VAR inaharibu utamu na uhondo wa soka?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Andy Cryer
- Nafasi, BBC Sport Senior Journalist
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Kama kuna mjadala mkubwa zaidi kuhusu Video Assistant Referee (VAR), teknolojia ya video inayosaidia uamuzi wa uwanjani, tangu ianzishwe, basi huenda ni ule uliotokea katika mechi ya Ligi Kuu kati ya West Ham na Arsenal. Tukio la dakika za jioni, goli lililodhaniwa kuwa la kusawazisha katika muda wa nyongeza, na kisha likafutwa baada ya uchunguzi mrefu wa VAR, limeacha maswali mengi kuliko majibu.
Callum Wilson alijipatia bao ambalo lingeweza kubadili kabisa picha ya mbio za ubingwa na hata vita ya kushuka daraja, lakini furaha ya West Ham ilikatizwa ghafla baada ya refa Chris Kavanagh kulifuta goli hilo kufuatia ushauri wa VAR. Kisa kilichoangaliwa kwa kina kilihusisha madai ya faulo dhidi ya kipa wa Arsenal, David Raya, katika hali iliyokuwa na mikono mingi, kuvutana na msongamano mkubwa wa wachezaji langoni.
West Ham sasa wanataka ufafanuzi wa kina kuhusu mawasiliano yaliyotokea kati ya Kavanagh na afisa wa VAR, Darren England. Klabu hiyo inaamini kuna haja ya kuelewa ni vigezo gani hasa vilivyotumika kufikia uamuzi huo, na pia wanatarajia kuomba kurekodiwa kwa mazungumzo hayo ili kuongeza uwazi wa tukio hilo lililoibua hisia kali.
Kwa upande wa uwanjani, tukio hilo limezua mjadala mpana kuhusu kama VAR inasaidia au inaharibu mchezo. Wapo wanaoona kuwa sheria zilifuatwa, hasa kwa kuzingatia kuvutwa kwa jezi ya Jean-Clair Todibo dhidi ya Raya, lakini wengine wanaamini kwamba kasi na "roho ya mchezo" imepotea katika uchunguzi wa sekunde nyingi na fremu zilizopunguzwa mwendo.
Hatimaye, tukio hili limeacha simulizi kubwa zaidi kuliko mechi yenyewe: je, VAR bado ni chombo cha haki katika soka la kisasa, au imekuwa chanzo kipya cha utata unaogharimu mechi muhimu na huenda hata mataji?
Si tukio la kwanza tata kuhusu VAR

Chanzo cha picha, Getty Images
Mashabiki, makocha na wachezaji wa Ligi Kuu England walikumbushwa jinsi maisha yalivyokuwa huko nyuma bila kuwa na Video Assistant Referee (VAR), teknolojia ya video inayosaidia uamuzi wa uwanjani. Walikumbushwa kupitia maamuzi katika mechi za raundi ya nne ya kombe la FA mapema mwaka huu.
Kwa msimu huu na ule uliopita wa Kombe la FA, VAR haikuwa inatumika hadi raundi ya tano, jambo lililowafanya mashabiki wengi kufurahia kurejea kwa soka lisilo na kusitishwa na teknolojia hiyo.
Baada ya msimu uliojaa utata, maamuzi yaliyochelewa na mkanganyiko uliosababishwa na VAR, baadhi wameanza kuhoji kama kweli mfumo huo unahitajika. Wapo wanaodai kuwa mchezo ungekuwa bora na soka lingekuwa tamu bila VAR.
Baada ya siku iliyojaa ucheleweshaji wa maamuzi, taarifa zinazochanganya na makocha wenye hasira mapema Februari, kiungo wa zamani wa Tottenham, Danny Murphy, alisema katika kipindi cha BBC Match of the Day:
"Kwa manufaa ya mchezo, ningependelea VAR iondolewe.
"Tatizo ni kile inachokifanya kwenye michezo na burudani yenyewe, hasa muda mrefu unaochukuliwa kufikia maamuzi.
Baada ya mabao kadhaa ya kuotea kuruhusiwa, penati ya wazi kukataliwa na maamuzi mengine yenye utata, mjadala kuhusu VAR umerudi tena kwenye hadhira ya wapenda soka
"Burudani tamu au maamuzi sahihi zaidi"?

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ushindi wenye utata wa Newcastle wa mabao 3-1 dhidi ya Aston Villa uliwapa hoja wanaounga mkono VAR na kuwa pigo kwa wale wanaoipinga.
Bao la kwanza la Tammy Abraham lilikuwa bao la wazi la kuotea, Lucas Digne wa Villa aliepuka penati ya wazi kwa mpira uliomgonga mkono, na pia angeweza kutolewa nje kwa kadi nyekundu kutokana na faulo mbaya.
Kocha wa Newcastle, Eddie Howe, alisema: "Nimechanganyikiwa kwa sababu mchezo huwa bora bila VAR kwa upande wa msisimko na burudani kwa mashabiki na sisi pia.
"Lakini VAR hutoa matokeo sahihi zaidi. Inaifanya michezo kuwa ya haki zaidi katika maamuzi."
Kocha wa Aston Villa, Unai Emery, alisema wazi: "VAR ni muhimu. Inahitajika kuwasaidia waamuzi."
Katika mechi ya Liverpool dhidi ya Brighton pia kulikuwa na maamuzi ya utata. Bao la Rio Ngumoha lilikataliwa kimakosa kwa kuotea, huku Brighton wakikasirishwa na penati aliyopewa Mohamed Salah.
Kocha wa Liverpool, Arne Slot, alisema: "Kwa ujumla, napenda kutazama soka bila VAR kwa sababu ukifunga unajua ni bao moja kwa moja.
"Ningependa VAR itumike tu kwa mambo yaliyo wazi kabisa kama kuotea au mpira kuvuka mstari wa goli. Mengine waachiwe waamuzi."
Pep Guardiola wa Manchester City alisema hana uhakika kama soka ni tamu au bora likiwa na VAR au bila VAR:
"Wakati mwingine naona ni bora, wakati mwingine nahisi VAR inasaidia kufanya mchezo uwe wa haki zaidi. Kwa kweli sijui."
Waamuzi wenalemazwa na VAR sasa?

Chanzo cha picha, Getty Images
Wengine wanaamini tatizo si VAR, bali ni waamuzi kutotekeleza majukumu yao ipasavyo.
Alan Shearer alisema:
"Ningependa waamuzi wafanye kazi yao vizuri. Si jambo kubwa sana kuomba hilo.
"Kama unataka ushahidi wa madhara ya VAR kwa waamuzi, Jumamosi ni mfano mzuri. Wanaonekana kuogopa kufanya maamuzi bila kuwa na 'kinga' ya VAR."
Lakini Shay Given alisema: "Hii inaonyesha kwa nini tunahitaji VAR. Maamuzi mengi yalikuwa mabaya. VAR ni msaada hata kama tunailalamikia mara nyingi."
Kocha Howe alikubali kuwa kuna uwezekano wa waamuzi kutegemea VAR kupita kiasi:
"Kuna hoja ya kusema ndio. Wakati VAR ipo, unaweza kufikiria 'sitatoa maamuzi sasa, VAR itaangalia'. Hilo linaweza kupunguza umakini wa maamuzi."
Hata hivyo, mwamuzi wa zamani Graham Scott alikataa wazo kuwa waamuzi wanajificha nyuma ya VAR:
"Sidhani kama hilo ni la haki. Michakato yao haibadiliki sana.
Kilichotokea kwenye mechi ya Westham dhidi ya Arsenal kinakumbusha safari ndefu kuhusu VAR na maamuzi yake. Wapo wanaoyakubali wapo wanaoona inaharibu uhondo wa soka.












