kitaingia kwenye anga ya dunia kwa kasi ya zaidi ya kilomita 40,000 kwa saa.
James anasema hatua ya kwanza ya kupunguza kasi ni kutumia anga yenyewe kama breki.
James anaeleza kuwa wanaanga wangetikisika sana kwa kasi hiyo, akiongeza kuwa vyombo visivyo na rubani vinaweza kuingia kwenye anga kwa nguvu ndani ya takribani dakika moja, lakini hali hiyo ni hatari kwa binadamu.
Ili kufanya hali iwe salama zaidi kwa wanaanga hao, pembe ya kuingia hubadilishwa, na hivyo kurefusha mchakato kutoka dakika moja hadi takribani dakika tano na kupunguza nguvu ya chombo hicho kuingia duniani.
Baada ya chombo kupita salama kwenye anga, mfululizo wa parachuti zitafunguka ili kupunguza kasi yake zaidi.
Henfling alisema, "Kwanza, parachuti mbili za kupunguza kasi zitafunguliwa. Hii itafanyika katika urefu wa takribani kilomita 6.7 kutoka usawa wa bahari na itapunguza kasi hadi karibu kilomita 322 kwa saa."
Parachuti za breki hutumika kuleta uthibiti na kupunguza kasi ya chombo hicho kabla ya parachuti kuu kufunguliwa.
Henfling alieleza kuwa parachuti kuu zitafunguliwa katika urefu wa takribani kilomita 1.8 juu ya usawa wa bahari, ili kutoa fursa kwa chombo hicho na wanaanga wake wanne kutua "kwa upole" kwa kasi ya takribani kilomita 32 kwa saa.
Kutua baharini
Timu ya uokoaji itakuwa ikiwangoja wanaanga hao karibu na pwani ya California.
Chombo hicho kinaweza kutua majini kikiwa wima, ikiwa imegeuka juu chini, au ikiegemea upande mmoja. Mifuko ya hewa ya rangi ya chungwa itajaa hewa ili kuirejesha chombo hicho katika hali ya kusimama wima, na hivyo kuruhusu wanaanga hao kutoka nje kwa usalama.

Chanzo cha picha, Getty Images
Meneja msaidizi wa programu ya Orion, Debbie Korth, alisema katika taarifa siku ya Jumatano, "Tunatarajia kuwaokoa wanaanga na kuwafikisha katika vituo vya matibabu ndani ya saa mbili."
Wanaanga hao watakuwa sehemu ya kundi maalum la wanaanga 24 pekee waliowahi kuzunguka mwezi.
James anasisitiza kuwa NASA inachukulia kwa uzito mkubwa sana jukumu lake la kuwarudisha wanaanga hao duniani salama, akihitimisha maelezo yake kwa kusema,
"sitakuwa na amani kabisa hadi nitakapowaona wakirudi duniani."















